Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,318
- 33,125
Mbunge wa Rombo, Basil Mramba.
Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro
Mbunge wa Rombo, Basil Mramba, ametumia fursa ya kuwahutubia wachungaji 42 wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT) kwa kujitakasa kwamba yu mtu safi na mchapa kazi na kwamba ataendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Sambamba na Mramba, pia Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro ambaye aliitisha mkutano wa wachungaji hao ulioanza saa 4:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, aliwasilisha rasmi maombi ya kutaka wamsaidie kuwasilisha ujumbe kwa waumini wao kwamba anakusudia kuwania tena ubunge katika jimbo hilo.
Katika mkutano huo ambao ni nadra kutokea katika kipindi hiki cha kupanda kwa joto la uchaguzi, Mramba na Kimaro, walitumia jukwaa hilo kujisafishia njia ya kuwania ubunge huku Mramba akitamba hakuna wa kumzuia isipokuwa kama tu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikimkataa.
Wachungaji hao wanatoka Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo linalojumisha sharika kutoka wilaya za Rombo na Moshi Vijijini.
Katika mkutano huo uliofanyika makao makuu ya jimbo hilo, Himo, Mramba ambaye aliwasili ukumbini saa 7:00 mchana na kulakiwa na Kimaro, alisema si kila mwanaume anayevaa suruali au mwanamke anayevaa sketi anastahili kuwa mbunge na kuwataka wananchi kuwa makini na watu wanaojipitisha pitisha katika majimbo yao.
Mramba alisema ingawa anakabiliwa na kesi mahakamani ambayo imempunguzia muda wa kuwahudumia wapigakura wake, bado anakubalika katika jimbo lake na hiyo inatokana na jitihada zake za kuwatumikia wananchi kwa moyo wake wote kuhakikisha wanajikwamua dhidi ya wimbi la umaskini.
Siasa sio kamari, kuwa kiongozi ni lazima uwe na wito fulani ndani yako na vile vile siasa ni kazi mbaya, alisema bila kufafanua.
Aidha, aliwaponda baadhi ya wabunge ambao kwa sasa wanahaha katika majimbo yao kwa kurudi kuwabembeleza wananchi dakika za mwisho ili hali muda wao wa miaka minne waliutumia kwa kukaa jijini Dar es Salaam na kuishi maisha ya starehe.
Wabunge wengi hawaendi kwenye majimbo yao kwa ajili ya kufanya mikutano na kujua kero za wananchi, wametoa ahadi lukuki, lakini hakuna walizotekeleza na kwa sasa ndio wanahaha..haya ni mambo ya kutisha sana kwani ni wachache sana wanaopata ubunge na kutatua kero, alisema.
Mramba alisema viongozi wanaandaliwa na hawaibuki tu kwa kuwa si kila mtu anaweza kuwa kiongozi na kama Mungu amepanga mtu awe kiongozi atakuwa tu hata wanadamu wakiweka vizuizi.
Alisema baadhi ya watu wanadhani kuwa mbunge ni mtu mwenye uwezo bila kujua kuwa mbunge ni yule ambaye ana nia ya dhati na uwezo katika kuwakwamua wananchi kwenye lindi la umaskini.
Alisema aliteuliwa na Mwalimu Julius Nyerere kama mbunge wa kuteuliwa miaka ya 80 ambapo alitumia miaka mitano kujifunza na baada ya hapo alikuwa mzoefu na kwamba kila mara anakumbuka kauli ya Mwalimu Nyerere iliyomwambia mimi nastaafu ila wewe baki Rombo wasaidie wananchi wa Rombojambo ambalo amekuwa akilifanya hadi sasa.
Alisema kuwa yeye ni mzoefu katika utumishi wa umma na ubunge na amefanya kazi na marais wote wa awamu nne.
Dunia ina watu wazuri na wabaya, tunaishi nao na tunafanya kazi nao, mimi ni mzoefu wa kushtakiwa na hilo halinikatishi tamaa ya kuwatumikia wananchi wangu ambao bado wana imani kubwa na mimi, alisema Mramba.
Mramba anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa Waziri wa Fedha kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
Akimzunguzia mbunge huyo, Mchungaji Elias Sillayo, alisema alimfahamu miaka ya 80 akiwa usharika wa Mengwe na kwamba wananchi bado wanamuhitaji na wanaomba kesi yake imalizike haraka ili aendelee kuwatumikia.
Naye Kimaro akizungumza na wachungaji hao alisema utumishi wa umma si fursa ya kunufaisha mtu binafsi, rafiki, wapambe na si fursa ya kutukuza itikadi za kisiasa.
Alisema utumishi wa umma ni dhamana na fursa adimu kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya wananchi wote.
Kimaro alisema daima ataendelea kuwa mkweli kwani mtu anapokosea asipoambiwa kuwa amekosea ni kutenda dhambi na anapoona maovu na kutokusema ni kumkosea Mungu na ndio maana amekuwa akisimama kidete bungeni na kuwaeleza.
Wachungaji hao kwa kauli moja waliunga mkono kazi zilizofanywa na Kimaro na kuahidi kuhakikisha anarudi tena jimboni kwa kusoma maazimio yao.
Akisoma azimio la wachungaji hao kutoka katika sharika za jimbo hilo, Mchungaji wa Usharika wa Karimeni Mwika, Elias Sillayo, alisema kwa kauli moja wachungaji hao wataenda kuwaeleza waumini wao kuwa mapungufu yaliyopo yanarekebishwa hivyo ni vyema wakampa nafasi nyingine ya uongozi.
Alisema kipindi cha miaka mitano amejitahidi kufanya mambo mengi na alitumia muda huo kujifunza hivyo ni vyema wakampa nafasi ya kumaliza aliyoyaanza.
Mchungaji Sillayo aliongeza kuwa jimbo hilo linahitaji viongozi bora na si bora viongozi na kuhoji kama wanaweza kuchagua viongozi wazuri wa kanisa ni kwanini washindwe kuchagua viongozi wazuri wa jamii.
Mbunge wetu huyu tumpe nafasi nyingine ya kutuwakilisha bungeni, alisema.
Aidha, wachungaji hao walimtaka mbunge huyo iwapo atapata ridhaa ya wananchi katika kipindi kingine atekeleze ahadi zote alizoahidi.
Alisema wachungaji hao wanafanya ibada maalum kwa ajili ya kuombea uchaguzi mkuu wa Oktoba ili uwe wa amani na utulivu ikiwa ni pamoja na wananchi kufunuliwa katika kuchagua kiongozi mwenye nia ya kuwaletea maendeleo na si kujinufaisha binafsi.
Mkutano huo ulifanyika chini ya uenyekiti wa Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Luca Kessy.
Akiwakaribisha wachungaji hao, Mchungaji John Mlay alisema kila serikali ni lazima imkubali Mungu kwani hakuna serikali inayoweza kufanikiwa bila kumtambua Mungu kwani pasipo yeye hakuna serikali inayoweza kusimama.
Tambueni kuwa mnaongoza kwa niaba ya Mungu, pasipo Mungu hatuwezi lolote na ni vyema tukawa macho uchaguzi usitufikishe katika machafuko ya kupoteza lulu ya amani na utulivu iliyopo kwa sasa, alisema.
Mbali na wachungaji na wabunge hao, pia mkutano huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Musa Samizi, ambaye aliwataka viongozi wa dini waombee amani wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Alisema Serikali inatambua mchango wa makanisa katika elimu, afya, maji kwani yamekuwa yakitoa huduma bora ndiyo maana shule zake ni bora katika kufaulisha.
Alimsifu Kimaro kwa kusema Vunjo wana bahati ya kuwa na mbunge muwazi kwani kama mtu ni mlarushwa anampa wazi kuwa ni mlarushwa; ni jasir.
Pia alikuwapo Katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Stephen Kazidi, ambaye aliwataka viongozi wa dini kutokukubali makanisa kutumika kama majukwaa ya kisiasa; wasaidie kuhubiri amani; waonye wanaoleta chokochoko; wasikubali nchi kuingia katika machafuko kama majirani zetu. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu CCM Wilaya ya Moshi, Kingazi, ambaye hakusema kitu. Mkutano huo ulifungwa saa 12 jioni.
CHANZO: NIPASHE