Mshtakiwa wa kesi ya Mirungi akusudia kuomba majadiliano na DPP ili kumaliza Kesi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,352
8,034
Mshtakiwa Rhoda Salum (48) anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 23.84 za mirungi, anakusudia kumwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), akiomba kukiri shtaka lake na kupunguziwa adhabu ili waweze kuimaliza kesi hiyo.

Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya kilo 23.84 za mirungi, kinyume na sheria.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Februari 16, 2023 na kusomewa kesi inayomkabili.

Leo, wakili wa Serikali Ashura Mnzava aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH) lakini mshtakiwa anakusudia kuandika barua ya kufanya majadiliano na DPP ili aweze kuimaliza kesi yake.

Mnzava ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate anayesikiliza shauri hilo.

Mzava baada ya kueleza hayo, aliiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ili wakapitie jalada ili kujua kiasi kinachostahili kufanyiwa majadiliano (Plea bargaini).

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 11, 2023 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili halina dhamana.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 26, 2023 katika mtaa wa Wailes uliopo Wilaya ya Temeke.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha kilo 23 za Mirungi, kinyume cha sheria.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, alikana kutenda kosa hilo.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom