Mshtuko mkubwa Fidia ya Dowans

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
Waandishi Wetu
BAADA ya kupigwa mwereke kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, serikali imeliamuru Shirika la Umeme (Tanesco) kuandaa taarifa ya kuueleza umma sakata hilo dhidi ya kampuni ya Dowans Tanzania, lakini wananchi wamepokea vibaya uamuzi wa kulitaka shirika hilo lilipe fidia ya Sh185 bilioni wakisema umesababishwa na viongozi wazembe na wasio na uchungu na nchi.

Katika hukumu ya mahakama hiyo ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, ICC, iliyotolewa Novemba 15, Tanesco imetakiwa kuilipa Dowans fidia ya Sh185 bilioni kutokana na kuvunja mkataba wake wa kuzalisha umeme bila ya kufuata taratibu. Tanesco ilitangaza kuvunja mkataba huo wa Dowans Agosti mosi, 2008 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya mkataba huo kumalizika.

Mkurugenzi wa Tanesco wa wakati huo, Dk Idris Rashid alieleza wakati huo kuwa shirika lake limeamua mkataba huo kwa kuwa unakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2004 na kwamba ulihamishwa kutoka kampuni ya Richmond Development LLC bila ya kufuata taratibu.

Mwaka uliofuata, Tanesco iliibuka na pendekezo la kutaka serikali iikubalie inunue mitambo hiyo wakati tatizo la umeme lipoibuka tena, lakini Bunge likakataa kupitisha pendekezo hilo likisema kuwa litakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma inayokataza serikali au taasisi zake kununua mitumba.

Wakati uamuzi huo wa mahakama hiyo iliyo na makazi yake jijini Paris ukipokewa vibaya na wananchi, jana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliliambia gazeti hili kuwa kutokana na unyeti wa suala hilo, wameiagiza Tanesco kutoa taarifa rasmi ya maelezo ya kina kwa wananchi.

“Ninapozungumza na wewe sasa, natumaini watendaji wa Tanesco wapo katika kujiandaa kutoa maelezo kuhusu suala hilo. Nimewataka wafanye hivyo haraka iwezekanavyo,’’ alisema Ngeleja

Hata hivyo, Waziri Ngeleja hakuwa tayari kutaja siku rasmi ambayo serikali imeliagiza shirika hilo kutoa taarifa hiyo.
“Unajua tukianza kutoa taarifa kwa chombo cha habari kimoja baada ya kingine, taarifa zinaweza zisifike vizuri na kwa usahihi. Wakati wowote, Tanesco wataitisha mkutano na vyombo vya habari na kutoa taarifa,’’ alisema Ngeleja.
Hadi jana jioni watendaji wa Tanesco walikuwa katika kikao cha dharura kujadili pamoja na kuandaa taarifa hiyo.
“Mkurugenzi bado yupo katika kikao, mtafute baadaye,’’ alijibu msaidizi wa Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando majira ya saa 1130 jioni.

Taarifa za uhakika ambazo zililifikia gazeti hili jana jioni zilieleza kwamba Tanesco wanatarajia kuweka wazi suala hilo leo kwa waandishi wa habari.

Baadhi ya wadau wamesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno na kwamba kinaweza kuwa sawa na makusanyo ya mwezi mzima ya Mamlaka ya Tanzania (TRA).

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wachumi na wanasheria walisema uamuzi huo ni hasara na balaa kwa taifa na uchumi wake.

Profesa Abdallah Safar alisema hayo ni matokeo ya wimbi la mikataba mibovu inayoingiwa baina ya serikali ya Tanzania na mashirika au makampuni ya kimataifa, jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu bungeni.

Alisema mikataba mingi haipitishwi bungeni ili kupitiwa na baadaye kuthibitishwa na wabunge kabla ya kusainiwa.
“Hilo ni balaa tu kwa taifa kwa sababu kila mchuma janga. hula na wa kwao. Janga hili ni la wote,” alisema Profesa Safar.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema fedha hizo ni nyingi na ikiwa zitalipwa ni balaa kwa uchumi wa taifa.

“Kiuchumi na kijamii mimi naona kama vile ambavyo hata mwananchi wa kawaida anaweza kuona kwamba ikiwa fedha hizi zitalipwa ni hasara na balaa kwa taifa na Tanesco yenyewe,” alisema Kibodya.

Kibodya alifafanua kuwa, fedha hizo ni sawa na makusanyo ya mwezi mzima ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Ikiwa zitalipwa, kimsingi mambo mengi ya kimaendeleo yatasimama au kuathirika kwa njia moja au nyingine, lakini kisheria Tanesco iliingia mkataba wa kisheria na Dowans hivyo migogoro yao lazima isuluhishwe na mahakama za usulihishi wa migogoro ya kibiashara,” alisema Kibodya.

Hata hivyo, Kibodya alisema hawezi kujua masharti ya mkataba na hukumu ilivyotolewa lakini kwa kuwa ni suala la kisheria, Tanesco inaweza ikakata rufaa.

“Hivi ndivyo namna mambo ya biashara za kimataifa yanavyoendeshwa na uamuzi wa ICC ndio hali halisi ya sheria. Tusichanganye siasa na sheria kama Tanesco ilivunja masharti ya mkataba, lazima msumeno ufanye kazi,” alisema Kibodya.

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shellukindo aliitahadharisha serikali kuwa makini na katika ulipaji wa fidia hiyo ya Sh185 bilioni kutokana na kile alichokiita ni kurejea upya mchezo wa kuigiza wa sakata zima la Richmond.

Shellukindo na kamati yake walikuwa mstari wa mbele kupinga sakata zima la Richmond pamoja na mpango wa Tanesco wa kununua jenereta hizo za Dowans kiasi cha kulifanya shirika hilo kutaka kuhamishia pendekezo hilo la kununua mitambo hiyo kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma iliyokuwa ikiongozwa na Zitto Kabwe, lakini Spika Samuel Sitta alikataa akisema msimamo wa kamati moja ni wa Bunge zima.

Shellukindo aliitaka serikali kukata rufaa kwa kuwa ilishapata hasara kutokana na Dowans kuchelewa kuanza kuzalisha umeme na hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Shellukindo alisema: "Tuko kwenye dunia ya kuliwa. Lazima Watanzania tusimame imara kuhakikisha hatuliwi... serikali haipaswi kulipa fedha hizo kwa kuhakikisha inakata rufaa."

Mbunge huyo wa zamani wa Bumbuli alisisitiza akisema: "Huu ni mchezo ule ule wa kuigiza wa Richmond. Lazima uangaliwe mkataba wenyewe; hao Dowans waliingiaje; mazingira yapi; walitokea wapi? Lakini, kama tukizubaa tutaliwa kweli maana hii ni dunia ya kuliwa kwa waliozubaa."

Taarifa hizo zinakuja wakati mmoja wa watuhumiwa wakuu wa mkataba wa Richmond aliyejiuzulu katika baraza la mawaziri mnamo Februari 2008, alitajwa kuwa safarini Ufaransa hivi karibuni kabla ya taarifa hizo kusambaa juzi.

Shellukindo aliliitaka Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilishughulikie suala hilo kwa umakini kwa kuwa hali ilivyo, inoanyesha kuna mchezo mchafu unaotaka kufanyika siku za usoni na kuwataka watanzania wasikubali sakata hilo lipite na kwamba mjadala wa Richmond ulishafungwa na utekelezaji wa maazimio ya Bunge umeanza, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa baadhi ya watuhumiwa.

Uamuzi huo wa ICC, ambao unaweza kuibua upya sakata la Richmond, ulitolewa na jopo la majaji chini ya uenyekiti Gerald Aksen na wasuluhihi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker.

Jopo hilo liliamuru Tanesco ilipe fidia ya zaidi ya Sh36 bilioni na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka inayofikia kiasi cha zaidi ya Sh26 bilioni tangu Juni 15, 2010 hadi fidia hiyo itakapolipwa.

Pia jopo hilo liliamuru malipo ya Sh60 bilioni na riba ya asilimia 7.5 ambayo ni sawa na Sh 55bilioni kuanzia Juni 15, 2010 hadi wakati wa malipo.

Katika uamuzi huo, jopo hilo lilisisitiza kuwa ada na gharama za wasuluhishi na za utawala Sh1bilioni kwa wasuluhishi wa ICC zinatakiwa zilipwe na pande zote.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu hukumu hiyo ya ICC, mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema: “No comment kwa hilo, isije ikaonekana nimefurahia.”

Hata hivyo, Zitto alisema kuwa anachosubiri ni taarifa ya serikali baada ya uamuzi huo wa ICC, lakini kwake ni jambo linalomuumiza mno.

“Nasema isije ikaonekana nimefurahia hukumu hiyo, tunasubiri taarifa ya serikali, lakini kwa kweli inauma. Inauma kwa sababu Watanzania bado wana tatizo la kukosa umeme maeneo mengi na bado serikali inatakiwa kulipa fedha hizo... ni nyingi mno nimesoma katika gazeti ni zaidi ya Sh185 bilioni,” alisema Zitto.

Alisema wanaoweza kutoa hukumu sasa ni wananchi kwa kuwa yeye alitimiza wajibu wake kwa taifa lake kama mbunge.

Wakati wa sakata hilo, Zitto aliishauri serikali itaifishe mitambo ya Dowans ili itumike kuzalisha umeme, uamuzi ambao ungeweza kukaribisha hatua nyingine za kisheria dhidi ya Tanesco.

Alikumbusha kuwa wakati wa sakata hilo la Dowans na kampuni tata ya Richmond, aliishauri serikali mara nyingi, lakini ushauri wake haukufuatwa wala kuzingatiwa hata akazushiwa mambo mengi.

“Ndio maana nasena no comment... walinizushia sana wakati mimi nilijitahidi sana kuishauri serikali. Sasa kwa uamuzi huo, court will be public opinions, (watakaohukumu ni wananchi),” alisema Zitto ambaye pia ni naibu kiongozi wa upinzani bungeni.

Zitto, ambaye pia ni kaimu katibu mkuu wa Chadema, alimtaka Waziri Ngeleja kutoa ufafanuzi wa hasara wanayotarajia kuipata kutokana na malipo ya fidia ambayo Tanesco inadaiwa na kampuni nyingine ya kufua umeme ya IPTL.

Naye mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alisema kimsingi serikali ndiyo iliyotakiwa kufungua kesi kwa niaba ya Watanzania kudai fidia kutokana Dowans kushindwa kutimiza masharti ya mkataba.

“Tulitaraji serikali ingefungua kesi sitahiki na kupata fidia kutokana na mkataba kutotimizwa na kusababisha tujikute katika mgao mkali wa umeme... mikataba mibovu ndiyo inayochangia kupanda kwa gharama za umeme,” alisema Mnyika.

Mnyika pia alimtaka waziri kutoa ufafanuzi kuhusu mgao wa umeme unaoendelea sasa kwenye maeneo mengi ya nchi kwa kuwa Tanesco halijaeleza suala hilo kwa mapana.

Alisema wananchi wa Tanzania wanapata adha ya mgao kutokana na sababu ambazo zingeweza kuzuilika huku shirika hilo likishindwa kutoa ufafanuzi wa kutosha.

Naye mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini(CTI), Christine Kilindu alisema fedha hizo ni mzigo mkubwa kwa Tanesco na akashauri ikate rufaa.

“Pamoja na kwamba sijajua kama katika kesi hii vifungu vya sheria vinatoa nafasi ya kukata rufaa, lakini ni vyema Tanesco wakate rufaa kwani fedha hizo ni nyingi na ni hatari sana kwa shirika hilo,’’ alisema Kilindu.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu suala hilo, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustapha Mkulo alisema: “Hilo nimelisoma kwenye magazeti, nisingependa ‘kucomment’ (kutoa maoni), mpaka nipate taarifa rasmi ya serikali.”

Habari hii imeandaliwa na Salim Said, Exuper Kachenje, Sadick Mtulya, Geofrey Nyang’oro, Ramadhani Semtawa na Fidelis Butahe

chanzo:Mshtuko mkubwa Fidia ya Dowans
 
• Baadhi ya vigogo washangilia serikali kubwagwa

na Mwandishi wetu


MAKUNDI hasimu ndani ya serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyokuwa yanavutana kuhusu kashfa za kampuni za kufua umeme wa dharura za Richmond na Dowans miaka miwili iliyopita, yameibuka upya, huku kila kundi likichekelea kimya kimya kuwa mshindi, na kulishutumu kundi jingine. Kundi moja linafurahia ushindi wa kampuni ya kigeni (Dowans) dhidi ya serikali, ambapo Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, linapswa kulipa sh bilioni 185; na kundi jingine linafurahia ushindi wa serikali dhidi ya kampuni nyingine ya kigeni (Richmond) ambayo inapaswa kuilipa serikali Dola za Kimarekani 1,201,933.08.

Taarifa ya TANESCO kwa umma iliyotolewa jana ilibainisha kuwa Richmond, ambayo iliishtaki TANESCO kwa kuvunja mkataba na kuikashifu, ilitaka ilipwe dola za Kimarekani milioni 169, lakini TANESCO ndiyo iliyoshinda keshi hiyo, hivyo kustahili mabilioni hayo ya shilingi. Hata hivyo, Richmond nayo ilishinda kipengele cha kukashifiwa, hivyo kustahili kulipwa dola za Kimarekani 50,000 (zaidi ya sh 50,000,000).

Hata hivyo, kesi ambayo imeibua msisimko mkubwa na ambayo imekuwa ikiripotiwa kwenye vyombo vya habari tangu juzi ni ile inayohusu ushindi wa Dowans dhidi ya TANESCO, ambayo watetezi wa Dowans wanaona kama ushindi kwao, lakini hawasemi hivyo waziwazi.

Mashauri yote mawili yaliamriwa katika Baraza la Usuluhishi la Kimataifa (ICC). La Richmond liipelekwa Septemba 2008 na la Dowans Novemba 2008.

Tanzania Daima imebaini kuwa kundi lililokuwa likiunga mkono mitambo hiyo inunuliwe na serikali, limeonekana kushangilia ushindi wa Dowans, likidai kwamba msimamo wao ulikuwa ukitetea maslahi ya taifa.
Wanadai kuwa madai yao yaliegemea kwenye utaalamu zaidi kuliko siasa, huku wakilishutumu kundi jingine kwamba lilizingatia zaidi siasa kuliko utaalamu.

Linadai njia rahisi ilikuwa ni kununua mitambo hiyo kwa sh bilioni 86 au njia ya pili ilikuwa ni kuendelea na mkataba wa kuilipa Dowans milioni 152 kwa siku, huku umeme ukipatikana.
"Sasa hivi Song Gas tunailipa milioni 256 kwa siku, IPTL tunailipa milioni 300 kwa siku, upi ni mkataba rahisi kama si Dowans au Richmond kama ingeendelea ambapo tungeilipa bilioni 172 ndani ya miaka miwili na tungepata umeme, tungeokoa mgao.
"Pesa hizo tungelipa na umeme tungepata…hili ni fundisho kwa wanasiasa kuingilia masuala la kitaalamu kwani deni hili ni kubwa na TANESCO haiwezi kulilipa. Wakisema watalipa watafilisika. Leo hii serikali ina nakisi ya bajeti sh bilioni 800. Tutatoa wapi bilioni 185 za kuilipa Dowans?" alisema mdau mmoja wa kundi hilo.

Lakini kundi lililokuwa linakataa serikali kununua mitambo hiyo, linasema heri gharama hizi za sasa kuliko kama serikali ingeendelea kuilipa Dowans sh 152 milioni kila siku kwa miaka miwili mfululizo.
Mmoja wa vinara wa kundi hilo alisema walichosimamia wao ni kulinda sheria ya nchi kuliko maslahi ya wageni na mafisadi wachache, ambao walikuwa radhi kuvunja sheria ya manunuzi ya umma inayokataza kununua mitambo mitumba.
"Hatukuwa tayari kupinda sheria kwa ajili ya kuwapa mafisadi ulaji, lakini pia kama wao wanadhani wameshinda, huu ni ushindi wa giza, shetani anaweza kushinda kwa muda mfupi tu," alisema mmoja wa vinara hao waliojipambanua kama makamanda wa ufisadi.
Mwingine, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema taarifa za magazeti zinazotolewa sasa hivi nyingi ni za kichochezi, kwani zinaficha ukweli wa serikali kuishinda Richmond, huku zikikuza mjadala wa Dowans kuishinda serikali.
Alisisitiza kwamba ushindi wa Dowans hauna uhusiano na kuvunjwa mkataba, kwani wao ndio walivunja kwa kisingizio kwamba mazingira ya kazi Tanzania si mazuri kwao, lakini walikuwa na makubaliano fulani na TANESCO ambayo walitaka yatimizwe, ndiyo maana wakaipeleka kwenye usuluhishi huo.
Wakati malumbano ya makundi hayo yakipamba moto, jama TANESCO ilitoa tamko ikisema:
"TANESCO imeomba Mahakama ya Kimataifa (ICC) kuandikisha maamuzi yake katika mahakama kuu ya Tanzania kama inavyotakiwa kisheria ili kuruhusu TANESCO iweze kuchukua hatua nyingine yoyote katika suala hili ikibidi."

TANESCO haijaweka wazi hatua inazotaka kuchukua, lakini mtaalamu mmoja wa sheria aliyezungumza na gazeti hili, alisema kuwa kesi za usuluhishi hazina kukata rufaa.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa serikali imeshinda shauri dhidi ya Richmond, hivyo inatakiwa ilipwe dola za Kimarekani 1,201,933.08 ikiwa ni asilimia 50 ya gharama za kisheria na gharama nyinginezo; na kwamba Richmond nayo imeshinda kesi katika kipengele cha kukashfiwa (haijaelezwa ni kashfa ipi) hivyo, TANESCO inatakiwa kuilipa Richmond dola za Kimarekani 50,000 kwa madai hayo ya kukashfiwa.
Lakini Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema kuwa wao kama serikali wanasubiri kauli ya TANESCO kuona kama ina ubavu wa kulipa fidia hiyo.
Serikali hadi jana ilishindwa kueleza bayana endapo iko tayari kuingilia kati juu ya ulipaji wa fidia hiyo inayodaiwa TANESCO.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Ngeleja alisema: "TANESCO wanaandaa taarifa juu ya deni hilo na mgao wa umeme, serikali haiwezi kueleza lolote kuhusiana na hayo ili tusigongane kimawazo..., tunasubiri wanasemaje kuhusiana na deni la Dowans, endapo wataomba msaada tuko tayari kuwasaidia.., ila kwa sasa siwezi kuyagusia hayo."

Tangu taarifa za ushindi na madai ya Dowans dhidi ya serikali zilipotangazwa juzi, serikali imekuwa ikihaha kutoa taarifa, lakini hata hivyo haijakidhi hoja za wananchi wanaotaka kujua hatima ya shirika lao iwapo ama litalipa gharama zote hizo au litashindwa kabisa kulipa.
Tangu juzi, viongozi kadhaa wa mamlaka husika wamekuwa wakikutana kwa dharura na katika vikao vya muda mrefu.
 
Kwa hiyo ndiyo kusema kufa kufaana.Wengine wanasikitika na wengine wanashangilia ushindi.Nyie wabunge mnaoshangilia serikali kubwagwa na Dowans kumbukeni ile nahau kuwa "Wapambanapo mafahari wawili ziumiazo ni nyasi".

Mzigo wote wa gharama za umeme utamwangukia mwananchi wa kawaida na kumfanya aendelee kuwa maskini.Eee Mungu utuepushe na kadhia hii ya umeme nchini Tanzania,tumeteseka vya kutosha.Amen
 
Sijui nani ataweza kututoa kwenye dimbwi hili na mchezo huu kuigiza!!!watu 3 tu wakiliwa hao michezo kama hii itaishia hapo hapo....
 
a king is always a king. Hapa ni uthibitisho kuwa tuna wanasheria bomu. Mikataba ni vipengele ukivunja, umevunja hivyo lazima uadhibiwe lakini kutotimiza masharti ni sawa na kuvunja mkataba, kile kitendo cha Richmond LLC kushindwa kuzalisha umeme ndiko kulikovunja mkataba rasmi sasa hao Dowans walirithi nini ilihali mkataba ulitakiwa uwe umevunjika?. Wanasheria tunao na hili waliliona ila kwa vile linamhusu the king maker, once the king, always the king.
 
Mimi nafikiri ni wakati muafaka sasa kwa Rais au mawaziri wake wa Madini na Nishati to come-out and tell wananchi nini hasa maana ya matokeo ya hizi kesi mbili yaani ya Richmond na hiyo ya Dowans. Haiwezekani hata kidogo kwa kampuni iloingia mkataba wa kisiri kati ya Richmond na Dowans BILA TANESCO kujua, leo hii ndio ishinde na Tanesco kutakiwa kuilipa kampuni hii fidia ya hizo Bilion 185. Mi nafikiri baada ya Richmond kuiuzia Dowans mkataba wa Tanesco, waliwajulisha kila kitu Tanesco, japo nahisi Tanesco hawakuwa wakweli kwa kamati ya bunge iliyowahoji Tanesco
 
Back
Top Bottom