Mnyika awaomba wananchi walete matatizo yao kwake

AMARIDONG

JF-Expert Member
Jun 24, 2010
2,502
180
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika, amewataka wakazi wa Kata ya Goba kuandika barua rasmi ya matatizo yanayowakabili ili aanze kuyashughulikia.
Miongoni mwa matatizo yanayowakabili wakazi wa kata hiyo ni ukosefu wa maji, umeme na miundombinu mibovu.
Hayo aliyasema juzi jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali katika shule tatu ambazo wanafunzi walihitimu mafunzo ya awali za Mount Moriah, Anazaki na Kings.
Alisema wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa kata hiyo kuwa akishinda atahakikisha anatatua kero hizo na amewaomba kuandika barua rasmi ya matatizo yanayowakabili ili aanze kuyashughulikia.
Alisema kukosekana kwa umeme na maji kunachangia kurudisha nyuma shughuli za kimaendeleo na kuongeza kuwa akishapata barua hiyo ataanza kufuatilia katika mamlaka husika ili kero hizo ziweze kutatuliwa.
Mnyika pia aliweka jiwe la msingi katika shule ya Kings kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi kutokana na kero ya usafiri iliyopo katika Jiji la Dar es Salaam. Alifafanua kuwa ujenzi wa mabweni ukikamilika, kutawasaidia wanafunzi wa shule hiyo kupata muda wa kutosha wa kujisomea.
Mnyika alitoa wito kwa wazazi waweze kutoa ushirikiano katika ujenzi wa mabweni ili watoto waweze kusoma vizuri na katika mazingira bora.
Wakati huo huo, uongozi wa Shule ya Msingi na awali ya Mount Moriah, umeiomba serikali kushughulikia kero ya maji na miundombinu ambayo imekuwa ni kikwazo kikuu katika maendeleo ya shule hiyo.
Akisoma risala kwa niaba ya Mkuu wa Shule hiyo, Josephat Joseph, alisema shule hiyo inakabiliwa na tatizo la maji hivyo wameiomba serikali kushughulikia tatizo hilo.
Alisema wenye shule binafsi wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutozwa gharama kubwa ya ushuru wa vibao wanavyoweka barabarani.
Alifafanua pia shule binafsi zinakabiliwa na ushindani mkali wa kukubalika katika jamii juu ya kiwango cha elimu bora wanachofundisha.
Jumla ya watoto 20 wamehitimu mafunzo ya awali katika shule ya Mount Moriah.
 
Back
Top Bottom