Moto wa Katiba wazidi kuwaka , WAPINGA KUZINDULIWA 2011

JOHN MADIBA

JF-Expert Member
Jan 30, 2011
251
155
Moto wa Katiba wazidi kuwaka

• WADAU WAPINGA KUZINDULIWA 2011

SIKU chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza kuwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazinduliwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano mwaka 2014, Jukwaa la Katiba limeibuka na kupinga hatua hiyo.

Jukwaa hilo limesema mchakato wa upatikanaji wa katiba hiyo na mambo yaliyomo ndani ya muswada umefanywa siri na wenye masilahi kwa viongozi wa serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema kuwa kitendo cha Waziri Mkuu Pinda, kutoa kauli ya kukamilika Katiba mwaka 2014 kinatia shaka kutokana na muswada huo kutojadiliwa kwa kina na wananchi ambao ni wadau wakubwa wa Katiba.

Alisema ili kutoa nafasi kwa wananchi, serikali inatakiwa kuwa wazi katika maandilizi hayo na kitendo cha kutangaza kuwa itawasilisha bungeni muswada huo Agosti mwaka huu ni kufanya kazi ambayo hawajatumwa na Bunge.

Alibainisha kuwa Bunge liliitaka serikali kuuandaa upya muswada huo ikiwemo kuratibu maoni ya wananchi juu ya Katiba wanayoitaka.

“Katiba ni moyo wa taifa lakini kwa hili serikali inaonekana dhahiri imeshamaliza mchakato wote wa Katiba na sasa inajiandaa na sheria ya uzinduzi wake mwaka 2014, je, hii ndiyo kazi waliyotumwa na Bunge la kuratibu na kuchukua maoni ya wadau na wananchi?

“Kwa hili ni aibu na hakika tunawataka wabunge kukataa tena muswada huu kwani hauna masilahi kwa Watanzania zaidi ya viongozi wa juu wa serikali pekee.

“Itakuwa ni aibu kwa rais kutoa hati ya dharura ili kuwasilisha muswada huu tena kwa mara ya pili na tunamuomba Rais Kikwete akatae kufanya hivyo kwa masilahi ya wananchi wote,” alisema na kuhoji Kibamba.

Alisema Jukwaa hilo linatambua kuwa serikali haikuagizwa kutafsiri na kuweka viraka katika muswada uliokataliwa zaidi lakini serikali imegoma kutangaza muswada huo katika Gazeti la Serikali ili wananchi waweze kuusoma na kuufahamu kwa kina.

Alisema usiri mkubwa uliopo sasa kuhusiana na kinachoendelea katika muswada wa mchakato wa Katiba uondelewe mara moja na kuitaka serikali kutoa tamko rasmi kama umekamilika au bado.

Kibamba, alisema ili kufikia lengo hilo ni lazima serikali itumie posho za wabunge hasa waliozikataa ili kutoa elimu kwa wananchi na hata kutoa matangazo kupitia vyombo vya habari mbalimbali nchini.

“Wananchi wanahitaji kupata nakala za muswada husika ili kuweza kuuchambua na kujadili kabla ya kutoa maoni yao kwa kamati ya Bunge, sasa serikali ichapishe na kutoa nakala kwa kila Mtanzania aliyeko Bara na Visiwani na si Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kufanya usiri na kugoma kutoa ushirikiano kwa kueleza nini kinachoendelea.

“Katika zoezi zima la kuandika Katiba mpya kusiwepo na udharura kwa sababu suala la Katiba haliwezi kuwa la dharura, Katiba ni kitu cha wazi kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo, hivyo mchakato ufanywe kwa utaratibu na umakini mkubwa wenye kutoa fursa pana,” alisema Kibamba.

Alisema kuwa mapendekezo yaliyokwisha kutolewa na wananchi na Jukwaa la Katiba Tanzania na kufanyiwa kazi na serikali kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya nchi ibara ya 8 ya katiba ya sasa, huku akionya kitendo cha kubeza maoni hayo ni dalili kwa serikali kupoteza usikivu.

Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Katiba alisema mchakato wa utoaji wa maoni ndio msingi wa kupata katiba bora hivyo ni vema michakato hiyo ifanyike kwa amani, usalama na utulivu ili kuepuka yaliyotokea awali hata kusababisha baadhi ya vyama kujaza watoto wadogo katika ukusanyaji wa maoni ya Katiba mpya.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma alipokuwa akifungua semina elekezi kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa iliyohusu mchakato wa kuelekea kuundwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kwa viongozi hao wa serikali.

Pinda alisema mchakato wa maandalizi ya kuandika Katiba mpya unatarajiwa kukamilika Aprili, 2014 na Katiba hiyo mpya inatarajiwa kuzinduliwa ifikapo Aprili 26, 2014 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Back
Top Bottom