SoC04 Mpango wa kanzitada ya taifa kudhibiti vyanzo vya mapato chini ya Wizara ya Fedha

Tanzania Tuitakayo competition threads

Librarian 105

JF-Expert Member
May 6, 2023
244
327
Dira hii inalenga udhibiti wa vyanzo vya mapato ili kukuza pato la taifa ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na ustawi wa jamii kupitia mamlaka zao za serikali za mitaa zikitekeleza mpango huu chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha. Awali kabisa mamlaka hizi hazina budi kuboreshwa kimuundo kwa kuanzishwa kitengo cha 'Biashara, Uchumi, na Kodi' ndani yake ambacho kitashirikiana bega kwa bega na Tawala za Mikoa, Brela na TRA kwa mujibu wa sera za kifedha za nchi pamoja na kanuni za utumishi wa umma.

Na utekelezaji wake ni ndani ya miaka kumi ambapo hatua kuu zifuatazo yafaa zizingatiwe 1. a} usanifu wa kanzidata yenye viungo muhimu vifuatavyo (i) orodha ya vyanzo vyote vya mapato ya ndani (aina ya biashara/huduma), (ii) Usajili wa Brela (iii) makadirio ya kodi; b} Msajili wake - Halmashauri au Serikali za Mitaa. 2. Utungaji wa sera za ushirikiano wa kimamlaka na kitaasisi wenye kuepuka mgongano wa kimaslahi baina ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa, brela na TRA. 3. Kuongezwa kwa kitengo pendekezwa kwa mujibu wa sheria.

Maono Makuu Ya Kanzidata Hii Ya Taifa Katika Udhibiti Wa Vyanzo Vya Mapato:
Uzoefu unaonyesha ya kuwa upotevu wa mapato unachangiwa zaidi na mapungufu kwenye mifumo ya kutunza taarifa za jumla za vyanzo hivi vya mapato ya ndani. Kiasi cha kupelekea udanganyifu na rushwa kwenye makusanyo ya kodi, ukwepaji kodi, na ugumu katika kusajili biashara/huduma hizi kwa wakati. Kwa sasa ndani ya Halmashauri nyingi nchini, kadhia ya udanganyifu kwenye masuala yanayohusu kodi na ushuru ni kubwa,na mamlaka hizi za serikali za mitaa huwa zinatumika tu kusaidia kuendesha kaguzi za kushtukiza za leseni za biashara na kodi.

Kwa upande mwingine huendeshwa kwa mtindo wa zimamoto kwa munasaba wa wahusika kujipatia vipato binafsi wakitumia kivuli cha serikali kisha kutoa maonyo kwa njia ya upigaji faini wafanyabiashara wenye hatia na au uzembe wa kusajili biashara zao. Hawa huikosesha serikali mapato ya aina mbalimbali na kuinyima pia fursa ya kusajili vyanzo vipya vya mapato. Kwani maduka mengi hufungwa mitaa kupisha kaguzi hizi hali inayosababisha kukithiri kwa biashara bubu mitaani.

Kwa mantiki hii, umuhimu wa kusanifiwa kwa kanzidata hii na Wizara ya Fedha, kutaisaidia serikali kudhibiti mapato yake sanjari na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi na ushuru. Kwa sababu uwajibikaji wa serikali za mitaa kusajili vyanzo vya mapato utakuwa wa kisasa unaokidhi vigezo vyote vya kitakwimu tena unaozingatia uhakiki wa mara kwa mara wa taarifa za biashara/huduma zilizopo kwenye mzunguko wa uzalishaji mali na huduma kuanzia katika mamlaka hizi za serikali za mitaa. Halikadhalika CAG atawepesishiwa kazi ya kukagua mahesabu ya mapato na matumizi ya mamlaka hizi. Kwani mwisho wa siku atatumia mizania ya Kanzidata hii dhidi ya mapato na matumizi ya Tawala za Mikoa na Mamlaka za serikali za mitaa nchini.

Majukumu Ya Kitengo cha Biashara, Uchumi, na Kodi:
Watendaji wa kitengo hiki watakuwa na jukumu kuu la kusajili biashara mlango kwa mlango mitaani kwa muongozo utakaoidhinishwa wa Brela/Halmashauri, kutoa makadirio ya kodi chini ya taratibu za TRA kisha kuzijaza kwenye viungo vya Kanzidata ya Taifa na kuhifadhiwa moja kwa moja kwenye server ya Wizara baada ya kupitia uhakiki wa kina na kitaalamu. Pia watajaza taarifa za vyanzo vya mapato vilivyofilisika na kufungwa na ambavyo havijakidhi vigezo vya usajili na kukadiriwa kodi kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

vilevile watakuwa wakikagua leseni za biashara na kutoa elimu ya ulipaji wa kodi wa hiari, na kufanya masuala mengineyo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ili kuharakisha maendeleo ya watu. Kwa njia hii hata sekta isiyo rasmi yenye kukisiwa kuajiri watanzania milioni 27.7 inaweza kufikiwa kwa haraka zaidi.

Kwenye kubuni vyanzo vipya vya mapato na kukuza wigo wa makusanyo ya kodi, nashauri serikali ya awamu hii ya sita ianzishe utoaji leseni kwa mafundi stadi kulingana na madaraja ya fani na mahitaji ya kwa jamii, huku ada zake zikitegemeana na fani husika pamoja na ngazi za kielimu. Awamu iliyopita ilifanya vizuri katika kuwasajili pamoja na kuwapa vyeti vya utambuzi mafundi wote. Zoezi hili liboreshwe zaidi ili nguvu kazi hii ichangie kodi na pato la taifa kwa malengo ya kutombebesha mzigo wa tozo za simu hata yule mwanachi aliye masikini sambamba na kupunguza gharama za huduma ya vifurushi nchini. Hii pia itadhibiti mafundi wasio na elimu mitaani na kuzipa thamani fani husika. Na eneo hili serikali pia itathmini 'ujira kwa saa' kulinda maslahi ya mafundi kwa maana kuna kazi zingine huwa hazichukui hata nusu siku kumalizika. Ikifanyika mapema fundi hupunjwa ujira wake hivyo wengi wao huchelewesha kazi zaidi. Hii ni sawa na kuchelewesha maendeleo ya nchi na ustawi binafsi wa fani za ufundi nchini.

Nao TRA wanapaswa kuja na mfumo risiti maalumu za biashara zenye mauzo ghafi yasiyovuka milioni nne kwa mwaka. Kuna uzembe mkubwa wa kutunza kumbumbuku za mahesabu kwa wamiliki wa biashara hizi na nia za makusudi kwa wengineo kukwepa kodi mitaani, masokoni na minadani. Biashara hizi zikisajiliwa na wamiliki kupewa vitabu hivi vya risiti pamoja na kufuatiliwa na kitengo pendekezwa mara kwa mara. uwezekano upo wa kuongeza vyanzo vipya vya kodi au vitabu hivyo vya risiti vinaweza kukadiriwa kulingana na mtaji na biashara husika, hapa zitaondolewa zile biashara dhaifu za kutafutia mkate wa kila siku, ambavyo vitauzwa kwa makadirio ya juu kidogo ya kodi pasina kuathiri mtaji wa mhusika. Unaombata na elimu ya kufunga vitabu vya mauzo kila mwezi na sheria zenye kuwabana kufanya hivyo.

Hitimisho:
Kanzidata hii ina asilimia kubwa ya kuisaidia serikali katika maeneo mengi ya kiutawala wa kifedha. Kubwa hasa serikali za mitaa zitakuwa kitovu katika kukuza uchumi wa nchi kusaka maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa huduma za kijamii. Kutokana na ushiriki wake katika udhibiti wa vyanzo vya mapato na makusanyo ya kodi na ushuru kwa njia ya kieletroniki.
 
Uzoefu unaonyesha ya kuwa upotevu wa mapato unachangiwa zaidi na mapungufu kwenye mifumo ya kutunza taarifa za jumla za vyanzo hivi vya mapato ya ndani. Kiasi cha kupelekea udanganyifu na rushwa kwenye makusanyo ya kodi, ukwepaji kodi, na ugumu katika kusajili biashara/huduma hizi kwa wakati
Hakika kabisa. Taarifa.
Na eneo hili serikali pia itathmini 'ujira kwa saa' kulinda maslahi ya mafundi kwa maana kuna kazi zingine huwa hazichukui hata nusu siku kumalizika.
Ujira kwa saa, kwa baadhi na baadhi ua kazi hiyo ujira kwa kazi maana..... tofauti na hivyo tumuajiri na mtu wa kuhakikisha kuwa katika saa hizo fundi afanya kazi kweli.
Kanzidata hii ina asilimia kubwa ya kuisaidia serikali katika maeneo mengi ya kiutawala wa kifedha. Kubwa hasa serikali za mitaa zitakuwa kitovu katika kukuza uchumi wa nchi kusaka maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa huduma za kijamii. Kutokana na ushiriki wake katika udhibiti wa vyanzo vya mapato na makusanyo ya kodi na ushuru kwa njia ya kieletroniki.
Sawa sawia
 
Back
Top Bottom