Moto wateketeza hoteli tatu na nyumba za raia

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
MOTO WATEKETEZA HOTELI TATU JAMBIANI

Salma Said, Zanzibar


JUMLA ya hoteli tatu za kitalii na zaidi ya nyumba sita za wananchi zimeteketea kwa moto jana asubuhi katika kijiji cha Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho walioshuhudia moto huo wamesema waliona moto mkubwa ukiwaka katika hoteli za kitalii na kutoka nje na kusaidiana na wamiliki wa hoteli hizo kwa kuuzima.

Hoteli zilizoungua ni pamoja na Visitors Inn, Sau Inn na Bungalow ambapo zote zipo eneo la Jambiani ukanda wa pwani ambapo moto huo uliwaka kwa kasi kutoka na hoteli hizo kuezekwa kwa makuti ambapo moto ilishika kasi kutokana na upepo mkubwa uliokuwa ukivuma nyakati za asubuhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Augustine Olomi amesema amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la moto na kuunguza hoteli za kitalii na nyumba zilizo karibu na hoteli hizo.

Kamanda huyo amesema hadi sasa thamani kamili ya vitu vilivyoungua ndani ya hoteli hizo pamoja na nyumba zilizo karibu na hoteli bado haijajulikana thamani yake lakini zimeteketea kwa kiasi kikubwa.

Katika hoteli ya Visitors inn zaidi ya vyumba 12 vya kulalia wageni na sehemu ya mkahawa zimeteketea kwa moto huo huku baadhi ya vitu vikiwa vimeteketea kwa kiasi kikubwa hasa katika maeneo ya jikoni na kumbi za hoteli hiyo.

Katika hoteli yote ya Sau Inn vyumba vingi vimeteketea na baadhi ya mizigo ya wageni na mali nyingine zilizokuwemo katika hoteli hizo zimeungu kabisa kwa moto huo.

Hoteli ya Bungalow nayo inaelezwa kuteketea vyumba vya wageni, kumbi za mikutano pamoja na eneo la jikoni lote kuteketea ambapo hadi sasa haijafahamika kama kuna baadhi ya wafanyakazi au wageni walioathirika na moto huo ambao walikuwemo vyumbani.

Kwa mujibu wa wanakijiji walioshuhudia moto huo wamesema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyoanzia sehemu ya jikoni katika hoteli ya Visitor Inn na baadae kusambaa katika hoteli nyengine ambazo zipo karibu na hoteli hiyo.

Haji Mati ni mmoja wa shuhuda aliyekuwa karibu na hoteli hizo amesema wakati akitoka nyumbani kwake aliona moshi mkubwa umetanda na kulazimika kukimbilia haraka sehemu ya hoteli ambapo aliona moto na kwenda kuwaita wenzake kwa kutoa msaada lakini tayari baadhi ya nyumba zilikuwa zimeshashika moto.

“Hatujui sababu za moto huu lakini tunasikia kuwa umeanzia katika hoteli ile ambayo ilikuwa na hitilafu huko jikoni lakini nyumba za wananchi ndio nyingi zimeungua” alisema Mati.

Hata hivyo baada ya kuitwa kikosi cha uokozi na kufika eneo la tukio hoteli hizo zilikuwa zimeshateketea pamoja na nyumba kadhaa ambazo zipo karibu na hoteli hizo.

Matukio ya kuungua moto hoteli za kitalii katika mikoa ya kusini na kaskazini yamekuwa yakishamiri katika kipindi cha jua kali ambapo inaelezwa kusababishwa na hitilafu za umeme na sababu nyengine ni kuwa makuti hushika moto haraka kutoka jikoni na kusababisha moto huo kusambaa haraka hasa nyakati za upepo mkali.
 
Back
Top Bottom