Kilimo cha Kisasa cha Mahindi: Mbegu bora, Mbolea bora na magonjwa

nimbagonza

JF-Expert Member
Jun 15, 2015
1,023
716
Habari wadau,

Baada ya kuwa kwenye ajira kwa miaka 10 na kuona msoto uko pale pale,nimeamua kuingia kwenye kilimo kama njia ya kuongeza kipato cha ziada.

Nimeanza kwa kukodi shamba Ruvu kwani mimi niko Dar na niko kamili kwa kuanza na heka 2.
GHARAMA

Nimekodi shamba laki 3(@150,000),nikafyeka 120,000/=(@60,000 hii ni kutoka na kwamba kule maji yalikiwa yamejaa so hakuna magugu majani yaliyobaki siyo marefu sana),mbegu PANNAR kg 10 kwani ndo mbegu wanayolima wenyeji kule elf 60(@6000)kupanda ni elfu 70(35000).

Nimeanza kupanda leo na nimeanzia hapo najua nitadaiwa mbolea,palizi na dawa kwani nitabase na mahindi ya kuchoma.

Nipe gharama na namna bora ya kilimo cha mahindi.

Pia soma => Nimeamua Kulima kwa mara ya Pili kilimo cha mahindi

------- Michango------

Mbegu Bora za mahindi
Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:
  • Mbegu za asili: Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimo
  • Mbegu zilizoboreshwa: Hizi ni zile zilizoboreshwa kutoka mbegu za asili. Kundi hili linagawanywa kwenye makundi mawili – composite varieties na mbegu chotara (Hybrids).

Ushauri wa matumizi ya mbegu zilizoboreshwa unatofautiana kutoka eneo moja na lingine kwa sababu ya:
  • Mwinuko kutoka usawa wa bahari
  • Kiasi cha mvua katika eneo husika
  • Muda unaotumia mbegu hadi kukomaa

Mbegu za mahindi zilizoboreshwa ni kama TMV1, TAN 250, TAN 254, Staha, Situka na zingine zote zinazoanza na herufi “H” kama vile H 250, H 251 na H 615. Pia mbegu mpya zilizotangawa na Kamati ya Taifa ya Mbegu mwaka huu ni WE4102, WE4106, WE4110, WE4114, WE4115 kutoka ARI ILONGA.


Jinsi Ya Kuweka Mbolea Za Kupandia
Mbolea hizi zinawekwa shambani kabla ya kupanda/kusia mbegu. Zinawekwa kwa njia mbalimbali kama vile kusambaza kwenye eneo husika na kuchanganya na udongo, au kuweka kwenye mistari au mashimo ya kupandia. Ni bora zaidi kuchanganya mbolea za Minjigu Phosphate au Minjingu Mazao na udongo kuliko kutia kwenye shimo la kupandia. Pia kuchanganya mbolea na udongo huondoa athari za mbolea kwenye uotaji wa mbegu, hasa kama kuna uhaba wa unyevunyevu.

Viwango Vya Mbolea Za Kupandia mahindi
Kiwango cha mbolea za kupandia kilichopendekezwa ni kilo 20 fosfati (P) kwa hektari ambayo ni sawasawa na kiasi cha mifuko 2 ya DAP (= mfuko mmoja kwa ekari). Ikiwa mbolea ya minjingu phosphate itatumika basi mifuko mitatu itatosa kwa hekta (= mfuko mmoja na nusu kwa ekari). Na endapo utaamua kuitumia mbolea ya minjingu mazao basi tumia mifuko minne na nusu kwenye hekta moja au mifuko miwili kwa ekari moja.


Upandaji wa mahindi
Muda wa kupanda:
Kulingana na msimu mahindi hupandwa mwanzonimwa mwezi wa 11 baada ya mvua za kwanza kunyesha (specifically from 1st to 15th day of November) ambayo huvunwa mwezi Machi mwishoni au aprili mwanzoni. Pia mahindi hupandwa mwanzoni mwa mvua za masika yaani mwezi wa pili mwishoni na mwezi wa tatu mwanzoni ambayo huvunwa mwezi Julai katikati na Agosti mwanzoni. Katika msimu huu utayarishaji wa shamba hufanyika mwezi wa pili mwanzoni.


Muda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia februari 15 hadi Machi 15. Mkulima anashauriwa afuate kalenda ya muda wa kupanda kama anavyoshauriwa na bwana shamba wake.

Nafasi ya kupandia mahindi
Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo. Zifuatazo ni nafasi za kupanda mahindi na idadi ya mbegu kwa kila shimo na kiasi cha mbolea (kwa vizibo vya soda) inayotakiwa kuwekwa kwa shimo:
  • Kwa nafasi ya 90 sm X 30 sm, panda mbegu moja na uweke kizibo kimoja cha mbolea
  • Kwa nafasi ya 90 sm X 25 sm, panda mbegu moja na uweke kizibo kimoja cha mbolea
  • Kwa nafasi ya 90 sm X 50 sm, panda mbegu mbili na uweke vizibo viwili vya mbolea

Kupalilia
Ni muhimu shamba lipaliliwe baada ya mimea kuota ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno. Magugu yaweza kuondolewa wa palizi ya mkono (yaani) kung’olea (ikiwa magugu yapo mbali mbali sana) au kulima kwa jembe la mkono au kwa kutumia dawa/viuagugu (herbicides) hasa 2-4D.

Mbolea za kukuzia mahindi
Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. zifuatazo ni mbolea za kukuzia na kiwango chake cha naitrojeni:
  • UREA: 46% N
  • Calcium Ammonium Nitrate, CAN: 23% N
  • Sulphate of Ammonia, SA: 21%

Urea inakirutubisho cha naitrojeni (N) kwa kiwango kikubwa na watu wengi wanauzoefu nayo. Vilevile bei yake ni nafuu ikilinganishwa na mbolea zingine za kukuzia. Mbolea hii iko katika hali ya chengachenga za mviringo (granules) za rangi nyeupe. Kiwango cha urea ni nusu kizibo cha soda kwa kila shina. Mbolea hizi hazidumu kwenye udongo kwa muda mrefu kwa hiyo huwekwa shambani wakati mimea inapokuwa na mahitaji makubwa ya kirutubisho cha naitrojeni na wakati udongo una unyevunyevu na shamba halina magugu.

Pia wakulima hutumia mbolea za kukuzia zinazopatikana kwa bei nafuu kama vile BOOSTER (foliage nitrogeneous fertilizers) ambayo hupigwa kwa kunyunyizia katika majani ya mmea kila baada ya wiki 3, kwa mara 2-3 mpaka mahindi kuvunwa. Kiwango cha kupiga ni mchanganyo wa mls 50-80 ktk lita 15 za maji. Mbolea za kukuzia huwekwa kuzunguka kila shina la mimea au pande mbili au tatu au nne za kila shina. Cha muhimu ni kwamba mbolea isirundikwe sehemu mmoja. Minjingu Mazao (kg 50/ekari = gramu 10kwa shimo) pia yaweza tumika kwa kukuzia, hivyo mkulima yko huru kuchagua kulingana na uwezo na upatikanaji wake.

Viwango Vya Mbolea Za Kukuzia Vinavyoshauriwa

Kiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ikiwa utatumia UREA. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. Hivyo basi utumie mifuko mitatu kwa hekta ambayo ni sawa na mfuko mmoja kwa ekari. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium na endapo utaitumia basi mifuko minne na nusu itatosha kwa hekta, ambapo kwa ekari moja utatumia mifuko miwili tu.

Kwenye mahindi mbolea ya kukuzia inawekwa baada ya palizi ya kwanza ambayo ni kama wiki tatu mpaka wiki nne baada ya kupanda. Kwa kila mmea mmoja weka kiasi hiki cha mbolea:
  • UREA: kizibo kimoja cha soda
  • CAN: vizibo viwili vya soda, na
  • SA: kizibo kimoja cha soda

Mambo Muhimu Ya Kuzingatia
Kuweka mbolea:
Sehemu za nchi ambazo muda wa kukua mahindi ni mrefu (zaidi ya miezi mitatu), ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili, yaani nusu ya kiwango kinachopendekezwa baada ya mwezi mmoja, na kurudia tena (kutumia nusu iliyosalia) baada ya wiki tatu.

Kupalilia: Katika kilimo cha mahindi, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Wataalamu wanashauri kwamba katika kilimo cha mahindi, shamba lipaliliwe mara 2-3, kufuatana na hali ya magugu katika shamba.

– Utafiti unaonyesha kwamba, shamba la mahindi ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.

KUVUNA, KUKAUSHA, KUSAFISHA NA KUHIFADIHI

Kuvuna

Mahindi yako tayari kuvuna wakati kikonyo kimekuwa dhaifu na mahindi yanaangalia chini. Mahindi yakishakauka vizuri yanatenganishwa na bua halafu majani ya mhindi kutolewa.

Kukausha
Kama mahindi hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi katika juani siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mahindi yakauke vizuri ili yasioze yakiwekwa ghalani. Ili kujua kama mahindi yamekauka vizuri, tia mahindi kadhaa kwenye chupa ya soda iliyokauka na uongeze kiganja kimoja cha chumvi. Tingisha chupa halafu uwache itulie kwa dakika tatu. Chumvi ikikwama kando ya chupa, basi mahindi hayajakauka vizuri.

Kusafisha
Mahindi yaliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mahindi mabovu huondolewa.

Kuhifadhi
Mahindi huhifadhiwa ghalani baada ya kuwekwa viatilifu vya kuzuia bungua wa mahindi Njia za kisasa za uhifadhi hutumiwa kama vile matumiz ya ACTELLIC SUPER DUST katika uwiano wa 1kg kwa gunia 5-10 za ujazo wa 100kg. Kiatilifu kingine ni actellic solution katika rate ya 5mls katika gunia moja la kg 100. Njia nyingine ya kienyeji katika kuhifadhi mahindi ni kuweka juu ya ghala ambalo chini yake kuna jiko la kupikia ambalo hutoa moshi unaotumika kufukuza na kuua wadudu.

SOURCE: Kilimo cha Kisasa cha Mahindi | Mogriculture Tz

Karibu kwa majadiliano...

maize.jpg

Mkulima wa Mahindi: Msimu wa kilimo umefika, zingatia sana yafuatayo

Kwa mikoa ya Iringa, Mbeya,Ruvuma, Njombe, Singida, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora na Shinyanga ni mwanzo msimu wa kilimo.

Ni vema mkulima wa mahindi akazingatia yafuatayo ili kupata ufanisi:

1.Muda huu ni vema uwe tayari umeandaa au unaandaa shamba.

2. Andaa samadi ya ng'ombe iliyoiva vizuri na isambaze shambani kabla ya kulima hasa maeneo ambao msimu uliopita mazao hayakustawi vizuri. Samadi/ mboji ndio siri kubwa ya ustawi mzuri wa mazao hasa mahindi. Mbolea za viwandani pekee si suluhisho la mavuno mazuri.

Maeneo mengi nchini yana upunguvu mkubwa wa virutubisho vya Nitrogen hivyo ni lazima mkulima arutubishe shamba lake ili kupata tija. Ukiweka samadi mfululizo kwa misimu 3 unaweza usiweke tena mbolea kwa miaka 5 hadi 7 ijayo.

3.Andaa mbegu bora mapema. Kwa mbegu chotara au Hybrids tumia mbegu km DK8053,DK90789,DK777,H614, H625Seedco nk. Waone wataalamu wa kilimo au maduka ya kilimo wakupe ushauri upande mbegu ipi kwa eneo lako, japo Dk. 9089,H625 zinastawi maeneo mengi.

4.Panda mbegu kwa nafasi mfano Sm75xSm30 ambapo ekari moja utapata miche 44,000.

5. Andaa pesa au nguvu kazi ya kutosha kupalilia shamba. Wakulima wengi hukosea hapa. Wengi huchelewa kupalilia shamba. Shamba la mahindi lipaliliwe wiki 3 hadi ya 4 toka kupanda. Ukichelewa mahindi hushindwa kukua vizuri na huenda yakadumaa.

6. Andaa mbolea ya kukuzia hasa kama Urea na CAN ili muda wiki 6 na isizidi wiki 8 uwekee mbolea. Wakulima wengi huchelewa kuweka mbolea kwa sababu huwa hajajiandaa.

7. Shamba lisiwe mbali sana na makazi yako utashindwa kulisimamia. Kwa kifupi haya ndio mambo ya msingi ya kuzingatia katika kilimo cha mahindi.

Mhitimu Chuo cha kilimo Uyole 2010, SUA 2017.

Mungu abariki kazi ya mikono yenu.
 
Hicho ni kilimo cha umwagiliaji?

Na hiyo kilo kumi kama utapanda vizuri sidhani kama inatosha kwa wastani eka ni kg 7 hadi 8 na kwa eka mbili unatakiwa uwe na kg si chini ya 14
 
Hicho ni kilimo cha umwagiliaji?
Na hiyo kilo kumi kama utapanda vizuri sidhani kama inatosha kwa wastani eka ni kg 7 hadi 8 na kwa eka mbili unatakiwa uwe na kg si chini ya 14
Ni umwagiliaji make niko karibu na mto, na bado upungufu wa mbegu si tatizo kwani naweza kuongeza lakini mpaka sasa nishapanda heka moja imetumika kilo sita tu, so naongeza kilo 2
 
Narudi ngoja nikusanye hints zote nije tujadili mambo ya msingi.
Utakaporudi naomba unijulishe ni kweli maeneo mengine waweza lima mahindi na ukapata bila ya kutumia mbolea mm ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma hivyo najua bila mbolea uko kwetu upati kitu ss nasikia Morogoro wanalima bila mbolea na baadhi ya maeneo uko Tanga.
 
utakaporudi naomba unijulishe ni kweli maeneo mengine waweza lima mahindi na ukapata bila ya kutumia mbolea mm ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma hivyo najua bila mbolea uko kwetu upati kitu ss nasikia Morogoro wanalima bila mbolea na baadhi ya maeneo uko tanga
Arusha, Manyara, Moro, Njombe
Hawatumii mbolea
 
Cjui ni uoga au uzembe, au nini cjui

Hivi kweli umekaa katika kazi miaka 10 ukaona msoto afu unataka ujikomboe kwa heka 3.

Inakuja akilini kweli? Sio ndio unajiongezea matatizo?

Ukiamua kutupa jiwe... litupe mbaali hata likirudi chini lisikupige.... next time tupa karibu uone km halikugongi kichwani
 
Nenda Morogoro au Babati.utakodi shamba kwa Tsh: 50000 or 70000/= kwa heka moja.uwe na mtaji iwapo unataka kulima kibiashara.kodi heka kuanzia 30 na ulime kwa trekta.

Kukodi trekta kulima kwa heka moja ni Tsh: 40000 or 50000/=.kumbuka kama mahindi umepanda kisasa na kumwaga mbolea na kupalilia vizuri bila kuacha majani yakazorotesha mazao utavuna gunia 10 mpaka 13 kwa heka.

Hesabu zingine piga mwenyewe.nimekusaidia kidogo.kulima heka mbili za mahindi ni kulima chakula cha familia yako tu.

Na si kilimo cha kupata mtaji kwa mtu aliechoka kuajiliwa na kuamua kua mkulima.huwezi toka kuajiliwa kama nilivyo mimi hapa then nikaenda kulima heka 2 au 3 ni kupoteza muda. Lima shamba heka kuanzia 30 mpaka 50.na kwa uchache kilimo hicho ili kikutoe andaa mtaji japo milion 8 mpaka 10m

JAH RASTAFARI MORNING AFRICA
 
Back
Top Bottom