Mnyika: Nitawahamasisha wakazi wa Goba kuandamana kudai maji

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Mnyika(50).jpg

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika


Sakata la ukosefu wa huduma ya maji katika Kata ya Goba jijini Dar es Salaam limechukua sura mpya, baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kutangaza kuwahamasisha wapiga kura wake waandamane hadi ofisi za Manispa ya Kinondoni.

Mnyika amesema tatizo la maji katika eneo la Goba, linatokana na hujuma zinazofanywa na watendaji wa ngazi mbalimbali zikiwemo za Manispaa na kwamba hivi sasa wananchi wamekosa uvumilivu.

“Matatizo ya maji katika Kata ya Goba ni matokeo ya udhaifu wa watendaji katika ngazi mbalimbali na natoa wito kwa mamlaka zinazowasimamia watendaji hao kuchukua hatua stahiki na kutoa taarifa kwa wananchi katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa,” alisema.

Alifafanua kuwa matatizo ya maji katika Kata ya Goba yanafahamika kwa mamlaka zote husika kuanzia Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na vyombo vya dola kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2011, lakini hatua kamili hazijachukuliwa.

“Katika kipindi cha wiki mbili, huduma ya maji isiporudishwa kwenye Kata ya Goba, nitatangaza mgogoro na Manispaa ya Kinondoni pamoja na mamlaka nyingine husika na kuwaunganisha wananchi kuchukua hatua watakazoona zinafaa,” alisema.

Alisema amefikia hatua hiyo ya kuwahamisisha wananchi kuandamana baada ya njia zote za kawaida kupitia vikao na mawasiliano ya kiofisi kushindwa kutokana na kukwamishwa na uzembe, hujuma, urasimu na udhaifu wa kiutendaji katika ngazi mbalimbali.

Katika taarifa yake jana, Mnyika alisema Oktoba 24, mwaka jana, aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kutoa wito wa kuchukua hatua za dharura kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji lakini udhaifu wa kiutendaji umefanya hatua ziwe za kusuasua.

Wakati Mnyika akitoa taarifa ya kuwahamisha wananchi hao kuandamana, kuna taarifa kuwa pampu ya kusukuma maji kutoka Tangibovu kwenda Goba yenye thamani ya zaidi Sh. milioni 50, imepasuka na hivyo kuondoa matumaini ya wananchi hao kupata huduma hiyo kwa sasa.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom