Mohamad Mlamali Adam alivyomweleza Abdulwahid Sykes mwaka 1988

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
15,589
2,000
1621958434348.png


Siku moja nimepita ofisini kwa Bwana Ally Sykes na katika mazungumzo yetu akaniambia kuwa alikuwa siku ya pili anasafiri anakwenda London.

Palepale ikanijia fikra nimpe Bwana Ally makala yangu ambayo nilikuwa nimeandika kuhusu historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika aifikishe jarida la Afrika Events.

Hili lilikuwa gazeti lililokuwa likichapwa London na Mhariri Mkuu wake alikuwa Mohamed Mlamali Adam na waandishi wengi katika gazeti hili na wafanyakazi wake walikuwa vijana kutoka Zanzibar kama Ahmed Rajab na wengine - ‘’birds of a same feathers...’’ na wachangiaji walikuwa kama Prof. Ali Mazrui, Abdilatif Abdallah, Prof. Mohamed Hyder, Prof. Mohamed Bakari, Fuad Nahdi wote kutoka Mombasa, Prof. Haroub Othman, Prof. Hamza Njozi kutoka Dar es Salaam na waandishi wengine.

Africa Events lilikuwa gazeti la Waswahili ingawa likiandikwa kwa Kiingereza.

Uzuri wa mkusanyiko huu ni kuwa hawa wote hawakuwa ‘’fellow carpetbaggers,’’ wakiliandikia gazeti kwa mahaba makubwa kwani kwa mara ya kwanza tulikuwa tumepata gazeti letu wananchi wa Afrika ya Mashariki.

Kama kulikuwa na kasoro katika jarida hili ni kuwa likiendeshwa na hao ‘’birds of the same feathers.’’
Hii ikafanya jarida kwa baadhi ya watu lisionekane kama jarida la Watanzania wala jarida la Wazanzibari wala la watu wa Afrika ya Mashariki.

Lakini kama alivyosema William Shakespeare, ‘’What in a name?’’
Ukipenda, rangi ya paka ina umuhimu gani madhali paka anakamata panya?

Bwana Ally Sykes akaifikisha ile makala kwa Mlamali Adam na siku zile wengi tukiandika kwa mkono na mimi makala yangu ilimfikia Mlamali katika hali hiyo.

Nakumbuka ilikuwa haina hata kichwa cha habari.

Mlamali aliipa kichwa, ‘’In Praise of Ancestors,’’ na Mlamali ni ‘’wordsmith,’’ muhunzi wa kufua maneno na misemo sisi wanafunzi wake tukimjua mwalimu wetu Mlamali kwa utaalamu huu.

Makala hii Mlamali kwa mkono wake mwenyewe akaiandikia utangulizi na akaichapa.

Utangulizi wake ulikuwa huu:

''There is a large body of Tanzania’s political history which has the effect, if not the avowed goal, of writing down the role of Muslims in the fight for independence. Yet it is a fact that their enterprise were not only crucial but daringly imaginative. Names like Mzee Saadani Abdu Kandoro and the Sykes brothers: Abdu and the ever-youthful Ali come easily to mind.

In a forthcoming book, Mohamed Said concentrates on these forgotten founders, what follows is a chapter from his work.’’


Mlamali alikuwa ‘’marksman,’’ mlenga shabaha bingwa ambae kwenye sare yake ya jeshi ukosini anavaa alama ya mkasi medali makhsusi anayotunukiwa mwanajeshi mwenye shabaha kali ambae siku zote anapiga ‘’bull.’’

Si kama hakujua maneno aliyoandika hayatakiwi na kwa miaka imekuwa hivyo kiasi historia za hao aliowataja zilikuwa zimepotea hazipo tena katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.

Mlamali alikuwa anajua fika lakini nilikuwa nimemsogezea bango la kulenga shabaha na vidole vyake vilikuwa vinamuwasha kwa kutaka kuitumia bunduki yake.

Si Abdul wala si mdogo wake Ally na Saadan Abdul Kandoro walikuwa wanafahamika na kutambulika kama waasisi wa TANU na wapigania uhuru wa Tanganyika achilia mbali kutaja mchango wa Waislam.

Huu utangulizi alioandika ulikuwa utangulizi uliovunja mwiko mkubwa ambao wengi hawakutamalaki kuuvunja huo mwiko.

Utangulizi huu ndiyo uliomghadhibisha Dr. Mayanja Kiwanuka kutoka CCM Dodoma akarudisha majibu makali sana lakini majibu yale yalielekezwa kwa mwandishi wa makala ile si kwa Mlamali mhariri wa gazeti.

Majibu ya makala yangu yalikuwa makali yaliyojaa kejeli na vitisho.

Jarida lile la mwezi March/April 1988 lilikusanywa lote nakala chache sana ziliwahi kuuzwa kabla kwa kifupi wasomaji walikosa nakala ya mwezi huo.

Mlamali alikuwa kanifungulia mlango wa uandishi na watu kunifahamu na pia kufahamu historia ambayo tayari ilikuwa imeshaanza kupotea kwa kupotezwa kwani kuanzia hapo Mlamali akawa anachapa kila makala niliyokuwa nampelekea.

Nami nikawa na kazi moja tu.
Kusoma kila alichoandika Mlamali na kuiga staili yake.

Kwa wale wanaoijua kalamu ya Mlamali hawawezi kukosa kuiona alama yake kwangu mimi ninavyojitahidi kutabaruku na mwalimu wangu kwa kugeza staili yake bila mafanikio makubwa kwani Mlamali alikuwa gwiji umahiri wake wa lugha ya Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza ulikuwa ukimfanya akiandika moja ya lugha kati ya hizo tatu utastaladha.

Lakini kabla ya utangulizi huu alioniandikia Mlamali kabla aliandika maneno kama haya kama utangulizi katika makala, ‘’Hero or Humbug,’’ aliyoandika katika kifo cha Sheikh Thabit Kombo:

‘’The death of Thabit Kombo reminds one of other old grand venerable founding fathers of the ruling party in Tanzania. The good Samatitan John Rupia whose property was later nationalised. The nice cheerful Mzee Sampat who toiled for measly wages and died a poor man. The Sweet Abdul Sykes who risked his job as Market Master under colonial government in order to set up the party. And others. They have passed away, their dedication and love of country not quite fully requited. Thabit, however, has all along had it good. Neither his power and reputation nor his immense wealth were ever assailed. How did he do it?’’

(Africa Events October 1986)


Mlamali alikuwa mshambuliaji hodari mwepesi wa kupokea pasi na kuelekeza mashuti golini.

Angalia alivyoitoa kutoka kusikojulikana historia ya Thabit Kombo na alivyoipenyeza katika historia ya TANU kiasi msomaji anajiuliza hii ni makala au ni taazia ya Thabit Kombo?

Kwa ufundi mkubwa sana makala ile ilikuwa mfano wa ufupisho ‘’absract,’’ ikieleza historia nzima ya Zanzibar kabla na baada ya mapinduzi.

Ikieleza raha na karaha zilizokuwako nyakati zile. Makala hii msomaji ukimaliza kuisoma lazima utashusha roho. Hakika mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964 yalikuja na mengi.

Kwangu mimi hii ni taazia na inanikumbusha taazia aliyoandika Erika Fiah mwaka wa 1940 baada ya kifo cha Martin Kayamba ambae kama Thabit Kombo alikuwa jirani ya milango ya watawala lakini yeye kuwapo kule hakukumnufaisha yeyote zaidi ya yeye mwenyewe na kuongeza machungu kwa wale waliodhani kuwa yeye angekuwa mkombozi wao.

Ajabu kuwa baada ya nusu karne ya taazia ya Fiah, Mlamali anaandika maneno yaliyofanana na maneno ya Fiah kama vile Mlamali na Fiah ni wanafunzi wawili watukutu, wezi wa mtihani waliochunguliana majibu ya maswali ya mtihani darasani.

Hakika historia hujirudia lakini bado hubakia kuwa historia.

Msomaji hebu msikilize tena Mlamali anavyozungumza kupitia kalamu yake.
Mlamali anaanza kama hadithi kichwa cha tahariri kinasema, ’The Old Man of the Forest.’’:

‘’All know him, who once were avid readers of a thousand – and – one – nights’ fables. He was a man of unaccountable years, his eyes laden with so many crow – feet as to drive to despair all but the most ardent face – lifter. He had a cavernous orifice where the mouth should have been.’’

(Africa Events December 1987).


Usitafsiri ukautoa ladha mchuzi.
Ukifanya hivyo utaondoa utamu wote.

Acha soma kama ilivyoandikwa kwa Kizungu na mwalimu wangu bingwa wa ung’eng’e na pia lugha ya Kiarabu.

Mlamali anawazungumza viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania madaraka ambao kawatumbukiza ndani ya hadithi ya Sindbad Baharia na safari zake saba, Sinbad akiwa kambeba Mzee wa Porini aliyemkaba shingo sawasawa asiyetaka kuteremka mabegani kwake ije jua ije mvua.

Hapo Mlamali kachaganya, ‘’satire,’’ na ukweli wa siasa za Afrika.

Lakini ukipita katikati ya mistari ya Mlamali utagundua kuna mengi anayozungumza ni kuliko hayo yaliyo machoni pako kwenye kurasa za jarida.

Kwa uandishi huu Mlamali aliwaudhi viongozi wengi ambao walijiona katika kurasa za kila alichoandika ndani ya jarida la Africa Events lakini hawakuwa na la kufanya. Huyu ndiye mwalimu wangu miye Mohamed Mlamali Adam.

Sasa baada ya mashambulizi na vitisho vile kutoka Dodoma Mlamali akanipa nafasi ya mimi kujibu yale niliyoshutumiwa kuwa nilikuwa nimepotosha historia ya TANU.

Mwezi September katika kumbukumbu ya ya miaka 20 ya kifo cha Abdul Sykes Mlamali alichapa makala yangu katika ukurasa ‘’column,’’ ‘’Once Upon a Time,’’ ‘’Founder of a Political Movement: Abdulwahid K. Sykes (1924 – 1968).’’

Makala hii ilisisimua wasomaji wengi sana kwa kuwa ilikuja na mengi ambayo hayakuwa yanajulikana katika uasisi wa chama cha TANU.

Wasiomjua Abdulwahid Sykes wakawa wanauliza waliomjua, ‘’Nani huyu Abdulwahid Sykes mbona historia yake inaingiliana na historia ya Julius Nyerere?’’

Mbali ya maswali ya pembeni hakuna kutoka Dodoma aliyegusa makala ile.

Hii ndiyo makala iliyomtoa machozi Mzee Ahmed Rashad Ali alipoisoma kisha siku ya Eid tukakutana Msikiti wa Kitumbini kwenye sala ya Eid akanikumbatia kunipongeza kwa makala ya rafiki yake huku akibubujikwa na machozi kwani nilikuwa nimemkumbusha kipenzi chake na mengi katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika ambayo yeye akiwa mtangazaji wa Radio Free Africa ikitangaza matangazo yako kutoka Cairo katika miaka ya 1950.

Rashad alikuwa akifanyia propaganda kulielezea bara la Afrika lilivyokuwa chini ya ukoloni. Mlamali alikuwa kila kukicha akichapa makala zangu na kwa kufanya hivyo kujenga jina langu na wasomaji wangu wakiniona njiani wataniuliza, ‘’Vipi Mohamed mwezi huu tutegemee kitu gani katika Africa Events?’’

Ilikuwa Ahmed Rajab ndiye aliyenipokea London na kuwa mwenyeji wangu.

Nilitoka Dar es Salaam nikiwa na barua kwa Mlamali iliyoandikwa na Mwanadiplomasia Ahmed Maulid ambae ndiye aliyenijulisha kwa Ahmed Rajab alipokuja Dar es Salaam na tukakutana nyumbani kwake Masaki.

Nilikuwa namfahamu Ahmed Rajab kwa kumsoma na kumsikia kwenye radio ya BBC Idhaa ya Kiswahili nakumbuka tulikuwa sote tumealikwa kwa Ahmed Maulid.

Mwanadiplomasia huyu alikuwa rafiki yangu na jirani yangu tukizungumza mengi katika siasa na historia ya Tanganyika na Zanzibar.

Ahmed Rajab siku ile alikuwa kaongozana na marehemu Ali Said mmoja wa vijana wa mrengo wa kushoto kutoka visiwani.

Nilifahamiana na watu wengi sana kupitia kwa Ahmed Maulid na kitu kimoja ni kuwa kila mtu aliyenifahamisha basi akawa rafiki ndugu kuanzia Ahmed Rajab hadi Salim Himid aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa visiwa vya Ngadzija na sasa anaishi uhamishoni katika mji wa Paris nchini Ufaransa.

Salim kila akija Dar es Salaam lazima atanitafuta na mimi nimemtembelea jijini Paris miaka michache iliyopita.

Hivi ndivyo nilivyokuja kujuana na Ahmed Rajab na Ahmed akanifikisha kuonana na mwalimu wangu uso kwa macho kwenye uradi nyumbani kwa Sheikh Mohamed Abubakar High Bennet, Mwanasayansi wa Kizanzibari katika taaluma ya Fizikia ya Nuklia ngazi ya kimataifa.

Nilipokwenda kumuaga Sheikh Aboud Maalim kuwa nakwenda Uingereza alinambia nijitahidi wenyeji wangu wanifikishe nikaonane na Sheikh Mohamed Abubakar.

Sikuuliza sababu ya msisitizo huu adabu ilikuwa inanizuia ndiyo mila zetu zilivyotuelekeza. Nilizijua sifa zake kutoka kwa Ahmed Rajab hata kabla sijakutananae na ikasadifu kuwa ni nyumbani kwa Sheikh Mohamed Abubakar ndipo nilipokutana na mwalimu wangu wa masafa marefu Mohamed Mlamali Adam.

Wakati huo Mlamali alikuwa hayupo tena Africa Events.

Lakini furaha yangu ilikamilika siku Ahmed Rajab aliponichukua BBC Idhaaa ya Kiswahili na kwa mipango yake nikapewa fursa ya kuandika na kufanya kipindi ambacho Mlamali alikuwa akikifanya kila juma, ‘’Barua Kutoka London.’’

Mimi kwa kuwa nilikuwa napita njia London kuelekea Glasgow Scotland kipindi changu nilikifanya katika studio za BBC Glasgow na anuani yake ikawa, ‘’Barua Kutoka Glasgow,’’ na kwa hakika sikuwa na lolote ndani ya ile studio ila kumuiga mwalimu wangu Mlamali nikiweka mguu wangu pale ulipobandua wake huku nimeshika kanzu na koti lake kwa nyuma nikiogopa kuteleza na kuanguka.

Allah amweke mahali pema Mohamed Mlamali Adam mtu ambae Allah alimpa vipaji vingi na yeye akavitumia kwa faida ya umma na nchi yake Zanzibar aliyoipenda sana inagawa alihajiri tangu mwaka wa 1968 na kutokukanyaga tena ila mapenzi yake palipozikwa kitovu chake yalimzunguka hadi kufariki.

Tunamuomba Muumba ampokee mja wake huyu na amjalie kati ya wale watakayoipata Janatul Firdaws, Amin.

8 Oktoba 2019
 

Do santos

JF-Expert Member
Feb 7, 2011
590
500
Mohamed Said
Shukrani sana kwa makala nzuri na tamu.

Nimekumbuka sana kipindi cha 'Barua kutoka London'.

Ingaww nilikua kijana mdogo lakini nilipenda sana kusikiliza kipindi hicho cha BBC, hasa namna zile barua zilivyokua na maneno matamu ya Kiswahili yaliwekwa.

Ilikua inanogesha na kupendeza sana. Hivi vile vipindi vinaweza kupatikana rekodi zake?
 

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
15,589
2,000
Mohamed Said
Shukrani sana kwa makala nzuri na tamu.

Nimekumbuka sana kipindi cha 'Barua kutoka London'.

Ingaww nilikua kijana mdogo lakini nilipenda sana kusikiliza kipindi hicho cha BBC, hasa namna zile barua zilivyokua na maneno matamu ya Kiswahili yaliwekwa.

Ilikua inanogesha na kupendeza sana. Hivi vile vipindi vinaweza kupatikana rekodi zake?
Do Santos,
Sina hakika.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom