Moto wateketeza ofisi za TAMESA Moshi

peno hasegawa

JF-Expert Member
Feb 24, 2016
12,799
21,370
Moto mkubwa ambao chanzo chake bado hakijajulikana, unateketeza majengo na vifaa mbalimbali vya ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) mjini Moshi.

Mashuhuda mbalimbali wameieleza Mwananchi Digital kuwa moto huo ulianza saa 11:30 alasiri leo Machi 25, 2022 katika ofisi hizo za Tamesa ambazo zipo karibu na Bohari ya Mafuta ya Serikali na ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro .

Mwananchi Digital imeshuhudia jitihada mbalimbali za uokoaji zikiendelea ambapo waokoaji walikuwa wanahamisha magari ya serikali na vifaa ili visifikiwe na moto.

Nao wafanyakazi wa duka la samani lililo karibu na ofisi hizo za Tamesa wamefanikiwa kutoa samani na kuziweka barabara ya Kristu Mfalime kuelekea mzunguko wa magari wa Bonite.

Hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyepatikana kuzungumzia moto huo, lakini Afisa Mtendaji wa Kiwanda cha Sukari cha TPC anayeshughulikia Utawala, Jaffar Ally akizungumza kwa njia ya simu amesema tayari wametuma gari la Zimamoto kwenda Moshi kusaidia kuzima moto huo.

"Ni kweli nimepokea simu kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Moshi juu ya moto huo mkubwa na tayari tumeshatoa gari letu limeelekea huko,"alisema Ally.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom