Mke wa marehemu Mengi atoa onyo kali kwa wanaonyemelea mali za marehemu

Boniphace Kichonge

JF-Expert Member
Jul 31, 2017
1,606
1,956
Jacqueline Mengi ametoa onyo kwa mtu yoyote atakayehusika na mauzo au ununuzi wa mali za marehemu mumewe kuwa ni kinyume cha sheria.

Katika tangazo alilolitoa kwa umma jana, Jacqueline amesema kesi ya mirathi namba 39/2019 iliyofunguliwa inaendelea kusikilizwa Mahakama Kuu na kwamba mtu atakayejihusisha na ununuzi au mauzo, hatatambulika.

Amesema kwa sasa hatua zinazoruhusiwa ni zinazohusiana na shughuli za kila siku za mali zake na kwamba endapo yatahitajika maamuzi makubwa ni lazima Mahakama Kuu itoe barua.

Kesi hiyo ya mirathi inasikilizwa mbele ya Jaji, Josi Myambina baada ya kutangazwa kwa wosia ulioandikwa na Mengi Julai 30, 2019 kwenye gazeti la Daily News na kuwasilishwa mahakamani.

Baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, upande wa wajibu maombi kwa niaba ya watoto wa marehemu na familia, mdogo wa marehemu Mengi, Benjamin Mengi alidai kuwa wosia huo ni batili kwa sababu wakati kaka yake, Dk Mengi akiuandika, alikuwa amechanganyikiwa.

Upande wa wajibu maombi unaowajumuisha Regina na Abdiel unaongozwa na Wakili Nikael Tenga huku upande wa usimamizi wa mirathi unaongozwa na Wakili Elias Msuya.

Wosia wa marehemu uliandikwa Agosti 17, 2017 na katika wosia huo, marehemu Dk Mengi aliwataja wasimamizi wanne wa mirathi ambao ni Benson Benjamin Mengi, William Mushi ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Bonite Bottlers Limited na Silvia Mushi ambaye ni Mwanasheria wa Makampuni ya IPP.

Mali alizoacha bilionea huyo na kuzirithisha kwa Jacqueline na wanaye kwa mujibu wa wosia huo ni pamoja na fedha, ardhi, magari, nyumba na hisa zake zilizopo kwenye kampuni zake.

Baadhi ya kampuni hizo ni IPP Limited, The Guardian, Tanzania Africa Limited, Diamonds Africa Limited, Energy Tanzania Limited na mengine huku nguo za marehemu vito na saa ya thamani kwa mujibu wa wosia vitarithiwa na watoto wake wadogo yaani Jarden na Ryan.

Inadaiwa wosia huo umeweka zuio la mrithi yeyote halali kuupinga mahakamani na endapo akifanya hivyo na kushinda atatakiwa kulipwa Sh 1,000.

Mengi (77) aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, alifariki dunia Mei 2, mwaka jana.
 
Back
Top Bottom