Mkate wa kidole/mkate wa majongoo

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,492
9,264
Mkate wa kidole ni mkate wa kiasili ulopikwa kutumia tui la nazi na ni mtamu sana. Ladha yake ni ya kipekee! Mkate huu una majina mingi kutokana na shepu unazoziunda madonge yake.

Kwa mfano unaitwa mkate wa majongoo au mkate wa jongoo kwa vile zile shepu ulounda umezikunja kama majongoo.

Majina mengine ni mkate wa kusukwa au mkate wa kusongwa, mkate wa mkeka, mkate wa shikamoo, mkate wa sukari kwa juu nk. Lakini usibabaike kwa majina yake, ukitunukiwa ukaribishe kwa chai, uji, sherbet au soda baridi!

mkate-wa-kidole-swahili-bread_1.jpg


MAHITAJI:

Unga vikombe 3 ( 650g)
Tui zito na tui jepesi: kiasi yake yawe 1¼ cup (about 350ml) -vuguvugu
Sukari kikombe ¼ - ½ (80g -160g) (Utamu wa mkate ni hiyari yako)
Hamira kijiko kikubwa 1 (7g)
¼ kijiko cha chai chumvi
Iliki ya kusagwa kijiko cha chai 1
Zabibu au lozi ( ukipenda) ¼ kikombe
Kungu manga ¼ kijiko cha chai (ukipenda sio lazima)

UKIPENDA UNAWEZA KUUPAMBA MKATE KWA SUKARI YA JUU (SIO LAZIMA) utahitaji kijiko kikubwa 1 cha sukari na maji upate kutengeza mchanganyiko/shira nyepesi MAELEZO

Paka mafuta kwenye sufuria utakayotumia kuoka. Weka kando. Umua hamira: Chukua kikombe utie tui jepesi vuguvugu hadi yafike ¼ .

Ongeza sukari kijiko cha chai 1 uchanganye kwenye hayo maji. Kisha mimina hamira yako. Weka mchanganyiko kando kwenye sehemu ya mvuke.

Baada ya robo saa, utaona povu limetenda juu ya mchanganyiko. Hio ni ishara hamira tayari kutumiwa.

Kumbuka mchanganyiko wa tui zito, na jepesi, pamoja na hiyo hamira uloumua, idadi yake kwa ujumla kipimo ni kikombe 1¼ cup (yaani kipimo chote cha maji yako ikiwemo hamira yawe 350ml).

Mimina unga kwenye besini au bakuli. Kisha mimina mahitaji yote makavu (sukari,chumvi,iliki na kungu manga, na zabibu kama utatumia) uichanganye pamoja.

Fanya kishimo katikati uongeze mchanganyiko wako wa tui na hamira. Anza na maji ya hamira uloumua, kisha tui zito, kisha tui jepesi. Changanya unga na tui mpaka ushikane, Hakikisha umechanganya upasavyo ndio uanze kuukanda. Ukande unga kwa mda wa dakika 10.

Hakikisha unga wako umekandika ipasavyo, umekuwa mwororo na haung'ati wala sio maji maji.

Gawa hilo donge ulokanda madonge madogo kama 6-8 itategemea unataka kutengeza shepu ya majongoo, au kusuka, au mkeka nk Ufunike unga wako na weka kando kwa mda wa dakika tano. .

Nyunyiza unga kwenye kibao cha kusukuma chapati kisha chukua kila donge dogoulokata uanze kulisokota ili upate ukambaa mwembamba.Sasa huo ukambaa ndio utatolea shepu utakayo.

Unaweza kuukunja kama jongoo, kusuka kamba mbili tatu, kusuka mkeka kwa kamba 4-6, ujuzi wako tu hapa.

Ukishatia shepu, chukua donge ulosokota uweke kwenye sufuria ambayo utauoka huo mkate. Usibane sana hayo majongoo-yape nafasi yapate kuumuka uzuri.

Funika uweke kando kwa mda wa masaa 1-2 hadi mkate uumuke ufure kama mara mbili ukilinganisha na ulivyoanza. Mkate tayari kuokwa/kuchomwa.

JINSI YA KUOKA MKATE WA KIDOLE/MAJONGOO.
Unaoka mkate huu kama unavyooka mkate wa mayai au mkate wa sinia.

Tumia moto wa kiasi. Tayarisha jiko lako, hakikisha moto wa makaa/mkaa upo tayari kabisa ndio upambizie moto. Moto wa juu uzidie moto wa chini ,Oka mkate wako kwa mda wa dakika 30 hivi uhakikishe sehemu ya katikati ya mkate imeiva kabla kuepua. Au oka kwenye oven.

Moto wa 180-200°C kwa dakika 30-45 mpaka mkate umeiva. Hakikisha oven limeshika moto kabla kuuweka mkate kuoka- au sivyo mkate utaharibika. Ukiona sehemu ya juu ya mkate inaungua au inakolea rangi kabla mkate kuiva, basi unaweza kupunguza moto au funika kwa mfuniko au tin foil, uendelee kuoka hadi uwive. Mkate ukisha kuiva, epua iweke kando.

TAYARISHA SHIRA/MAJI YA SUKARI
Chemsha maji na sukari pamoja kwa mda wa dakika 1-2.
Tumia brush kupaka hayo maji ya sukari/shira kwenye mkate wako.
USIMIMINE! Unapaka tu kidogo ilimkate ungare na uzidi kukolea sukari kwa juu.

Uache mkate upoe kidogo kabla hujautoa kwenye sufuria.

Uache upoe kabisa kabda kuukata (tumia kisu cha msumeno kama unacho au kisu kikali kama hauna cha msumeno). Andaa vipande vya mkate kwenye sahani tayari kuliwa.
 
Leo nimeamua kutembelea mambo ya maakuli! kupo vizuri kwa wachuchuz kuchukua maufundi ya jikoni
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom