Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano Hauwezi Kulisadia Taifa Kufikia Dira Yake

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,019
2,473
1624076469219.png

Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania akiwasili Bungeni Kusoma Bajeti ya Serikali 2021/22

I. USULI: KWA NINI NAANDIKA BANDIKO HILI?

Bandiko langu lisemalo “Rais Samia Ameanzia Mwanza Kujenga Hekalu Letu” limewafanya wachangiaji kadhaa, wakiongozwa na mwana JF aitwaye mwengeso (bandiko namba 16), wanitake kufanya uchambuzi rasmi wa kitabu kinachohakikiwa hapa. Ni “Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26,” ambao umeambatanishwa hapa chini.

Mpango huu ulianza kuandaliwa mnamo Februari 2021 na “Wizara ya Fedha na Mipango” kwa niaba ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Serikali iko mbioni kuukamilisha na kutekeleza yaliyomo.

Hivyo, tathmini hii imegawanywa katika sehemu saba zinazojibu maswali yafuatayo: Kwa nini naandika bandiko hili? Katika mipango ya maendeleo tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi? Kitabu kina muundo gani? Kitabu kina maudhui gani? Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe aliopaswa kupeleka kwa hadhira? Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kufikisha ujumbe stahiki kwa hadhira? Maboresho gani yafanyike na kwa nini?

Hatimaye hitimisho ni kwamba, kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika, mwandishi wa mpango huu amepata alama 49 kati ya 100, sawa na alama ya “C.” Hivyo, kadiri inavyowezekana, anashauriwa kuondoa dosari zilizobainishwa. Mapendekezo hayo ni kama ifuatavyo:

  • Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe wake? Sura ya pili na sura ya tano zipanguliwe na kupangwa upya kwa kuweka mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona Wizara gani inahusika na utekelezaji wa kazi na majukumu ya sekta ipi. Mfano mzuri wa mpangilio wa aina hii unapatikana kwenye Mipango ya Maendeleo ya nchi ya Botwana. Mfano mzuri mwingine ni Mpango Mkakati wa Saba wa Zambia.
  • Sisi ni nani na tumetoka wapi? Sura ya kwanza, ambayo ni “Utangulizi,” ipanuliwe na kuweka maelezo kuhusu Tanzania ni kitu gani kwa mujibu wa Katiba, historia, na jiografia, ili msomaji mpya aliyetoka sayari ya Jupita leo, aweze kupata uelewa mzuri juu ya kilichoandikwa na sababu zake.
  • Kwa sasa mwaka 2021 tuko wapi? Uchambuzi wa “SWOT Analysis” uliofanyika katika sura ya pili ufuatiwe na Uchambuzi wa “TOWS Analysis,” ili kwa njia hiyo, mikakati inayotajwa kitabuni ifungamanishwe kimantiki na uchambuzi wa kimazingira uliofanywa.
  • Tunataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? Pembetatu ya Maendeleo ya kiuchumi, Maendeleo ya kijamii na Maendeleo ya Kisiasa ikamilishwe kwa kutaja matokeo tarajiwa kwa ajili ya sekta ya “utawala bora” yaliyosahaulika chini ya fungu la 5.11.
  • Kusudi tuweze kufika mwisho wa safari yetu tutachukua hatua gani na kwa nini? Kuhusu habari ya kwa nini hatua hizi zichukuliwe, mpango umetaja nadharia ya mabadiliko na kuifupisha kwa njia ya mchoro kwenye ukurasa wa 70. Hata hivyo, baadhi ya maneno katika mchoro huu hayasomeki. Na mahusiano yaliyopo kati ya pingili zake tofauti hayaonekani bayana. Pia, hakuna marejeo kuhusiana na vyanzo vya dhana zinazoambatana na mchoro huu ili msomaji aweze kurejea na kujielimisha zaidi. Mapungufu haya yaondolewe.
  • Katika kila hatua ni kazi gani na majumu yapi yatafanyika ili tuweze kufika mwisho wa safari yetu?) Swali hili halijajibiwa isipokuwa katika hatua ya miradi ya kielelezo (fungu la 5.9). Kwa hiyo, kila kijisekta kilichotajwa kwenye mafungu ya 5.4 hadi 5.9, kipanuliwe kwa kuongeza “kazi na majukumu yatakayotekelezwa.”
  • Nani atachukua hatua gani, kufanya kazi zipi na kutekeleza majukumu yapi wakati wa safari yetu? Kuna mchoro kwenye ukurasa wa 148 wenye kuonyesha mahusiano ya watekelezaji wa mpango huu. Lakini, mchoro huu umeandikwa kwa Kiingereza, hauna kielelezo cha kumsaidia msomaji kuuelewa, na huu ni mchoro ambao hauonyeshi muundo wa serikali ya Tanzania kama ilivyo leo. Hivyo, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma iombwe kuandaa muundo wa uongozi wa nchi, kama ulivyo leo, na kisha uwekwe hapa.
  • Safari yetu ya miaka 5 inahitaji rasilimali kiasi gani, zitatoka wapi na zitatumikaje? Mpango umeonyea makadirio ya mapato ya fedha zitakazokusanywa ndani ya miaka mitano ijayo bila kuonyesha makadirio ya matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala. Kwa hiyo, kimantiki, makadirio ya makusanyo yaliyotajwa ni ya kubuni. Dosari hii iondolewe kwa kutaja matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala.
  • Mwishoni mwa safari yetu ya miaka 5 kuna alama gani zitakazotujulisha kwamba tumefika? Kuna viashiria na shabaha za sekta ya nishati zilizopitwa na wakati. Mfano, mpango huu unasema kuwa ifikapo 2025 ni 60% pekee ya watanzania watakaokuwa wamepata umeme, wakati Waziri, Waziri Mkuu na Rais Samia wanasema 100%. Pia, katika sura ya nane hakuna “jedwali la mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na taarifa,” yaani, “logical framework matrix,” ambao ni msingi wa ufanisi. Dosari hizi zirekebishwe.
  • Mapendekezo ya jumla: Kazi ya kukamilisha maandalizi ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa Kuelekea 2025 ifanyike sambamba na Mipango ya Maendeleo ya Wizara na Sekta husika. Mfano mzuri mwingine ni Mpango Mkakati wa Saba wa Zambia pamoja na Mikakati ya Wizara zake. Kwa mfano, Mikakati wa Wizara ya Maji, ambao umeandaliwa kwa kuzingatia metholojia ya "Balanced Scorecard" unapatikana hapa: Wizara ya Maji.
II. UTANGULIZI WA KIHISTORIA: KATIKA SUALA LA MIPANGO YA MAENDELEO TUMETOKA WAPI, TUKO WAPI NA TUNAKWENDA WAPI?

Tangu tarehe 9 Desemba 1961 Tanzania ilipopata uhuru, awamu tofauti za serikali ya nchi zimekuwa zinatunga na kusimamia sera, sheria na mipango ya maendeleo inayolenga kuwaunganisha wananchi katika harakati zao wa kusukuma gurudumu la maendeleo kutoka katika bonde la maadui wa ubinadamu (human bads) ili kulifikisha kwenye kilele cha mlima wa marafiki wa ubinadamu (human goods).

Kwa upande mmoja, katika bonde la maadui wa ubinadamu kuna magonjwa, ujinga, ikolojia duni, ofizi za utawala zinazotenda dhuluma, umaskini wa kipato na mali, uwongo, chuki, dharau, vita, ubaguzi, hofu, huzuni na mashaka.

Na kwa upande mwingine, katika kilele cha mlima wa marafiki wa ubinadamu kuna afya imara, elimu bora, ikolojia salama, ofizi za utawala zinazotenda haki kwa usawa na kwa wote, utajiri wa kipato na mali, ukweli, upendo, heshima, amani, usawa, kujiamini, furaha na matumaini.

Kwa ajili ya kufanikisha lengo hili, awamu tofauti za serikali zimekuwa zikiandaa mipango ya muda mrefu na kuitekeleza kupitia mipango ya muda mfupi. Hadi sasa mipango ya muda mrefu ifuatayo imebuniwa na kutekelezwa, baadhi ikiwa inatelekezwa njiani kwa sababu za kimazingira:

  • Mpango wa Muda Mrefu kwa Miaka 16 (LTPP: 1964-1980) ulioakisi sera za uchumi wa soko uliorithiwa kutoka kwa wakoloni;
  • Mpango wa Muda Mrefu kwa Miaka 13 (LTPP: 1967-1980) ulioakisi sera za uchumi wa Ujamaa baada ya Azimio la Arusha;
  • Mpango wa Muda Mrefu kwa Miaka 19 (LTPP: 1981-2000) ulioambatana na mageuzi ya kisera yaliyokaribisha uchumi wa soko; na
  • Mpango wa Muda Mrefu kwa Miaka 25 (TDV: 2000-2025), wenye kuongozwa na falsafa ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini, na
  • Mpango wa Muda Mrefu kwa Miaka 15 (LTPP: 2010-2025), wenye kuongozwa na falsafa ya umuhimu wa vigezo vya kupima kasi na ufanisi katika utendaji wa kazi za serikali.
Hivyo, mpaka sasa tumekuwa na mipango sita ya muda mrefu ambayo majina yake hayasomani, kiasi cha kutufanya kushindwa kujua tumeotoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi.

Hali ni kama hiyo kwa upande wa mipango ya muda mfupi. Kuanzia 1961 hadi mwaka 2000, ifuatayo ni mipango ya maendeleo ya muda mfupi ambayo imetekelezwa hapa nchini, baadhi ikiwa inatelekezwa njiani kwa sababu za kimazingira:

  • Mpango wa Miaka 3 (1961-1964);
  • Mpango wa Miaka 5 (1964-1969);
  • Mpango wa Miaka 5 (1969-1974);
  • Mpango wa Miaka 5 (1975-1980);
  • Mpango wa Miaka 2 (NESP: 1981-82);
  • Mpango wa Miaka 3 (SAP: 1982-1985);
  • Mpango wa Miaka 3 (ERP I: 1986-1989);
  • Mpango wa Miaka 3 (ERP II: 1989-1992); na
  • Mpango wa Miaka 8 (1992-2000), ambao haukuandikwa popote.
Na kuanzia mwaka 2000 hadi sasa mipango ya maendeleo ya muda mfupi ifuatayo imeandaliwa na kutekelezwa:
  • Mkakati wa Miaka Mitatu wa Kupunguza Umaskini (2000/01-2002/03);
  • Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania Awamu ya Kwanza (MKUKUTA I: 2005/06-2009/10);
  • Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania Awamu ya Pili (MKUKUTA II: 2010/11-2014/15);
  • Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa (FYDP I: 2011/12-2015/16), ulioongozwa na falsafa ya “Kufungulia Fursa Fiche za Ukuaji wa Uchumi”;
  • Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa (FYDP II: 2016/17-2020/21), ulioongozwa na falsafa ya “Kujenga Uchumi wa Viwanda”; na
  • Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III: 2021/22-2025/26), unaoongozwa na falsafa ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu."
Hivyo, mpaka sasa tumekuwa na mipango kumi na tano ya muda mfupi ambayo majina yake hayasomani, kiasi cha kutufanya kushindwa kujua tumeotoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi.

III. MUHTASARI WA FOMATI: KITABU KINA MUUNDO GANI?

Kitabu kiitwacho “Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26,” kinazo kurasa 194.

Baada ya kurasa za awali kuna kurasa zinazojadili sura nane za kitabu kama ifuatavyo:

  • Sura ya Kwanza ni “Utangulizi” unaojadili mazingira ya kihistoria ya mipango ya maendeleo tangu 2000.
  • Sura ya Pili ni “Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa,” kwa kumulika utekelezaji uliofanyika kisekta; na mwelekeo wa mpango wa maendeleo wa tatu.
  • Sura ya Tatu inajadili umuhimu wa “Kukuza Ushiriki wa Sekta Binafsi Kwenye Maendeleo ya Kiuchumi.
  • Sura ya Nne inajadili “Msingi wa Utekelezaji wa Mikakati ya Mpango,” kwa kubainisha Muundo wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo na masuala mengine.
  • Sura ya Tano inajadili “Nguzo Kuu, Vipaumbele na Hatua za Kimkakati za Utekelezaji wa Mpango.
  • Sura ya Sita inajadili mfumo wa “Ugharamiaji wa Utekelezaji wa Mpango,” kwa kubainisha vyanzo vya fedha; mchango wa wadau mbalimbali katika kugharamia mpango, na mambo kama hayo.
  • Sura ya Saba inajadili Mwongozo wa “Utekelezaji wa Mpango” kwa kubainisha mgawanyo wa majukumu.
  • Na Sura ya Nane inajadili “Ufuatiliaji na Tathmini” ya utekelezaji wa mpango kwa kubainisha yafuatayo: mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa.

IV. MUHTASARI WA YALIYOMO: KITABU KINA MAUDHUI GANI?

1. Sisi ni nani na tumetoka wapi? (Identity analysis)

Kwa mujibu wa sura ya kwanza, ambayo ni “Utangulizi,” uchambuzi uliomo katika mpango wa tatu wa maendeleo unaojadiliwa hapa unaanzia “katika kipindi cha miaka ya 1990” (uk.1). Kuna ufafanuzi wa jitihada za kitaifa za kutengeneza sera, sheria na program za maendeleo tangu 2000 hadi leo.

2. Kwa sasa mwaka 2021 tuko wapi? (Situation analysis)

Sura ya pili, tatu na nne katika mpango huu zimeeleza kwa kina hali ya sasa kisiasa, kiuchumi na kijamii (uk. 9-50). Kwa upekee, sura ya pili imeandaa Jedwali Na.8 lenye kuchambua uimara, udhaifu, fursa na vihatarishi (SWOT Analysis) vilivyojitokeza wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Pili, kwa lengo la kupata mafunzo katuika kutekeleza Mpango wa Tatu. Na sura ya tatu inaongelea mazingira yanayohusiana na haja ya kuundwa kwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi.

3. Tunataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? (Impact, outcome and output analysis)

Katika sura ya tano, kwenye kipengele cha 5.11, kuna matokeo tarajiwa kumi katika sekta ya “uchumi wa ushindani,” matokeo tarajiwa sita katika sekta ya “ustawi wa jamii,” na hakuna matokeo tarajiwa yaliyotajwa katika sekta ya “utawala bora.”

4. Kusudi tuweze kufika mwisho wa safari yetu tutachukua hatua gani na kwa nini? (Strategic analysis)

Sura ya tano, hasa katika fungu la 5.3, inataja vipaumbele vya kimkakati vitano yafuatayo: Kuchochea Uchumi Shirikishi na Shindani; Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma; Kukuza Uwekezaji na Biashara; Kuchochea Maendeleo ya Watu; na Kuendeleza Rasilimali Watu. Kisha, kwenye mafungu ya 5.4 hadi 5.9, sura hii inataja hatua zitakazochukuliwa na serikali katika vijisekta vipatavyo 30 bila kuonyesha bayana kijisekta kipi kinaanguka chini ya sekta gani.

5. Katika kila hatua ni kazi gani zitafanyika ili tuweze kufika mwisho wa safari yetu? (Tactical analysis)

Swali hili halijajibiwa kwa ukamilifu. Ni kweli kwamba, katika hatua ya miradi ya kielelezo (fungu la 5.9), mpango unataja kazi zitakazofanyika. Mbali na hii hatua, hakuna hatua zingine zilizofafanuliwa kwa kutaja kazi zitakazofanyika ndani ya kila hatua.

6. Nani atachukua hatua gani wakati wa safari yetu? (Responsibility analysis)

Kwa mujibu wa sura ya saba, utekelezaji wa Mpango utahusisha Wizara za Kisekta, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretariati za Mikoa na Mamalaka za Serikali za Mitaa pamoja na Sekta Binafsi. Wadau hawa watahusika na utekelezaji wa Mpango kupitia mipango mikakati ya kisekta. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango itakuwa na jukumu la kuratibu utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya Mpango. (uk. 147).

7. Safari yetu ya miaka 5 inahitaji rasilimali kiasi gani, zitatoka wapi na zitatumikaje? (Budget analysis)

Sura ya sita inaonyesha kuwa, fedha zitakazokusanywa ili kugharamia utekeleaji wa Mpango Mkakati ni shilingi trilioni 114.8. Mpango huu utagharamiwa kupitia Bajeti ya Maendeleo ya Serikali ambayo ni shilingi trilioni 74.2. Mapato ya ndani ni shilingi trilioni 62.02 wakati misaada na mikopo yenye masharti nafuu ni shilingi trilioni 12.2. Vyanzo vya sekta binafsi vinakadiriwa kuchangia shilingi trilioni 40.6 ikijumuisha shilingi trilioni 21.03 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 19.6 kutoka vyanzo vya nje. (uk. 131).

8. Mwishoni mwa safari yetu ya miaka 5 kuna alama gani zitakazotujulisha kwamba tumefika? (Monitoring, evaluation and kearning framework)

Sura ya Nane inajadili utaratibu wa “Ufuatiliaji na Tathmini” ya mpango. Kutakuwepo na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini utakaojumuisha miundo ya kitaasisi na miongozo ya kiutendaji. Nyenzo hizio zitatumika kubaini kiwango na ubora wa utekelezaji wa mpango kwa kutathmini mwenendo na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli za kiuchumi. Mfumo huo utahusisha udhibiti, ukaguzi, mapitio, kuandaa taarifa za mwenendo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na maoni na mapendekezo ya kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa Mpango.

V. TATHMINI YA MUUNDO WA KITABU: MWANDISHI AMEFANIKIWA NA KUFELI KWA KIASI GANI KATIKA KUUPA UMBO UJUMBE WAKE?

Mosi, Sura ya Pili kuhusu “Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa,” na Sura ya Tatu kuhusu “Kukuza Ushiriki wa Sekta Binafsi Kwenye Maendeleo ya Kiuchumi,” zimeandikwa vizuri zaidi kuliko sura nyingine zote. Hata hivyo, sura hizi mbili zinaongelea “Uchambuzi wa Mazingira” ya mpango wa maendeleo. Kwa hiyo, zingeweza kuunganishwa chini ya sura moja ili kutoa fokasi kwa msomaji kwamba sasa anasoma kuhusu “Uchambuzi wa Mazingira.”

Pili, Sura ya Nne kuhusu “Msingi wa Utekelezaji wa Mikakati ya Mpango,” na Sura ya Tano kuhusu “Nguzo Kuu, Vipaumbele na Hatua za Kimkakati za Utekelezaji wa Mpango,” zinaongelea kitu kile kile, yaani “Mwelekeo wa Kimkakati.” Kwa hiyo, zingeweza kuunganishwa chini ya sura moja ili kutoa fokasi kwa msomaji kwamba sasa anasoma kuhusu “Mwelekeo wa Kimkakati.”

Tatu, kwenye sura ya 5, mafungu ya 5.4 hadi 5.9, sura hii inataja hatua zitakazochukuliwa na serikali katika vijisekta vipatavyo 30 bila kuonyesha bayana kijisekta kipi kinaanguka chini ya sekta gani kubwa, ambapo sekta kubwa zilizotajwa ni uchumi, jamii na siasa. Yaani, hakuna mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona vijisekta gani vinaanguka katika sekta ipi.

Nne, katika sura hii, anatomia ya sekta na vijisekta vilivyotajwa haionyeshi mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona mambo yafuatayo: mchango wa sekta na kijisekta kwa Taifa, mabadiliko yatakayoleta mchango huo, matokeo yatakayoleta mabadiliko hayo, na majukumu yatakayozalisha matokeo yanayotarajiwa.

Yaani, kwa kila sekta na vijisekta vilivyotajwa, mnyororo wa mchango, mabadiliko, matokeo, na majukumu haukubainishwa kwa ukamilifu. Njia nyingine ya kusema dosari hii ni kusema kuwa, kwa kila sekta na kila kijisekta kilichotajwa, mnyororo wa shabaha, malengo, madhumuni na kazi haukubainishwa kwa ukamilifu.

Hivyo, kwa kila kijisekta kilichotajwa katika mafungu ya 5.4 hadi 5.9, kunahitajika maelezo yafuatayo: utangulizi, lengo la kisekta, hatua zitakazochukuliwa, mbinu zitakazotumika kuchukua hatua husika, vigezo vya ufanisi, sakafu ya kila kigezo cha ufanisi, na dari ya kila kigezo cha ufanisi.

Tano, katika sura hii, hakuna mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona Wizara gani inahusika na utekelezaji wa vijisekta na sekta zipi. Yaani, kadiri mpango huu unavyoonekana kwa sasa haujawalenga Mawaziri kama wasomaji wake wakuu. Ukweli huu unaonekana wazi kuanzia kwenye ukurasa wa “yaliyomo.”

Ingependeza kuunganisha sura ya nne kuhusu “uchambuzi wa mazingira ya kimkakati” na sura ya tano kuhusu “mweleko wa kimkakati” zingeuganishwa ili mambo haya mawili yajadiliwa chini ya kichwa cha marejeo kimoja, mfano “Wizara ya Afya.” Mfano mzuri wa mpangilio wa aina hii unapatikana kwenye
Mipango ya maendeleo ya nchi ya Botwana. Mfano mzuri mwingine ni Mpango Mkakati wa Zambia.

Na sita, kitabu hiki hakina “muhtasari mahsusi” yaani “executive summary.” Muhtasari huu unahitajika mwanzoni kabisa ili kuwapa nafasi wasomaji wenye muda kidogo kupata picha kubwa kuhusu yaliyomo.

Kwa sababu hizi zote, nampatia mwandishi wa Mpango huu asilimia 65 kati ya mia zinazowezekana. Kwa mujibu wa mfumo wa alama wa elimu ya sekondari, hii ni gredi ya “B.”

VI. TATHMINI YA MAUDHUI YA KITABU: MWANDISHI AMEFANIKIWA NA KUFELI KWA KIASI GANI KATIKA KUFIKISHA UJUMBE WAKE?

1. Sisi ni nani na tumetoka wapi? (Identity analysis)

Katika sura ya kwanza, ambayo ni “Utangulizi,” uchambuzi wa historia ya mipango ya maendeleo unaanzia “katika kipindi cha miaka ya 1990” (uk.1). Hakuna maelezo yoyote kuhusu Tanzania ni kitu gani kwa mujibu wa Katiba, historia, na jiografia.

Kwa hiyo, kwa msomaji aliyetoka sayari ya Jupita leo, hawezi kupata uelewa mzuri juu ya kilichoandikwa na sababu zake. Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 65 kati ya 100, yaani alama ya “B.”

2. Kwa sasa mwaka 2021 tuko wapi? (Situation analysis)

Sura ya pili na tatu zimefanya uchambuzi wa mazingira ya kimkakati. Hata hivyo, sura ya pili imefanya uchambuzi wa uimara, udhaifu, fursa na vihatarishi (SWOT Analysis) bila kufanya Uchambuzi wa Kufungamanisha Fursa na Udhaifu ili Kuzalisha Uimara (TOWS Analysis).

Watu kama Profesa Heinz Weihrich (1982) wanaeleza vema kwa nini hili nitatizo. Kwa mfano, katika andiko lake “
The TOWS Matrix: A Tool for Situational Analysis,” ameeleza vema jinsi ya kufanya “SWOT-and-TOWS analysis.”

Kwa mujibu wa Weihrich (1982), itaonekana kuwa, SWOT Analysis inayofanyika bila kufungamanishwa na TOWS analysis haina maana yoyote zaidi ya kujaza karatasi. Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 65 kati ya 100, yaani alama ya “B.”

3. Tunataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? (Impact, outcome and output analysis)

Sura ya tano, kwenye fungu la 5.11, imetaja matokeo tarajiwa kumi katika sekta ya “uchumi wa ushindani,” matokeo tarajiwa sita katika sekta ya “ustawi wa jamii,” na hakuna matokeo tarajiwa yaliyotajwa katika sekta ya “utawala bora.” Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 63 kati ya 100, yaani alama ya “B.”

4. Kusudi tuweze kufika mwisho wa safari yetu tutachukua hatua gani na kwa nini? (Strategic analysis)

Kuhusu habari ya kwa nini hatua hizi zichukuliwe, mpango umetaja nadharia ya mabadiliko na kuifupisha kwa njia ya mchoro kwenye ukurasa wa 70. Mchoro husika ni huu hapa:

1624079183209.png

Muundo wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (Mpango wa Tatu, uk. 70)

Hata hivyo, kama mchoro unavyoonekana, baadhi ya maneno hayasomeki. Na mahusiano yaliyopo kati ya pingili zake tofauti hayaonekani bayana. Aidha, nadharia husika haikupewa jina rasmi, na hakuna marejeo yaliyotajwa, japo inaonekana kuwa nadharia bora zaidi kuliko ile iliyotumika katika mpango uliotangulia.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kitabuni, nadharia hii inafanana na “mnyororo wa ongezeko la thamani kwa mujibu wa nadharia ya Porter,” yaani “Porter’s value chain map theory.” Aidha, nadharia husika inafanana na “ramani za kimkakati kwa mujibu wa nadharia ya Kaplan,” yaani “Kaplan and Norton’s strategy map theory.”

Kutokana na ninachokifahamu kwa mujibu wa maandiko ya kina Porter na Kaplan, sasa naweza kutafsiri nadharia ya mabadiliko inayopendekezwa katika kitabu kinachojadiliwa hapa, kwa kutumia mchoro ufuatao:

1624290203441.png

Mchoro: Mnyumbulisho wa Mchoro Unaoonyesha Nadharia ya Mabadiliko katika FYDP III, uk. 70 (Usanifu wangu).

Itapendeza sana kama mchoro ulioko ukurasa wa 70 utafanyiwa maboresho kwa misingi hii. Pia inafaa sana kuweka marejeo kuhusiana na chanzo cha michoro kama hii ili msomaji aweze kurejea na kujielimisha zaidi. Kwa sasa, kitabu chote hakuna rejeo hata moja. Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 61 kati ya 100, yaani alama ya “B.”

5. Katika kila hatua ni kazi gani na majumu yapi yatafanyika ili tuweze kufika mwisho wa safari yetu? (Tactical analysis)

Swali hili halijajibiwa kwa ukamilifu. Ni kweli kwamba, katika hatua ya miradi ya kielelezo (fungu la 5.9), mpango unataja kazi zitakazofanyika. Mbali na hii hatua, hakuna hatua zingine zilizofafanuliwa kwa kutaja kazi zitakazofanyika ndani ya kila hatua.

Yaani, kazi zitakazotekelezwa katika kila hatua iliyotajwa katika mpango zinakosekana. Yaani, mbali na kipengele cha miradi ya kielelezo (fungu la 5.9), mpango unaojadiliwa hapa kutaja ni kwa vipi hatua za kisekta zilizotajwa zitachukuliwa, hakuna kijisekta kingine kimeeleza hatua hizo zitachukuliwaje. Na bila jambo hili kufanyika ni vigumu kuchambua mahitaji ya kibajeti ya mpango huu.

Kusudi tatizo hili liweze kueleweka, nitatumia tena mfano wa sekta ya “afya,” inayojadiliwa katika fungu la 5.4.20 la mpango unaojadiliwa hapa, ili kueleza dosari iliyoko hapa.

Katika sura ya tano inayotaja mikakati mipya, Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, akiokota nakala ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo, atakutana na maandisho yafuatayo pekee kuhusu Wizara yake:

“Afya: Sekta ya afya ni muhimu kwa maendeleo ya watu. Sekta hii inajumuisha miundombinu, wataalamu, vifaa na vifaa tiba, vitendanishi, dawa, tiba, kinga na bima ya afya. Hivyo, Mpango huu unalenga kuimarisha mifumo ya usimamizi, upatikanaji na utoaji wa huduma za afya. Aidha, Mpango utajielekeza pia katika kutatua changamoto ya ubora wa huduma za afya.

“Hatua muhimu zinahusisha: (i) Kujenga na kukarabati vituo vya huduma za afya; (ii) Kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wa afya, dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo; (iii) Kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma za bima ya afya; (iv) Kuimarisha huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za kikanda, maalumu na kitaifa; (v) Kuboresha huduma za tiba asilia/tiba mbadala; (vi) Kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha chanjo, dawa na vifaa tiba; (vii) Kuhamasisha na kuwezesha sekta binafsi kuwekeza katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa na huduma za afya; (viii) Kuimarisha mifumo ya kusafirisha na kuhifadhi bidhaa za afya; (ix) Kuimarisha mifumo ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko; na (x) Kuimarisha huduma za dharura za afya.

“Viashiria na Shabaha Katika Sekta ya Afya (2020/21 hadi 2025/26): Idadi ya vifo vya watoto, kwa kila vizazi hai 1000 (36 hadi 30); Idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano, kwa kila vizazi hai 1000 (50 hadi 40); (Asilimia ya) uzazi uliohudumiwa na wakunga waliohitimu (80 hadi 85); Idadi ya vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kwa kila akina mama 100,000 (220 180); Umri wa miaka ya kuishi (66 hadi 68); Asilimia ya Kuenea kwa UKIMWI kitaifa (4.7 hadi 3.1); (Asilimia ya) matumizi ya Serikali katika afya (10 hadi 12.2)” (uk. 116).

Baada ya kusoma maelezo haya, Dk. Gwajima anapaswa kuanza kazi yake kama Waziri na kuiongoza Wizara husika kwa miaka mitano kwa kutumia mwongozo huu. Lakini, mwongozi huu haukidhi mahitaji. Kwa njia ya mfano tu, swali lifuatalo halina jawabu: Ni kazi gani zitatekelezwa katika hatua ya “(i) Kujenga na kukarabati vituo vya huduma za afya”?

Bila kujibu swali hili haiwezekani kubainisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kuitekeleza kazi hii. Tatizo hili limejitokeza katika vijisekta vyote 30 vilivyoorodheshwa katika mpango huu. Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 15 kati ya 100, yaani gredi ya “F.”

6. Nani atachukua hatua gani, kufanya kazi zipi na kutekeleza majukumu yapi wakati wa safari yetu? (Responsibility analysis)

Kwa mujibu wa sura ya saba, utekelezaji wa Mpango utahusisha Wizara za Kisekta, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretariati za Mikoa na Mamalaka za Serikali za Mitaa pamoja na Sekta Binafsi.

Kuna mchoro kwenye ukurasa wa 148 wenye kuonyesha mahusiano ya watekelezaji wa mpango huu. Lakini, mchoro huu umeandikwa kwa Kiingereza na hauna kielelezo cha kumsaidia msomaji kuuelewa.

Na tatizo kubwa zaidi ni kwamba huu ni mchoro ambao hauonyeshi muundo wa serikali ya Tanzania kama ilivyo leo, kuanzia Ikulu hadi kitongojini, kwa upande mmoja, na kuanzia serikalini, kupitia mahakamani hadi Bungeni, kwa upande mwingine. Kwa sababu huu, mchoro huu haina msaada mkubwa. Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 45 kati ya 100, yaani alama ya “C.”

7. Safari yetu ya miaka 5 inahitaji rasilimali kiasi gani, zitatoka wapi na zitatumikaje? (Budget analysis)

Sura hii imeonyea makadirio ya mapato ya fedha zitakazokusanywa ndani ya miaka mitano ijayo bila kuonyesha makadirio ya matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala. Lakini, kama hujui matumizi yatakayofanyika huwezi kujua mapata yanayopaswa kukusanywa.

Kwa hiyo, maswali yanazuka, mwandishi wa mpango amejuaje kwamba anapaswa kukusanya trilioni 115 ndani ya miaka mitano? Na je, mawaziri, wakuu wa idara, na wakuu wa wakala za serikali watajuaje ni kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa ajili ya maeneo yao ndani ya miaka mitano ijayo? Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 36 kati ya 100, yaani alama ya “D.”

8. Mwishoni mwa safari yetu ya miaka 5 kuna alama gani zitakazotujulisha kwamba tumefika? (Monitoring, evaluation and kearning framework)

Sura ya Nane inajadili utaratibu wa “Ufuatiliaji na Tathmini” ya mpango. Ndani ya sura hii kuna matatizo kadhaa. Kwanza, kuna taarifa ambazo tayari zimepitwa na wakati. Kwa mfano viashiria na shabaha za sekta ya nishati. Mpango huu unasema kwamba, “kiasi cha watu walioungnishiwa umeme” kwa mwaka 2021/22 ni 39.9% na kwamba, “kiasi cha watu walioungnishiwa umeme” kwa mwaka 2025/26 itakuwa ni 60% (uk. 104).

Lakini, Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati na Rais Samia, wamesikika mara kadhaa wakisema kuwa dhamira ya serikali ni kwamba, “kiasi cha watu walioungnishiwa umeme” ifikapo 2024 itakuwa ni 100%.

Pili, vigezo vya ufanisi katika baadhi ya sekta havina uhalisia. Kwa mfano, katika sekta ya nishati, ukisema kuwa “kiasi cha watu walioungnishiwa umeme” ifikapo 2025 watakuwa ni 100%, maana yake ni hii:

Kwamba, kutakuwepo na umeme katika kila kaya ya kila kitongoji; Kwamba, kutakuwepo na umeme katika kila kaya ya kila kijiji; katika kila kaya ya kila tarafa; Kwamba, kutakuwepo na umeme katika kila kaya ya kila wilaya; Kwamba, kutakuwepo na umeme katika kila kaya ya kila mkoa; na Kwamba, kutakuwepo na umeme katika kila kaya ya Taifa hili. Uhalisia wa kasi ya kusambaza umeme kwa miaka mitano iliyopita unaonyesha mashaka juu ya uwezekano wa makisio haya.

Na tatu, sura hii haikuweka msingi wowote wa maana kwa ajili ya kujenga mazingira ya kufuatilia, kutathmini na kuripoti utendaji wa kazi za serikali.

Kwa kawaida, kila mpango mkakati unapaswa kuwa na “jedwali la ufuatiliaji, tathmini na taarifa,” yaani, “logical framework matrix.” Hili ni jedwali linaloonyesha mahusiano ya kimantiki yaliyopo kati ya vipengele vyote vya mkakati. Jedwali hili hujenga msingi thabiti wa kuhoji na kufuatilia utendaji wa kazi zilizotajwa.

Kwa ajili hii, jedwali hili huonyesha mchango utakaoletwa katika maisha ya watu, mabadiliko yatakayoleta mchango huo, matokeo yatakayoleta mabadiliko hayo, majukumu yatakayozalisha matokeo tajwa, rasilimali za kuwezesha utekelezaji wa majukumu yaliyotajwa, vigezo vya kupima ufanisi, shabaha za ufanisi, vyanzo vya taarifa za utekelezaji wa kazi, na vigezo vya kimazingira vinavyotarajiwa kuendelea kuwepo ili mafanikio yanayotarajiwa yawezekane.

Badala ya mpango huu kuweka “jedwali la ufuatiliaji, tathmini na taarifa,” baadhi ya sehemu za jedwali hili zimetawanywa katika maeneo tofauti ya sura ya tano, wakati sehemu nyingine zimetupwa kabisa nje ya mpango huu. Hivyo, kwa sababu ya jinsi mwandishi alivyojibu swali hili, nampatia alama 38 kati ya 100, yaani alama ya “D.”

VII. HITIMISHO NA MAPENDEKEZO: MABORESHO GANI YAFANYIKE NA KWA NINI?

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika hapo juu, ni wazi kwamba, mwandishi wa mpango huu amepata alama 49 kati ya 100, sawa na alama ya “C.” Kwa hiyo, mapendekezo yafuatayo yanahusika.

1. Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe wake?

  • Vijisekta vipatavyo 30 vinavyotajwa kwenye mafungu ya 5.4 hadi 5.9, vipanaguliwe na kuopangwa upya kwa kuonyesha bayana kijisekta kipi kinaanguka chini ya sekta gani kubwa, ambapo sekta kubwa tano zimetajwa, yaani Kuchochea Uchumi Shirikishi na Shindani; Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani; na Utoaji Huduma; Kukuza Uwekezaji na Biashara; Kuchochea Maendeleo ya Watu; na Kuendeleza Rasilimali Watu.
  • Anatomia ya kila sekta na kila kijisekta kilichotajwa ifumuliwe na kuandikwa upya kwa kuonyesha mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona mambo yafuatayo: utangulizi, lengo la kisekta, hatua zitakazochukuliwa, kazi na majukumu yatakayofanyika katika kila hatua, vigezo vya ufanisi, takwimu ambazo ni kikonyo cha kila kigezo cha ufanisi, na takwimu ambazo ni tajeti ya kila kigezo cha ufanisi.
  • Sura ya pili na sura ya tano zipanguliwe na kupangwa upya kwa kuweka mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona Wizara gani inahusika na utekelezaji wa kazi na majukumu ya sekya ipi. Mfano mzuri wa mpangilio wa aina hii unapatikana kwenye Mipango ya Maendeleo ya nchi ya Botwana.
  • Aidha uandikwe “muhtasari mahsusi,” yaani “executive summary,” ili kuwapa nafasi wasomaji wenye muda kidogo kupata picha kubwa kuhusu yaliyomo.
2. Sisi ni nani na tumetoka wapi? Sura ya kwanza, ambayo ni “Utangulizi,” ipanuliwe na kuweka maelezo kuhusu Tanzania ni kitu gani kwa mujibu wa Katiba, historia, na jiografia, ili msomaji mpya aliyetoka sayari ya Jupita leo, aweze kupata uelewa mzuri juu ya kilichoandikwa na sababu zake.

3. Kwa sasa mwaka 2021 tuko wapi? Uchambuzi wa uimara, udhaifu, fursa na vihatarishi (SWOT Analysis) uliofanyika katika sura ya pili ufuatiwe na Uchambuzi wa Kufungamanisha Fursa na Udhaifu ili Kuzalisha Uimara (TOWS Analysis), ili kwa njia hiyo, mikakati inayotajwa kitabuni ifungamanishwe kimantiki na uchambuzi wa kimazingira uliofanywa.

4. Tunataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? Pembetatu ya Maendeleo ya kiuchumi, Maendeleo ya kijamii na Maendeleo ya Kisiasa ikamilishwe kwa kutaja matokeo tarajiwa katika sekta ya “uchumi wa ushindani,” matokeo tarajiwa katika sekta ya “ustawi wa jamii,” na matokeo tarajiwa kwa ajili ya sekta ya “utawala bora.” Kwa sasa, kwenye fungu la 5.11, hakuna matokeo tarajiwa kwa ajili ya sekta ya “utawala bora.”

5. Kusudi tuweze kufika mwisho wa safari yetu tutachukua hatua gani na kwa nini? Kuhusu habari ya kwa nini hatua hizi zichukuliwe, mpango umetaja nadharia ya mabadiliko na kuifupisha kwa njia ya mchoro kwenye ukurasa wa 70. Hata hivyo, baadhi ya maneno katika mchoro huu hayasomeki. Na mahusiano yaliyopo kati ya pingili zake tofauti hayaonekani bayana. Aidha, nadharia husika haikupewa jina rasmi, na hakuna marejeo yaliyotajwa.

Nadharia ya mabadiliko ndio moyo wa mpango mkakati wowote. Hivyo, mchoro ulioko ukurasa wa 70 unapaswa kufanyiwa maboresho stahiki kwa kuzingatia mawazo ya waandishi kama vile Robert Kaplan na Robert Norton (2004), katika kitabi chao kiitwacho “Strategy Maps: Converting Intangible Assets into Tangible Outcomes (Boston: Harvard Business Press).” Pia inafaa sana kuweka marejeo kuhusiana na vyanzo vya dhana zinazoambatana na mpango huu ili msomaji aweze kurejea na kujielimisha zaidi. Kwa mfano, hautoshi kusema “katika maandiko mengi” (uk. 72) bila kutaja maandiko hayo.

6. Katika kila hatua ni kazi gani na majumu yapi yatafanyika ili tuweze kufika mwisho wa safari yetu?) Swali hili halijajibiwa isipokuwa katika hatua ya miradi ya kielelezo (fungu la 5.9). Yaani, kazi na majukumu yatakayotekelezwa katika kila hatua iliyotajwa kwenye mpango zinakosekana. Hili ndilo kosa kubwa zaidi lililofanywa na mwandishi wa mpango huu. Kwa hiyo, kila kijisekta kilichotajwa kwenye mafungu ya 5.4 hadi 5.9, kipanuliwe kwa kuongeza ufafanuzi wa “kazi na majukumu yatakayotekelezwa.”

7. Nani atachukua hatua gani, kufanya kazi zipi na kutekeleza majukumu yapi wakati wa safari yetu? Kuna mchoro kwenye ukurasa wa 148 wenye kuonyesha mahusiano ya watekelezaji wa mpango huu. Lakini, mchoro huu umeandikwa kwa Kiingereza na hauna kielelezo cha kumsaidia msomaji kuuelewa. Na tatizo kubwa zaidi ni kwamba huu ni mchoro ambao hauonyeshi muundo wa serikali ya Tanzania kama ilivyo leo, kuanzia Ikulu hadi kitongojini, kwa upande mmoja, na kuanzia serikalini, kupitia mahakamani hadi Bungeni, kwa upande mwingine. Watu wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma waombwe kuandaa muundo wa uongozi wa nchi, kama ulivyo leo, na kisha uwekwe hapa.

8. Safari yetu ya miaka 5 inahitaji rasilimali kiasi gani, zitatoka wapi na zitatumikaje? Mpango umeonyea makadirio ya mapato ya fedha zitakazokusanywa ndani ya miaka mitano ijayo bila kuonyesha makadirio ya matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala. Kwa hiyo, kimantiki, makadirio ya makusanyo yaliyotajwa ni ya kubuni. Dosari hii iondolewe kwa kutaja matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala.

9. Mwishoni mwa safari yetu ya miaka 5 kuna alama gani zitakazotujulisha kwamba tumefika? Kuna viashiria na shabaha za sekta ya nishati zilizopitwa na wakati. Mfano, mpango huu unasema kuwa ifikapo 2025 ni 60% pekee ya watanzania watakaokuwa wamepata umeme, wakati Waziri, Waziri Mkuu na Rais Samia wanasema 100%. Pia, katika sura ya nane hakuna “jedwali la mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na taarifa,” yaani, “logical framework matrix,” ambao ni msingi wa ufanisi wa mkakati wowote. Dosari hizi zirekebishwe.

10. Mapendekezo ya jumla: Kazi ya kukamilisha maandalizi ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa Kuelekea 2025 ifanyike sambamba na Mipango ya Maendeleo ya Wizara na Sekta husika. Mfano mzuri mwingine ni Mpango Mkakati wa Saba wa Zambia pamoja na Mikakati ya Wizara zake. Baadhi ya Mikakati ya Wizara, ambayo imeandaliwa kwa kuzingatia metholojia ya "Balanced Scorecard" inapatikana hapa:

Nawasalimia kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Attachments

  • Mapendekezo ya Mpango wa serikali.pdf
    1.7 MB · Views: 5
Da! bandiko refu sn
Uhakiki wa Kitabu cha Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka 5 hauwezi kuwa mfupi.
Hivyo, kuna usuli kwa ajili ya watu kama Babati. Huu hapa...

I. USULI: KWA NINI NAANDIKA BANDIKO HILI?

Bandiko langu lisemalo “Rais Samia Ameanzia Mwanza Kujenga Hekalu Letu” limewafanya wachangiaji wanitake kufanya uchambuzi rasmi wa kitabu kinachohakikiwa hapa. Ni “Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26,” ambao umeambatanishwa hapa chini.

Mpango huu ulioandaliwa mnamo Februari 2021 na “Wizara ya Fedha na Mipango” kwa niaba ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Serikali iko mbioni kuukamilisha na kutekeleza yaliyomo.

Hivyo, tathmini hii imegawanywa katika sehemu saba zinazojibu maswali yafuatayo: Kwa nini naandika bandiko hili? Katika mipango ya maendeleo tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi? Kitabu kina muundo gani? Kitabu kina maudhui gani? Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe aliopaswa kupeleka kwa hadhira? Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kufikisha ujumbe stahiki kwa hadhira? Maboresho gani yafanyike na kwa nini?

Hatimaye hitimisho ni kwamba, kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika, mwandishi wa mpango huu amepata alama 49 kati ya 100, sawa na alama ya “C.” Hivyo, kadiri inavyowezekana, anashauriwa kuondoa dosari zilizobainishwa. Mapendekezo hayo ni kama ifuatavyo:

  • Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe wake? Sura ya pili na sura ya tano zipanguliwe na kupangwa upya kwa kuweka mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona Wizara gani inahusika na utekelezaji wa kazi na majukumu ya sekya ipi. Mfano mzuri wa mpangilio wa aina hii unapatikana kwenye Mipango ya Maendeleo ya nchi ya Botwana.
  • Sisi ni nani na tumetoka wapi? Sura ya kwanza, ambayo ni “Utangulizi,” ipanuliwe na kuweka maelezo kuhusu Tanzania ni kitu gani kwa mujibu wa Katiba, historia, na jiografia, ili msomaji mpya aliyetoka sayari ya Jupita leo, aweze kupata uelewa mzuri juu ya kilichoandikwa na sababu zake.
  • Kwa sasa mwaka 2021 tuko wapi? Uchambuzi wa “SWOT Analysis” uliofanyika katika sura ya pili ufuatiwe na Uchambuzi wa “TOWS Analysis,” ili kwa njia hiyo, mikakati inayotajwa kitabuni ifungamanishwe kimantiki na uchambuzi wa kimazingira uliofanywa.
  • Tunataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? Pembetatu ya Maendeleo ya kiuchumi, Maendeleo ya kijamii na Maendeleo ya Kisiasa ikamilishwe kwa kutaja matokeo tarajiwa kwa ajili ya sekta ya “utawala bora” yaliyosahaulika chini ya fungu la 5.11.
  • Kusudi tuweze kufika mwisho wa safari yetu tutachukua hatua gani na kwa nini? Kuhusu habari ya kwa nini hatua hizi zichukuliwe, mpango umetaja nadharia ya mabadiliko na kuifupisha kwa njia ya mchoro kwenye ukurasa wa 70. Hata hivyo, baadhi ya maneno katika mchoro huu hayasomeki. Na mahusiano yaliyopo kati ya pingili zake tofauti hayaonekani bayana. Pia, hakuna marejeo kuhusiana na vyanzo vya dhana zinazoambatana na mchoro huu ili msomaji aweze kurejea na kujielimisha zaidi. Mapungufu haya yaondolewe.
  • Katika kila hatua ni kazi gani na majumu yapi yatafanyika ili tuweze kufika mwisho wa safari yetu?) Swali hili halijajibiwa isipokuwa katika hatua ya miradi ya kielelezo (fungu la 5.9). Kwa hiyo, kila kijisekta kilichotajwa kwenye mafungu ya 5.4 hadi 5.9, kipanuliwe kwa kuongeza “kazi na majukumu yatakayotekelezwa.”
  • Nani atachukua hatua gani, kufanya kazi zipi na kutekeleza majukumu yapi wakati wa safari yetu? Kuna mchoro kwenye ukurasa wa 148 wenye kuonyesha mahusiano ya watekelezaji wa mpango huu. Lakini, mchoro huu umeandikwa kwa Kiingereza, hauna kielelezo cha kumsaidia msomaji kuuelewa, na huu ni mchoro ambao hauonyeshi muundo wa serikali ya Tanzania kama ilivyo leo. Hivyo, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma iombwe kuandaa muundo wa uongozi wa nchi, kama ulivyo leo, na kisha uwekwe hapa.
  • Safari yetu ya miaka 5 inahitaji rasilimali kiasi gani, zitatoka wapi na zitatumikaje? Mpango umeonyea makadirio ya mapato ya fedha zitakazokusanywa ndani ya miaka mitano ijayo bila kuonyesha makadirio ya matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala. Kwa hiyo, kimantiki, makadirio ya makusanyo yaliyotajwa ni ya kubuni. Dosari hii iondolewe kwa kutaja matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala.
  • Mwishoni mwa safari yetu ya miaka 5 kuna alama gani zitakazotujulisha kwamba tumefika? Viashiria na shabaha za sekta ya nishati zilizopitwa na wakati zirekebishwe. Pia, katika sura ya nane liwekwe “jedwali la mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na taarifa,” yaani, “logical framework matrix.”
 
tatizo jf wanasomaga maneno mia mbili tu
Sio wote. Lakini, nimeweka usuli wenye maneno 670 kwa ajili ya watu wa aina hiyo...
I. USULI: KWA NINI NAANDIKA BANDIKO HILI?

Bandiko langu lisemalo “Rais Samia Ameanzia Mwanza Kujenga Hekalu Letu” limewafanya wachangiaji wanitake kufanya uchambuzi rasmi wa kitabu kinachohakikiwa hapa. Ni “Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26,” ambao umeambatanishwa hapa chini.

Mpango huu ulioandaliwa mnamo Februari 2021 na “Wizara ya Fedha na Mipango” kwa niaba ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Serikali iko mbioni kuukamilisha na kutekeleza yaliyomo.

Hivyo, tathmini hii imegawanywa katika sehemu saba zinazojibu maswali yafuatayo: Kwa nini naandika bandiko hili? Katika mipango ya maendeleo tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi? Kitabu kina muundo gani? Kitabu kina maudhui gani? Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe aliopaswa kupeleka kwa hadhira? Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kufikisha ujumbe stahiki kwa hadhira? Maboresho gani yafanyike na kwa nini?

Hatimaye hitimisho ni kwamba, kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika, mwandishi wa mpango huu amepata alama 49 kati ya 100, sawa na alama ya “C.” Hivyo, kadiri inavyowezekana, anashauriwa kuondoa dosari zilizobainishwa. Mapendekezo hayo ni kama ifuatavyo:

  • Mwandishi amefanikiwa na kufeli kwa kiasi gani katika kuupa umbo ujumbe wake? Sura ya pili na sura ya tano zipanguliwe na kupangwa upya kwa kuweka mchanganuo unaomwezesha msomaji kuona Wizara gani inahusika na utekelezaji wa kazi na majukumu ya sekta ipi. Mfano mzuri wa mpangilio wa aina hii unapatikana kwenye Mipango ya Maendeleo ya nchi ya Botwana.
  • Sisi ni nani na tumetoka wapi? Sura ya kwanza, ambayo ni “Utangulizi,” ipanuliwe na kuweka maelezo kuhusu Tanzania ni kitu gani kwa mujibu wa Katiba, historia, na jiografia, ili msomaji mpya aliyetoka sayari ya Jupita leo, aweze kupata uelewa mzuri juu ya kilichoandikwa na sababu zake.
  • Kwa sasa mwaka 2021 tuko wapi? Uchambuzi wa “SWOT Analysis” uliofanyika katika sura ya pili ufuatiwe na Uchambuzi wa “TOWS Analysis,” ili kwa njia hiyo, mikakati inayotajwa kitabuni ifungamanishwe kimantiki na uchambuzi wa kimazingira uliofanywa.
  • Tunataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? Pembetatu ya Maendeleo ya kiuchumi, Maendeleo ya kijamii na Maendeleo ya Kisiasa ikamilishwe kwa kutaja matokeo tarajiwa kwa ajili ya sekta ya “utawala bora” yaliyosahaulika chini ya fungu la 5.11.
  • Kusudi tuweze kufika mwisho wa safari yetu tutachukua hatua gani na kwa nini? Kuhusu habari ya kwa nini hatua hizi zichukuliwe, mpango umetaja nadharia ya mabadiliko na kuifupisha kwa njia ya mchoro kwenye ukurasa wa 70. Hata hivyo, baadhi ya maneno katika mchoro huu hayasomeki. Na mahusiano yaliyopo kati ya pingili zake tofauti hayaonekani bayana. Pia, hakuna marejeo kuhusiana na vyanzo vya dhana zinazoambatana na mchoro huu ili msomaji aweze kurejea na kujielimisha zaidi. Mapungufu haya yaondolewe.
  • Katika kila hatua ni kazi gani na majumu yapi yatafanyika ili tuweze kufika mwisho wa safari yetu?) Swali hili halijajibiwa isipokuwa katika hatua ya miradi ya kielelezo (fungu la 5.9). Kwa hiyo, kila kijisekta kilichotajwa kwenye mafungu ya 5.4 hadi 5.9, kipanuliwe kwa kuongeza “kazi na majukumu yatakayotekelezwa.”
  • Nani atachukua hatua gani, kufanya kazi zipi na kutekeleza majukumu yapi wakati wa safari yetu? Kuna mchoro kwenye ukurasa wa 148 wenye kuonyesha mahusiano ya watekelezaji wa mpango huu. Lakini, mchoro huu umeandikwa kwa Kiingereza, hauna kielelezo cha kumsaidia msomaji kuuelewa, na huu ni mchoro ambao hauonyeshi muundo wa serikali ya Tanzania kama ilivyo leo. Hivyo, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma iombwe kuandaa muundo wa uongozi wa nchi, kama ulivyo leo, na kisha uwekwe hapa.
  • Safari yetu ya miaka 5 inahitaji rasilimali kiasi gani, zitatoka wapi na zitatumikaje? Mpango umeonyea makadirio ya mapato ya fedha zitakazokusanywa ndani ya miaka mitano ijayo bila kuonyesha makadirio ya matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala. Kwa hiyo, kimantiki, makadirio ya makusanyo yaliyotajwa ni ya kubuni. Dosari hii iondolewe kwa kutaja matumizi ya serikali kwa kila wizara, kila idara, na kila wakala.
  • Mwishoni mwa safari yetu ya miaka 5 kuna alama gani zitakazotujulisha kwamba tumefika? Viashiria na shabaha za sekta ya nishati zilizopitwa na wakati zirekebishwe. Pia, katika sura ya nane liwekwe “jedwali la mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na taarifa,” yaani, “logical framework matrix.”
 
Uhakiki wa Kitabu cha Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka 5 hauwezi kuwa mfupi.
Hivyo, kuna usuli kwa ajili ya watu kama Babati. Huu hapa...
Wavivu wa kusoma ndio hao mabingwa wa kukosoa.

Nitarejea baada ya tafakari na tafakuri ya bandiko lako. Ila kwa haraka haraka mapitio yangu hoja zako nyingi zimejirudirudia na kuna dalili ya wewe kutokuhuisha Mapendekezo hayo na Dira ya Maendeleo ya Taifa, 2025 (Development Vision 2025)
 
5 Reactions
Reply
Back
Top Bottom