MZK
JF-Expert Member
- Sep 13, 2012
- 223
- 303
Mradi wa Umeme wa maporomoko ya Mto Rusumo uliopo mpakani wa Tanzania na Rwanda, unazishirikisha Nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi unaendeshwa kwa mkopo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika kupitia taasisi au mtu kati anayeitwa NELSAP, mradi huu unatarajiwa utakapokamilika utazalisha umeme wa kiasi cha 80MW, ambazo zitagawanywa kwa Nchi tatu Mradi huu mpaka utakapokamilika unatarajiwa kutumia kiasi cha Zaidi dola za Kimarekani milloni 500, ambazo ni Zaidi ya trilioni moja ya Tanzania
Mradi huu ni mojawapo ya miradi ya gharama sana Duniani ,ni mara 4 hivi ya gharama za mradi wa Umeme wa Stieglers Gorge (mradi wa Rufiji Stieglers gorge ni kama 3.9trilioni lakini 2100MW, ) Gharama hizi za mradi wa wa Umeme wa Maporomoko ya Rusumo zilitakiwa zijenge miradi kama 4 mingine ya 80MW ukilinganisha na mradi wa Umeme wa Stieglers Gorge. Ugharama huu wa mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Rusumo ni kutokana na muundo wa wa usimamizi wa mradi huu.
Mradi huu una wasimamizi takribani Wanne, World Bank, African Development Bank, Nelsap, Rusumo Power Company limited, na Mshauri Mwelekezi, wote hawa wanatafuna pesa itakayolipwa na mlala hoi kutoka Tanzania, Burundi na Rwanda. Pesa za mradi huu zimetafutwa na taasisi au mtu kati anayeitwa NELSAP, akakopa kwa niaba ya Serikali hizi tatu na kampuni tarajiwa itakayoendesha mradi huu(Rusumo Power Company Limited) ambayo ipo hewani hewani kama Nchi ya Kusadikika mpaka sasa hivi.
Wasimamizi hawa wa Mradi na waliokopa hizi pesa NELSAP wamejitengea takribani dola za Kimarekani miliono 37 sawa na takribani Zaidi ya Tsh bilioni 70. Wanaishi katika Mbingu ya Saba kwa kulipana mipesa minono kupitia semina, warsha, makongamano na tour mbali mbali yote haya yakifanyika Ughabuni ili mipesa ya mkopo itakayolipwa na walalahoi iendelee kuteketea kama Msitu wa AMAZON. Wananchi wanaoishi eneo la Mradi ( Kijiji cha Rusumo Tanzania na Rusumo Rwanda) wanaendelea kuishi katika maisha duni wakikosa hata huduma za msingi za Kiafya, maji, barabara n.k
Wakati mradi huu ukianza ulitengewa kiasi cha Zaidi ya dola za Kimarekani milioni (sawa takribani billioni 70 za Kitanzania) kwa ajiri shughuri za maendeleo ya Jamii kwa vijiji vinavyozunguka mradi huu (LOCAL DEVELOPMENT AND BENEFIT SHARING) Fungu hili lilikuwa hasa kwa ajiri ya kazi kuu mbili, Resetlement Action Plan (RAP) na Local Area Development Plan (LADP). Wasimamizi wa Mradi NELSAP waliahidi miradi kadhaa watakayoifanya kwa vijiji vilivyopo eneo la mradi kama, Ujenzi wa Shule, Kituo cha Afya, Kuleta Maji na Kusaidia Wananchi wa Chini kupitia miradi ya Ujasiramali. Hadi naandika Makala hii hizi pesa za mafungu hayo imebaki ni kitendawili huku kina mama na watoto wa eneo hili wakitaabika kwa huduma za maji na afya.Ziko wapi hizi bilioni 70?
Wananchi wa Eneo hili kabla ya kuanza mradi waliopo ndani ya eneo la mradi waliahidiwa watalipwa na kuhamishwa kwa nyumba zilizopo karibu na eneo laulipuaji wa miamba kupitia fungu la Resettlement Action Plan (RAP) na NELSAP ili kupisha ulipuaji wa miamba , tofauti yake walifanyiwa tathimini na wengine hawakulipwa pesa yoyote. Nyumba nyingi za wakazi maskini wa eneo hili hasa upande wa Tanzania zimepasuka na kuharibiwa vibaya na ulipuaji wa miamba hali inayotishia usalama wa wakazi wa hizi nyumba
Wasimamizi hawa wa mradi huu NELSAP wanasuasua hata kuhamia kwene nyumba za kisasa zilizopo eneo la mradi ili kuweza kufuatilia kwa Makini kinachoendelea katika mradi , nyumba nzuri wamejengewa ili waishi kupunguza gharama lakini wamezipuuzia na wameamua kuishi katika Mahoteli makubwa upande wa Rwanda, huku wakendesha magari ya kifali kila siku Zaidi ya Kilometer 60 kwa kila siku kuja eneo la mradi.
Kwa ushauri wangu hawa wasimamizi World Bank, African Bank na NELSAP ambao maamuzi yao yamekuwa ni ya kuchelewesha mradi huu usiishe kwa wakati maana mpaka hivi sasa hata nusu ya uj(mradi ulitegemewa kukamilika mwaka 2019) ili pesa za mradi huu ziendelee kuteketea kupitia semina, warsha, makongamano na tour mbali mbali wajiondoe kwenye usimamizi wa mradi huu wamwachie TANESCO wa mradi huu kutoka Nchi Tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda (RUSUMO POWER COMPANY LIMITED) ili asimamie usimamizi kwa kushirikiana na Mshauri mwelekezi ambao wanatosha kabisa. Muda wote toka mradi huu umeanza 2016 mpaka leo pesa tuliyopoteza walala hoi wa hizi Nchi Tatu imetosha kwa kuhudumia hawa watu wa kati wa mradi huu. Kinachofanyika kwa hawa ni kuona huu mradi ni wa Nchi Tatu hivyo hakuna atakayekuwa anafuatilia na mwenye uchungu nao
Mawaziri wa husika wa hizi Nchi Tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda wafanye mchakato haraka wa kuipa meno kampuni ya Kizalendo ya Rusumo Power Company Limited ili iwe na maamuzi ya mradi huu hawa NELSAP , World Bank na African Development Bank wasubiri ripoti ya utekelezaji tu, maana huu mkopo hawatatusaidia kulipa bali tutalipa sisi Walalahoi wa Tanzania, Rwanda na Burundi.
Hongera ziende kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania Dk JOHN POMBE MAGUFULI(PhD) kwa kuamua kujenga miradi mikubwa kwa kutumia Pesa zetu za ndani na kukataa mikopo ya hawa Wafadhili wenye masharti magumu yanayoongeza Gharama mara dufu ya miradi kama huu wa Umeme Maporomoko ya Rusumo.