Mkasa wa wakimbizi wa Sudan na Apeth (na mikasa mingine)

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,331
23,504
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Karibuni tena.

Kwa tahadhima, ninaomba nijibu mahitaji ya watu juu ya mfululizo huu wa 'nyuzi' za visa vya filamu kwa kutuma uzi huu wa tisa sasa kwa mfululizo.

Nakiri ni muda sasa lakini natumai hakuna kilichoharibika. Kwa 'weekend' hii hebu tutazame visa hivi, na basi vikikivutia waweza kuzipakua na kuzitazama kwa muda wako.


01. HIS HOUSE (2020)

0b9ba346318ac46a8575c9666a533e64.jpg


Jamii ya Dinka (nchini Sudani Kusini) wanaamini kisa hiki ...

Hapo kale paliongokea bwana mmoja mwenye moyo mwema ambaye kwa kutaka mno kuwa na nyumba ya mikono yake, akaanza kuibia wengine.

Bwana huyo, pasi na kujua, akaiba kwenye nyumba ya Apeth. Kiumbe aishiye mtoni akiaminika kuwa mchawi wa usiku (the night witch). Na kwasababu hiyo basi, akajikuta anajenga nyumba ambayo ilikaliwa na wakazi wawili, yeye na huyo aliyemwibia!

Ikawa ikifika usiku, anasikia kuta zikinong'ona.

Na Apeth hakukoma mpaka pale mwivi alipolipa deni lake!

MKASA WENYEWE: Bwana Bol na Rial ni wakimbizi toka Sudani kusini waliotoa sadaka vingi ili kufika katika nchi ya Uingereza.

Nchi yao imeharibiwa na vita na karibia kila mtu wao wa karibu ashafyekwa na makundi ya waasi wanaozunguka huku na kule na silaha za moto.

Nchini Uingereza, baada ya kukaa kwa kitambo katika 'kempu' ya wakimbizi, hatimaye ndoto yao inatimia. Wanapatiwa makazi ambayo watajihifadhi huku wakiendelea kufuata utaratibu waliopewa.

Ingawa makazi hayo hayana mazingira mazuri, ni pachafu na pakuukuu, kwa wawili hawa ni ngekewa ya mtende! Wanaweka maadhimio ya kufuata taratibu zote walizopewa ili tu wafuzu kuwa raia wa kudumu nchini humo.

Lakini kitumbua kinakuja kuingia mchanga pale wanapobaini hali ambayo si ya kawaida!

Kuta za nyumba hii zinaongea! ... Kuna watu wanatembea ndani yake ... Kuna macho yanawatazama toka kutani, na si ya mtu mmoja!

Usiku unakuwa mrefu na mchana ni wa kuchosha.

Wanakuja kubaini ya kwamba, ni moja ya sadaka waliyoitoa kufika hapa ndiyo inawaadhibu ... Sadaka ya unyang'anyi ...

Sadaka ambayo wameitumia kujengea 'nyumba' yao, na sasa mwenye mali anaidai. Anataka roho ya mmoja wao, huku akitaka mwengine amsaidie kutimiza adhma yake.

02. SPELL (2020)

ef5747b403d5e0ac164ea8a9bb31d994.jpg


Hamna anayechagua familia.

Ni tunajikuta tu tumezaliwa na watu ambao maisha yetu yote tunatakiwa kuwajali na kuwaonyesha upendo.

Ndo' tunawajibika hivyo.

Lakini kama ingekuwa kinyume na hapo, wengine katu wasingegeuza shingo zao nyuma pindi wanapozipa mgongo nyumba za familia zao.

MKASA: Japokuwa malezi yake yalikuwa ni ya tabu mno, mateso na vipigo vikiwa ni vya kawaida, Marquis analazimika kupanga kutembelea nyumbani kufuatia habari za msiba wa baba yake mzazi.

Tangu atoke huko kijijini hakuwahi kurejea kamwe. Maisha yake yanamwendea vema sana mjini akiwa pamoja na mkewe na watoto wake wawili.

Anakodisha ndege ndogo, anapakiza familia yake nzima na kushikilia usukani kwenda kutoa heshima zake za mwisho huko Appalachia.

Wakiwa njiani, hali ya hewa inabadilika. Wanakumbana na kimbunga kikali kinachomshinda Marquis kumudu ndege kiasi kwamba wanapata ajali mbaya!

Marquis anakuja kupata fahamu yupo kitandani kwenye chumba asichokifahamu. Hajui familia yake iko wapi, na mguu wake umejeruhiwa kiasi cha kutoweza kutembea!

Uso kwa uso anakutana na Bibi Eloise pamoja na mumewe. Ni kwa mara ya kwanza anawaona watu hawa machoni pake.

Upesi Bi Eloise anamtoa hofu akimuahidi kumsaidia kurudi kwenye hali yake buheri akitumia kifaa kazi chenye uwezo wa 'ku-control' mwili wa mtu, kwa jina 'boogity', kifaa kinachotengenezwa kwa ngozi na damu halisi ya mlengwa!

Kitambo kidogo, Marquis anabaini kuwa si kwa msaada yu hapa, bali yumo kwenye MIPANGO dhalimu ya wenyeji ambao wameushikilia mji huu mzima pamoja na vyombo vya usalama.

Mpango wa kutolewa sadaka!

Sasa atatokaje hapa ingali mwenyeji wake ana kifaa kinachoweza kuuendesha mwili wake mzima na huku yeye ni dhaifu kwa majeraha?

Na je familia yake iko wapi?

03. DEATH NOTE (2017)


7fc98b191e44a7a4ed4fd463b448a926.jpg


Ni kawaida yake binadamu kuwa mwepesi kumhukumu mwengine pale anapokosea, kuona wengine hawafai hata pale wanapofanya matendo ambayo yeye mwenyewe huwa anayafanya muda mwingine.

Lakini vipi tungeacha kuhukumu wengine na tukajitahidi haswa kwenye kujua nini kinachopelekea matendo yao? ... Unadhani dunia ingeendelea kuzunguka hivi ama ingebadili mwelekeo?

Amini, kuna watu wangetamani kufanya uhalifu mkubwa mno kwasababu zao za ndani, lakini shida tu ni kwamba hawana uwezo huo. Hawajui pa kuanzia.

Vipi ukiwapa uwezo huo mikononi mwao?

MKASA WENYEWE: Mwanafunzi aitwaye Light Turner anakumbana na kitabu chenye jina la 'Death Note' ingali akiwa shuleni.

Hakijui kitabu hiko na wala yaliyomo ndani yake, lakini punde anajifunza kwamba kitabu hiko kina nguvu ya kukatisha uhai wa mtu yeyote yule!

Kinachohitajika ni jina la mhusika na picha yake tu kichwani mwa anayenuwia kifo hiko.

Baada ya kufahamu, Light anaanza mara moja kuwaadhibu waliomkosea. Anamuua mwonevu wake wa shule, mwizi wa benki na mwanaume aliyemuua mama yake mzazi.

Light pia anabaini ana uwezo wa 'kucontrol' matendo ya mtu anayeandikwa kwenye kitabu hiko ndani ya masaa 48 kabla ya kifo chake kutukia. Basi kwa kushirikiana na girlfriend wake wanafanya matukio ya mauaji huku kila tukio marehemu akiwa ameandika neno 'Kira' kabla ya kukata pumzi yake.

Mfululizo huo wa mauaji unawafanya polisi kuunda kitengo rasmi cha kumtafuta muuaji, huku baba yake Light akiwa ni mmoja wa maafisa hao.

Je, wataweza kumkamata Light na girlfriend wake? Kama ndio, ni kwa ushahidi gani?

Na je, Light anaweza kukitumia kitabu hiki kujikomboa?

04. READY OR NOT (2019)

b3171f4682f8ad9f5a258216b4fda8a1.jpg



'Sometimes malaika wa heri nao hutembelea motoni' - Fid Q

Amini hii, kuwa muda mwingine njia sahihi ndiyo inayokufikisha motoni.

MKASA: Kama ilivyo kwa wasichana wengine, kwa Grace kuolewa, tena kwenye familia inayojiweza kiuchumi, ni baraka tosha kabisa. Ni ndoto ya karibia kila mwanamke.

Lakini usiku huohuo wa harusi, wala si miaka na miezi, Grace anagundua kuwa alifanya KOSA la kuolewa.

Kosa ambalo si kama yale mengine ya kudai talaka, bali linalohitaji uhai wake!

Katika usiko huo, Grace anaalikwa pamoja na wanafamilia katika kijikao chao ambapo anaambiwa achague mchezo kwa kutumia njia ya kadi.

Huo ni utamaduni wao.

Grace anajikuta akichagua mchezo wa kujificha na kutafutwa (Hide and seek), ambapo analazimika kujificha huku familia nzima ikihangaika kumtafuta kwa hali na mali.

Ajabu ni kwamba familia hiyo inabebelea silaha za kweli kama bunduki na mishale kwenye msako wa mkwe wao Grace. Kitendo ambacho kinamjuza Grace kuwa huu si mchezo wa kufurahia bali wa mauaji!

Kitambo kidogo, anajifunza kuwa familia hii inalazimika kumuua kabla ya jua kuchomoza na wasipofanya hilo basi kuna jambo baya litawasibu kwani hii ni ibada kwao.

Hivyo huu si mpambano wa yeye kujiokoa tu bali ni mpambano wa wote kupambania uhai wao, ni aidha yeye ama familia ya wakwe zake, Le Domas family.

Sasa nini hatma yake? Na ni nini kipo nyuma ya mauaji ya familia hii?

Ukitazama filamu hii ndo' utajua kwanini huwa mnaambiwa chunguzeni kwanza familia za mnaotaka kuwaoa ama kuolewa nazo.

05. KNIVES OUT (2019)

54adf7d9e02b0f21f1653c360fb058dc.jpg


Ukiniuliza ipi ilikuwa movie yangu bora kabisa mwaka 2019, sitajifikiria mara mbili kuitaja hii.

Hata ukiniuliza tena kwa mara nyingine, sitasita kulirudia hili. Hii ndiyo movie bora kwangu. Namna ambavyo mwandishi alivyoandika na namna ambavyo ilichezwa, hakika ilifanikiwa kuniteka kiasi kwamba nikawa naona nikitafuna nitapitwa na kitu.

Nikawa naachama.

KISA NA MKASA WAKE: Bwana Harlan Thrombey ni mzee mwenye ukwasi wa kutosha kutoka kwenye biashara yake ya uandishi na uuzaji wa vitabu.

Ndani kwake kuna kila kitabu kilichoandikwa kwa mkono wake na haitakuchukua muda kujua mzee huyu ni mwandishi nguli wa vitabu aina gani - 'mystery books' - hata mpangilio wa nyumba yake unashuhudia hilo.

Akiwa anatimiza miaka 85, kusheherekea, anaitisha tafrija inayokusanya familia yake yote. Na ni katika tafrija hiyo inabainika kuwa ana hitilafu na wanae, wakwe na hata wajukuu zake kila mmoja kwa sababu yake binafsi.

Moja, alimjuza Richard, mkwe wake wa kiume, kuwa anafahamu ya kwamba anamsaliti mwanae, Linda, na hivyo akamtishia kufikisha habari hizo kwa binti yake.

Pili, akamwambia mkwe wake wa kike kuwa atasitisha mara moja kutoa fedha zake kwa ajili ya binti yake anayesoma kwasababu amebaini huwa anamwibia kwa kusema uongo.

Tatu, anamfukuza mwanae aitwaye Walt kutoka kwenye kusimamia kampuni yake kubwa ya uchapishaji vitabu kwasababu ya ukosefu wa uadilifu.

Nne, anasikika akipazana sauti ya ugomvi na mwanae Ransom ikidhaniwa sababu ni utovu wa nidhamu wa mtoto huyo machachari wa mwisho.

Kesho yake asubuhi, mzee Harlan anakutwa akiwa amekufa. Amekatwa shingo, kajilaza kwenye kiti!

Taharuki inapanda! ... Ni nani muuaji katika familia hii ambayo kila mmoja anaonekana ni mtuhumiwa?

Maafisa polisi wanaingia kazini pamoja na mpelelezi binafsi, nguli Blanc, ambaye anapewa tenda ya kupeleleza kesi hii huku aliyempa tenda hiyo akiwa hamjui ni nani. Alikuta tu bahasha yenye fedha na maelekezo.

Lakini tukirudi nyuma kidogo, bwana Harlan kabla hajafa alikuwa pamoja na nesi wake aitwaye Martha, ambaye kwa kutokudhamiria alijikuta anachanganya chupa za dawa na kumzidishia dozi mzee huyu.

Kwa kutambua kuwa hana muda mrefu wa kuishi sasa na pia Martha ni binti asiye na makosa huku akiwa anamlea mama yake ambaye yuko Marekani kihalifu, bwana Harlan anaamua kupanga mpango kabambe, kwa kutumia maarifa yake ya uandishi, ili kumwokoa Martha asiingie matatizoni kwa kusababisha kifo chake.

Baada ya kumweleza mpango huo, anamsihi sana aufuate kila nukta na kisha baada ya hapo anajikata koo asingoje kifo kumkuta!

Sasa kwa kuona hilo, unaweza dhani kuwa mchezo umeishia hapa lakini hapa ndo unapoanzia! Yaani ndo hatua ya kwanza kabisa kwenye safari ya maili na maili.

Kwa ufupi ni kwamba; Martha hausiki kivyovyote vile na haya mauaji, lakini kivipi?

Nani aliyempa tenda bwana Blanc kwenye mzozo huu? Na alijuaje yatayojiri?

Alafu Martha kuongopa hawezi, akiongopa anatapika. Aisee .... Atajiokoaje?

Hapa ndo utakapoona namna gani unavyoshiriki kwenye kutatua tatizo.


Enjoy!
Stress ujitakie mwenyewe.
SteveMollel.
 

Similar Discussions

10 Reactions
Reply
Back
Top Bottom