Mkosamali aingia bungeni na rekodi kibao


Geza Ulole

Geza Ulole

JF-Expert Member
Joined
Oct 31, 2009
Messages
16,680
Likes
9,031
Points
280
Geza Ulole

Geza Ulole

JF-Expert Member
Joined Oct 31, 2009
16,680 9,031 280
Mkosamali aingia bungeni na rekodi kibao
Saturday, 06 November 2010 09:21 0diggsdigg

MWANAFUNZI ALIYESHINDA UBUNGE AKIWA NA UMRI MDOGO ZAIDI LAKINI ASILIMIA KUBWA YA KURA Na Denis Maringo KILA uchaguzi mkuu humalizika na mambo yake na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 umemalizika kwa Jimbo la Muhambwe kuwa na mshindi mwenye rekodi nyingi na za aina yake.

Kwa kawaida uchaguzi wa ubunge huambatana na matukio tofauti, ikiwa ni pamoja na kukataliwa kwa matokeo, mshindi kupingwa mahakamani na matokeo kubatilishwa na mahakama. Lakini ushindi wa Felix Mkosamali kwenye Jimbo la Muhambwe haukuwa na matukio hayo ya kukataliwa au kufikishwa mahakamani, lakini wenye rekodi za aina yake baada ya kijana huyo mdogo kuibuka kuwa mshindi mwenye umri mdogo kuliko wote; aliyepata kura nyingi kuliko mshindi mwingine yeyote; mbunge wa kwanza kutoka upinzani kutwaa jimbo hilo; na mtu wa kwanza kushinda kiti cha ubunge akiwa anasoma nje ya jimbo lake na pia kushinda akiwa kwenye chama ambacho hakijawahi kuwa na mbunge. Mkosamali, ambaye alizaliwa Juni 24, 1986 na ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa sheria anayeingia mwaka wa mwisho kwenye Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Mwanza), alipata ushindi mkubwa kuliko wa mgombea yeyote aliyeshinda mwaka huu.

Akigombea kupitia NCCR-Mageuzi, Mkosamali alizoa kura 25,391 (sawa na asilimia 97.72% ya kura zote zilizopigwa na ambazo hazikuharibika) akiwazidi kwa mbali sana wagombea wengine. Alifuatiwa na Athuman Masoud wa CUF aliyepata kura 481 na Baziyaka Zefania wa SAU aliyepata kura 111 ambao kwa ujumla wao walipata asilimia 2.38% tu ya kura zote halali. Mbunge huyo mpya anaingia kwenye chombo hicho cha kutunga sheria akiungana na wabunge wengine ambao waliwahi kushikilia rekodi ya kuwa wadogo zaidi. Wabunge wengine ni pamoja na S.N. Nghusule wa Tanualiyeshinda Jimbo la Dodoma Kaskazini mwaka 1965. Alimshinda Mzee M.A. Mwaugali ambaye alikuwa mgombea mwenye umri mkubwa na hivyo kinyang'anyiro hicho kuwa baina ya mgombea mwenye umri mkubwa zaidi na mwenye umri mdogo zaidi.

Wengine walioingia na umri mdogo ni mbunge mteule wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema, John Mnyika ambaye ana umri wa miaka 29, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alishinda uchaguzi wa Septemba 1957, Kabwe Zitto wa Chadema aliyekuwa kijana zaidi kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini, Jakaya Mrisho Kikwete wa CCM kwenye Jimbo la Bagamoyo mwaka 1990, David Kafulila wa NCCR-Magezi ambaye alishinda kiti cha Kasulu Kaskazini mwaka 2010, Edward Vincent Nyerere wa Chadema kwenye Jimbo la Musoma Vijijini mwaka huu, Alfred Rulegura wa Tanu kwenye uchaguzi wa mwaka 1965 na Musobi Mageni wa Tanu kwenye Jimbo la Kwimba Kusini mwaka 1965.

Kwa kumuangalia kwa juu juu, unaweza kufikiri ni mpole na mkimya, lakini ni mtu anayetumia sauti yake nzito kujenga hoja thabiti na kuonyesha hali ya kujiamini sana na pengine ndicho kitu kilichomfanya aanze kupewa madaraka kwenye chama mapema. Aliingia NCCR-Mageuzi Februari 19, 2010. Aliitisha mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) wakati akiwa likizo fupi ya chuo na kutangaza rasmi kuwa amerudisha kadi ya Chadema na kuhamia NCCR. Siku hiyo aliitumia pia kukiponda chama chake cha Chadema na CCM, mbali na kutangaza nia ya kugombea ubunge wa jimbo hilo. Hilo liliwastua wengi kuwa atawezaje kufanya kazi kwa ushirikiano na wapinzani wenzake kama ana mtazamo tofauti kiasi hicho. "Misingi ya katiba ya nchi inampa mtu uhuru wa kuchagua chama au itikadi ninayoitaka ili mradi tu sivunji sheria au haki za wengine," alisema alipoongea na Mwananchi.

"Mambo ya kisiasa huwa majukwaani zaidi na mfumo wa kisiasa anaoumiani ni wa kuwa wazi na kulumbana bila kupigana ngumi au kujengeana chuki binafsi. "Linapokuja suala la kuwatumikia wananchi, tofauti za kisiasa hazina tija na mimi sitalipa hilo nafasi... ninafanya kazi na wabunge wengine wote wa chama tawala na upinzani kuona taifa linasonga mbele ili kuondoa umaskini, uhalifu na ufisadi uliokithiri na matatizo mengine ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi haraka." Ukweli kwamba kwa sasa anaendelea na masomo ya digrii yake ya kwanza ya sheria unatia wasiwasi kama mbunge huyo mteule ataweza kumudu masomo na majukumu yake ya kuwakilisha wananchi wa Jimbo la Muhambwe wakati wa vikao vya Bunge na pia kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika kama alivyoahidi kwa wananchi. "Ni kweli mshika mbili, moja humponyoka lakini pia ni vema tujikumbushe kuwa kuna msemo wa Kiswahili usemao kuwa ‘Wa Mbili havai moja'.

Yote ni misemo ya hekima inayotumika kulingana na mazingira," alisema akianza kufafanua jinsi atakavyobeba majukumu hayo tofauti. "Kama umepewa uwezo wa kutenda makubwa zaidi katika jamii, itakuwa dhambi ukikisaliti kipaji kimojawapo ulichopewa na muumba. Muhimu tu ni kuvitumia kwa uwiano sahihi hasa katika dunia ya leo ambayo inahitaji kukabiliana na mambo mengi mazito kwa wakati mmoja. Kufuzu elimu kutaniimarisha na kuniaaminisha zaidi kisiasa, lakini pia siasa nitaitumia kuiboresha elimu ya nchi hii. Hapa utaona namna mambo yanavyohusiana. "Wanasiasa wanaoliangamiza taifa ni wale sanaofikiri wananchi ni taburra rassa, hawa hawatufai nchini…hawa ndio wanaoliangamiza taifa katika nyanja zote." Alitumia neno taburra rassa akimaanisha hali ya ubongo kuwa changa isiyo na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Mkosamali anasema hata wapigakura wake walielezwa kuhusu majukumu hayo mawili, lakini bado wakamuamini kwa sababu walielewa wajibu wa kulitumikia taifa ni wa kila mmoja "awe au asiwe masomoni au kazini".

Anatoa mifano ya viongozi kama Mwalimu Julius Nyerere ambaye alijishughulisha na siasa akiwa masomoni na pia hata wabunge kama Kabwe Zitto ambaye amekuwa akisomea shahada ya juu huko Ujerumani akiwa bungeni. Wanafunzi wenzake kwenye Chuo cha Mtakatifu Augustino wanamuelezea Mkosamali kuwa ni mchapakazi aliye na uwezo wa kumudu masomo na siasa kwa wakati mmoja na kwa ufanisi. Walisema kuwa alifaulu masomo yake wakati akibeba majukumu mazito ya uenyekiti wa Chadema wa wilaya na mjumbe wa baraza kuu la taifa na baadaye kupewa uongozi wa juu wa NCCR-Mageuzi ambako alimudu kufanya kampeni mikoa miwili tofauti ya Mwanza na Kigoma. Pamoja na hayo, Mkosamali anakabiliwa na changamoto nyingi za kuwa na ufanisi katika majukumu hayo tofauti ya ubunge na masomo.

Atalazimika kuendelea na masomo chuoni na wakati mwingine atatakiwa kwenda Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge na pia vile vya kamati. Changamoto nyingine ni kusimamia maslahi ya wapigakura wake kwenye Jimbo la Muhambwe ili kuhakikisha mipango yote ya serikali inatekelezwa vizuri na kuwanufaisha wananchi badala ya fedha za mipango hiyo kutafunwa na wachache. Lakini umri wake mdogo utakuwa ni changamoto nyingine ya kukabiliana na viongozi wa juu wenye umri mkubwa, hasa wanapofanya makosa ambayo yanataka kumkemea.
Akizungumzia ushindi wake, Mkosamali anawasifu wapigakura wa Muhambwe na Kigoma kwa ujumla kwa kuwa makini na wakomavu kisiasa. "Waliangalia sifa za mgombea mwenyewe na si chama; hawakuangalia uwezo wa kifedha, jina la mtu au umri," alisema akizungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu mkoani Kigoma ambako CCM ilipoteza majimbo mengi. Mikoa mingine ambayo chama hicho tawala hakikufurukuta ni Arusha, Mwanza, Mbeya, Dar es salaam, Kilimanjaro na Shinyanga. *Denis Maringo ni mwanasheria, mwanahistoria na Mkurugenzi wa Kituo cha Haki na Demokrasia (CJD). Anapatikana kwa simu: 0719270067. Email: HYPERLINK "mailto: dnmaringo@gmail.com This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it " This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
Mkosamali aingia bungeni na rekodi kibao

MY TAKE
Kuna haja ya CHADEMA kuliangalia swala la uongozi ndani ya chama kwa mapana! Viti vinne vilivyosombwa na NCCR vilipaswa kuwa vya CHADEMA ikizingatiwa jinsi chama kilivyowajenga huko hapo awali! sometimes compromise makes things better! lets learn a lesson
 

Forum statistics

Threads 1,239,056
Members 476,371
Posts 29,340,793