‘Mo’ Dewji kuiteka EAC kwa uwekezaji

Majs

JF-Expert Member
Dec 21, 2012
229
485
MFANYABIASHARA maarufu wa Tanzania ambaye ni bilionea kijana zaidi barani Afrika, Mohammed `Mo’ Dewji anayemiliki kampuni ya MohammedEnterprises Tanzania Limited (MeTL) Group, amepania kuiteka Afrika Mashariki kibiashara.

Mbali ya kuwa amekwishawekeza katika nchi 12 Afrika, jicho la uwekezaji la Dewji kwa sasa limelenga zaidi Afrika Mashariki, amesema lina soko kubwa la wastani wa watu milioni 160, lakini pia lina fursa za kila aina zinazoruhusu ukuaji kibiashara.

Akizungumza na HabariLEO, Dewji ambaye kampuni yake imejikita katika sekta ya viwanda, kilimo, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa, uuzaji nishati za bidhaa za petroli ambavyo kwa pamoja vimeifanya MeTL iwe taasisi kubwa na ya kwanza binafsi, inayoongozwa kwa kutoa ajira nchini kutokana na kuajiri watu 28,000, akisema penye nia pana njia. “Mipango ni mingi, na ninaona mwanga mbele. Kufikia mwaka 2025, dhamira ni kuifanya MeTL iwe na kuongeza mapato na kufikia Dola za Marekanibilioni 5 (Sh trilioni 10.05) kwa mwaka.

Na katika ajira, tunataka tuajiri watu 100,000,” anasema Dewji (pichani) mwenye utajiri wa Dola za Marekani bilioni 1.14 (Sh trilioni 2.4). Amezitaja nchi alizokusudia kufanya uwekezaji mkubwa kuwa ni Burundi, Rwanda na Uganda kwa upande wa Afrika Mashariki, lakini pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Msumbiji na Zambia. “Kuwekeza katika nchi hizi tumeona kunalipa,” alisema Dewji ambaye kampuni yake inauza chai katika mnada wa zao hilo Mombasa huku akisema wanatarajia pia kujenga kiwanda cha kusindika nafaka nchini humo.

Aidha, amesema MeTL inakusudia kujenga kiwanda cha nguo na sabuni ya unga huko Ethiopia. Anasema viwanda vya nguo ni eneo muhimu la uwekezaji, akitolea mfano nchi za Tanzania, Ethiopia, Zambia na Msumbiji zenye pamba nyingi. “Lakini unahitaji umeme wa uhakika. Umeme ni ghali sana, tunaangalia uwezekano wa kuzalisha umeme kwa ajili ya viwanda vyetu vya nguo.

Nina uhakika hili linawezekana Tanzania na Msumbiji, angalau kwa kuanzia kwa sababu tayari kuna gesi,” anasema bilionea huyo. Aidha, kwa Tanzania, amesema anakusudia kuongeza vituo vya usambazaji wa bidhaa za kampuni hiyo, kwa sasa akisema vipo zaidi ya 100 na magari zaidi ya 2,000. “Tuna mtandao mpana wa usambazaji nchi nzima pengine kuliko kampuni nyingine yoyote,” alisema na kuongeza kuwa, miundombinu ya usafirishaji ikiboreshwa, lakini pia huduma katika Bandari ya Dar es Salaam zikiendelea kuboreshwa, kuna uwezekano mkubwa wa kutimiza ndoto za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania ipige hatua kwa kasi kuelekea uchumi wa kati.

CHANZO: Habari Leo
 
Back
Top Bottom