TataMadiba
JF-Expert Member
- Feb 7, 2014
- 9,866
- 5,742
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameahirisha kwa muda kwenda bungeni mjini Dodoma, kufuatia kuungua moto kwa mabweni ya Shule ya Sekondari Bwilingu.
Akizungumza shuleni hapo juzi jioni, Ridhiwani alisema katika vipaumbele vyake elimu ni mojawapo, hivyo hawezi kuondoka na kuwaacha wanafunzi waliounguliwa vifaa wakishika tama na wengine kushindwa kuhudhuria darasani kwa kukosa nguo na madaftari.
Alisema moto ni kitu cha dharura na kwa kutambua hivyo, amewasiliana na wadau mbalimbali na wahisani ambao wameamua kulivunja jengo lililoungua na kulijenga upya, kazi iliyoanza jana.
Ridhiwani alisema wamechangia misaada mbalimbali ikiwamo magodoro, vitanda, nguo, vyombo, madaftari, sabuni, vyandarua, mafuta, dawa ya mswaki na miswaki kwa wanafunzi hao.
“Unajua moto ulitokea usiku, sasa muda huo ina maana hao wanafunzi 65 walikuwa na kalamu moja na daftari moja au mawili wanajisomea darasani, vingine vyote vilikuwa mabwenini na vimeungua,” alisema.
“Kwa hiyo nimeona bora nishirikiane na wenzangu kutatua hili na nimetoa tayari magodoro 70 na mashuka 140 na nguo kadhaa waanze navyo, huku vingine vikifuata baadaye.”
Mkuu wa sekondari hiyo, Emmanuel Kahabi alisema pamoja na kupata maafa hayo, jana wanafunzi waliendelea na masomo kama kawaida kwa kuwa baada ya tukio, wadau mbalimbali walikutana na kuanza kutoa misaada.
Moto huo ulitokea Jumapili usiku na kuteketeza vifaa na mali zote zilizokuwa ndani wakati wanafunzi wakiwa kwenye masomo ya usiku madarasani.