Mkasa wa Kweli Namna Mwanamuziki Jerry Nashoni Dudumizi Alivyoachwa Solemba na Binti Mrembo Aendaye kwa Jina la Imakulatha

Uzalendo Wa Kitanzania

JF-Expert Member
Mar 8, 2020
729
1,000
Jerry kijana aliyekulia Musoma kijiji cha Kigera alianza kuingiwa na "pepo la Muziki" tangu akiwa kijana barobaro. Alikua akipenda sana kupiga gitaa. Hakua na ndoto za uimbaji wala hakuwaza hata siku moja kuwa atakuja kuwa muimbaji.

Alikua akipenda sana kwenda klabu ya Musoma Catholic Mission ambayo ilikua ni social club maarufu ambapo alikua akipenda kujifunza kupiga gitaa.

Akiwa hapo akaonekana kipaji chake kama maskhara na kuchukuliwa na mmiliki wa bendi ya Special Baruti Bandi iliyokua haina muda mrefu tangu kuanzishwa kwake mwanzoni mwa miaka ya 80.

Huko Special Baruti Band Jerry akakabidhiwa kuwa chini ya mpigaji rythim wao Bwana Charles Koya ili azidi kumpika kukuza kipaji chake.

Nyota ya Jerry ikazidi kung'aa akawa mpiga gitaa la rythim mahiri kabisa akaweza hata kumudu kupiga program za bendi hiyo na hata baadae aliweza kurekodi nao TFC, RTD na baadaye wakaenda nae hadi Kenya katika studios mbalimbali na producers mbalimbali ambapo pia waliweza kupiga nae muziki katika klabu mbalimbali jijini Nairobi ikiwemo Bombax Hotel na wakazunguka nje ya Jiji katika mikoa takribani yote ya Kenya kasoro Mombasa na Kisumu wakishirikiana na mwanamuziki hodari Joseph Kamaru.

Ni katika kipinda akiwa huko Kenya ndipo Jerry alipoanza kuvutiwa na fani ya uimbaji na ndipo akaanza taratibu kujifunza kuimba hata bendi ya Magereza Musoma ikamuona na kuvutiwa nae na kuamua kumchukua na ndipo nyota ya Jerry ilipoanza kuchanua zaidi na hatimaye Jerry kuanza kuwa mwanamuziki tegemeona hata baadae kufanikiwa kutimkia Dar es Salaam kwenye kitovu cha manguli na wakongwe wa kila aina wa muziki wa dansi.

Baada ya mafanikio hayo ya kimuziki, Jerry alianza kujijenga pia taratibu kimaisha. Sasa alikua "amekua". Hakua mtoto tena.

Purukushani za muziki zilimkutanisha na watu wa kila aina na starehe za kila aina. Muziki ulikua na ibilisi kubwa kuanzia ibilisi ya wanawake, ibilisi ya ulevi na zinginezo.

Jerry hakutaka kuharibikiwa na maisha mapema. Alitambua wazee wake walivyomlea na kumuusia kuishi maisha yenye adili ikiwemo kuoa mke wa kukaa ndani badala ya kuruka kuruka na viruka njia.

Ndipo kama zali huko huko Musoma akakutana na dada mmoja mrembo aitwae Immaculate. Ingawa alikua mweusi wa rangi, Immaculate alikua na uzuri wa asili na macho yenye kuita. Akibinua na kukufinyia jicho lazima ukatike network zote kichwani.

Basi Jerry akadata ile mbaya. Aliota kabisa kwamba Immaculate ndiye alikua mke aliyeletewa na Mungu duniani.

Ni kuamini hivyo ndio maana Jerry hakutaka ajizi na akapania kwenda moja kwa moja hadi kwao na Immaculate bila hofu yoyote. Ikabaki kazi ya Immaculate tu kumpiga danadana. Msimamo wa Immaculate ukawa haueleweki.

Siku zile kazi ya Muziki ilichukuliwa kama kazi ya kihuni au uhuni. Hivyo Immaculate nae alikumbwa na hofu hiyo hiyo aliona kuolewa na Jerry itakua sawa na kuolewa na mhuni na yeye alitoka kwenye familia yenye ukwasi nk.

Hivyo Immaculate akawa hasomeki anaingia na kutoka, mara akubali mara alete hoja na visingizio alimuradi tu ahadi ya kukubali kuolewa imekua ngumu kutoka mdomoni mwake. Jerry akahisi labda hali hiyo ya kukosa msimamo Immaculate ni sababu ya yeye Jerry kuwa umasikini hivyo akajiona mnyonge sana.

Baada ya kuona Immaculate hasomeki mwishowe Jerry akaamua kutinga moja kwa moja hadi nyumbani kwao na Immaculate akaamua kama mbwai basi iwe mbwai hata akifukuziwa mlangoni.

Kiukweli ni kwamba Jerry Nashon alidata sana tangu alipokutana na huyo dada mrembo Immaculata.

Jerry alivutiwa sana na binti huyo na akaamini hatopata mwanamke mwingine kuliko huyo. Hivyo kwake kumpata Immaculate ilikua ni Vita ya kufa na kupona.

Basi Jerry akaamua siku moja kwenda nyumbani kwao na Immaculate huko huko Musoma lakini kwa bahati mbaya alipofika hakumkuta akaambiwa Immaculate yupo nje ya mkoa wa Mara. Kama Immaculate alikua amesafiri kweli au alikua amefichwa humo humo ndani Mungu ndio anaejua na malaika wake.

Balaa zaidi wakati huo hakukuwa na mawasiliano mengine ya Jerry kuweza kumpata Immaculate zaidi ya simu za mezani.
Jerry alibaki mlangoni ameduwaa na kufadhaika kama msukule uliotolewa shimoni.

Hakuna na namna. Akaamua kuacha namba za simu ya mezani ili Immaculate atakapokuja basi amjulishe.

Jerry akaondoka zake. Akaona namba ya simu aliyoacha haitoshi. Bado silaha moja. Nayo ni tungo. Jerry akajichimbia na kufika Dar es Salaam akamtungia wimbo Immaculate ili kumpa ujumbe wake na akamkumbusha ampigie simu huku akimaliza viapo vyote hadi kwa lugha yake ya kimila ili kuonyesha hisia kali za mapenzi alizokuwa nazo juu ya binti huyo Immaculate.

Hebu ona Jerry alivyotia huruma hadi kuamua kupasuka kijaluo. Labda pengine Immaculate angesikia na kutoka huko alikokua amejificha. Wajaluo watasahihisha hapo.😄

Nyasaye achiel merwa kende, an aheri 'Immculata, nyar pacho ibi mak lweta itera mbele ya wazee!!!!

Naam. Wazee wa Immaculate hawakua na shida na Jerry. Alisubiriwa tu Immaculate. Na Jerry alishampitisha Immaculate kwa 100%.
Jerry alimkubali Immaculate na kumpitisha kwa tabia zote.

Immaculate hakua na visirani au umawenge hata kidogo. Alikua msichana mwenye kujiheshimu na mwenye wajihi na sifa zilizomvutia sana Jerry. Tofauti na wanawake wengi Immaculate hakuwa mwanamke mwenye tamaa wala hakua na makuu.

Jerry akabaki kusubiri simu ya Immaculate kimyaa... Tena namba ya simu aliiweka hadharani 26561. Shida ya Jerry ilikua moja tu kupata uhakika wa msimamo wa Immaculate kama kweli yuko tayari kuolewa nae.

Lakini Immaculate aliamua kula bati. Akamwachia Jerry wa watu msongo wa mawazo na maumivu ya roho. Kweli kupenda ni mateso.

Hebu tuone Jerry alivyolalamika:

[Wote]
Bibi Eee Immaculata mama, halooo Immaculata mama

Nakutafuta sikuoni bibi, Napiga darubini sikupati yeyeyeyeee

[Jerry] Ni umbali Gani ulipo?

[Wote] Nijulishe, nipigie simu namba 26-56-1

[Jerry]
Wakila eya melakembe, walakembe Immaculata

Yalobanzii Immaculata e sela mbele ya wazeee

Usifanye mchezo na pendo

[Wote] Nakupenda aaaaaa

[Jerry] Naapa kwa jina la mama Suzana eeh

[Wote]Nakupenda aaaaaa

[Wote]
Popote ulipo nakuhitaji uje unihakikishie mapenzi yetu

Kama kweli tutaoana

Uendelee na tabia yako ya ukarimu (x2)

Tamaa mbali mbali mbali nawe

Pesa mbalimbali nawe.....uendeleee....na tabia yako ya ukarimu eeh....
 

jojipoji koromije

JF-Expert Member
Mar 22, 2017
895
1,000
Asante sana Mkuu kwa kukileta kisa hiki cha Dudumizi!! Ama kweli wanamuziki walikuwepo zamani sikuhizi tuna wasanii tu!!

Katika wimbo huu Dudumizi aliimba ile mbaya!! Mpangilio wa sauti yake ulikuwa balaa!!! Kumbe wimbo huu ulitokana na kisa cha kweli!! Asante sana kiongozi!! Ukipata kisa kingine turushie Mkuu.

Nasikia hata wimbo wa Neema wa kwake Chidumule akiwa DDC Mlimani Park nao ulitokana na kisa cha kweli!!! Sina uhakika lakini.
 

Tate Mkuu

JF-Expert Member
Jan 24, 2019
6,646
2,000
Inaonekana kweli enzi hizo wanamuziki walikuwa wanachukuliwa poa sana! Ingekuwa ndiyo sasa, wala asingepata usumbufu wowote ule.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom