Kuelekea 2025 Mkutano wa Kitaifa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja wa Sheria za Uchaguzi zilizopitishwa kuelekea Chaguzi za 2024/2025

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,994
12,346
TCD kuwakutanisha wadau kutafakari Sheria za Uchaguzi zilizopitishwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Mkutano huu wa Kitaifa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria za Uchaguzi zilizopitishwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wa Mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa Mwaka 2025.


Miongoni mwa watakaopata fursa ya kuzungumza wafuatao:
  • Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot
  • Balozi wa Marekani, Mh. Michael Battle
  • Msajili wa vyama vya Siasa, Mh.Jaji Francis Mutungi
  • Mwenyekiti wa TCD, Prof. Ibraim Lipumba
  • Dr. Rasul Minja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  • Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga
  • Mwakilishi wa wadau wa maendeleo (DPs), Hodan Adou
Mjadala huo unafanyikia kwenye Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) unaongozwa na Deus Kibamba ambaye ni Mkurugenzi TCIB.

UPDATES

Michael Battle, Balozi wa Marekani

Kupiga kura so kwamba ni Haki pekee bali ni wajibu, pia kupiga kura sio tu ni nafasi bali ni jukumu. Uwepo wa Demokrasia imara unasaidia kutimiza mahitaji ya Wananchi ikiwemo Afya, Elimu na ongezeko la ajira

Kama alivyowahi kusema Maxence Melo, mmoja wa Waanzilishi wa JamiiForums, namnukuu Demokrasia inahusisha kuwapa Wananchi taarifa sahihi, Uhuru wa Kujieleza ni Uti wa Mgongo wa Demokrasia.


Nilifurahishwa kuona maandamano ya amani yakifanyika Dar es Salaam mnamo Aprili 21, 2024 ikiwa ni sehemu ya kwanza ya maandamano ya amani kufanyika baada ya muda mrefu na baada ya hapo kuna maandamano mengine yaliyofuata

Kuelekea katika uchaguzi wa Mwaka 2024 na 2025 inawezekana yakatokea maandamano mengi zaidi ya ilivyo wakati huu

Vyama vya siasa vimefanya maandamano kwa amani na vimeshirikiana na Serikali, ni jambo zuri kuwa watu wanatambua uhuru wa kujieleza ambao unajumuisha pia haki ya kuandamana

Marekani inatambua na kuthamini mchango wa Rais Samia katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki kwa kuzingatia Falsafa yake ya 4R

Didier Chassot, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania
Uwisi na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu uliojengwa kwa kuaminiana na kuheshimiana.

Tunashiriki katika kuthamini pamoja jinsi demokrasia inavyoboresha maisha ya watu. Ibara ya 8 ya katiba ya Tanzania inathibitisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayozingatia misingi ya demokrasia na haki za kijamii na kwamba "wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii."

Nianze kwa kuipongeza serikali ya Rais Samia kwa hatua mbalimbali alizochukua tangu alipoingia madarakani kuboresha demokrasia na kurejesha nyuma mwenendo uliokuwa unashangaza. Demokrasia ni mapambano (struggle) ambapo watu hupata matumaini na maendeleo lakini mara nyingine hukumbana na vikwazo. Hata hivyo, bado demokrasia ni ‘force’ isiyoepukika kwa ukuaji wa taifa na ustawi wa raia wake.

Chassot.jpg

Demokrasia ni ngumu na yenye utata; siyo njia moja iliyonyooka. Kama ilivyosemwa, ni soko lenye shughuli nyingi (lively marketplace) la mawazo ambapo sauti tofauti hukutana, maoni yanagongana, na makubaliano huunda nguvu ambayo inaweza kusababisha kishindo cha sauti zinazopingana.

Uchaguzi unaweza kuleta fujo, mabishano na mizozo, na matokeo yake yanaweza kutuachia na mamlaka zilizogawanyika, huku ushirika wa vyama vya siasa (coalitions) ukibaki pamoja ili tuweze, licha ya changamoto zote hizo, kuendelea mbele. Lakini nafasi hiyo ya watu kujadiliana ndiyo moyo wa demokrasia.

Demokrasia ni makubaliano kati ya serikali, wananchi wanaotawaliwa, na wawakilishi wao. Inatupa haki ya kusema, kukusanyika, na kutofautiana kwa maoni. Inatupa uwezo wa kuunda mustakabali wetu, kuwajibisha viongozi, na kutamani zaidi ya hali zetu. Demokrasia ni ardhi yenye rutuba ambapo ubunifu unakua, ambapo wasanii huchora na kuimba maono yao kwa uhuru, na biashara zinafanikiwa.

Katika nchi za karibu na mbali, tunashuhudia mwenendo wenye wasiwasi. Tawala za kimabavuzinaibuka na kuzidisha ukandamizaji, kudhibiti upinzani, kuziba midomo ya vyombo vya habari, na kuwatenga wapinzani. Wanaojifanya wanasimamia maslahi ya wananchi wanapotosha na kuwagawanya wananchi, wakichafua mazingira ya mazungumzo ya kidemokrasia.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwnyekiti - TCD
Profesa mmoja wa Uchumi, Amartya Sen, wa India, alisema kwenye andiko lake kuwa Democracy is universal value – yaani demokrasia ni tunu ya wananchi wote, ni tunu ya mataifa yote. Siyo jambo la magharibi, siyo jambo la mashariki, ni jambo la ulimwengu mzima. Na Mwalimu Nyerere alikuwa akisisitiza kwamba hata kwenye vijiji vya kiasili, palikuwa na demokrasia watu wanafanya maamuzi chini ya mti. Na akaeleza tulikuwa na kasoro moja kuwa ushiriki wa wanawake ulikuwa mdogo n ani lazima tulirekebishe hilo.

Lipumba.jpg

Suala la kuunga mkono demokrasia ni suala la ambalo sote tunapaswa kuliunga mkono. Kwa mara ya kwanza, Tanzania imeanzisha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi. Katika mkutano huu tutajadili sheria hii kama inakidhi matarajio ya wadau.

Serikali haikuona umuhimu wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba, badala yake ikapeleka bungeni miswada mitatu ya mabadiliko ya Sheria za uchaguzi

Nilikuwa mwanafunzi wa hapa chuo kikuu miaka ya 1970’s. Wakati huomtulikuwa tunakutana kufanya ujenzi wa ujamaa, kupambana na ubeberu na ukombozi wa Afrika. Sasa tunahitaji kujadili ujenzi wa Demokraisia na kujenga uchumi shirikishi utakaowatoa Watanzania katika dimbwi la umasikini.

Sheria ambayo imepitishwa inasema kwamba jukumu la Tume Huru ya Uchaguzi ni kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sasa hili likoje kwamba Sheria tayari imepitishiwa lakini Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utasimamiwa na TAMISEMI, labda pana maelezo ya namna gani katika kipindi hiki cha mpito.

Isihaka Mchinjita, M/Mwenyekiti (Tanzania Bara) ACT-Wazalendo
Zipo changamoto kubwa kama 3 ambazo ACT Wazalendo tunaziona. Kwanza, ni sheria hizi kutungwa bila kufanya mabadiliko madogo ya Katiba kwasababu Sheria zetu za uchguzi ni reflection ya katiba yetu. Unapokwenda kutunga sheria ya Tume Huriu ya Uchaguzi, Sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge, unajikuta kati mapendekezo ambayo tumetoka nayo kwenye kikosi kazi au mapendekezo kadhaa unashindwa kuyafanyia kazi.

Kwa mfano, tulipendekeza matokeo ya uchsguzi wa Rais yawe na uwezo wa kuhojiwa. Kwa sababu Katiba imeprotect hilo, hatuwezi kuwa na sheria ambayo inaweza kuja na resolution kwenye hilo eneo. Kwahiyo, kukosekana kwa minimum reforms ya katiba yetu kama mapendekezo ya muda mfupi kuelekea kwenye mabadiliko makubwa ya katiba yetu yote kwa ujumla, kama tulivyokubaliana Watanzania wote kwenye Tume ya Jaji Warioba, ni jambo linalofanya sheria zetu hizi ziwe na mapungufu.

Eneo la pili ni namna ambavyo zinakwenda kufanya kazi. Imeelezwa hapa na Mwenyekiti wetu wa TCD kwamba tuna Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ambayo hii sheria nikama vile umepewa mkate upande wa kulia huku ikiwa inatarajiwa kuwa mkate kabla huu haujafika mdomoni, hapa katikati kuna haramia atauchukua. Msingi wa mjadala ulikuwa ni kwenye uchaguzi wa 2024 tunakwenda kwenye uchaguzi wa 2025. Unapokuwa na sheria ambayo yale ambayo mmefanyia jitihada kuwa myafanyie mabadiliko, yameweka kizuizi cha kuanza kufanya kazi kwenye uchaguzi unaofuata amablo ni jambo linalorejesha kwenya hofu ileile kuwa hamjaanza nayo. Kwahiyo nadahani hili ni eneo ambalo limekuwa na changamoto kubwa.


Ndiyo maana ACT Wazalendo tulitoa wito kuwa, kwakuwa sheria haiondoshi wajumbe wa Tume ya Uchaguzi, ni vema wakajiondoa kwa kujiuzulu kwasababu hatuwezi kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kwakuwa na wajumbe ambao hawakupitia mchakato wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, ambayo pamoja na madhaifu kadhaa yanayoweza kuonekana, anagalau ilianza kuweka msingi wa namna gani tunaweza kupata wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Kwahiyo tutoe wito kuwa ni vema wajumbe hawa wakajiuzulu kama sheria imeendelea kuwalinda, lakini pia kutafuta namna bora ya kurejesha yale matumaini ambayo yalijengwa kutokea maoni ya wadau kwenye kikosi kazi nah apo ambapo tumefikia.

Pia, suala la Serikali za mitaa. Chaguzi za Serikali za Mitaa ni jambo ambalo liliharibika sana mwaka 2019. Wagombea wa upinzani karibia 89% waliondoshwa katika uchaguzi. Vyama vingi wakati ule tulilazimika kujitoa kwakuw tuliona kama vyama vyetu vimeondoshwa basi hakuna sababu ya kushiriki.

Prof. Palamagamba Kabudi
Ni fursa nzuri kuwa na aina hii ya mkutano. Ukiangalia historia ya nchi yetu toka uchaguzi wa mwaka 1958 mpaka sasa naona kuna hatua kubwa imepigwa. Taifa hili limevuka nyakati ngumu kwa sababu, mwisho wa siku Tanzania ni muhimu kuliko sisi sote. Uwepo wa Tanzania imara, uwepo wa Tanzania yenye amani, uwepo wa Tanzania yenye umoja, uwepo wa Tanzania inayoangalia maslahi na matlaba (aspirations) ya Watanzania ni jambo muhimu sana.

Katika vipindi vyote hivi, yamechkuliwa maamuzi ambayo labda ni chanya na mengine yamekuwa hasi. Uchaguzi wa ’58 haukuwa mwepesi, ndiyo maana unaitwa uamuzi wa busara. Masharti ya mtu kuwa na sifa ya kuandikishwa na sifa ya kugombea, moja ilikuwa ni lugha ya Kiingereza. Nilikuwa nasoma kitabu cha Joan Wickens; anasema alikuwa na kazi ya kumfundisha Bi. Titi Mohamed Kiingereza.

Utaona katika nyakati zote utaona kuna mambo yameboreshwa na kuna mabo yamekwenda yakarudi nyuma. Na kama mwanataaluma, taifa lolote katika historiaya Maisha yake lazima lina ups and downs. Cha msingi ni mafunzo gani tunachukua kutokana na mambo yaliyotokea. Kwa mataifa yote. Hii ni kwakuwa kila taifa lin a tajiriba (experience) yake. Na inawezekana isiwe sahihi kabisa kuchukua tajiriba ya nchi nyingine.

Nimekaa Ujerumanikwa kipindi kirefu kabisa. Ujerumani hawana tume ya uchaguzi. Uchaguzi wao unasimamiwa na mtakwimu mkuu. Mpaka leo, uchaguzi wa serikali za mitaa India unasimamiwa na district magistrate. Na mpaka leo Tume ya Uchaguzi ya India inasimamiwa na watumishi waandamizi wa serikali.

Na sisi tutengeneze tajiriba yetu kulingana na muktadha wetu, tamaduni zetu, changamoto zetu, hali halisi yetu.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti CHADEMA
Katika vikao vyetu vya maridhiano tulivyokaa mwaka mzima tumejadili masuala ya uchaguzi kwa kina, hata wenzetu wa TCD, Kikosi Kazi, Asasi za Kiraia na Taasisi za Dini nao walijadili pia, lakini kwasababu kuna kiburi kwa wenzetu wa CCM hawayataki mambo hayo

Hawataki mabadiliko hayo, tusilishane maneno malainilaini, wenzetu upande wa CCM hawataki mabadiliko, wao ndio wanufaika wa mapungufu ya Sheria za uchaguzi.

Hata tungefanya maboresho ya Sheria kiasi gani kama upande wa pili hakuna utashi wa Kisiasa na Utashi wa Kisiasa itakuwa ni kazi bure, tutakuwa tunapoteza muda

Yapo mambo mengi yanafanyika katika Utawala huu. Tunaweza kulaumu na kukiri kuwa utawala na Awamu iliopita ulifanya makosa katika Uchaguzi wa 2019 na 2020

Mbowe.jpeg

Uchaguzi mdogo wote uliofuata baada ya Mwaka 2020 mpaka leo sisi CHADEMA tulikataa kushiriki kwa kuwa tulikuwa tunaona ni uhuni tu. Walioshiriki wenzetu wa ACT na wengineo wanaweza kuelezea machungu waliyopitia

Yale tuliyokuwa tunalalamikia Mwaka 2019 na 2020 mpaka leo 2024 yanaendelea kufanyika licha ya Wadau wote kuishauri Serikali ya CCM ambayo imekuwa haisikii, yenyewe inapenda kufanya yale ambayo inakuwa ni faida kwao

Kama hatutaacha tabia ya kudanganyana hatutapiga hatua, matendo yanazungumza zaidi ya maneno. Uchaguzi tunaoutaka ili ueze kuwa huru na haki nakubali kwamba ni mchakato, ambapo unaanzia katika uhuru wa kufanya kazi za Siasa

Uhuru wa kufanya vyama vya Siasa kujijenga hilo naweza kusema kwa kiwango kikubwa nafasi imefunguka, nikisema nafasi haijafunguka Hapana, hilo limefunguka

Kama hatutakuwa na umakini wa kusimamia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura basi tutakuwa tumepoteza vita.

Daftari la Kura tulilonalo leo lilichezea sana Mwaka 2019 na 2020 na Mamlaka, kuliingizwa wapiga kura vivuli kwa wingi na ushahidi upo, tunapaswa kujiuliza Wadau, tutaliboresha au kuanza upya?

Tuna tatizo la kwenda mbele bila kuangalia tulijikwaa wapi na kwa staili gani na nani alisababisha na hatua zilizochukua kurekebisha

Waliochafua uchaguzi uliopita ndio walewale waliopo katika mfumo na ndio haohao wanategemewa wakarekebishe mifumo, katika mazingira kama hayo tutajikuta tunarudi katika mazingira yaleyale ili watawala wabaki kwenye utawala na wageni wawe wageni

Maftaha Nachuma, M/Mwenyekiti CUF
Sisi kama CUF tumekuwa na matumaini sana na hizi 4R’s ambazo amekuwa akizungumza. Na Mh. Mbowe hapo amezungumza. Kwamba ni namna gani sasa Tanzania tunaenda kuponywa na uchafuzi wa kidemokrasia uliofanywa na wenzetu wa chama tawala (Serikali) mwaka 2019 na 2020.

Tumekuwa na mategemeo kuwa sheria hizi 3 zingekuwa ni mwarobaini kwa yale yaliyotokea mwaka 2019 na 2020. Bado tunaonakuna yaleyale ambayo tumekuwa tukiyazungumza kuwa hayakutendwa kwa usahihi. Kwa mfano sheria inaonesha kuwa Wakurugenzi bado wataendelea kuwa custodians wa daftari la kudumu la wapiga kura. Na tuliona 2019 wa kurugenzi waliongeza majina hewa mwaka 2020

Lakini pia, wakurugenzi wengine walikuwa wanarudufisha majina ya wana CCM. Wanachama wa CCM walikuwa wanapewa vitambulisho viwili, vitatu ili waweze kupiga kura mara kadhaa.

Joseph Selasini, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi
Uchaguzi umekuwa kama mnada, Mgombea mwenye fedha anapata nafasi kubwa, kijana mwenye sifa ya uongozi hata kama katoka chuo na anataka udiwani hali ilivyo ni ngumu kupata nafasi.

Hizi Sheria zinatakiwa kugusa matumizi ya fedha katika uchaguzi, tusipoangalia tunaweza kupata Wagombea ambao wamefadhiliwa na makundi ya kihuni.

Sheria ya Takrima imeongeza kiwango kikubwa cha Rushwa katika mchakato wa uchaguzi mbalimbali Nchini


Pia, soma muendelezo wa mjadala siku ya pili hapa: Mkutano wa Kitaifa kutafakari na kujenga uelewa juu ya Sheria za Uchaguzi zilizopitishwa kuelekea Chaguzi za 2024/2025 (siku ya pili)
 
Hujamuona Lipumba?
Nimemwona Mwenyekiti, na katoa neno la maana zaidi, ambalo najuwa hakuna jipya litakalofanyiwa kazi, kwani CCM tayari wanaelekea kwenye uchaguzi wasiokuwa na shaka juu yake kuushinda.

Mpira upo miguuni mwenu sasa hivi, sijui mtaucheza vipi. Sina hakika kama hata mazoezi mmefanya?
 
Vikao vya kupotezeana muda Ili kuhadaa wazungu, lakini hakuna lolote la maana litafanyiwa kazi. Bila machafuko ama mapinduzi ya kijeshi, hivyo vikao ni kama vikao vya walevi.
 
Wasiwasi Wangu ni kwamba,wanachodai wapinzani Kiko sawa kabisa katika mustakabali wa Nchi yetu. Sina hakika kama haya matakwa yao ya kisiasa yatakubaliwa kwa asilimia mia,hivyo ningeliendelea kuwaomba wawe wavumilivu waache jaziba.
 
Demokrasia ni mchakato wa muda mrefu,na haswa pale maslahi binafsi yanaposhindwa kukamilika.Hivyo ni wito Wangu kwa Wanasiasa na wadau wasiasa tuijenge Tanzania kwa njian ya maelewano.
 
Nimepitia baadhi ya Makala ya Viongozi wa vyama vya Siasa,nimegundua kunamapungufu jinsi ya uwasilishaji Hoja zao tunaposema Chama tawala wanakiburi hii kauli haina afya katika ujenzi wa Demokrasia Nchini Mwetu.Kwani kufanya hivyo nikuendelea kupanda chuki na kushidwwa kufikia mwafaka wa kitaifa wa kuijenga Tanzania Moja.
 
Back
Top Bottom