Mkapa: UKIMWI bado tishio, Watanzania tusibweteke

AbelFernandes

Member
Mar 20, 2013
16
1
RAIS mstaafu Benjamini Mkapa, amewataka Watanzania kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na VVU, kwa kuwa bado tishio.

Aidha amesema kwa kuwa Serikali imeendelea kutegemea misaada kwa wahisani katika kudhibiti janga hilo, ni jukumu la kila Mtanzania kusaidiana na serikali katika mapambano hayo.

Mkapa alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati akizindua harambee ya kupanda mlima Kilimanjaro inayofahamika kwa jina la ‘Kili Challenge, kwa ajili ya kuchangisha fedha za kutunisha mfuko wa kupambana na UKIMWI na VVU.

Alisema takwimu zinaonyesha kupungua kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7.0 kwa utafiti wa mwaka 2003/2004, asilimia 5.7 mwaka 2007/2008 na asilimia 5.3 kwa utafiti wa viashiria vya UKIMWI na Malaria kwa mwaka 2011/2012.

"Hata hivyo UKIMWI bado ni tatizo kubwa nchini mwetu, kwani athari na madhara yatokanayo na UKIMWI yameongezeka kama vile ongezeko la watoto yatima, ongezeko la maambukizi mapya kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24, wajane/wagane, Watu wanaoishi na VVU ambao wanatakiwa kusajiliwa kwa ajili ya kupatiwa dawa pamoja na umasikini unaotokana na kaya kupoteza wazalishaji mali.

"Katika hali hiyo, jitihada za kupanda hadi kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro zinalandana na mahitaji ya jitihada za kufikia kilele cha mapambano dhidi ya UKIMWI. Dhamira hiyo izingatie mustakabali wa kuwa na sufuri tatu yaani : Sifuri maambukizo mapya.

Sifuri vifo vitokanavyo na UKIMWI na Sifuri ya Unyanyapaa na ubaguzi kwani hii ni ishara kubwa ya ubunifu na ujuzi mlionao kwenye kushughulikia masuala ya Udhibiti wa UKIMWI. Dhana hii inajengwa na msingi wa kujituma na kuweka mbele moyo wa kujitolea kwa ajili ya kuwakinga watanzania dhidi ya maambukizi ya VVU pamoja na athari za UKIMWI," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini, (TACAIDS), Dk. Fatma Mrisho, alisema kumekuwapo na mapambano dhidi ya Ukimwi zaidi ya miaka 30 sasa kuanzia mwaka 1983 tulipogundua wagonjwa watatu wa mwanzo, Pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu.

Alisema Ukimwi bado hauna chanjo wala dawa na bado ni tishio kwa maisha ya watanzania. Wahisani wameendelea kutoa misaada mbalimbali hali inayoonyesha kuwa utegemezi bado ni wa kiwango cha juu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita, (GGM), Terry Mulpeter, alisema hadi sasa zaidi ya watu 500 duniani wameshiriki na zaidi sh milioni 800 zimekusanywa kwa ajili ya harambee hiyo ya kupanda mlima Kilimanjaro;

"Hii ni juhudi ya pamoja inayokusudia kuwa na Tanzania isiyokuwa na UKIMWI. Naona fahari kusema kwamba GGM,pamoja na washirika wake nchini na duniani wanayo ari kubwa sasa kuliko ilivyo wahi kutokea.Tunalenga kufikia wakati ambapo Tanzania haitakuwa na maambukizi mapya ya VVU.Na inawezekana.

"Pia kutokana na amsaada ambao tumekuwa tukipata kutoka serikalini kila mwaka na kutoka kwa wafadhili wetu, GGM kamwe haitakoma katika kuhakikisha kuwa Kili Challenge inaendelea kuwepo kwenye shughuli na mipango yetu hapa Tanzania," alisema.

Katika harambee hiyo zaidi ya milioni 33 zilikusanywa huku wadau wengine wakiendelea kujitokeza kuchangia harambee hiyo inayofanyika kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.
 
Back
Top Bottom