MeinKempf
JF-Expert Member
- Jun 11, 2013
- 11,094
- 7,225
Asilimia 49 kati ya asilimia 100 ya matokeo ya uchunguzi wa makosa ya vinasaba (DNA) yanayowasilishwa katika ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mwaka yanaonyesha kuwa baba si mzazi halali wa mtoto katika kesi hizo.
Hayo yamesemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa wadau wa wakala wa afya ya mazingira leo jijini Dar es Salaam.
Kesi zinazopokelewa katika maabara yetu zinazohusu sampuli ya Vinasaba kwa mwaka zinaonyesha kuwa asilimia 49% kati ya asilimia 100% ya matokeo hayo huonyesha mzazi mmoja ambaye ni baba kuwa si mzazi halali wa mtoto huyo?.
Vinasaba ni utambulisho wa kipekee wa kila kiumbe ambao unabeba taarifa muhimu na inayorithisha tabia au umbile fulani la mhusika. Vinasaba ni kama vile kitabu cha kumbukumbu kinachohusu maisha binafsi?, aliongeza Prof. Manyele.
Profesa Manyele aliongeza kuwa mikoa ya kanda ya Ziwa, Arusha, Dar es Salaam na Mbeya ndio inayoongoza kwa matokeo ya uchanguzi huo wa makosa ya Vinasaba nchini.
Akizungumza kuhusu lengo la mkutano huo, Profesa Manyele amesema kuwa ni kuimarisha uhusiano uliopo kati ya wadau wa kemikali na wadau wa afya ya mazingira kutoka katika halmashauri tofauti nchini pamoja na ofisi ya Mazingira.
Aidha Profesa alibainisha baadhi ya majukumu yanayofanywa na wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni kufanya uchunguzi ili kuhakiki ubora na usalama wa vyakula, dawa, maji, maji machafu, bidhaa za viwanda na mashambani, sampuli za mazingira na sampuli zinazohusiana na makosa ya jinai.
Matokeo ya uchunguzi wa makosa ya jinai na vinasaba (DNA) huviwezesha vyombo husika kufikia maamuzi stahili na kusaidia kutendeka kwa haki katika tuhuma za kesi za jinai ikiwemo ulevi, mauaji, ubakaji, wizi wa
watoto, uhalali wa mtoto kwa mzazi, kwa kupitia vyombo husika? alifafanua Profesa.
Mbali na hayo, alisema wakala kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuwasilisha mapendekezo ya kutunga sheria ya kuunda maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Sheria ya kusimamia taaluma ya Wakemia, kuimarisha upatikanaji wa mitambo na vifaa vya maabara kila teknologia inapobadilika pamoja na kuimarisha zaidi taratibu za uchunguzi ziwe za kisasa ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknologia.