Mkutano wa Sullivan na kisa cha Mzee Meko

Fidel80

JF-Expert Member
May 3, 2008
21,947
4,444
Lula wa Ndali-Mwananzela Juni 18, 2008

Ninachotaka kusema ni kuwa mkutano wa Sullivan uliofanyika mapema mwezi huu na kuuzwa kwa Watanzania kuwa “Ni mkutano wa nafasi ya pekee ya maisha” kimsingi ulikuwa ni mkutano ambao umetutapeli Watanzania mchana kweupe huku tunashangilia! Siyo tu kututapeli bali pia kutufanya tubakie na matambala tambala kwenye mifuko yetu huku fedha yetu ikiwa imechukuliwa si kwa kuibwa kama walivyofanya watu wa EPA bali kwa kuitoa wenyewe kwa hiari tukitarajia vitu vizuri.

Vinginevyo utaweza vipi kuelezea mkutano ambao kuwaalika watu wa Sullivan kuja nchini mwetu ilitubidi tulipe ada ya kuwa wenyeji? Nchi ambazo tayari zimekuwa mwenyeji baadhi yao zimelipa hadi Dola milioni 3 kuwakaribisha kina Andrew Young na wenzake kwenye “Mkutano wa Sullivan”. Habari ambazo nazisikia kutoka sehemu za uhakika sana zinasema kuwa hata Serikali yetu ilitoa ada ya kuwaalika Sullivan! Kama hili ni kweli (na nina sababu kubwa ya kuamini kuwa ndivyo) basi tutakuwa tumeingizwa mjini kwa kuuziwa mbuzi kwenye gunia na tulipofika nyumbani kulifungua tukakuta gogo na nyasi tu!

Kama hatukutapelewa unaweza vipi mtu kuelezea jinsi Serikali ilivyojitahidi kushawishi wafanyabiashara wadogo wadogo kujiandikisha ili wapate nafasi ya kushiriki maonyesho haya? Ninaamini Serikali ilifanya hivyo ikiamini kuwa wale Wamarekani Weusi watakaokuja watakuwa ni watu wenye fedha na hawatasita kuzitumia kununua bidhaa zetu na hivyo kuwapa utajiri wajasiriamali wetu na kuchochoea uchumi wetu.

Wizara ya Viwanda na Masoko ilitoa waraka ambao ulielezea kwa kina suala la mkutano wa Sullivan. Ilipofikia kwenye suala la wajasiriamali wadogowadogo wizara hiyo ilisema hivi “Wajasiriamali wadogo wana nafasi ya kushiriki kwa kufanya maonyesho na kuuza bidhaa za Kitanzania wakati wa mkutano huo katika maeneo yatakayoandaliwa. Fursa hiyo itumike kushawishi wanunuzi wa nje kuweza kupata biashara kubwa zaidi na hata kufanya ubia wa uwekezaji kwa miradi ya kazi hizo”

Na waraka huo ukatoa wito kwa wafanyabiashara wote wakubwa na wadogo kuwa “Watanzania wote na hasa wafanyabiashara wakubwa na wajasiriamali wadogo wanahimizwa kuchangamkia fursa hii na kuitumia ipasavyo. Serikali kwa upande wake imejipanga kuhakikisha kuwa mkutano huu unaleta matunda yaliyokusudiwa.”

Ni kutokana na rai hiyo ambayo ilipigiwa debe na viongozi mbalimbali ndipo wajasiriamali wadogo wadogo wakiamini kuwa Serikali yao kweli itahakikisha mkutano huu unaleta matunda yaliyokusudiwa wakajiorodhesha na wengi wao wakafunga safari kutoka mikoani, na kulipa ada kidogo na hatimaye kwenda Arusha kusubiri bahati yao.

Mkutano ukaja, wajumbe wakaja, vikao vikafanyika na ndugu zetu wajasiriamali kule Njiro wakawa wanasubiri kuona msururu wa magari na wafanyabiashara kwenda kununua bidhaa zao mbalimbali. Ikawa jiiii!! Hakuna cha wanunuzi wala watoto wake wanunuzi. Ni hadi mwisho wa mkutano ambapo wafanyabiashara walipoanza kulalamika ndipo Waziri wa Viwanda, Mary Nagu alipotokea na inasemekana alikoromewa ikabidi aondoke; mwisho Rais Jakaya Kikwete akaja naye kutembelea na hatimaye kina Andrew Young mwenyewe na wenzake wakaja na kutembeza tudola twao.

Matokeo yake wajasiriamali wetu wakahisi wametapeliwa (kitu ambacho ni kweli). Lakini walitapeliwa si kwa sababu hawakushtukia mambo yaliyoyanaendelea, bali waliweka imani yao kwa Serikali yao kuwa haiwezi kuwa sehemu ya utapeli. Bahati mbaya sana haya mambo ya kuamini Serikali kwa kila isemalo ndiyo iliwafikisha hapa. Kwanini walimuamini Andrew Young na Carl Masters? Je, Wamarekani hawa Weusi wana rekodi ya kuonewa wivu? Je, rais msitaafu Olusegun Obasanjo alipokuja alikuwa kwa ajili ya mkutano au kwa ajili ya urafiki wake na Andrew Young? Hivi Chris Tucker alikuja kuwekeza kwenye vitu gani?

Kilichofanywa na ambacho kimekuwa kikifanywa na kina Andrew Young ni utapeli wa nchi za Kiafrika kwa sababu ya ngozi yetu tu. Kwamba Wazungu walipokuja na ngozi nyeupe tunaweza kuwashtukia, lakini sasa wakiwatumia jamaa zao kina Andrew Young ambao ni “Weusi wenzetu” basi tutafungua milango hadi ya chumbani!

Balozi Young pamoja na mafanikio yake mengi katika harakati za kisiasa na haki za raia ana rekodi yenye madoa linapokuja suala la makampuni ya kimataifa na jinsi ambavyo amekuwa akitumika na wakubwa kusafisha walipochafua. Wengi tunaomfahamu tunakumbuka jinsi alivyojaribu kuisafisha kampuni ya Nike na kushindwa baada ya ripoti yake kuonyeshwa kuwa haikuwa na msingi wowote katika ukweli zaidi ya kutumia jina lake na hadhi yake wakati wa mwamko wa haki za Watu Weusi. Ni huyu huyu Young ambaye alilazimishwa kujiuzulu kutoka kwenye Bodi ya kampuni kubwa kabisa yenye kutoa ajira kwa Wamarekani ya Walmart, baada ya kutoa maneno yaliyoonyesha uzandiki dhidi ya Waarabu!

Lakini zaidi ya yote ni uhusiano wake na Obasanjo ambao ulimfanya Andrew Young kuonekana kana kwamba ni kibaraka wa makampuni makubwa ya mafuta. Amekuwa na mahusiano na makampuni mengi ya mafuta na madini na miongoni mwao ni kampuni ya Barrick Gold ambayo ina uhusiano wa karibu na yule mwekezaji mwingine James Sinclair. Kampuni yake ya Goodworks International ndiyo imekuwa ikitumiwa kumtengenezea fedha ya ajabu kwa migongo ya Waafrika. Kampuni yake hiyo iliajiriwa na ECOWAS (Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi) kuiwakilisha katika mahusiano na Waafrika walioko nje ya Bara lao kwa malipo ya dola 500,000. Vyanzo vya kuaminika vinaonyesha pia kuwa kampuni hiyo hiyo imeajiriwa na Serikali yetu kwa malipo ya dola 350,000 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanasafisha jina la nchi yetu linapochafuliwa katika vyombo vya habari vya Marekani. Ndiyo hatukuambiwa kuhusu hilo.

Kama hatukutapeliwa tutawezaje kuelezea malipo ya vyombo vya habari ambavyo vilijitokeza kuripoti kuhusu mkutano huu na kutumia gharama kubwa ya kutuma waandishi, vyombo n.k kwenye jambo ambalo umaarufu wake uliishia Tanzania? Hakuna chombo chochote kikubwa cha kimataifa ambacho kilifuatilia mkutano wa Sullivan. Hata wakati Barack Obama amemshinda Seneta Hillary Clinton na kuwa mgombea mtarajiwa wa chama cha Democrat Mchungaji Jesse Jackson aliyekuwa Tanzania wakati ule alizungumza na shirika la ABC kuelezea furaha ya kuona Obama anakuwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuweza kusimamishwa na chama chake kugombea Urais. Cha kushangaza ni kuwa hata ABC hawakutaja kuwa Jackson alikuwa Tanzania kwenye mkutano wa Sullivan!

Kama killichofanyika si utapeli wa wazi kwa nini hao kina Andrew Young na wenzake na makampuni yao ambao wanataka kujenga daraja na Afrika wasianze kujenga daraja na Waafrika walioko huko huko Marekani? Kama kweli wao wanataka kutoa msaada wa aina yoyote ni kwa kiasi gani wamefanya hivyo kwa Waafrika walioko Marekani na watu Weusi wenzao wanaohangaika kila kukicha na hali ngumu ya Marekani. Hawa wanaokuja kuzungumzia miundo mbinu ya huku Afrika ni kwa kiasi gani wametoa michango katika matatizo ya miundo mbinu ya nchi yao?

Hivi kweli mkutano kama wa Sullivan ulitarajiwa kufanya mjadala wa kina wa matatizo yetu? Hivi ni kitu gani kilichosemwa na Sullivan ambacho kisingeweza kusemwa na wasomi wetu UDSM, Mzumbe, Sokoine n.k ? Ni jambo gani ambalo lilijadiliwa kwenye mkutano huo ambao Watanzania wenyewe tulishindwa kulijadili bila kutumia mabilioni ya shilingi? Hivi wazo la kuwakamata viongozi mafisadi na kuwafikisha kizimbani kama lilivyosemwa na Obasanjo na kupigiwa makofi ni wazo jipya kabisa kusikika Tanzania? Hivi kuboresha elimu yetu ili kuweza kuhimili ushindani wa soko la ajira la kimataifa ni wazo ambalo linahitaji Mmarekani kutuambia?

Kama lengo ni kubadilishana mawazo tu na ndugu zetu hawa kwa nini basi tusiende kufanyia huko huko kwao na Serikali ingejitahidi kuwasaidia wajasiriamali wetu kwenda huko huko Marekani kujifunza mambo ambayo Sullivan inafanya kuinua wajasiriamali wa Marekani? Watanzania tumeingizwa mjini na kina Andrew Young na tukikubali hilo ndio utakuwa mwanzo wa mabadiliko ya kifikra, ndipo tutakapotambua kweli kuwa hakuna mtu kutoka Marekani kwingineko, ambaye atatutatulia matatizo yetu; ndipo tutakapotambua kuwa hatuna “mjomba” Ulaya ambaye atakuja na ushauri wa matatizo yetu. Na kwa hakika hata tufanye mikutano elfu moja ya Sullivani na hata tuwaalike kina Sinclair na Andrew Young kwa mamia, matatizo ya Watanzania mwisho wake yatatuliwa na Watanzania wenyewe.

Rafiki zetu wa nje wanaweza kutusaidia, wanaweza kutushauri wanaweza kutupa mwanga lakini mwishowe ni sisi wenyewe tutakaotakiwa kusimamia sheria zetu, ni sisi tutatakiwa kuchagua viongozi wazuri, na ni sisi tutakaotakiwa kuwawajibisha. Anayefikiri vinginevyo itabidi tumpeleke katika nchi ya wagagagigikoo akakae na Bulicheka na mkewe Lisabeti kwenye nyumba ya juu ya mnazi!

Je, tunaweza kuona kweli faida ya mkutano huu? Je, ni kweli kuwa mkutano huu ulikuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania? Je ni kweli kuwa wafanyabiashara wetu wakubwa walipata dili kubwa na za nguvu, vipi kuhusu wafanyabiashara wadogo wadogo?

Kilichonikera mimi zaidi ni jinsi gani Serikali mkoani Arusha inakejeli akili za Watanzania pale Mkuu wa Mkoa Isidore Shirima alipodai kuwa “Kamati ya maandilizi ilitakiwa kuwahamasisha mapema wajasiriamali hawa… lengo lao kubwa lilitakiwa kuwa kujifunza kupitia wageni, namna ya kuendesha biashara zao kimataifa na si kuja kuuza kama walivyotarajia” Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi. Shirima alikuwa wapi wakati wote wa maandalizi? Kama hakukuwa na maonyesho kwa nini basi Katibu Mkuu wa Viwanda na Masoko kuwataka watu waje na kupata vibanda vya kufanyia maonyesho yao na kuuza bidhaa?

Pamoja na hayo yote, Watanzania walitapeliwa mchana kweupe kwa kuamini kuwa kundi lililokuja lilikuwa ni “wafanyabiashara wakubwa” ambao wangeweza kusababisha mamilioni ya dola kuingia nchini. Ushahidi ni kuwa kundi la hao Wamarekani waliokuja ni wale waliodunduliza fedha zao kwa muda mrefu ili waje kutembelea bara la asili yao. Hawakuja na fedha nyingi za kutumbua kama wengi walivyotarajia. Ushahidi ni pale walipojaribu kufanya ile harambee na matokeo yake kushindwa kukusanya hata Shs. 70 millioni! Si wangejifunza toka CCM walivyoweza kufanya kweli Butiama au jinsi wabunge wetu walivyoweza kukusanya papo kwa papo karibu nusu bilioni?

Hata hivyo, kuna watu walitengeneza pesa na hao sina ugomvi nao kwa sababu “walichangamkia tenda”. Hawa ni wale waliokuwa na magari ya kifahari ambayo yalikodishwa na Serikali na wenye hoteli na nyumba za wageni.

Kwa hawa biashara haikuwa mbaya na isingeweza kuwa mbaya kwani ujanja ni kupata si kuwahi. Lakini kama lengo lilikuwa ni kuleta mwamko fulani wa kibiashara kwa wafanyabiashara wetu au kusababisha mambo ya miundo mbinu kubadilika hukumu yangu ni kuwa Serikali na waandaji wetu wamefeli na kupata sifuri tena yenye masikio!

Lakini kwa ndugu zetu wajasiriamali wadogo wadogo, Serikali ifanye kitendo cha kiungwana kwa kuwarejeshea gharama zao walizotumia na hasara waliyoingia kule Arusha, kwani ni kutokana na uzembe, na makosa ya Serikali kujaribu kumuuza mbuzi kwenye gunia huku wakiwataka wajasiriamali waandae meza ya chakula huku wameshikilia matonge mkononi wakisubiri kulumangia kwa samaki wa picha!

Na haitakuwa vibaya sana kama Serikali itaomba radhi kuwa mkutano haukugeuka jinsi ulivyotarajiwa, na huo utaitwa uungwana. Jinsi mkutano huu ulivyokwenda na yaliyotokea liwe funzo kwa viongozi wetu kuwa si kila king’aacho ni dhahabu, na huu mtindo wa kuwaleta marafiki zetu kwa kisingizio cha wafanyabiashara umefika wakati ukome. Binafsi sitaki tena kusikia lolote wala chochote kuhusu Sullivan Summit, Andrew Young au Goodwork International. Naamini si lolote wala chochote isipokuwa kundi la wajanja Weusi ambao bila haya wanashiriki kulinyonya Bara letu kama wakoloni Weupe walivyofanya kabla yao.

Na huu mtindo wa kupapatikia watu kwa vile ni Wamarekani iko siku utatutokea puani na ndipo tutakapojua kuwa Tanzania bado itajengwa na Watanzania wenyewe na si kina Andrew Young na James Sinclair na washirika wao wa makampuni makubwa ya kimataifa yanayopita duniani kukomba wanachokomba, kuchuma wasichopanda, na kula wasichopika. Mambo haya ya kufanywa sisi watoto na wajukuu wa mzee Meko mwenzenu yamenichosha na kunishinda.


source;http://www.raiamwema.co.tz/08/06/18/lula.php
 
Tulimlipa Andrew Young dola laki tatu na ushee ili atuteee kwenye vyombo vya habari vya Marekani? Balozi wetu yuko wapi?
 
Back
Top Bottom