“Mpishi wa Putin” na dhamira za Urusi Afrika

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
KUNA mkasa ambao kamwe sitousahau. Nilisimuliwa mkasa huyo na rafiki yangu aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Jerry Rawlings huko Ghana. Hiyo ilikuwa serikali aliyoiunda Rawlings baada ya kumpindua Rais Hilla Limann Desemba 31, 1982. Yalikuwa mapinduzi ya pili aliyoyafanya Rawlings. Ya kwanza yakiwa ya Mei 14, 1979 yaliyoipindua serikali ya kijeshi ya Jenerali Fred Akuffo.

Huyo rafiki yangu siku moja alinishangaza aliponieleza aliyokuwa akiyafanya alipokuwa waziri. Alinambia kwamba kila baada ya kumalizika mkutano wao wa Baraza la Mawaziri alikuwa akifululiza moja kwa moja kwenda nyumbani kwa balozi wa Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) jijini Accra.

Akifika huko akimwagia balozi wa Sovieti yote yaliyojiri siku hiyo katika mkutano wao wa mawaziri. Hakuwa akibania kitu. Ulikuwa wakati ambapo Rawlings alikuwa yu moto. Akihamaki alikuwa akiwatandika makonde mawaziri wake walipokuwa na vikao vyao vya Baraza la Mawaziri.

Rafiki yangu hakuona junaha kufanya aliyokuwa akiyafanya. Kuna jambo moja tu lililokuwa likimshangaza. Alinambia kwamba kila alipokuwa akenda kwa balozi na mkewe basi huyo balozi naye alikuwa akimwita mke wake na akiwaambia mabibi hao wawili waondoke sebuleni na wende behewani kupunga upepo.

Nilishtuka nilipoyasikia niliyoyasikia. Waziri wa nchi huru ya Kiafrika akizitoa siri za serikali yake kwa hiyari yake na akimpa balozi wa taifa la kigeni. Rafiki yangu hakufanya aliyoyafanya kwa tamaa ya fedha.

Siku hizo zilikuwa ni siku za “Vita Baridi” baina ya kambi ya nchi za kibepari, ikiongozwa na Marekani, na ile ya nchi za kisoshalisti, iliyokuwa ikiongozwa na Muungano wa Jamhuri za Kisovieti. Rafiki yangu akifuata itikadi ya kisiasa iliyokuwa ya mrengo wa kushoto zaidi ya ile ya Rais wake, Rawlings. Alikuwa mfuasi wa Marx na Lenin.

Akiamini kwamba alikuwa akifanya ndivyo kuliarifu dola la Sovieti kuhusu sera na mikakati ya serikali ya Ghana. Kwa vile Muungano wa Sovieti ulikuwa na itikadi moja ya kisiasa na ile ya kwake, akihisi ilikuwa ni jukumu lake kulisaidia dola hilo la Kikomunisti.

Wakomunisti wa nchi moja wakitakiwa kuwaunga mkono wakomunisti wa nchi nyingine. Mshikamano wa aina hiyo ulikuwa wa kihalisia. Nchi zikishikamana, vyama vikishikamana na hata wafuasi binafsi wa itikadi hiyo wakishikamana.

Mara ya mwisho rafiki yangu kwenda kwa balozi wa Sovieti ilikuwa siku Rawlings alipomfukuza uwaziri. Aliona ende kumuarifu rafiki yake, comrade mwenzake, na wayazungumze yaliyomfika. Alipofika kwa balozi alizuiwa chini akiambiwa asubiri asipande juu.

Alisubiri na kusubiri na mwishowe subira zilivyokuwa zinamuishia akang’amua kwamba balozi hakuwa na haja naye. Hakutaka kumuona. Ndipo akajiendea zake. Hawakuonana tena hadi leo.

Niliikumbuka kadhia hiyo majuzi, Oktoba 25, Rais Vladimir Putin wa Urussi alipoufungua mkutano wake na viongozi wa Kiafrika uliofanywa Sochi, Urussi. Mkutano huo ulikuwa wa muhimu kwani kama alivyoashiria Putin unafungua ukurasa mpya katika uhusiano baina ya Urussi na mataifa ya Kiafrika.

Ni ukurasa mpya kwa sababu uhusiano baina ya Urussi na nchi za Kiafrika ulikuwa umepwaya tangu Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti usambaratike katika miezi ya mwisho ya 1991. Hali hiyo ilizuka licha ya kwamba Urussi, iliyokuwa nchi kubwa na yenye nguvu katika Muungano wa Kisovieti, ilikuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi za Kiafrika katika mapambano yao dhidi ya wakoloni.

Wasovieti hali kadhalika waliwekeza kwa kiwango kikubwa sana katika kuwapatia elimu ya juu Waafrika. Kutokana na mchango wao na wa nchi nyingi nyingine za Ulaya ya Mashariki Afrika imeweza kupata madaktari, wahandisi na wataalamu wengine wa nyanja mbali mbali.

Bila ya fursa za masomo ambazo Waafrika walizipata katika Muungano wa Kisovieti Afrika isingeweza kuwa na idadi ya wataalamu na wasomi waliochomoza kuzisaidia nchi zao baada ya uhuru. Katika siku za ukoloni, madola ya Kikoloni yalikuwa na uchoyo mkubwa kuwapatia elimu ya kuridhisha Waafrika waliokuwa wakiwatawala.

Lengo la wakoloni lilikuwa kuendelea kuwaweka Waafrika katika hali duni. Hawakutaka tuendelee. Na hadi sasa hawataki tuendelee. Kila tukiwa nyuma kimaendeleo ndivyo watawala wetu wa zamani wa kikoloni wanavyozidi kufurahi kwani kutokana na ujinga wetu au kutoendelea kwetu ndipo wanapozidi kuvuna fursa za kujipatia wao mafanikio makubwa. Ndivyo wanavyotula kwani wajinga ndio waliwao.

Kama nilivyogusia hapo juu uhusiano baina ya Urussi na mataifa ya Kiafrika ulianza kuzorota tangu Muungano wa Kisovieti ulivyokuwa ukipapatika katika siku za mwisho wa uhai wake.

Mikhail Gorbachev, Rais wa mwisho wa USSR, hakuwa na hamu na Afrika. Kwa hakika, alikuwa amezongwa na mengi na zaidi macho yake yakiangaza ndani mwa nchi yake alikokuwa amekusudia kuleta mageuzi ya kiuchumi ambayo alihisi hayawezi kupatikana bila ya kuwako mageuzi katika mifumo ya kisiasa na kijamii.

Boris Yeltsin, aliyeibuka kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la Urussi baada ya kuvunjika kwa USSR, hakulitia kabisa maanani bara la Afrika. Alizifunga balozi za Urussi katika nchi tisa za Kiafrika. Kadhalika alizifunga balozi ndogo katika nchi tatu za Kiafrika. Taasisi za kitamaduni za Kirussi pia zilifungwa katika nchi kadhaa za Kiafrika na Urussi ikasitisha misaada ya kiuchumi iliyokuwa ikiitoa kwa nchi za Kiafrika.

Ilikuwa kana kwamba Urussi haikuona kama kuna faida yoyote ya kuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na nchi za Kiafrika. Urussi ilikuwa haikuzitathmini vizuri fursa za kiuchumi zilizo Afrika. Nafikiri ilifanya kusudi kupunguza tashwishi zake katika bara la Afrika kwa sababu haikuamini kwamba uwekezaji wa maana katika sekta mbali mbali za kiuchumi barani Afrika utaipatia natija.

Wakati Urussi ilipokuwa inapunguza au inazikata kabisa funganisho zake na nchi za Kiafrika China, kwa upande wake, ikawa inazikuza zake. Matokeo yake ni kwamba katika miaka ya karibuni China imeipiku Urussi katika ukuzaji wa ushawishi wao barani Afrika.

Putin, kwa upande wake, ameamka na ameona jinsi barani Afrika taifa lake linavyopitwa na China pamoja na madola ya Magharibi. Ndio maana ameamua kulifanya bara zima la Afrika liwe kama kitivo cha Urussi. Inasemekana kuwa amemkabidhi kazi hiyo mshirika wake mkuu Yevgeny Prigozhin. Yeye ndiye anayeusimamia mkakati mzima wa Urusi kuhusu Afrika.

Prigozhin ni mtu mzito miongoni mwa wenye kumzunguka Putin. Kati ya shughuli zake nyingi ni za kuiuzia vyakula serikali ya Urussi kwa mujibu wa kandarasi alizopewa. Kwa sababu hiyo amepachikwa jina la “mpishi wa Putin”.

Prigozhin ananuka Marekani ambako wizara ya hazina ya huko imemuwekea vikwazo kwa shutuma za kuhusika na njama za kuuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2016. Kuna uvumi pia kwamba kampuni yake ilimsaidia Andry Rajoelina ashinde uchaguzi wa urais wa Madagascar Novemba 2018.

Jijini London kuna kitengo kimoja kijulikanacho kwa jina la Dossier Center. Kitengo hicho hufanya uchunguzi wa kina kuhusu nyendo za Putin na washirika wake na kinafadhiliwa na mmoja wa mahasimu wake wakubwa aitwaye Mikhail Khodorkovsky, bilionea anayeishi uhamishoni. Kwa hivyo, lazima tuwe waangalifu tunapozisoma ripoti zake.


Hata hivyo, hatuna budi ila tuzipitie na tutumie bongo zetu tunapozipima na kuzifanyia maamuzi. Kwa mujibu wa kitengo hicho “mpishi wa Putin” ana mawakala wake wa mbinu na mikakati ya kisiasa katika nchi 20 za Kiafrika.

Kwa sasa Urussi ndiyo nchi yenye kuliuzia bara la Afrika silaha nyingi kushinda nchi yoyote ile yenye kuuza silaha Afrika. Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani iliyo nchini Sweden nchi za Kiafrika zilinunua asilimia thelathini na tano 35% ya silaha kutoka Urusi, kutoka China zilinunua 17%, Marekani 9.6% na Ufaransa 6.9%. Si ajabu basi kwamba Rosoboronexport, shirika la uuzaji silaha lenye kumilikiwa na serikali ya Urussi, lilitangaza kwamba mwaka huu wa 2019 ni “mwaka wa Afrika”. Wenye utaalamu wa mambo ya silaha wanasema kwamba silaha za Urussi ni rahisi kwa bei na rahisi kuzitumia.

Katika miaka ya karibuni biashara kati ya Urussi na nchi za Kiafrika imekua. Mwaka 2009 ilikuwa ya thamani ya dola za Marekani bilioni $5.7 na 2017 ilifikia dola bilioni $17.4. Bila ya shaka imepitwa vibaya sana na China ambayo biashara yake na Afrika ni ya thamani ya dola za Marekani $170. Miaka 30 iliyopita thamani ya biashara hiyo ya China ilikuwa ni ya dola za Marekani bilioni moja tu.

Sasa Urussi inaazimia kujitanua zaidi kibiashara Afrika. Inazungumzia ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, reli, bandari na mabomba ya mafuta. Inataka kujenga reli kutoka Sudan hadi Senegal na barabara kutoka Sudan hadi Cameroon.

Kuna tetesi kwamba Urussi imeamua “kuzishughulikia” nchi 13 za Kiafrika kwa kukuza uhusiano na viongozi wao leo na wa miaka ijayo, na pia kwa kuwa na majasusi wazawa wa nchi hizo katika nchi zao.

Nchi za Magharibi zinazionea uchoyo China na Urusi kwa ustawi wa uhusiano wao na Afrika. Kuna hatari kwamba Afrika huenda ikawa tena medani ya kupigania “vita baridi” baina ya pande hizo mbili. Utawala wa Rais Donald Trump huko Marekani unadai kwamba kustawi kwa funganisho baina ya Urussi, China na nchi za Kiafrika ni kitisho kwa usalama wa taifa wa Marekani.


Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Chanzo: Raia Mwema
 
Mabwana wakubwa wanaigombea tena Afrika. Viongozi wa afrika wanajipangaje kukabiliana? Au ndio ya Rawlings yanakuja tena?
 
Ahsante kwa makala hii ya kufikirisha. Kuna hatari ya vita baridi mda sio mrefu na nionavyo 'non aligned movement' yetu haitatusaidia, hapa lazima uwe baridi au moto kwa msimamo wa mtu kama Trump.
Kuna haja viongozi wa Afrika kukaa pamoja na kutafakari mahusiano yao, changamoto, fursa na vipaumbele vyetu.
Ukoloni mamboleo hautatuacha salama.
 
kwa nchi makini yenye watu makini hii ndio fursa ya kupaa juu sasa tunajua kuna makundi makubwa manne yanaitolea macho afrika, China, Russia, Usa na Umoja wa ulaya kwa hiyo hakuna taifa litakalokuja kwa masharti mazito kwani tayari kuna ushindani
 
Back
Top Bottom