Mkoa wa Kigoma na ujenzi wa masoko kudhibiti umasikini

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
MKOA wa Kigoma unatekeleza miradi miwili ya ujenzi wa masoko katika maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi ili kutatua changamoto ya mazao ya kilimo kukosa soko.

Masoko hayo ni yale yanayojengwa katika Kijiji cha Muhange, wilayani Kakonko na lile la Kijiji cha Mkarazi Wilaya ya Kibondo. Masoko hayo yanajengwa kupitia Programu ya Pamoja ya Mkoa wa Kigoma (Kigoma Joint Program - KJP) inayotekelezwa na mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa.

Mratibu wa KJP, Evance Siangicha anasema mradi wa soko la Muhange unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani 225,000 (takriban Sh milioni 520) na unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa Mitaji ya Maendeleo (UNCDF), wakati Serikali kupitia halmashauri ya Kakonko inachangia Sh milioni 170.

Anasema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya lengo la kwanza la malengo ya maendeleo endelevu ambalo ni kufuta umasikini wenye sura zote kila mahali.

Ujenzi wa masoko hayo unafanywa kipindi ambacho Mkoa wa Kigoma unapambana kuondoa wananchi wake katika umasikini uliokithiri, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za asili na mazao ya kilimo.

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Emmanuel Maganga amekuwa akisisitiza kuwa, masoko ya mpakani ya Muhange wilayani Kakonko na Mkarazi wilayani Kibondo ni muhimu katika kukuza uchumi wa mkoa na kuondoa umasikini kwa jamii.

Maganga anasema serikali ya mkoa itashirikiana na Halmashauri kuona namna ambavyo programu mbalimbali zinazolenga kuleta tija na faida ya uwepo wa masoko hayo ili kuleta mabadiliko ya uchumi kwa mkoa na kwa mtu mmoja mmoja huku makundi maalumu yakipewa umuhimu wa pekee.

Tathmini ya umaskini katika ngazi ya mikoa na wilaya iliyofanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2016 inaonesha kuwa, asilimia 48.9 ya wananchi wa Kigoma wanaishi katika hali ya umasikini ikilinganishwa na Mkoa wa Dar es Salaam ambao kiwango chake ni asilimia 5.2.

Kwa takwimu hizo, Mkoa wa Kigoma umekuwa ukitajwa kuwa na kiwango kikubwa cha umasikini licha ya kwamba ni mhimili wa uzalishaji wa chakula Kanda ya Magharibi.

Katika mikutano yake mbalimbali Mkuu wa mkoa huyo amekuwa akisema kuwa takwimu za hali ya umasikini wa mkoa Kigoma zilizotolewa na serikali hazilingani na uhalisia wa sasa, hivyo kutoa mwito wa kufanyika kwa tathmini mpya.

Kwa nini Kakonko? Uwekezaji katika Wilaya ya Kakonko unatokana na wilaya hiyo kutajwa kuwa asilimia 63 ya watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini, hivyo kuchangia sehemu kubwa ya umasikini wa Kigoma kwa mujibu wa tathmini ya umaskini iliyofanywa na Serikali kupitia NBS mwaka 2016.

Tathimini hiyo ilitumia taarifa za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 pamoja na Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (Household Budget Survey) wa Mwaka 2011/12.

Katika kupima hali ya umaskini, tathmini ilizingatia mahitaji ya msingi kwa kila mwanakaya ambayo ni elimu, afya, maji na chakula.

Mkuu wa Wilaya Kakonko, Hosea Ndagala anasema soko la Muhange ni moja ya miradi ya kimkakati katika kuondokana na umasikini na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi hasa kipato kwa kaya na mtu mmoja mmoja na kwamba, vikundi vya wanawake vitapewa kipaumbele.

Anasema sokoni ni sehemu ya mwisho ya mpango mkakati utakaohusisha kuimarisha kilimo kwa kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao.

“Kupitia halmashauri, ipo miradi mbalimbali iliyoanza kutekelezwa, yapo maandiko kwenda maeneo mbalimbali ya wadau na tunafanya hili kwa kushirikisha pande tatu; serikali, wananchi na wadau wetu wa maendeleo,”anasema Ndagala.

Anaongeza: “Ni dhahiri soko hili litaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kuondokana na takwimu za hali ya umasikini zinazoelezwa.”

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kakonko anasema soko hilo litakuwa kituo kikubwa cha kuuzia bidhaa za kilimo hasa kwenda Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Rwanda ambazo wafanyabiashara wake wameonesha mwitikio mkubwa kulitumia kununua bidhaa.

Ujenzi wa Soko la Muhange unawaweka wananchi na viongozi katika eneo hilo la Kakonko kuwa katika harakati za maandalizi ya jinsi ya kunufaika na kuwepo kwake, usimamizi na uendeshaji wa kibiashara utakaolifanya kuwa endelevu katika siku zijazo.

Miongoni mwa mambo yaliyokwishakufanyika ni kuundwa kwa Ushirika wa Wafanyabiashara Wanawake ambao ndio utakuwa ukisimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za soko hilo.

Mwenyekiti wa ushirika huo, Justina Amanto anasema ujenzi wa soko hilo ni mkombozi kwao katika kuondokana na umasikini hasa kwa wakulima wanawake ambao wamekuwa wakilima mashamba madogo licha ya kuwepo kwa eneo kubwa linalofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali.

“Moja ya sababu ya kulima kilimo cha kujikimu ni ukosefu wa masoko ya kuuzia bidhaa zetu. Sehemu kubwa tunauziana kijijini, kidogo yanakwenda nje ya wilaya na siku ya Jumatano tunauza kwenye soko la pamoja la mpakani ambalo huanza saa 10 jioni hadi saa 3:00 usiku ambako hakuna hata maghala ya kuhifadhia bidhaa zetu zikibaki au mvua ikinyesha,” anasema Amanto.

Anasema kwa sasa soko limejengwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wafanyabiashara hasa wanawake, ambao ni kundi linalopaswa kupewa msukumo kwa sasa.

Mjumbe wa ushirika wa wafanyabiashara wa Soko la Muhange, Zayana Masudi anasema wamekutana na kupanga biashara za kimkakati zinazozingatia bidhaa zenye soko kubwa hasa kwa wanunuzi kutoka Burundi ambao ndiyo tegemeo kubwa la wateja wa soko hilo.

Naye Katibu wa ushirika huo wa wafanyabiashara, Yolanda Rufuyo anasema ujenzi wa soko hilo unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa kupitia mradi wa pamoja Kigoma (KJP) ni ukombozi kwao na kwamba litawawezesha kufanya biashara zenye tija na kuinua uchumi wa vipato vya familia zao.

Anasema wanawake wamehamasika kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuongeza thamani ya mazao hayo na kubainisha kwamba matarajio ya soko hilo kuwakomboa wanawake kiuchumi ni makubwa.

“Tumeshapata mafunzo ya uendeshaji biashara lakini pia ushirika kama wasimamizi tumepata mafunzo ya uendeshaji kwa tija wa soko hivyo ni wajibu wetu kuyafanyia kazi mafunzo hayo na kuleta mabadiliko kwenye maisha yetu,” anasema katibu huyo.

Mkakati wa halmashauri Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kakonko, Masumbuko Stephano anasema kwao soko hilo ni sehemu ya kitega uchumi ambacho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri.

Stephano anasema pamoja na bidhaa za viwandani, pia bidhaa za kilimo ndiyo msingi wa soko hilo hasa kwa wakulima wadogo vijijini kuhakikisha wanapata mahali pa uhakika kwa ajili ya soko la mazao yao.

“Hapa tunatarajia kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima kwa kuwekwa kwenye vifungashio,” anasema.

Anasema lengo la ujenzi wa soko hilo ni kuinua uchumi wa vijana na wanawake na kwamba, wanawake wameandaliwa ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wanafaidika na uwepo wa soko hilo.

Anasema tayari kundi hilo limepatiwa semina za ujasilimali za ukulima bora wa mazao, kilimo cha matunda na usindikaji wa bidhaa huku bidhaa za chakula na kilimo zikipewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta), lengo la kwanza ni kukuza uchumi na kupunguza umasikini wa kipato, kuongeza ubora wa maisha na ustawi wa jamii na kuimariha utawala bora na uwajibikaji ambapo ujenzi wa soko hilo unahusiana na lengo hilo.

Diwani wa Kata ya Muhange, Ibrahim Katunzi anasema ujenzi wa soko la Muhange ni moja ya maeneo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kuondoa umasikini na kuleta hali bora ya maisha kwa wananchi.

Katunzi anasema soko hilo ni miongoni mwa miradi inayotoa kipaumbele cha utekelezaji kwa makundi maalum yakiwemo wanawake, vijana na walemavu hivyo kushiriki kwa karibu katika utekelezaji wake.

“Kwa sasa baada ya mipaka kufunguliwa na hali ya amani kuwa nzuri nchini Burundi ni wazi ujenzi wa soko hilo utawapa wafanyabiashara nafasi nzuri ya kupata mahali pazuri na penye uhakika wa kuuza bidhaa zao tofauti na lilipokuwa soko la awali la vibanda vya nyasi,”anasema Katunzi.

Ofisa Kilimo na Mifugo wa Kata ya Muhange, Paul Yohana yeye anasema kutokana na uhakika wa mahali pa kuuzia na kuhifadhia bidhaa, wameanza programu za kuongeza uzalishaji ili kuondokana na kilimo cha mazoea cha kujikimu na sasa wanaendesha kilimo biashara.

“Hadi sasa vikundi 25 vya wakulima na wafugaji vimeundwa ambapo hapa tunatarajia kutoa elimu ya kilimo na ufugaji mazao makubwa yakiwa mahindi, mpunga, karanga, maharage na muhogo ambapo ufugaji umejikita sana kwenye kuku, mbuzi na ng’ombe,” alisema ofisa huyo.

Sambamba na hilo, anasema vipo vikundi 13 vilivyoundwa kwa ajili ya kilimo bora cha maharage na muhogo kupitia mradi wa usimamizi wa maliasili kwa maendeleo ya wananchi kiuchumi (SARKIP), unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la Ubelgiji (ENABEL).

Anasema kupitia mpango huo, wana hakika yatapatikana mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika wilaya hiyo.

Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Muhange, Saidi Shaban anasema wameshafanya mikutano mbalimbali na wananchi kuhamasisha utekelezaji wa mipango iliyopelekwa kwao ya kuongeza uzalishaji wa mazao, kulima kilimo bora chenye tija lakini kuona umuhimu wa kutumia uwepo wa soko la Muhange katika kupeleka bidhaa zao kwenye soko hilo.

Joseph Rubuye ni Mshauri wa Kilimo katika Sekretarieti ya Mkoa Kigoma. Anasema, idara yake imeshatoa maelekezo kwenye wilaya na kata ikiwemo utekelezaji wa mipango ya kuongeza uzalishaji. Anasema yapo mazao mengi yanayolimwa katika maeneo ya kuzunguka soko la Muhange yakiwemo ya karanga, maharage, mahindi, mpunga na muhogo waliohamasisha wakulima kulima kwa wingi.

Ripoti ya Mpango wa Maendeleo Endelevu iliyotolewa mwaka 2015 inaonesha kuwa, mataifa ya Asia Kusini na Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiko hasa wanakoishi watu wengi waliokumbwa na umasikini uliokithiri na maeneo yenye migogoro na vita hali ni mbaya zaidi.

Kutokana na ripoti hiyo Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekuwa wakiwekeza katika kusaidia nchi zilizoathirika na hali hiyo na ndiyo chimbuko la kuanzishwa kw mradi wa ujenzi wa masoko ya mpakani ya Muhange na Mkarazi ili kuleta hali nzuri ya maisha kwa wananchi wa maeneo hayo.
 
Back
Top Bottom