Moyo Uliojaa shukrani kwa 2007

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,695
40,721
MAKALA yangu ya wiki iliyopita, nilitaka iwe makala ya mwisho kwa mwaka huu. Pia nilitamani nisiandike kitu kingine chochote hadi mwaka mpya.
Hata hivyo, dhamira yangu ikanisuta kuwa nitakuwa si muungwana kama nitamaliza mwaka bila ya kufanya jambo moja la kiungwana na la kidugu. Kama sitatoa shukrani.

Kwa mtu ambaye amejaliwa mengi na kukarimiwa vingi, kwa mwaka huu kuumaliza bila kuonyesha moyo wa kushukuru ni kutokuwa mtu wa ‘asante’.

Hivyo basi, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine, wamemfanya Mwanakijiji awe jinsi alivyo.

Kuna watu wengi ambao wamenisaidia katika kuongoza mapambano haya ya kifikra na wapo ambao wamenisaidia kutimiza mambo kadha wa kadha nyumbani. Hivyo nimeona nitumie nafasi hii kutoa shukrani zangu hadharani, tena kwa kuwataja kwa majina na jinsi walivyonisaidia.

Kwanza kabisa nitumie nafasi hii kulishukuru gazeti la Tanzania Daima, kwa kunipa nafasi ya kusambaza mawazo yangu kila Jumatano na wakati mwingine pale inapobidi.

Uamuzi wao wa kunipa nafasi ya kuandika makala kwa gazeti hili, kimekuwa ni kitendo cha kijasiri ambacho miaka michache huko nyuma, labda hakikuweza kufikirika. Katika kutoa nafasi kwangu na bila ya shaka waandishi wengine, wamejiweka mahali pabaya pa kuonekana ‘kinyume’ na serikali.

Ni kutokana na sababu hiyo, wanajikuta kuwa si kipenzi cha watuma matangazo ya kibiashara wa serikali. Jaribio la kufuatilia ni matangazo mangapi yanatoka serikalini yanayochapishwa kwenye gazeti hili ukilinganisha na magazeti mengine, utaona kuwa kuna kutokuwakilishwa vizuri kwa matangazo ya serikali.

Wakati magazeti ambayo yanaonekana ni ‘marafiki’ yanapata kila aina ya matangazo hadi mengine yanashindwa hadi ‘next day’, magazeti kama Tanzania Daima yana nafasi bwelele. Hivyo wahariri na wamiliki wangeamua kusalimu amri na kuanza kuimba sifa za serikali na chama tawala ili wapate ‘tu-matangazo’ kidogo.

Kwa hili sina budi kuwashukuru wasomaji wa Tanzania Daima, ambao kila siku wamekuwa wakinunua gazeti hili na wengine kuhakikisha hawalikosi kila Jumatano.

Ni wao ambao kwa kweli wamekuwa wakiliendesha gazeti hili kwa manunuzi yao. Ni matumaini yangu kuwa, mwaka ujao watahakikisha wananunua zaidi na kuwanunulia wengine, kwani mwendo hapa haupoi na tuna mengi zaidi ya kuliamsha taifa letu!

Mwaka uliopita, nilipata nafasi ya kufanya mahojiano na viongozi na watu mbalimbali nchini katika kutafuta habari na mitizamo yao kuhusu mambo mbalimbali.

Sina budi kuwashukuru viongozi wote ambao walikubali kupokea simu na kuzungumza nami japo kwa dakika chache. Shukrani za kwanza na dhati zimuendee Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa, mawaziri kadhaa wakiwemo Mhe. Mohammed Seif Khatib, Mhe. Mary Nagu, Mhe. Nazir Karamagi, Mhe. Anthony Diallo, na Mhe. Hussein Mwinyi.

Pia nilipata nafasi ya kuzungumza na wabunge mbalimbali wakiwemo Mhe. Adam Malima, Mhe. Zitto Kabwe na Mhe. Willbroad Slaa. Pia niwashukuru wanasiasa wengine kama Christopher Mtikila, John Mnyika na Mhe. Ndesamburo. Wengine ambao sina budi kuwashukuru ni watendaji mbalimbali ambao hawakusita kunipa nafasi ya kuzungumza nao kuhusu masuala mbalimbali.

Hapa niwashukuru Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hosea, Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Kassim Mpenda na pia Mkurungezi wa Taasisi ya Utangazaji, Tido Mhando.

Wengine ni viongozi wa vyama vya upinzani ambao sina budi kuwashukuru sana kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa sakata la vijana wetu Ukraine.

Wakati watoto wale wamekwama na kususwa na taifa lao na wakiwa nchi ya ugeni kukimbilia ubalozi wa Uingereza, ni wao ambao walijaribu kwa uwezo wao wote kuwashawishi Watanzania wenzao kuwa vijana hawa waliahidiwa mikopo na ya kuwa serikali imeamua kuwawekea ngumu.

Michango yao kwenye mfuko wa vijana hawa iliwasaidia kwa namna moja au nyingine kumudu maisha ya nchi hiyo ya kigeni. Hivyo nawashukuru sana Mhe. James Mbatia, Mhe. Seif Hamad, Mhe. Augustine Mrema na Mhe. Freeman Mbowe.

Katika hili la vijana wa Ukraine, haitatosha hivihivi bila kuwashukuru pia marafiki zangu waliotawanyika pote duniani na ambao walijitolea kama watu binafsi na kutumia taasisi zao.

Hapa sina budi kumshukuru Dk. Sengodo Mvungi na Mwalimu Ndera Kessy wote toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na jinsi ambavyo asasi ya TANLET ilivyoweza kujitokeza na kusaidia vijana wetu. Ni mbinguni tu wanajua ni jinsi gani tunaweza kuwashukuru!

Lakini sitakuwa mwenye shukrani kama sitawashukuru wanachama wenzangu na wachangiaji wa tovuti ya jamboforums.com ambao kwa mwaka mzima wamekuwa tayari kusimama na kusaidia pale panapohitajika, na hasa wakati vijana wetu walipokwama Ukraine.

Kwa karibu miezi kadhaa, ni wana jamboforums.com ambao walisimama kidete kuhakikisha kuwa vijana hawa wana fedha kidogo za chakula na mahitaji mengine, hadi pale waliporudishwa nyumbani kimabavu na serikali yao.

Kuna wale ambao kutokana na usiri wa jamboforums.com, majina na nafasi zao zinatambulika mbinguni tu. Hata hivyo wapo wachache ambao wanajulikana kwa majina ya kwenye mtandao tu na ambao hata mimi mwenyewe siwafahamu, lakini nilipowaomba kusaidia walisimama kishujaa na kutoa msaada.

Nitawataja kwa majina hayo ya mtandaoni; Rpg, Mlalahoi, Mtanzania, Kalamu, Defunkadelic, Rufiji, Nyani Ngabu, Madela wa Madilu, SteveD, Ogah, Mkandara na Kafara. Wengine ni pamoja na Tishy, Sophia, Monica, Mwafrika wa Kike na wengine ambao wangependa majina yao yabakie kapuni.

Kwenu nyote, ninawashukuru sana kwa niaba ya vijana hawa ambao nina uhakika hawatasahau ukarimu wa watu wasiowajua.

Mwaka huu pia kuna mambo kadhaa ambayo nimeyafuatilia nyumbani na sina budi kuwashukuru watendaji wengine ambao walitusaidia kupata taarifa na kufuatilia mambo fulani muhimu.

Kwenye ajali ya moto ya Mwanjelwa, napenda kumshukuru Kamanda Kova kwa kutupa muda wake, kwenye suala la binti mdogo aliyebakwa Kunduchi sina budi kumshukuru Kamanda Rwambow na pia mwendesha mashtaka mwandamizi pale Kisutu kuweza kuifuatilia kesi hiyo na kuifikisha mahakamani, hasa baada ya familia kukata tamaa kuwa haki haiwezi kutendeka.

Na mwisho sina budi kuwashukuru watu mashuhuri wawili ambao walikubali kuzungumza nami na ambao binafsi naweza kusema ni kilele cha mahojiano yangu ya mwaka huu. Kwanza ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha Rose Migiro ambaye licha ya shughuli zake, alichukua muda kuzungumza nami kuhusu uteuzi wake. Sina budi pia kumshukuru Dk. Salim Ahmed Salim kwa kutumia muda wake siku ile ya kumkumbuka Mwalimu kuweza kuzungumza nami kuhusu mambo mbalimbali.

Watu hawa wawili wamenifundisha kitu kimoja, nacho ni kuwa tayari kutumika taifa lako linapokuita!

Kwenu nyote ambao nimewataja kwa majina na hata wale nisiowataja kwa majina, naomba mjue kabisa moyo wangu umejaa shukrani tele na ninaona fahari kuwa mwananchi mwenzenu.

Wengi wenu tunatofautiana katika mambo mengi, mitazamo, mwelekeo n.k. Wengine tunatofautiana kiasi cha kuonana kama ‘maadui’ wa aina fulani na wengine kuhisi ninawaandama kila kukicha.

Baadhi ya tofauti zetu ni za msingi sana, ambazo zitadumu, lakini tofauti nyingine ni ndogo na ambazo zinaweza kusahauliwa mapema. Kwa vyovyote vile, heshima yangu kwenu nyote haijapungua na haiwezi kupungua na imani yangu kuwa mwaka huu mtajitahidi zaidi iko pale pale.

Kuelekea mwaka 2008 hatimaye nimefanikiwa kuanzisha tovuti yangu mpya ambayo itakuwa inawaletea habari na mambo mbalimbali. Bado ni tovuti changa, lakini lengo lake ni kuinua kiwango cha upashanaji habari nchini na pia kwenda pale ambako hakuna chombo kingine cha habari kimethubutu kwenda.

Tovuti hiyo ya www.klhnews.com itakuwa ndio mahali ambako kazi zangu nyingi zitaonekana kuanzia mwakani na ni matumaini yangu kuwa wale wengine ambao walikwepa kuzungumza nami (niseme mtu mmoja tu ndiyo alifanya hivyo, sitamtaja jina kwani kama umefuatilia makala zangu unaweza kuhisi mara moja na ukapatia) wajue ya kuwa sijui kukata tamaa. Wenye taasisi za vyombo vya habari tarajieni barua pepe yangu mapema mwakani ya kuomba ushirikiano wenu.

Kuna mahali bila ya shaka nimekosea au sikufanya sawasawa kama nilivyotaka. Kwenu nyote ninawaomba radhi na naahidi mwakani nitajitahidi kufanya kwa ubora zaidi, kwa kuthubutu zaidi na nikiweka maslahi ya wananchi wenzangu mbele zaidi.

Tuombeane uzima na ikimpendeza aliye juu, tukutane mwakani kwenye ukurasa huu! Kwani taifa ni letu sote! Nawatakia heri na fanaka za 2008.
 
Nashukuru sana.. yaani sina la kusema. Mngejua ni kwa kiasi gani watu wa JF wamekuwa msaada... Sina cha kuwalipa kwa ushauri, ukosoaji, kunoana, kupingana n.k kwani vyote vimechangia kwa kiasi kikubwa kuninoa na kunifanya niendelee kukaa chini na nisiache libichwa langu liguse udongo! Msisite kunikosoa na kuniweka sawa..mnishauri na kunipa mwongozo.. najua ni pamoja tutafika... !
 
Back
Top Bottom