Moshi wa EPA wafukuta upya

mwanaizaya

Senior Member
Apr 26, 2008
133
1
Patakuwa hapatoshi hapa bungeni
Moshi wa EPA wafukuta upya


Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango ambaye aliapa bungeni kwamba pesa iliyoliwa kwenye akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) isiporudi bungeni patakuwa hapakaliki, ameisumbua mno serikali ambayo inatakiwa kutoa taarifa ya pesa iliyokusanywa hadi sasa.

Hivi karibuni, Kilango aliibip serikali alipoulizwa swali bungeni akitaka kujua juhudi zinazofanyika kukusanya pesa hiyo ambayo serikali kwa kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya EPA, Johnson Mwanyika iliahidi kwamba itaendelea kukusanywa ambayo jumla yake ni shilingi bilioni 133.

Moshi wa EPA unafukuta tena bungeni hasa baada ya kamati ya Rais Jakaya Kikwete kukamilisha kazi yake huku watuhumiwa wakipita huku na kule kuona kama bungeni pataweza kukalika.

Habari kutoka bungeni zinaeleza kwamba serikali, pamoja na kwamba kazi ya kamati kuchunguza waliokula pesa hizo imekwishamalizika tangu mwanzoni mwa mwezi huu, inaona vigumu kutangaza kwa sababu bado kuna maswali mengi yanayohitajika kujibiwa kabla ya kufanya hivyo.

Kwanza haijaeleweka ni kiasi gani cha fedha hadi sasa kimekusanywa na kwa kutumia vigezo gani, Pili kuna utata wa hatua gani zichukuliwe kwa waliochota pesa hiyo kwa njia za kifisadi wakiwamo vigogo, wafanyabiashara, wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali na tatu fedha hiyo itapelekwa kwenye mfuko upi.

Utata huo unakuja kwa sababu hadi sasa serikali haijaweka wazi kama fedha hiyo ilikuwa ya wafanyabiashara kama alivyodai Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo au ilikuwa mali ya umma kama ambavyo Katibu Mkuu Kiongozi, Philemo Luhanjo alivyosema alipokuwa akisoma taarifa ya ulaji huo na kumfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa BoT, Daud Ballali.

Habari kutoka bungeni zinasema kuwa Anne Kilango, Dk Wilbroad Slaa, Zitto Kabwe na wabunge wengine machachari wamekamia kuona maswali yote hayo yanajibiwa vinginevyo wataiweka pabaya serikali ambayo nayo inajipanga kutafuta namna nzuri ya kutuliza kiu ya wabunge na Watanzania ambao wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa karibu.

Aliyekalia kuti kavu ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye wakati fulani aliwahi kusema kwamba pesa hiyo ni ya umma bila kufafanua lakini kwa kuwa ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni atatakiwa kuweka suala hilo sawa ili wananchi wajue yupi yuko sahihi, Luhanjo au Mkullo.

Pesa ya EPA iliwahi kuleta mzozo mdogo wakati fulani miezi mitatu iliyopita ambapo wabunge walitofautiana walipokuwa kwenye vikao vya kamati za bunge kabla ya mkutano wa bunge kuanza mjini Dodoma.

Wapo waliopendekeza kwamba pesa hiyo itakapokuwa imerudishwa ipelekwe kusaidia sekta ya elimu ambayo kwa muda mrefu imeachwa nyuma huku walimu wakikosa vitendea kazi na wanafunzi wengi nchini wakilazimika kukaa chini kwa kukosa madawati.

Wengine walitaka zipelekwe kwenye sekta ya nishati hususan kwenye umeme ili kuimarisha miundombinu kwenye umeme ambayo kwa muda mrefu imehujumiwa na vitendo vya ufisadi na kusababisha bei ya umeme kupanda na usumbufu kwa wateja wengi wa nishati hiyo nchini. Ni suala la kusubiri na kuona pesa hiyo itapelekwa kwenye mfuko gani ikibainika kuwa ilikuwa ya wafanyabiashara na siyo ya BoT.

Ballali alifariki dunia huku kukiwa na kashfa ya EPA ambayo ilianzia bungeni huku Mbunge wa Chadema Dk Wilbroad Slaa akimtuhumu Balali kwa kuidhinisha Sh.133 bilioni isivyo hali kwa makampuni 22 ya watu binafsi yakiwamo hewa.

Baada ya kelele nyingi ndani na nje ya bunge Balali alipelekwa nje kwa matibabu, lakini hakurejea nchini. Wiki kadhaa baadaye, Rais Kikwete alimfukuza kazi kwa ufisadi.

Rais Kikwete aliunda kamati ya kuchunguza fedha na mali za wenye makampuni hayo 22 mwenyekiti wa kamati hiyo akiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika. Kamati hiyo inatarajia kuwasilisha ripoti yake hivi karibuni.
 
Back
Top Bottom