Mkono: CCM Haina Budi Kuwatambua Wafanyabishara Kama Kundi Rasmi. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mkono: CCM Haina Budi Kuwatambua Wafanyabishara Kama Kundi Rasmi.

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mafuchila, Jan 18, 2010.

 1. M

  Mafuchila JF-Expert Member

  #1
  Jan 18, 2010
  Joined: Apr 29, 2006
  Messages: 752
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 35
  Rostam, Chenge, waonyesha jeuri ya fedha kwa John Cheyo
  Na Anceth Nyahore
  18th January 2010

  Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, ni miongoni mwa waliochangia fedha na kushiriki katika harambee maalum iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bariadi, ambayo inadaiwa kuwa ina lengo la kulikomboa Jimbo la Bariadi Mashariki. Jimbo la Bariadi Mashariki kwa sasa linashikiliwa na Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Momose Cheyo.

  Hata hivyo, uongozi wa CCM Wilaya ya Bariadi umesema kuwa lengo la harambee hiyo ni kuhakikisha kwamba chama hicho tawala kinafanya vizuri katika uchaguzi mkuu hususan wilayani Bariadi.Katika harambee hiyo, chama hicho kimefanikiwa kujipatia zaidi ya Sh. milioni 190 ambapo kati ya hizo, Chenge pamoja na marafiki zake takriban 10 akiwemo Rostam, walichangia Sh. milioni 55.

  Harambee hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Mkono, ilifanyika mwishoni mwa wiki. Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Mohamed Mbonde, aliliambia Nipashe kuwa harambee hiyo iliyoandaliwa na chama hicho, ni kwa ajili ya kufanikisha gharama za uchaguzi mkuu na ujenzi wa jengo la CCM la Wilaya ya Bariadi.Lakini Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi, Jumanne Kasote, alisema harambee hiyo ni kwa ajili ya kukijengea uwezo chama hicho kuwa na fedha katika uchaguzi mkuu na ujenzi wa ofisi ya CCM ya Wilaya ya Bariadi.

  Jumla ya Sh. milioni 69.368 fedha taslimu zikiwemo hundi, zilitolewa na ahadi ya Sh. milioni117.705 na mabati 2,000 yenye thamani ya Sh. milioni tatu yalipatikana.
  Habari kutoka kwa baadhi ya wanachama, wakereketwa na wapenzi wa chama hicho waliopewa kadi za mwaliko wa harambee hiyo zilidai kuwa lengo lake ni kuhakikisha CCM kinalirudisha mikononi Jimbo la Bariadi Mashariki.

  Mbali na mkakati wa kumg’oa Cheyo, pia lingine ni kuhakikisha kuwa CCM inaibuka na ushindi mnono katika uchaguzi wa madiwani wa halmashauri hiyo yenye kata 23. Katika Halmashauri ya Bariadi, UDP ina kata 12 na CCM kata 11 na hivyo halmashauri hiyo kuongozwa na chama hicho cha upinzani.

  Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi, Kasote alisema harambee hiyo iliwashirikisha Mbunge wa Viti Maalum, Anna Lupembe kutoka mkoani Rukwa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yohana Balele, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Shinyanga, wanachama, wakereketwa na wapenzi wa CCM na baadhi ya wafanyabiashara maarufu wilayani humo.

  Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Balele, aliahidi kutoa Sh. milioni tano, Mweka Hazina wa CCM Wilaya ya Bariadi, Emmanuel Silanga, alitoa Sh. milioni 10 yeye na marafiki zake wengine 10 ambao kwa pamoja walitoa Sh. milioni 20 akiwemo mfanyabiashara Njallu Silanga ambaye ni ndugu wa Mweka Hazina wa CCM wa wilaya hiyo.

  Aidha, mwanachama mwingine, Martine Makondo, anayedaiwa kulinyemelea Jimbo la Cheyo, alichangia Sh. milioni tatu huku akitoa fedha taslim Sh. milioni moja na ahadi ya Sh. milioni mbili.Christina Chenge ,ambaye ni mke wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, alichangia Sh. 500,000.

  Aidha, mgeni rasmi katika harambee hiyo, Nimrod Mkono, alisema wakati umefika kwa CCM kuwa na mafiga matatu kwa kuwa na makundi ya wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara na siyo wakulima na wafanyakazi tu. Alisema katika harambee hiyo yeye kama mmoja wa wafanyabiashara sasa CCM haina budi kulitambua kundi la wafanyabiashara.

  Cheyo akizungumzia mkakati na harambee hiyo, alisema kamwe haoni jambo jipya kwake na kwa chama chake kwa kile alichodai kuwa hata mwaka 2005, CCM ilichanga mamilioni kwa ajili ya mgombea wao, Danhi Makanga lakini yeye alimbwaga kwa kura nyingi.

  Hata hivyo, Mbunge huyo amewatahadharisha wananchi kutoruhusu kununuliwa kwa fedha kutoa kura zao kwa viongozi wasio waadilifu.

  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...