Mkapa kalewa au kapotoka?

Dingswayo

JF-Expert Member
May 26, 2009
4,019
2,923
http://www.mwanahalisi.co.tz/mkapa_kalewa_au_kapotoka-

Imechapwa 03 November 2010

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa si mtu anayependa kusema au kuhojiwa, lakini pale anapofanya hivyo huzua kasheshe na kauli yake kulalamikiwa.
Katika mkutano wa mwisho wa kampeni za Jakaya Kikwete, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkapa aliibuka na kushambulia wapinzani wake wa kisiasa. Akiongea kwa mbwembwe na tambo zilizozidi mipaka, Mkapa alishambulia kila mmoja.
Kwanza, Mkapa alisema vyama vya upinzani havistahili kukabidhiwa madaraka ya dola kwa sababu vinahubiri udini. Pili, Mkapa alijitosa kutetea Mwenge wa uhuru.


Kwa wanaomfahamu Mkapa wameona kuwa tabia yake haijabadilika hata baada ya kukaa nje ya ulingo wa kisiasa kwa miaka mitano sasa.
Bado amebaki Mkapa yule yule mwenye tabia na hulka zilezile. Baadhi yao wanasema, Mkapa utampenda pale anaposoma hotuba yake kwenye karatasi, maana watu husikia kwa masikio na kutafakari kwa mioyo.


Lakini akihutubia bila karatasi, watu husikia kwa masikio na mikono huiweka kifuani kama ishara ya kuomba Mungu awaepushe na maneno yatakayotoka katika mdomo wake.
Hivyo ndivyo ilivyotokea Jumamosi iliyopita wakati CCM wanahitimisha kampeini zao katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Wahenga husema, tabia haina dawa. Naye Mkapa kwa kuwa ni mzee, bila shaka amejaliwa mengi na pia kuna mengine mengi ambayo ameyakosa.


Kwanza, nguvu yake ndiyo udhaifu wake. Pili, ni mwelewa wa mambo mengi, mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, lakini pia huitumia karama hii vibaya. Wengi wanaomfahamu vema wanamwona mwenye kiburi na majivuno mbele ya wananchi.


Binafsi, nilibahatika kuongea na Mkapa huko nyuma na kumuuliza ikiwa alikuwa na marafiki wa aina yake hapa nchini. Alinijibu hana kabisa rafiki nchini.
Nilishangaa, maana nilidhani kwa uzalendo wake anaodai kuwa nao, alipaswa kuwa na marafiki wengi ndani ya taifa lake.


Katika mkutano ule wa Jangwani, Mkapa alisema mengi, yasiyo na mpangilio na yaliosheheni hasira. Kwa mfano, alituhumu watu aliodai wanasambaza udini katika kampeni za uchaguzi mkuu. Matokeo yake, alipotosha hata maana halisi ya kuomba kura kwa mgombea na kimsingi kwa jinsi alivyoporomosha shutuma, aliwaudhi hata waliohudhuria, wasikilizaji na waliokuwa wanamtazama.


Bila kujali kuwa yeye ni mzee wa taifa, mlezi wa maadili mema katika taifa na mhimili wa amani na utulivu, Mkapa alilaani vyama vya upinzani na wagombea wake, kama ‘mzee asiye na busara.” Alianza kwa kukejeli. Akatamba kuwa hajali hata kama wanaoeneza udini wanavaa majoho ya namna gani.


Udini alioulaani ukageuka majoho aliyoyalaani badala ya wavaa majoho aliodai wanaeneza udini.


Lisemwalo lipo, kama halipo laja. Udini katika uchaguzi unaenezwa kwa kulaaniwa kuliko ukweli halisi. Wanaodai kuna udini kama ilivyo kwa Mkapa, wanasali katika makanisa na misikitini.


Lakini sidhani kama kuna siku waliona udini huko, wakausema na kuonya kuwa utaangamiza taifa. Badala yake, wananchi walishuhudia Mkapa anayejifanya muumini mzuri wa dini ya kikirsto, akitua Jangwani kukemea wale alioita, “Wanaoeneza udini.”


Ni kwa sababu, marafiki wa Mkapa, wakiwamo wanaotuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini wamekataliwa katika uchaguzi wa mwaka huu. Ndiyo msingi wa yeye na wenzake kujificha ndani ya kwapa la tuhuma za udini.


Laana ya Mkapa kwa wanaoeneza udini, haina uzito wowote kuliko laana ya wananchi kwa ufisadi uliofanywa katika kipindi cha utawala wake na mwingine kwa mikono yake mwenyewe.


Kwa mfano, nani asiyefahamu kuwa katika ukwapuaji wa fedha uliofanywa na kampuni ya Kagoda, Mkapa alikuwa miongoni mwao?
Kila mmoja anajua kuwa mafisadi wamelaaniwa katika misahafu yote ya dini, na Mkapa kwa kuwa hajawahi kukana kuhusika na ufisadi, anaweza kuwa anakumbwa na laana hiyo.


Mkapa akawaita wale wanaopingana na sera za CCM kuwa ni “kokoto.” Hulka ya udikteta ni kuwageuza watu kuwa vitu badala ya viumbe hai.
Kama kupingana na CCM ni kugeuka kokoto, basi Mkapa ni zaidi ya kokoto, maana ni yeye aliyeasisi upinzani wa kweli wa sera za CCM pale alipozama katika lindi la fikra za kibeberu na kifisadi.


Mkapa amekuwa akilia anaonewa na kudiriki hata kuomba huruma za wenye majoho aliowalani pale Jangwani. Ushahidi wa hili upo wazi.
Akiongea kana kwamba hana kumbukumbu, Mkapa alisahau hata alichowahi kukisema na hata kukitenda huko nyuma.


Kwamba ni chini ya uongozi wake ambapo sera ya udini ilianzishwa ndani ya chama chake pale chama hicho kilipoingiza Mahakama ya Kadhi katika ilani yake ya uchaguzi.
Ilipodaiwa kuwa ni Mkapa alilalamika pembeni akidai watesi wake hawajui nini maana ya “dola.” Ni kiburi hicho hicho kinachomfanya sasa, kuwadharau wapinzani kwa kuwaita wambea, waongo na kokoto. Mmbeya ni yule anayeshindwa kueleza fikra zake wazi na badala yake akaisha kupika majungu pembeni.


Matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa nchi nzima yanamsuta Mkapa kwa sababu ni yeye aliyefunga kampeni kwa matusi badala ya kuwanyenyekea wapiga kura.
Si ajabu ni yeye aliye nyuma ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) sasa kushinikiza kubadili matokeo ili laana ya kukosa kura isimrudie maana wana mtandao tayari wanadai aliyewaharibia kampeini zao ni Mkapa.
Wanadai walianza peke yao na walikuwa wanaenda vizuri bila msaada wake, lakini kwa kitendo chake cha kuwatukana wapiga kura alitia dosari kubwa katika kampeini za CCM.


Mkapa anapaswa kuelewa kuwa wananchi wamebadilika, na kwamba mtindo wa kiimla anaoutumia, umepitwa na wakati. Hata utetezi wake kwa Mwenge wa Uhuru hauna nguvu kwa sababu, kazi ya Mwenge wa Uhuru aliouasisi Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni kuleta nuru palipo na giza, na matumaini mahali watu walipokata tamaa.


Sambamba na jukumu hilo, Mwenge ukachoma mabepari na wanyonyaji wa raslimali za taifa. Lakini wakati huu, mwenge unatumika kuzalisha mafisadi na kuwalea.


Ni muhimu Mkapa akafahamu kuwa Mwenge tunaoutaka ni ule wenye uwezo wa kuchoma mafisadi waliokwapua mabilioni yetu ya shilingi, viwanda vya umma, waliojiuzia nyumba za serikali na wanaotumia raslimali za taifa kuanzisha vitega uchumi vyao. Mwenye wa aina hiyo, hautufai na Mkapa anatakiwa kuelewa hivyo.
 
Sikutegemea kumwona Mkapa akiwa katika hamaki ya juu kiasi kile!...Alitumia 90 ya muda aliopata kwa kulaumu na kudharau na kuponda kila anayesogea anga zao!
Wenye busara wako wapi?...Kama hakuna mtu wa kubalance hali pindi kunapokuwa na wimbi baya au mustakabali usioridhisha wa mahusiano ya kisiasa?...Hivi busara ya uzeeni huanzia umri gani?
 
Back
Top Bottom