Moshi wa tumbaku usiwepo Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere

654

Senior Member
Feb 1, 2012
172
40
Wakuu,
Nimeguswa sana na makala ambayo imeonekana kwenye gazeti la Tanzania Daima leo iliyoandaliwa na Lucy Ngowi. Hii inahusiana na kampeni ya kuufanya Uwanja Wa Kimataifa wa JN kutokuwa na moshi wa sigara. Hoja yenewe iko wazi ila mwitikio wa Mkuu wa uwanja umenistua kiasi, naomba tuiangalie hii na kujadili itakapowezekana, mtanisaheme wakuu kwani sikuweza kuhariri, nawasilisha:
MEI 31 kila mwaka huwa ni Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani. Tarehe hii iliteuliwa na Shirika la Afya Duniani, kuuelimisha ulimwengu kuhusu janga na vifo vinavyozuilika, ambavyo husababishwa na matumizi ya tumbaku.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘zuia makampuni ya tumbaku kuingilia juhudi za kudhibiti matumizi ya tumbaku’.
Kama tujuavyo tumbaku ni chanzo kikubwa sana cha vifo vinavyozuilika duniani, huua watu takriban milioni sita kila mwaka. Pia moshi wa tumbaku huua takriban watu zaidi ya 600,000 ambao sio wavutaji.
Hapa nchini utafiti uliofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road 2008, ulidhihirisha kuwa asilimia 32 ya magonjwa yote ya saratani yanahusishwa moja kwa moja na matumizi ya tumbaku.
Na kwamba serikali hutumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa mwaka kujaribu kutibu wagonjwa wa saratani zinazosababishwa na tumbaku, hata hivi wengi wao hupoteza maisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku (TTCF), Lutgard Kagaruki, anasema muingiliano wa makampuni ya tumbaku ni tishio kubwa kuliko yote kwa mikakati ya kuokoa maisha iliyomo kwenye mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Katika kuadhimisha siku hiyo, chama cha TTCF kiliadhimisha siku ya kutotumia tumbaku duniani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Kagaruki anasema wamechagua eneo hilo kwa kuwa 2007 kwenye maadhimisho kama hayo duniani, TTCF na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), waliungana pamoja na kuadhimisha siku hiyo kwenye uwanja huo.
Anasema siku hiyo TAA ilivitangaza viwanja vyake vyote kutokuwa na moshi wa tumbaku, yaani ‘smoke-free airports’, ili kuboresha afya ya jamii, tangazo ambalo lilitekelezwa mara moja.
“Katika hali isiyotegemewa, makampuni ya tumbaku yamerudisha tena moshi wa tumbaku kwenye uwanja huu, kwa kuweka vibanda vya sigara za Camel vinavyouza aina mbalimbali za sigara, pia makampuni yametawanya vifaa vya kuhifadhi majivu ya sigara kona tofauti.
‘Hali hii imechochea ununuzi wa sigara na pia kuwafanya wavutaji kuvuta hovyo, wakiendelea kuhatarisha afya zao na za wale wasiovuta. Moshi wa tumbaku huua watu wasiovuta 600,000 kila mwaka duniani,” anasema.
Mkurugenzi huyo wa TTCF anaziomba mamlaka zinazohusika na viwanja vya ndege kuondoa vibanda vyote vya sigara aina ya Camel kwenye sehemu ya lango la Terminal II, meza ya wavutaji iliyowekwa mbele ya mgahawa wa Flamingo na sigara ziondolewe kwenye ‘menu’ ya vyakula kwenye mgahawa wa Flaming, kwani tumbaku si chakula bali ni sumu inayoangamiza binadamu.
Vile vile wanaomba lirudishwe tangazo la awali lililokuwa linatolewa kabla ya ndege kutua, linalozuia abiria kuvuta sigara kwenye ‘terminal building’ lirejeshwe, tofauti na wanavyotangaza sasa, kuwa abiria wanaruhusiwa kuvuta kwenye sehemu maalumu ya kuvutia ndani ya ‘terminal building’.
“Tunaomba hadhi ya zamani ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere ya kutokuwa na moshi wa tumbaku kwa asilimia 100 irudishwe,” anasema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere, Moses Malaki, anasema kuwa atazingatia maoni yaliyotolewa na kupitia upya mikataba ya wapangaji katika eneo hilo ambayo inahusiana na mabango ya sigara.
Pia anasema atafuatilia yote yaliyosemwa ili uwe uwanja wa ndege ambao watu hawavuti sigara kama ilivyo kwa viwanja vingine katika nchi za wenzetu.
Anatumia nafasi hiyo kuwakaribisha TTCF kwa ushauri wowote pale watakapoona wanatoka nje ya maagizo.
“Yote tumeyachukua sasa vita imeanza kwa wote watakaokiuka,” anasema mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa wamewaruhusu TTCF kuweka mabango yao bure bila malipo yanayozuia uvutaji wa tumbaku katika kiwanja hicho.
Wakati huohuo, Dk. Ayoub Magimba, ambaye alimwakilisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, anasema kuwa viwanda vinatumia juhudi za ziada kuhakikisha wanatoa matangazo ili bidhaa zao ziuzike.
Na kwamba udhibiti wa bidhaa za tumbaku unahitaji ushirikiano wa kimataifa.
Anasema hivi sasa wizara itakaa na taasisi husika kuangalia mambo yote yanayokwamisha jitihada hizo zisifanikiwe na kuyapatia ufumbuzi.
Anashauri kuwekwa kwa utaratibu wa kudhibiti uvutaji wa sigara katika viwanja vyote kwa kuwa nchi za wenzetu wamefanikiwa katika hilo.
Anatoa wito kwa jamii ishiriki ili kuelimisha madhara ya moshi wa tumbaku.
Awali alielezea baadhi ya madhara yatokanayo na utumiaji wa tumbaku kuwa ni nywele kunyonyoka, mtoto wa jicho, kukunjamana kwa ngozi, kutokusikia vizuri, kansa ya ngozi, meno kuonza na mapafu kushindwa kufanya kazi vizuri.
Vile vile mifupa kuwa laini, magonjwa ya moyo, vidonda vya tumbo, kubadilika rangi vidole, kansa ya kizazi na kuharibika kwa mimba, kupungua nguvu za kiume, ukurutu, kuziba kwa mishipa midogomidogo ya damu na kansa ya mapafu na viungo vingine.

 
Back
Top Bottom