KWELI Msichana mwenye Haemophilia anaweza kufariki dunia pale anavunja ungo

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Hii imekaa vipi kitaalam, Msichana mwenye Haemophilia anaweza kufariki dunia pale anavunja ungo?

IMG_6738.jpeg
 
Tunachokijua
Haemophilia ni ugonjwa wa kurithi ambao hufanya damu isigande vizuri. Madhara ya ugonjwa huu huonekana pindi mwili unapopatwa na majeraha, upasuaji au baada ya kupatwa na jambo lolote linalofanya damu itoke nje ya mwili.

Ni ugonjwa unaosababishwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye jini (gene) zinazotoa amri ya utengenezwaji wa aina fulani za protini zinazoongoza utaratibu wa kuganda kwa damu mwilini, changamoto ambayo hupelekea kutokea kwa uchache wa viunganishi namba 8 au 9 vinavyohitajika kwenye kuganda kwa damu.

Dalili zake
Ugonjwa wa changamoto ya kuganda kwa damu (Haemophilia) huwa na dalili nyingi, baadhi yake ni hizi;
  • Kuvuja damu kwenye maungio ya mwili. Mara nyingi huambatana na kuvimba au maumivu kwenye magoti, ugoko na enka za mwili.
  • Kuvuja damu kwenye ngozi
  • Kuvuja kwa damu isiyoganda kirahisi kwenye fizi na meno hasa baada ya kung’oka kwa jino.
  • Kuvuja kwa damu isiyokoma wakati wa tohara, sindano na chanjo
  • Kuvuja kwa damu kichwani kwa mtoto hasa baada ya kuzaliwa kwa njia ya kawaida (uke)
  • Uwepo wa damu kwenye mkojo na choo
  • Kuwa na changamoto ya kutokwa na damu puani mara kwa mara.
Kifo cha wasichana wenye Haemophilia wakati wa hedhi
Pamoja na uwepo wa dalili tajwa hapo juu, wanawake na wasichana hupatwa na changamoto za ziada za kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi zao, wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.

Upotevu huu mkubwa wa damu huwafanya wapatwe na changamoto za upungufu wa damu, maarufu zaidi kama anemia ambayo huwafanya wawe na uchovu mkubwa, kupauka kwa rangi ya ngozi, kuishiwa nguvu na wengine huenda mbali zaidi kwa kupoteza maisha.

JamiiForums imebaini mambo yafuatayo kuhusu ugonjwa huu;
  1. Asilimia kubwa ya wanawake wenye ugonjwa huu huwa na kiwango kisicho cha hatari sana cha madhara yanayoweza kuua moja kwa moja baada ya kufikia umri wa kuvunja ungo, wakati wa hedhi zao.
  2. Pia, tunatambua kuwa huduma sahihi kwa wanawake na wasichana wenye changamoto hii ikitolewa huokoa uhai, huboresha hali ya maisha na kuwafanya waishi maisha ya kawaida pasipo kupatwa na madhara makubwa.
  3. Hata hivyo, kutokana na kukosekana kwa huduma sahihi pamoja na ukosefu wa tahadhari za kutosha za kuukabili pindi unapotokea, wasichana wenye ugonjwa huu hupatwa na changamoto nyingi zinazoweza kuwafanya wapoteze uhai baada ya kupoteza damu nyingi kwa muda mrefu.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa huduma sahihi inatolewa kwa waathirika wa ugonjwa huu unaoathiri takriban 1% ya watu wote duniani ili waishi maisha marefu huku wakifurahia haki zao kama walivyo binadamu wengine.
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom