Moyo Ulioonja Maumivu

SEHEMU YA 31

Alipoona amechoka, akausogelea mlango na kuanza kuugonga, alihitaji ufunguliwe ili aone kile kilichokuwa kimeendelea humo..

“Dokta! Fungua mlango...fungua mlango...” alisema Theo huku machozi yakianza kumtoka, aliisikia sauti moyoni mwake ikimwambia kuna moja limetokea, inawezekana mke wake akawa amefariki ama watoto wake.

Alijitahidi kuipinga sauti hiyo kwa nguvu kubwa, haikupingika, iliendelea kumwambia hivyohivyo kitu kilichomfanya kuwa na hofu zaidi na zaidi.

Baada ya dakika kadhaa za kugonga mlango ule, mara ukafunguliwa na kukutanisha macho yake na daktari.

Kwa muonekano wa mtu huyo tu ulimwambia kulikuwa na jambo kubwa lililokuwa limetokea huko, alionekana tofauti, kama kweli mke wake alijifungua salama, inamaanisha daktari huyo angeonekana kuwa na furaha na si kama alivyokuwa.

“Nini kinaendelea?” aliuliza Theo huku akimwangalia daktari huyo ambaye alionekana kuwa na jambo zito moyoni mwake ila hakutaka kumwambia mahali hapo.
“Naomba twende ofisini kwangu,” alijibu daktari huyo.

“Subiri kwanza. Naomba uniambie! Amejifungua salama?” aliuliza Theo huku akianza kutetemeka kwa hofu, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, mwili wake ulikuwa ukitetemeka kana kwamba alikaa sehemu iliyokuwa na baridi kali.
“Naomba twende tukaongee,” alisema daktari yule.

Hakuwa na jinsi, yeye na marafiki zake wakaanza kuelekea kule ofisini kwa daktari, aliogopa, alimuomba Mungu kusiwe na habari mbaya ya kupewa, aliujua moyo wake, kwa jinsi ulivyompenda Violeth, kama angeambiwa mke wake amekufa basi maumivu ambayo angeyasikia yangekuwa makubwa mno.

Walipofika ndani ya ofisi hiyo, wakakaa kwenye viti na kuanza kuangaliana. Moyo wa Theo ulikuwa kwenye maombezi mazito, hakukuwa na siku ambayo alikuwa akimuomba Mungu kama siku hiyo.

“Theo....tumejitahidi sana, mke na watoto wako wamekufa...” aliisikia sauti hiyo moyoni mwake, sauti ambayo ilimtisha mno.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane siku nyingine.
Shangazi hiyo sauti yantisha mi pia.!
 
SEHEMU YA 32

Theo aliendelea kuwa na hofu tele, muonekano wa daktari Yule haukumpa furaha hata kidogo. Kichwa chake kilikuwa na majibu kwa kile kilichokuwa kimetokea ndani, alimuomba Mungu moyoni mwake, aliikemea roho ya mauti ambayo alihisi kabisa ilikuwa ikiinyemelea familia yake.

Daktari yule alimwangalia Theo, aliiona hofu yake, alikuwa na jambo kubwa moyoni mwake lakini hakujua ni kwa jinsi gani angemwambia mwanaume huyo kwani aliogopa mno, alihisi kabisa kama angemwambia kilichotokea, kingemchanganya mno.

“Naomba uniambie chochote kile, hata kama wamekufa, naomba uniambie,” alisema Theo huku akimwangalia daktari huyo, machozi yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake.

Hapo ndipo daktari akaanza kumwambia kilichokuwa kimetokea, hakutaka kumficha, alimwambia tu kwamba mkewe alikuwa na watoto mapacha, alijifungua mtoto mmoja wa kike, mzima, pacha mwingine wa kiume alikuwa amefariki hata kabla ya kumtoa tumboni.

Moyo wa Theo ukapiga paa! Hakuamini alichokisikia, alisikia maumivu ambayo hakuwahi kuyasikia kabla, pale alipokuwa kwenye kiti, akakiinamisha kichwa chake chini, akaona kama kulikuwa na uzto kubaki pale, akapiga magoti chini na kuanza kulia.

Kile kilichotokea kilikuwa kama ndoto kwake, alikuwa na mipango mingi juu ya watoto wake, aliumia mno na hakuamini hata kidogo kilichokuwa kimetokea. Waliandaa majina mazuri ya watoto wao wawili, sasa ilikuwaje wapate mtoto mmoja?
“Mungu! Kwa nini? Kwa nini umeruhusu hili?” aliuliza Theo huku akilia kama mtoto.

Marafiki zake ambao walikuwa humo pamoja na daktari wakaanza kumbembeleza ili anyamaze lakini haikuwa kirahisi namna hiyo. Alishindwa kunyamaza kwa kuwa hakukuwa na kitu alichotamani kukiona kama watoto wake wote wawili.

Alilia sana na baada ya dakika arobaini za maombolezo, daktari akamtoa na kuelekea naye katika chumba alichohifadhiwa mke wake na watoto wake. Alipofika huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwaangalia watoto wake.
 
SEHEMU YA 33

Mmoja alikuwa akilia sana lakini mwingine ilikuwa ni maiti tu ambayo ilifungwa vizuri. Maumivu yakazidi kuongezeka kwa Theo, aliiangalia maiti ile ya mtoto wake, hakuamini kama alikuwa amekufa baada ya kuzaliwa.

“Harry mtoto wangu, amka uniangalie baba yako, fumbua macho yako mtoto wangu, nitazame, baba yako nimefika, fumbua macho yako mwanangu,” alisema Theo kwa sauti ya chini huku akiiangalia maiti ya mtoto wake aliyekuwa katika kitanda kidogo.

Maiti ilikuwa kimya, macho yalifumbwa, roho yake haikuwa hapo tena. Moyo wake ulimchoma mno, macho yake yalikuwa mekundu, manesi na daktari ambao walikuwa ndani ya chumba kile, wote walikuwa wakilia, maneno aliyoyaongea Theo yaliwachoma mno, yalionyesha ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa ameumia.

Akatoka hapo na kusoge kule alipokuwa mtoto wake mwingine, aliyeamua kumpa jina la Rachel, akamwangalia mtoto huyo alikuwa akikunjakunya vidole vyake huku wakati mwingine akilia. Alimwangalia moyo wake ulifurahia lakini bila kuwa na mtoto mwingine, furaha ile haikuwa imekamilika hata kidogo.

Alipotoka hapo akasogea mbele, akafika katika kitanda alichokuwa mke wake, Violeth, alikuwa kimya, alipumilia mashine ya hewa safi. Moyo wake ulimuuma mno, hakujua ni kwa jinsi gani angemwambia kuhusu mtoto wao mmoja aliyekuwa amefariki dunia.

Aliganda tu akimwangalia mke wake huyo alivyokuwa akiutetea uhai wake kitandani pale. Alitamani kumuamsha, ampeleke nyumbani na kumsahaulisha kila kitu, yaani asahau kama alijifungua watoto maoacha wazuri mno.

“Mke wangu! Umepambana, umepigana mno! Wewe ni mwanamke shujaa, una moyo wa chuma, umepigania uhai wa watoto wetu, hata kama mmoja amefariki, ila bado ulipambana....” alisema Theo na kunyamaza, akaendelea kulia kama kawaida.

“Nashukuru kwa kunifanya kuwa baba tena,” alisema Theo na kuifuata maiti ya mtoto wake, akaibeba.
 
SEHEMU YA 34

Aliishika, aliibeba kana kwamba alikuwa mtoto mzima, alilia huku ikiendelea kuwa mikononi mwake.

Hakujua ni kwa namna gani Mungu aliruhusu maumivu hayo katika maisha yake, alitamani arudishe mishale ya saa nyuma ili kila kitu kianze upya lakini si kupitia maumivu makali aliyokuwa akiyapitia.

“Nitakupenda maisha yangu yote Harry!” alisema Theo huku mwili wa mtoto wake ukiwa mikononi mwake.

Alikaa humo kwa dakika kadhaa, alipomaliza, madaktari wakamwambia kuhusu kumzika mtoto huyo. Hakutaka kufanya hivyo mpaka pale ambapo mke wake angerudiwa na fahamu. Hilo halikuwa tatizo, kulikuwa na jambo jingine ambalo dokta alihitaji sana kuzungumza naye.

Moyo wa Theo ukapiga paa! Hakuamini kama kulikuwa na jambo jingine tena, lilikuwa nini? Kuhusu hali ya mke wake ama?

Hakuwa na jinsi, akaondoka na marafiki zake na kuelekea katika ofisi ya daktari yule na kukaa pamoja.

Alijua kabisa kwamba Theo aliumia moyoni mwake, hakuwa na jinsi, alitakiwa kumwambia ukweli kuhusu jambo jingine, yaani kama kulia, alitakiwa kulia tena lakini si kumruhusu aondoke na siku nyingine amwambie kuhusu tatizo jingine, kilio kingeanza upya.

“Niambie kuna nini? Ni kuhusu mke wangu? Dokta, naomba usinifiche kitu, kama kuumia, nimeumia sana, na kama kulia nimelia sana, naomba uniambie, mimi mwanaume,” alisema Theo japokuwa moyoni mwake alijua hakuwa na moyo wa kuvumilia maumivu makali.
“Ni kuhusu mtoto wako!” alisema dokta.
“Nani? Rachel?”
“Ndiyo!”

“Amefanyaje?” aliuliza Theo, akaishiwa pozi, akabaki pale kwenye kiti huku akili yake ikizidi kuchanganyikiwa.

“Ana tatizo pia!”
“Tatizo gani?”
“Moyo wake umevimba, mishipa yake haina nguvu ya kusukuma damu vizuri,” alijibu daktari kitu kilichoanzisha kilio kingine kabisa ndani ya ofisi ile.

Hilo likawa jambo jingine jipya! Theo alilia sana, aliumia zaidi, hakuamini kile alichokisikia, yaani mtoto wake aliyebaki alikuwa na tatizo jingine tena, moyo wake kuvimba na mishipa yake haikuwa na nguvu ya kusukuma damu.
 

Similar Discussions

14 Reactions
Reply
Back
Top Bottom