Mkutano wa JK, madaktari kimya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mkutano wa JK, madaktari kimya

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Mar 10, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 10, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Hakuna matokeo yaliyotangazwa
  [​IMG] Madaktari waahidi kuzungumza leo
  [​IMG] Mgomo waendelea hospitali nyingi  [​IMG]
  Rais Jakaya Kikwete


  Rais Jakaya Kikwete jana alikutana na madaktari Ikulu, jijini Dar es Salaam, kuzungumzia madai yao yaliyosababisha wagome kuhudumia wagonjwa, ikiwa ni awamu ya pili ya mgomo wao, huku madaktari hao wakidai kwamba, kikao hicho kimemalizika bila taarifa zozote rasmi kutolewa.
  Hii ni mara ya kwanza Rais Kikwete kuingilia kati tangu mgogoro wa madaktari uanze mwishoni mwa mwaka jana.
  Awali, Rais Kikwete alikuwa akutane jana na wazee wa mkoa wa Dar es Slaam, lakini mkutano huo haukuweza kufanyika kwa kile kilichoelewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais kuwa ni kutoa nafasi kwa Rais kufanya mashauriano zaidi na wadau mbalimbali kuhusu suala ambalo atalizungumzia kwenye mkutano wa wazee.
  “Mkutano huo umeahirishwa ili kutoa nafasi kwa Mheshimiwa Rais kufanya mashauriano zaidi na wadau mbali mbali kuhusu suala ambalo Mheshimiwa Rais atalizungumzia kwenye mkutano huo,” ilisema taarifa ya aya tatu kutoka Ikulu jana.
  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu, Peter Ilomo, aliliambia NIPASHE jana kuwa hadi saa 9.00 alasiri jana, Rais Kikwete na madaktari hao walikuwa wakiendelea na mazungumzo.
  “Mpaka sasa (saa 9.00 alasiri jana) wanaendelea kuzungumza,” alisema Ilomo.
  Hata hivyo, alisema kwa wakati huo asingeweza kuzungumza lolote kwa vile walikuwa hawajafikia mwafaka. “Akimaliza tutatoa taarifa,” alisema Ilomo.
  Alisema mazungumzo hayo yanalenga kuwekana sawa baada ya Rais Kikwete kusikiliza matatizo yanayolalamikiwa na madaktari.
  “Wanachokifanya ni kuwekana sawa. Madaktari wanataka nini na uwezo wa serikali ni kiasi gani,” alisema Ilomo.

  JK, MADAKTARI WASHINDWA KUAFIKIANA?
  Hata hiyo, habari zilizotufikia wakati tukienda mitamboni, zinaeleza kuwa hatma ya mgomo huo ulioanza Jumatano wiki hii, haijajulikana baada ya kikao hicho kati ya madaktari na Rais Kikwete kumalizika bila makubaliano yoyote kufikiwa.
  Kiasi cha madaktari sita wanaodhaniwa kuwa ni viongozi, walikutana na Rais Kikwete Ikulu, jijini Dar es Salaam jana kwa siku nzima, lakini kikao hicho kilimazika bila kutolewa taarifa yoyote kwa umma.
  Akizungumza na NIPASHE muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, alisema hakuna walichokubaliana na Rais Kikwete.
  Kuhusu walichozungumza na Rais Kikwete Ikulu, Dk. Ulimboka alisema jana jioni watakutana na madaktari na kujadiliana na kwamba leo watatoa tamko lao la pamoja.
  Akizungumzia amri ya mahakama iliyotolewa juzi ambayo inawataka kusitisha mgomo kwa maelezo kwamba ni batili na kurudi kazini, Dk. Ulimboka alisema kwa sasa (jana jioni) hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yote yatatolewa majibu leo.
  Mazungumzo hayo yamefanyika siku moja baada ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, kusitisha mgomo wa madaktari juzi usiku.

  KANDA KASKAZINI WATANGAZA MGOMO

  Chama cha Madaktari Kanda ya Kaskazini (Mati), kimetangaza rasmi mgomo wa madaktari na hatatoa huduma yoyote kwenye hospitali za mikoa ya kanda hiyo.
  Katibu wa Chama hicho, Dk. Lairumbe Silangei, alisema katika tamko lake kuwa wanaungana na wenzao kitaifa katika mgomo na kwamba madaktari wataendelea na shughuli nyingine na si kufanya kazi ya kuhudumia wagonjwa.
  “Sasa rasmi tumeanza mgomo. Kwa kila anayeitwa daktari hatafanya kazi yoyote ile hadi hapo tutakapopata maelekezo mengine kutoka kwa wenzetu,”alisema.
  Alisema wachache wanaoendelea na kazi ni wale ambao kwa imani za dini zao hawaruhusiwi kugoma kama mapadri, watawa na wale ambao ni raia kutoka nje ya nchi.
  Silangei alisema hawafurahii wagonjwa kuendelea kuumia na wengine kupoteza maisha kwa kukosa msaada wa madaktari, lakini akasema watarejea kazini serikali itakapotimiza madai yao ya msingi.
  “Tumekubaliana kuanza mgomo rasmi. Sasa hivi tunahamasishana na wenzetu ambao hawakuweza kufika kwenye vikao vyetu vilivyofanyika mfululizo tangu juzi,” alisema mmoja wa madaktari.
  Baada ya tangazo hilo, baadhi ya madaktari waliokuwa wameingia kazini jana, waliacha kazi na kwenda kupumzika, huku wagonjwa wakikosa huduma na nyingine zikitolewa na wanafunzi wa mwaka wa tano.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk. Moshi Ntabaye, alipotafutwa simu yake iliita bila majibu na alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo, Askofu. Dk. Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema yupo kwenye kikao.

  MADAKTARI 37 WAENDELEA KUGOMA
  Zaidi ya madaktari 37 wa mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma jana waliendelea na mgomo na kusababisha wagonjwa kukosa huduma.
  Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani, Dk. Zainab Chaula, alisema jana kuwa hali ni mbaya hospitalini hapo kutokana na madaktari wengi kugoma.
  Alisema licha ya madaktari hao kugoma, uongozi wa hospitali hiyo umejipanga kuhakikisha unatoa huduma kwa wagonjwa.
  Mmoja wa wagonjwa, Hassan Saidnn, alisema alifika hospitalini hapo jana asubuhi, lakini alishindwa kupata huduma kwa wakati.
  “Serikali inatakiwa kuchukua hatua mapema kabla tatizo hili halijawa sugu kwa sababu watu ambao tunaumia zaidi ni sisi ambao tupo kwenye hali ya chini na si wao,” alisema.
  Rebeca Simon alisema kutokana na kipato chao kuwa cha chini, wameshindwa kwenda kwenye hospitali binafsi na kukimbia kwenye hospitali ya mkoa.
  Alisema hospitali nyingi za binafsi huwa hazina vipimo vikubwa na vingi huwa vinapatikana kwenye hospitali kubwa za mkoa.

  IRINGA MGOMO BARIDI

  Hali bado si shwari katika baadhi ya hospitali za serikali za Mkoa wa Iringa kutokana na mgomo baridi na kuzorotesha utoaji wa huduma.
  Tangu mgomo wa madaktari ulipoanza Jumatano, madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa walifanya mgomo baridi.
  Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo aliliambia NIPASHE jana kuwa madaktari na wauguzi wanafika kazini na kurandaranda wodini, huku wengine wakitoa huduma kwa kusuasua.
  “Ni kweli hapa mgomo baridi upo kama kawaida. Watu wanakuja kazini, lakini wanazungukazunguka tu wodini na kutibu watu katika hali ya ucheleweshaji,” alisema.
  Aliongeza: “Hiyo ndiyo hali halisi. Lakini ukitaka kuongea na Mganga Mfawidhi, sasa hivi yuko chumba cha upasuaji na anaweza kupatikana baada ya saa nne kuanzia sasa.”
  Hospitali nyingine za serikali ambazo zimo katika hali isiyoeleweka kiutendaji kutokana na mgomo huo ni Kibena, Kituo Kikuu cha Afya katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Makambako, Mafinga na Hospitali ya Wilaya ya Kilolo ya Ilula.
  TANGA HUDUMA HOI
  Huduma za tiba bado zinasuasua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, (Bombo) na kuwalazimu baadhi ya watu kuwaondoa wagonjwa wao.
  Aidha, mgomo huo pia jana ulionekana kuvikumba vituo vya afya vya serikali baada ya madaktari na wauguzi kusaini daftari la mahudhurio bila ya kufanya kazi.
  Wananchi hao waliamua kuondoa wagonjwa wao kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosa huduma kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea katika hospitali za serikali kote nchini na hivyo kuzifanya baadhi ya wodi kubaki tupu.
  Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika hospitali za serikali, umebaini kuwa mgomo huo pia umeviathiri vituo vya afya vya Ngamiani na Makorora ambako hali ilikuwa tete na kuleta usumbufu kwa wagonjwa.
  Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wananchi hao walidai kuwa baadhi ya wagonjwa wamehamishiwa katika hospitali za binafsi kwa wale wenye uwezo wakati wasio na uwezo kifedha wamekwenda kwenye tiba asilia.
  “Sasa tusio na uwezo wa fedha tunakwenda kwa waganga wa tiba asili…tutafanya nini sasa,” alisema Salehe Abdulrahman, mkazi wa Mabawa, Tanga ambaye ni mmoja kati ya ndugu wenye wagonjwa katika Hospitali ya Bombo.
  Aidha, malalamiko kama hayo yametolewa na wagonjwa na ndugu katika vituo vya afya vya serikali ambako walikimbilia, wakidhani wangepata huduma huko.
  “Mimi natoka Bombo, hakuna huduma. Sasa nimekuja Ngamiani nikidhani hakuna mgomo. Mambo ni yaleyale….sisi ni watu wa kufa tu,” alilalamika Anna Joseph ambaye alidai kuwa mtoto wake wa miaka minne anasumbuliwa na homa ya manjano.
  Ramadhani Juma ambaye alikutwa katika kituo cha afya cha Makorora, alisema mgomo wa madaktari utasababisha vifo vingi kwani watu watakwenda kwa waganga asilia hata katika magonjwa ambayo hayahusiani na tiba hizo.

  WATANO MBEYA WAITII SERIKALI
  Ni madaktari watano tu kati ya 75 walioanza mgomo Jumatano wiki hii katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, ndio waliotii wito wa serikali uliowataka kurejea kazini, huku wengine 70 wakiendelea na mgomo.
  Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Omary Salehe, jana aliliambia NIPASHE kuwa licha ya serikali kutoa wito wa kuwataka madaktari waliogoma kurejea kazini, walio wengi wamekaidi agizo hilo na ni madaktari watano tu waliokubali kurudi kazini.
  Alisema kufuatia madaktari wengi kutoingia kazini kwa siku tatu mfululizo, hali ya utoaji wa huduma katika Hospitali hiyo ya Rufaa imeanza kutetereka na kudai kuwa endapo mgomo huo utaendelea hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
  “Madaktari watano pekee ndio waliorudi kazini mpaka sasa. Wengine wanaendelea na mgomo na sielewi ni lini watakubali kurudi kazini,” alisema Dk. Salehe.
  Alisema kwa sasa kazi inawawia ngumu madaktari bingwa 10 wanaoendelea na kazi kutokana na kutakiwa kuwasikiliza wagonjwa kuanzia katika hatua za awali wanapopokelewa hospitalini hapo mpaka kuwapatia matibabu, hali ambayo ni tofauti kama mgomo usingekuwapo kwani kazi nyingine za awali hufanywa na madaktari ambao wamegoma.
  NIPASHE ilitembelea hospitalini hapo jana na kushuhudia baadhi ya madaktari wakiwa wamejikusanya katika vikundi vidogo vidogo nje ya hospitali hiyo wakijadiliana kuhusiana na mgomo huo.
  Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutoandikwa gazetini, madaktari hao walisema wanasubiri tamko la Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), ambalo litatoa msimamo wao kama wanaamua kurudi kazini au kuendelea na mgomo.

  BUGANDO MAMBO MABAYA

  Mgomo wa madaktari bingwa bado unaendelea katika Hospitali ya Rufaa Bugando, ingawa madaktari hao wamegawanyika katika makundi mawili; wanaoendelea na kazi pamoja na kundi lingine ambalo limeshikilia msimamo wa kutoingia kazini hadi madai yao yatakapotekelezwa.
  Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa mgomo huo umeanza kusababisha baadhi ya wagonjwa wapya kwenda kutafuta matibabu katika hospitali binafsi jijini hapa.
  Baadhi ya madaktari hao waliliambia NIPASHE kwa nyakati tofauti kwamba hawako tayari kubadili msimamo, kwa kuogopa vitisho vinavyotolewa na serikali.
  “Sisi wataalamu bwana. Tena wenye taaluma ya udaktari na wala siyo watoto wadogo kwamba tutadanganywa kwa ahadi za kuletewa pipi na viongozi ama watendaji wa serikali. Kwa ufupi ni kwamba bado tunaendelea na mgomo hata kama serikali itaendelea kututisha,” alisema mmoja wao.

  AMRI YA MAHAKAMA YAPUUZWA

  Licha ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Jijini Dar es Salaam juzi kuwaamuru madaktari kusitisha mgomo na kurudi kazini kwa kuwa mgomo wao ni batili, wamepuuza amri hiyo na badala yake wameendeleza mgomo.
  Hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana iliendelea kusuasua hali iliyosababisha wagonjwa waliokuwa wakifika hospitalini hapo kurudi walikotoka, wakiwamo wale waliofikishwa katika kitengo cha dharura.
  Hali hiyo pia ilisababisha baadhi ya wagonjwa kuondolewa na ndugu zao na kupelekwa katika hospitali za binafsi ili kupatiwa matibabu.
  Stephen Peter, ambaye ni ndugu wa mgonjwa aliyelazwa katika wodi ya Mwaisela namba nane alionekana akimhamisha ndugu yake kutoka wodi hiyo na kumpeleka hospitali binafsi ya Regency.
  Baadhi ya wagonjwa waliozungumza na NIPASHE katika hospitali hiyo walisema walipokuwa wakifika mapokezi walikuwa wakirudishwa na kuelezwa kuwa wasubiri hadi Rais Kikwete atakapotoa tamko juu ya hatma ya mgomo huo.
  Katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), NIPASHE iliwahoji baadhi ya wagonjwa, akiwamo Richard Dickson, ambaye jana alitakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mguu katika taasisi hiyo.
  Alisema tangu jana asubuhi hakupata huduma yoyote, badala yake aliambiwa arudi hadi mgomo utakapomalizika.
  Mariam Michael kutoka mkoani Morogoro alisema siku ya tatu yuko jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata kliniki, lakini hajafanikiwa kuipata.

  MWANANYAMALA HUREE

  Wakati MNH kukiwa hivyo, huduma ya matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala jana iliendelea kutolewa kama kawaida, huku kukiwa na idadi ndogo ya wagonjwa waliofika kupata huduma.
  Katibu wa Afya wa Hospitali hiyo, Edwin Bisakala, alisema vitengo vyote hospitalini hapo jana vilikuwa vinafanya kazi, lakini kutokana na taarifa za mgomo, wananchi wamekuwa na hofu kufika kupatiwa matibabu.
  Madaktari wanaoendelea na kazi kulingana na ratiba zao kuwa ni madaktari wa kawaida 20, madaktari bingwa saba na madaktari wasaidizi 35 na kwamba wote walikuwa kazini kama kawaida.
  Alisema madaktari ambao wapo kwenye mafunzo kwa vitendo hospitalini hapo ni 51 na kati yao, 30 hawapo kazini bila ya taarifa zozote.


  Alisema mgomo umewaathiri wagonjwa wanaowapa rufaa kutoka katika hospitali hiyo kwa kuwa hawapokelewi MNH na badala yake wanarudishwa.


  NIPASHE ilitembelea katika wodi za wanawake, watoto pamoja na ile ya watoto waliozaliwa kabla ya siku zao na kushuhudia wahudumu wa afya wakiendelea na kazi zao kama kawaida.

  AMANA HALI MBAYA
  Hali ya utoaji wa huduma katika Hospitali ya Amana, Ilala, jijini Dar es Salaam, jana ilizidi kuwa mbaya kutokana na wagonjwa wengi kuonekana wakirudishwa majumbani au kuhamishiwa katika hospitali binafsi kutokana na madaktari kuendeleza mgomo.
  Kutokana na ukosekanaji wa huduma, viti vilionekana kuwa wazi, huku wagonjwa wengine wakilalamika kwa kukaa hospitalini hapo bila kupata huduma kwa muda mrefu huku wakiambiwa baadhi ya huduma zimesitishwa.
  Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Meshack Shimwela, alithibitisha kuwapo kwa hali mbaya ya utoaji wa huduma.
  Alisema amefanya jitihada za kutafuta madaktari wa ziada kutoka katika vituo vingine vya manispaa.
  Dk. Shimwela alisema madaktari walioko katika hospitali hiyo, ni 79, lakini kati ya hao 14 ndio walikuwa kazini hadi jana na kwamba alifanikiwa kupata madaktari kutoka sehemu tofauti.
  Hata hivyo, Dk. Shimwela alisema baadhi ya huduma katika hospitali hiyo zimesimamishwa, ikiwamo huduma ya kliniki zote.

  WAGONJWA WAKACHA TEMEKE
  Wagonjwa katika Hospitali ya Temeke ‘wamekacha’ ambapo waliojitikeza ni wale waliokuwa wakisubiri kupatiwa huduma katika kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD).
  Aidha, baadhi yao walilalamikia hudumu duni, huku madaktari wakiwa wamekaa ndani ya vyumba vyao bila kuwahudumia.
  Upendo Lukui, mkazi wa Yombo Kilakala, aliliambia NIPASHE kuwa alifika hospitalini hapo ili kupata matibabu, lakini amekuwa akizungushwa bila ya msaada wowote.
  Alisema alikwenda hospitalini hapo siku tano zilizopita na alipatiwa matibabu na kutakiwa kurudi tena jana, lakini jana alipofika mapokezi aliambiwa aende moja kwa moja kumuona daktari, lakini alipokwenda kwa daktari, alikataa kumpokea, badala yake alimwambia arudi mapokezi.
  Hata hivyo, upande wa huduma za vipimo vya X- ray, zilionekana zikiendelea kama kawaida ingawa wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma hiyo walikuwa wachache.
  Hali ilikuwa tofauti katika wodi za hospitali hiyo kwani wagonjwa waliolazwa walionyesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa, na waliiambia NIPASHE kuwa madaktari wamepita na kuwapa huduma ingawa madaktari hao hawakuwa kwenye sare zao kama ilivyozoeleka.
  Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, alisema Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Zaituni Mgaza, aliiomba manispaa kuwaongezea madaktari ili kuziba nafasi za waliopo kwenye mgomo na kufanikiwa kupata 12. Alisema madaktari hao walianza kufanya kazi tangu jana.
  Alisema madaktari hao wametoka katika zahanati za Vijibweni, Kigamboni, Mbagala Rangi Tatu, Yombo Vituka, Kizuiani, Buza, pamoja na kitengo cha kifua kikuu (TB) na Ukimwi.


  Imeandikiwa na Muhibu Said, Alipipi Gwamaka, Jimmy Mfuru, Sharifa Marira, Leonce Zimbandu, Samson Fridolin, Beatrice Shayo na Richard Makore, Dar; Jacqueline Massano na Ibrahim Joseph, Dodoma; Salome Kitomari, Moshi; Godfrey Mushi, Iringa; Dege Masoli,Tanga; Emmanuel Lengwa, Mbeya na Juma Ng’hoko, Mwanza.
  SOURCE: NIPASHE
   
 2. Boonabaana

  Boonabaana JF-Expert Member

  #2
  Mar 10, 2012
  Joined: Oct 22, 2011
  Messages: 227
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 33
  Ngoja tusubiri, labda mkuu wa kaya alipiga biti kali!
   
 3. Dark City

  Dark City JF-Expert Member

  #3
  Mar 10, 2012
  Joined: Oct 18, 2008
  Messages: 16,277
  Likes Received: 241
  Trophy Points: 160
  Katika mazingira ya technology kama tuliyonayo, ni jambo la kusikitisha kwamba mtu anaweza kuleta habari ambazo zinakaribia kuwa na umri wa masaa 48!

  Mie nilitegemea kwenye issue hot kama hii, tupate yaliyofukunyuliwa leo leo (in the past 12hours) na siyo outdated news.
   
 4. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #4
  Mar 11, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Sis wengine sio waandishi wa habari wa Rais au wewe ni muandishi wa habari wa Rais ? Ilitakikana Rais wetu ahutubia Taifa matatizo yamekwishaje sio kimya kimya na kama mwendo wa kobe tupe Habari za nyeti basi Rais amemaliziana na Madakatari kivipi? wamerudi Madaktari Mahospitalini kimya kimya tu?
   
Loading...