Moto wa ajira sasa wafukuta Bandari

Gangi Longa

JF-Expert Member
Feb 5, 2010
275
135
17th February 10
Moto wa ajira sasa wafukuta Bandari

Mwandishi Wetu

Moto umeanza kufukuta katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini, (TPA), ambapo wafanyakazi wamemshutumu Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Mamlaka hiyo, Dk. Maimuna Mrisha kuwa amekuwa akiwaajiri ndugu zake katika nafasi mbalimbali hata kama hawana sifa katika kazi wanazopewa kuzisimamia.
Ndugu wanaodaiwa kuajiriwa na Dk. Maimuna ni wadogo zake ambao ni Masoud Mrisha, Neema Mrisha, Amina Mrisha na Fatuma Mrisha.
Dk. Maimuna alikiri kuwa hao ni wadogo zake lakini alisema wameajiriwa kwa kuwa wanasifa stahili na kwa juhudi zao binafsi na kwamba hakutia mkono wake kushinikiza waajiriwe.
Baaadhi ya wafanyakazi wa TPA , walidai kuwa Mkurugenzi huyo amekuwa akitumia upendeleo wa dhahiri kwa kuwapa ajira ndugu zake na kisha anatafuta wale wa kabila lake ambao huwa hawana sifa za kuajiriwa wala kupandishwa vyeo.
Wakizungumza kwa sharti kwamba majina yao yasitajwe gazetini, wafanyakazi hao walimwomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati suala hilo kabla hali haijawa mbaya ndani ya mamlaka hiyo na Bandari ya Dar es Salaam.
“Uozo na usimamizi mbovu katika ajira ni pale ambapo Mkurugenzi Mkuu amekuwa akimrudishia mara nyingi nyaraka za ajira na upandishaji vyeo wafanyakazi zenye udhaifu mkubwa kama vile kuchomekea majina ya ndugu zake au kuongeza sifa ambazo hawana ili tu wafanikiwe kuajiriwa ama kupandishwa cheo,” alisema mmoja wa wafanyakazi.
Walidai kuwa katika hali ya kawaida Mkurugenzi wa Utumishi ndiye anatakiwa awe chachu ya maendeleo na maslahi bora ya wafanyakazi lakini, Dk. Maimuna badala yake amekuwa kikwazo cha maslahi ya wafanyakazi.
Walidai kuwa kila mapendekezo yanapopelekwa kwake na wakurugenzi wenzake amekuwa akiyapuuza bila kutoa sababu yoyote ya kufanya hivyo.
“Wafanyakazi tunajiuliza hivi huyu Mkurugenzi Mkuu (DG) anaridhika na vitendo vya huyu Mkurugenzi wa Utumishi ambaye hana maadili ya uongozi? Je, ni kweli Ikulu imemuonya (DG) asimguse mama huyu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jana, Dk. Maimuna alisema hizo ni porojo tu za watu waliokosa vyeo kwa kutokujiendeleza kielimu.
Alisema yeye binafsi hahusiki hata chembe katika suala la ajira kwani inayohusika ni Kamati ya Nidhamu na Ajira yenye wajumbe 13.
Kamati hiyo inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraem Mgawe.
Dk. Maimuna alisema ndugu zake hao waliajiriwa kwa jitihada zao binafsi na hakuwahi kutoa mchango wowote ili waajiriwe.
“Mfano huyu mdogo wangu Masoud Mrisha, alianza hapa Bandari tangu mwaka 1997, nikiwa Junior Officer hapa, juzi juzi amepata promotion imekuwa nongwa, huyu aliajiriwa muda mrefu sana na baada ya kupata Sahahada yake ya Usimamizi wa Biashara na Utawala mwaka 2008 (UDSM) ndipo akapewa cheo cha uafisa operesheni,” alisema.
Alisisitiza kuwa masuala yote yanayohusu uteuzi na ajira za watumishi zinapitia katika kamati ya ajira na yeye hahusuki kwa namna yeyote na hata Mkurugenzi Mkuu hahusiki na ajira za watumishi.
Dk. Maimuna ambaye ana mwaka mmoja tangu ashike wadhifa huo, alisema hata mdogo wake mwingine Neema Mrisha aliajiriwa katika mamlaka hiyo kabla yeye hajawa Mkurugenzi.
Alisema Neema kabla ya kushika nafasi aliyonayo sasa alikuwa Idara ya Usalama lakini alijiendeleza katika chuo cha bandari na ndiyo sababu ameteuliwa kushika nafasi mpya aliyosomea.
“”TPA kwa sasa tuna zoezi la kuweka muundo mpya, sasa tunaweka vijana wapya na wasomi, wale wanaofanya kazi kwa mazoea na wasiojiendeleza wanapiga vita mabadiliko haya, lakini wanapaswa kujua utekelezaji wowote wa muundo mpya unazingatia kamati ya ajira inasema nini, si matakwa ya mtu binafsi, wazee wanakasirika wanasema mnatuletea vijana wanajua nini hawa,” alisema na kuongeza kuwa hata barua za kuajiriwa ama kuteuliwa zinaandikwa na kamati hiyo.
Aliongeza kuwa bodi imeuagiza uongozi wa TPA kutekeleza muundo mpya haraka iwezekanavyo hivyo mageuzi yanayofanyika yana baraka za bodi si uamuzi wa mtu binafsi.
Kuhusu Fatuma Mrisha, Dk. Maimuna alisema ana cheti cha juu cha Port Operations kinachomwezesha kufanya kazi aliyopewa sasa na yanayosemwa kuwa hana sifa ni majungu.
“Hapa bandarini si jambo la ajabu kukuta mtu anandugu zake zaidi ya saba wanafanya kazi hapa, lakini kama wanasifa za kuwawezesha kumudu majukumu yao yakila siku tatizo liko wapi? Alihoji.
Nafasi aliyopewa mdogo wake aitwaye, Masoud Mrisha, inaonyesha kuwa alipewa nafasi ya assistant operations officer TPGs 5 kwa majaribio kwa miezi sita kuanzia Juni 1, 2009.
Barua iliyoandikwa na aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi wa utumishi, Samuel Simpilu, ilisema Masoud amepewa nafasi hiyo na kamati ya ajira iliyoketi Mei 6, 2009 na kutoa maagizo hayo.
Barua nyingine inaonyesha kuwa kamati hiyo iliketi tena Desemba 2009 na kumthibitisha Masoud kuendelea kushika wadhifa wake baada ya muda wa miezi sita ya majaribio.
Ingawa moja ya sifa za kushika wadhifa huo ilikuwa mtu mwenye uzoefu wa miaka mitatu, Masoud alithibitishwa baada ya miezi sita yamajaribio, jambo lililozua manung'uniko kwa wafanyakazi wenye sifa hiyo.
Kuhusiana na mdogo wake mwingine aitwaye Neema Mrisha, inaonyesha kuwa kabla ya kuwa na nafasi ya sasa ya clerk A Officer TPDS 4 alikuwa kitengo cha usalama TPOS 2.
Taarifa zinaonyesha kuwa kamati ya ajira ilimpa nafasi hiyo mpya katika kikao kilichoketi Novemba 17, 2009.
Kuhusu Fatuma Mrisha, taarifa zinaonyesha kuwa awali alikuwa na nafasi ya Clerk TPGS 3 lakini kikao kilichoketi Novemba 17, 2009, kilimpa nafasi mpya na kuwa Clerk A TPGS 4.


NIPASHE
http://www.ippmedia.com/frontend/functions/print_article.php?l=13603
 
Back
Top Bottom