real G
JF-Expert Member
- Feb 7, 2013
- 5,227
- 5,292
Ujio wa watalii wengi wanaoingia mjini Moshi kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vya utalii, imegeuka shubiri kwa wamiliki wa hoteli, baada ya watalii kwenda kula kwenye vibanda vya mamantilie.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini watalii wengi wanaolala Moshi Mjini na maeneo ya jirani, hawali vyakula na vinywaji katika hoteli hizo.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, hoteli nyingi zimeishia kuona idadi kubwa ya watalii wanaolala katika hoteli hizo, lakini hawaoni wakitumia migahawa yao kwa ajili ya chakula.
Vyanzo hivyo vimedokeza hali hiyo inajitokeza baada ya watalii kugundua vyakula wanavyouziwa kwenye hoteli hizo ni ghali, wakati chakula kama hicho wanakipata mitaani kwa bei ya chini.
Mathalan, baadhi ya hoteli za kitalii, vyakula huuzwa kati ya dola nane za Marekani (Sh17,000 za Tanzania) hadi dola 20 za Marekani (Sh43,000), lakini wanapata chakula hicho mitaani kwa Sh5,000 hadi Sh6,000.
Pia, baadhi ya watalii wanakwenda kunywa pombe kwenye baa za mitaani, ambako bia huuzwa kati ya Sh2,000 na Sh4,000 wakati katika hoteli hizo huuzwa kati ya Sh4,000 na Sh8,000.
Mkurugenzi wa Hoteli ya Leopard ya mjini Moshi, Priscus Tarimo, alisema hali hiyo imechangiwa na hoteli nyingi kupika aina zile zile za vyakula ambavyo watalii wanavipata nchini kwao.
“Kosa kubwa ni kutoweka vyakula vya asili. Unapomuekea vyakula kama wanavyokula kwao halafu ukampigia kwa standard (viwango) vya chini moja kwa moja ataikimbia hoteli yako,” alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya King of Kilimanjaro Expedition, Shatiel Mhina, alisema tatizo ni hoteli kujikita kupika vyakula vya kizungu.
“Hao watalii wanakuja wakiwa na information (taarifa zote). Anakuambia anataka kula pilau au mtori au machalari (ndizi nyama) na atakuambia na bei ya huko mitaani. Hotelini hawapiki,” alisema.
Mamalishe Mwajuma Hamisi, alisema japo hafahamu Kiingereza, lakini watalii wanaofika kwenye kijiwe chake hutaka vyakula vya asili ambavyo havijawekwa kwenye friji muda mrefu.
Mfanyabiashara huyo alisema bei za vyakula vyake ni ya chini na kutolea mfano kuwa sahani moja ya pilau huuza kwa Sh2,000, bei ambazo watalii hao huzifurahia kuwa ni za chini tofauti na hoteli
Chanzo: Mwananchi