Mpeni ushirikiano Mnyika anaweza

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
KATIKA kampeni zilizopita kila mgombea aliweka ahadi zake kuwa kama angepewa ridhaa na wananchi angefanya nini katika kuwaondolea kero zinazowakabili.
Hatimaye kampeni zilimalizika na uchaguzi ukafanyika Oktoba 31 mwaka huu. Madiwani na wabunge wa majimbo mbalimbali wakapatikana.

Sasa kikubwa kinachosubiriwa ni utekelezaji wa hizo ahadi zilizoahidiwa na waheshimiwa hao wakiongozwa na mkuu wa nchi.

Lakini pamoja na hayo yote kilichonivutia katika kuandika mtazamo wangu huu ni hili la kuhusiana na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, katika kutekeleza wa ahadi zake.

Hivi karibuni nilipata bahati ya kuhudhuria mikutano yake mitatu aliyokuwa mgeni rasmi ambapo nilishangaa sana kutokana na mapokezi aliyoyapata.

Mapokezi hayo yalitawaliwa na imani kubwa kutoka kwa wananchi kwa kuamini kwamba kumchagua mbunge wao huyo hawakufanya makosa bali wamelamba dume.

Katika mikutano yake hiyo mitatu aliyoifanya katika Kata za Msigani, Goba na Salanga, ambazo ziko katika Jimbo la Ubungo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam aliweza kukutana na changamoto mbalimbali anazotarajiwa kuzipatia ufumbuzi katika kipindi chake hiki cha miaka mitano.

Changamoto hizo hazitofautiani kutoka kata moja hadi nyingine, zote zinafanana na zinahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka kadiri iwezekanavyo.

Nilichokiona kutoka kwa wananchi ni kule kuamini kwamba uwepo wa mbunge wao huyo, kila kitu kinawezekana bila shaka yoyote.

Nilijiuliza mzigo wote aliobebeshwa mbunge huyo atautatua vipi, lakini hata hivyo mbunge huyo alinitoa mashaka pale alipoanza kujibu risala mbalimbali alizopewa katika mikutano hiyo.

Kikubwa alichosema ni kwamba uchaguzi umekwisha kilichobaki ni kuweka itikadi za vyama kando na kuungana pamoja kuwa kitu kimoja kwa lengo la kujenga nchi.

“Tukubali maendeleo hayana itikadi ni ya kila mtu hivyo tofauti zetu za kiitikadi tusizipe nafasi katika hatua za kuwatafutia wananchi maendeleo ambao ndio waajiri wetu sisi (wanasiasa) hivyo tufanyeni kazi kwa bidii,” anasema Mnyika.

Pia katika kutekeleza ahadi zake atatumia njia ya kukutana na wakazi wa Jimbo la Ubungo katika maeneo mbalimbali kuangalia ni kero gani wanaipa kipaumbele katika kuitatua.

Aidha, anaamini kuwa njia shirikishi ya wananchi ndiyo itakayokuwa muarobaini wa kumaliza kero za wakazi wa Jimbo la Ubungo.

Niliwahi kumsikia akisema wafanyabiashara na wadau wengine wa Jimbo la Ubungo ni watu wapenda maendeleo na wamekuwa mstari wa mbele kutoa michango mbalimbali kwa ajili ya kuondoa kero zinazowakabili katika maeneo yao.

Ila kilichokuwa kikirudisha nyuma jimbo hilo ni baadhi ya viongozi waliokabidhiwa dhamana kushindwa kuweka maslahi ya wananchi mbele na badala yake michango hiyo ilitolewa na kupelekwa kusikojulikana kwa maslahi binafsi ya wachache.

Mnyika atawatumia vizuri wadau wote wenye nia ya kuondoa kero zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo kwa kusimamia michango yao kwa malengo yaliyokusudiwa hadi mwisho.

Katika hatua nyingine aliwatoa wasiwasi wakazi wa jimbo hilo kwa kusema akiwa kama mbunge, kuna Mfuko wa Jimbo ambao uko chini yake ambapo nao ni moja ya chanzo cha fedha zinazoweza kutumiwa kwa kutatua matatizo ya wananchi.

Anahakikisha mfuko huo atausimamia kwa uadilifu mkubwa ili hadi mwisho wa siku matunda yake yaonekane na yamnufaishe kila mwana Ubungo.

Mtazamo wangu katika hili nakubaliana na mbunge huyo, ila nataka kumtahadharisha kuwa awe makini na baadhi ya viongozi wa chama tawala ambao bado wana mawazo ya kutokuwa na imani na wapinzani.

Wanaweza kumhujumu kwa kumuwekea vikwazo mbalimbali katika kutimiza ahadi zake alizoahidi kwa wananchi katika kipindi chake hicho.

Labda nitoe mfano mmoja ambao umewahi kutokea kwenye Kata ya Makangalawe wilayani Temeke jijini Dar ambako Chama cha Wananchi (CUF) kiliwahi kushika serikali ya mtaa.

Hivyo ikatokea mradi wa visima kwa watumiaji maji uliotakiwa kujengwa katika eneo la serikali ya mtaa, ambapo kwa kipindi hicho eneo hilo liliongozwa na CUF.

Kilichotokea ni uongozi wa serikali ya chama tawala kuamua mradi huo usijengwe katika eneo husika bali ujengwe kwenye kiwanja cha mtu binafsi ambaye ni mwanachama wa CCM.

Walifanya hivyo kwa kuzuia kujenga umaarufu zaidi wa CUF ambayo huenda ingeweza kutumia kisima hicho katika kampeni zake za kuingia tena madarakani.

Hata hivyo kisima hicho hivi sasa kiko katika mgogoro mkubwa baada ya serikali ya mtaa iliyokuwa ikiongozwa na CUF kushindwa kwenye uchaguzi wa serekali za mitaa uliopita.

Hivi sasa mtaa huo unaongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo sasa wanaudai tena ule mradi wa maji urudi kwenye serikali ya mtaa lakini mmiliki aliyemikishwa mwanzo hataki anasema huu ni mradi wake.

Ni vema Mnyika akatambua kuwa bado wapo watu wanaoweza kukwamisha juhudi zake hizo hata kwa kuwatisha wale wafanyabiashara anaotegemea kushirikiana nao katika hatua za kutatua kero za jimbo hilo.

Ushauri wangu ni kwamba kila mtu anahitaji huduma muhimu katika maisha ya kila siku, hivyo ni bora wakazi wa Ubungo kuwa karibu na kumuunga mkono mbunge mwenye dhamira ya dhati ya kumaliza kero za wananchi bila kujali anatoka chama gani.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom