Mkapa atinga mahakamani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mkapa atinga mahakamani

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by MziziMkavu, May 8, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 8, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Amtetea Profesa Mahalu
  [​IMG] Ashangaa mashitaka yake
  [​IMG] Amtaja kuwa mwadilifu  [​IMG]
  Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akisindikizwa kuelekea chumba cha mahakama kutoa ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana.(PICHA:TRYPHONE MWEJI)


  Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa (73), amekiri mahakamani kwamba alikuwa na taarifa za kuwepo kwa mikataba miwili ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia, na kwamba kama Rais (wakati huo) alibariki ununuzi huo kufanywa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo, Profesa Costa Mahalu (63).

  Kadhaka, Mkapa anakuwa Rais Mstaafu wa kwanza nchini kupanda kizimbani kutoa ushahidi wa kumtetea aliyekuwa mteule wake.

  Profesa Mahalu na mwenzake wanakabiliwa tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya Euro 2,065,827.60.

  Mkapa alidai kuwa, yeye pamoja na serikali yake walifahamu utaratibu mzima uliotumika kuanzia mchakato hadi mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo kukamilika.

  Mkapa alitoa ushahidi wa utetezi wa Profesa Mahalu, jana mbele ya Hakimu Mkazi, Mfawidhi, Illivin Mgeta, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam.

  Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, Mkapa alidai kuwa, kati ya mwaka 1995 na mwaka 2005 alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Profesa Mahalu alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.

  Alidai kuwa, alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na Profesa Mahalu kuhusu mchakato mzima na umuhimu wa kununua jengo la ubalozi nchini Italia ambalo lilinunuliwa kwa Euro 3,098,741.40 ili kuepukana na kero ya majengo ya kupanga.

  Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Mgongolwa na Mkapa:

  Wakili Mgongolwa: Shahidi katika mwaka 1995 na mwaka 2005 ulikuwa wapi na wadhifa gani?

  Mkapa: Nilikuwa Dar es Salaam kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Wakili Mgongolwa: Kabla ya kushika wadhifa huo ulipitia nyadhifa gani nyingine?

  Mkapa: Kabla sijawa Rais niliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Canada na Marekani.

  Wakili Mgongolwa: Ukiwa Rais wa nchi hii katika kipindi hicho, ulifahamu nini kuhusu ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia?

  Mkapa: Nilifahamu jengo la ubalozi wa Italia lilinunuliwa kwa Euro milioni 3.09 kwa maagizo ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Wakili Mgongolwa: Unakumbuka Balozi wa nchi hiyo wakati huo alikuwa ni nani?

  Mkapa: Nakumbuka, wakati huo Balozi alikuwa ni Profesa Mahalu.

  Wakili Mgongolwa: Je, Mheshimiwa serikali mlifahamu utaratibu uliotumika katika ununuzi wa jengo hilo?
  Mkapa: Ndiyo.

  Wakili Mgongolwa: Nani alikufahamisha machakato mzima?
  Rais Mkapa: Balozi wetu Profesa Mahalu.

  Wakili Mgongolwa: Katika manunuzi ya jengo hilo ulipewa taarifa kuhusu masharti ya mmiliki?
  Mkapa: Nilitaarifiwa kabla ya ununuzi kufanyika kwamba mmiliki anataka alipwe kwa awamu mbili tofauti.

  Wakili Mgongolwa: Kupitia akaunti za nani?
  Mkapa: Kupitia akaunti za muuzaji wa jengo.

  Wakili Mgongolwa: Je, Mheshimiwa kama Rais wakati huo, ulitoa baraka kuhusu ombi hilo?
  Mkapa: Serikali yangu ilitoa baraka na mimi nilitaarifiwa kuhusu hilo.

  Wakili Mgongolwa: Walikubaliana mkataba kwa maandishi au kwa njia gani?
  Mkapa: Ninachofahamu walitakiwa kulipwa kwa mikataba miwili, lakini kama kulikuwa na suala jingine sifahamu.

  Wakili Mgongolwa: Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa uongozi wako, Martin Lumbanga, alikana kufahamu suala la mikataba miwili unasemaje kuhusu hilo?
  Mkapa: Ninashangaa kwanini alisema hivyo, lakini serikali ilitoa idhini.

  Wakili Mgongolwa: Kama wewe Rais ulijua inawezekana Lumbanga asijue suala hili?
  Mkapa: Inawezekana asijue, lakini inakuwa vigumu sana.

  Wakili Mgongolwa: Wewe ulijua na ukabariki?
  Mkapa: Ndiyo mimi nilijua na nikabariki.

  Wakili Mgongolwa: Kwa kumbukumbu zako, wizara ngapi zilihusika?
  Mkapa: Wizara za Ujenzi, Ardhi na Fedha.

  Aidha, Mkapa aliisomea mahakama taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (wakati huo Rais Jakaya Kikwete), aliyoitoa Bungeni kwamba kati ya mwaka 2001 na 2002 wizara ilinunua jengo la ubalozi nchini Italia kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na ya Fedha.

  Aliendelea kumnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo Kikwete kwa kusema:

  “Mheshimiwa Spika hati ya jengo hilo tayari iko wizarani,” alimalizia kusoma taarifa hiyo iliyotolewa bungeni kuhusu ununuzi wa jengo hilo.

  Wakili Mgongolwa: Una taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matumizi mabaya ya fedha juu ya ununuzi wa jengo hilo?
  Mkapa: Hapana sikuwahi kupata malalamiko.

  Wakili Mgongolwa: Nini ufahamu wako kama Mstaafu kwa aliyekuwa Balozi wako?
  Mkapa: Profesa Mahalu ni msomi, mfanyakazi mzuri, mwadilifu na mwaminifu.

  Wakili Mgongolwa: Mawasiliano ya Balozi na serikali yalikuwa namna gani?
  Mkapa: Balozi anaweza kuandika barua kwa Wizara ya Mambo ya Nje, Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Rais.

  Wakili Mgongolwa: Ni lazima kuwasiliana kwa njia ya maandishi?
  Mkapa: Hapana, mara nyingi kwa maandishi, lakini hata kwa njia ya mdomo.

  Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Visent Haule na Mkapa:

  Wakili Haule: Je, Mheshimiwa jumla ya fedha zilizotumika ni kiasi gani?
  Mkapa: Euro milioni 3.098 ndiyo ninavyofahamu mimi.

  Wakili Haule: Nani aliagiza upelelezi ufanyike kuhusu ununuzi wa jengo hilo?
  Mkapa: Mimi sijui.

  Wakili Haule: Uchunguzi wa kesi hii ulifanyika ukiwa madarakani?
  Mkapa: Mimi sijui nilishtukia Balozi ameshtakiwa nikiwa nimetoka madarakani.

  Wakili Haule: Lini ulipata taarifa?
  Mkapa: Siku aliyoletwa mahakamani kwa mara ya kwanza nilisikia kutoka kwa watu niliowateuwa kushika nyadhifa mbalimbali wakati nikiwa madarakani na siku ya pili yake nilisoma kwenye magazeti ndipo nikahakikisha.

  Wakili Haule: Nani alikupa taarifa kama mmiliki wa jengo anataka kulipwa kwa awamu mbili (akaunti mbili) tofauti?
  Mkapa: Kwa njia ya mdomo.

  Wakili Haule: Nani alikupa taarifa?
  Mkapa: Profesa Mahalu ndiye alinipa taarifa za kupata jengo.

  Wakili Haule: Alikupa kabla au baada ya ununuzi?
  Mkapa: Alikuwa ananipa taarifa kabla kwa sababu wakati huo kuna nchi zilikuwa na shida kama hiyo.

  Wakili Haule: Unasema ulitaarifiwa na hukuzuia kwani ulitakiwa kuzuia?
  Mkapa: Ningeweza kuzuia kwa sababu nilikuwa Mkuu wa nchi, lakini niliona umuhimu wake kama Profesa alivyonieleza.

  Wakili Haule: Ulimruhusu Profesa Mahalu kununua jengo kwa awamu mbili au?
  Mkapa: Nilimruhusu Mahalu kununua jengo masuala mengine hayakuwa mikononi mwangu.

  Wakili Haule: Wakati unatoa ruhusa hiyo kulikuwa na mtu mwingine?
  Mkapa: Hapana.

  Wakili Haule: Ulitoa kwa njia ya mdomo au simu?
  Mkapa: Ilikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana kabisa.

  Wakili Haule: Baada ya maagizo hayo nani mwingine ulimuagiza kuhusu ununuzi wa jengo hilo?
  Mkapa: Nilitoa maagizo utekelezaji ni suala la wizara.

  Wakili Haule: Sawa. Je, nani alihusika?
  Mkapa: Ilikuwa ni wajibu wake Profesa Mahalu kuieleza wizara yake kwamba hayo maamuzi yalikuwa sahihi.

  Wakili Haule: Kwa hiyo, wizara hukuiambia chochote bali ni Mahalu tu ni kweli au siyo kweli?
  Mkapa: Kama Rais ilikuwa wajibu wangu kutoa amri tu.

  Wakili Haule: Mheshimiwa jibu kama kweli au siyo kweli?
  Mkapa: Sikumbuki.

  Wakili Haule: Je, unafahamu kuna viongozi wengine uliowahi kuwateua wakati wa uongozi wako na wameburuzwa mahakamani?

  Mkapa: Ndiyo, nafahamu kuwa Basil Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja.

  Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi Ponsiano Lukosi, alimhoji shahidi kama ifuatavyo:

  Wakili Lukosi: Mheshimiwa, Lumbanga alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa utawala wako?
  Mkapa: Ni kweli.

  Wakili Lukosi: Aliongoza miaka mingapi?
  Mkapa: Miaka yote niliyokuwa madarakani.

  Wakili Lukosi: Sifa za Lumbanga na Mahalu zinalingana?
  Mkapa: Yah, ni sawa.

  Wakili Lukosi: Lumbanga alikanusha kufahamu mikataba miwili ni sawa?
  Mkapa: Nashangaa kama hili hakulijua.

  Wakili Lukosi: Ulizindua lini jengo hilo la ubalozi?
  Mkapa: Nilizindua Februari 23, mwaka 2003.

  Wakili Lukosi: Ulikwenda Italia kuzindua jengo au?
  Mkapa: Hapana, nilikwenda nchini Italia kikazi hivyo nikaalikwa kuzindua jengo hilo.

  Naye Wakili wa Utetezi Mabere Marando alimhoji shahidi kama hivi:

  Wakili Marando: Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) waliwahi kukuambia kama kuna uchafu umetokea kuhusu ununuzi wa jengo hilo?
  Rais Mkapa: Hapana hawakuniambia.

  Kesi hiyo inaendelea leo ambapo mshtakiwa wa pili, Grace Martin, atatoa ushahidi wake.

  ILIVYOKUWA MAHAKAMANI

  Mapema saa 3:45 asubuhi, Rais Mstaafu Mkapa, aliingia kwenye viunga vya mahakama hiyo akiwa kwenye gari yenye namba za usaji T 745 BQE aina ya Toyota Land Cruiser V8 ya rangi nyeusi pamoja na walinzi wake.

  Rais huyo maarufu kwa jina la Mzee wa Uwazi na Ukweli, alikuwa amevaa kaunda suti ya rangi ya kijivu na viatu vya rangi nyeusi na aliongozwa moja kwa moja hadi ofisi ya Hakimu Mfawidhi kwa ajili ya kusubiri muda wa kuingia mahakamani kutoa ushahidi wake.

  Saa 4:45 alianza kutoa ushahidi wa kumtetea Profesa Mahalu kwa kuongozwa na Wakili Mgongolwa hadi saa 7:17 mchana kisha kuondoka katika viwanja vya mahakama hiyo.

  Mapema jana saa 1:45 asubuhi NIPASHE lilishuhudia walinzi wa Rais huyo wa zamani wakiwa katika viunga vya mahakama hiyo kwa ajili ya maandalizi ya bosi wao kufika mahakamani hapo.

  Wakili Marando alisema kuwa Mkapa alipaswa kutoa ushahidi wake leo, lakini aliombwa kufika jana kwa kuwa leo atasafiri nje ya nchi.

  CHANZO: NIPASHE

   
Loading...