nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,862
- 5,797
Mwandishi Wetu
17 Aug 2011
Toleo na 199
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendeleza mchakato wa kujivua gamba na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiwafukuza madiwani wake watano wa mkoani Arusha, hali si shwari ndani ya NCCR-Mageuzi ambako kuna shinikizo la kumtaka Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, ‘kujivua' gamba.
Hali hiyo ndani ya vyama hivyo vya siasa inaendelea katika wakati ambao kipyenga cha uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga, Tabora kimekwishakupulizwa na NCCR kimetangaza hakitashiriki.
NCCR-Mageuzi kimetangza kutokushiriki uchaguzi huo na badala yake kitamuunga mkono mgombea wa chama kingine chochote ambacho hakijatajwa japo matarajio ya wengi ni kuwa hakitamuunga mkono mgombea wa CCM.
Taarifa za uhakika zinabainisha kuwa tayari vimekwishafanyika vikao viwili mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, kumshinikiza Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, chama kilichopata kuwa na nguvu kubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Mbatia, kujiuzulu nafasi hiyo.
Mbatia anashinikizwa kujiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kukiongezea nguvu chama hicho na ushahidi wa kushindwa kwake kinyang'anyiro cha ubunge Jimbo la Kawe, Dar es Salaam ni kati ya sababu zinazotumika kuthibitisha ya kuwa hana tena mvuto, ingawa yeye mwenyewe Mbatia anadai hiyo si sababu ya msingi.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, kimoja cha vikao vya shinikizo kwa Mbatia kilifanyika Agosti 13, mwaka huu, ofisini kwa mwanachama wa cha chama hicho, Dk. Seng'odo Mvungi, kikiwa kimetanguliwa na kikao kingine wiki mbili zilizopita.
Kikao hicho cha pili (Agosti 13) kinatajwa kufanyika ikiwa ni mwendelezo wa kikao cha kwanza ambacho Mbatia anadaiwa kukwepa shutuma zilizoelekezwa kwake na timu maalumu ya wazee wa chama hicho.
Mbatia anatajwa kukwepa shutuma kwamba amekipotezea mvuto NCCR-Mageuzi na kumsukumia shutuma hizo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Sam Ruhuza.
"Kikao kilifanyika ofisini kwa Dk. Mvungi Chuo Kikuu cha Bagamoyo, walikuwapo baadhi ya viongozi wakuu, lengo lilikuwa kumshawishi Mbatia ajiuzulu. Na ushawishi huo ulifanywa na timu ya wazee wa NCCR-Mageuzi ambao wamewakilisha maoni ya wanachama wetu wengi mikoani.
"Huko site watu wamepoteza imani na uongozi wa juu wa chama chetu. Wazee walimweleza namna anavyozidi kukosa sifa za kuendelea kuwa mwenyekiti, ikiwa ni pamoja na yeye binafsi tofauti na wenyeviti wenzake kupoteza ubunge si kwa CCM bali kwa chama kingine cha upinzani.
"Kushindwa chaguzi ni suala la kawaida lakini mazingira ya kushindwa huko ni suala muhimu sana kuzingatiwa kwa mustakabali wa chama kinachopaswa kujiongezea uhai. Mwenyekiti anaposhindwa ubunge kwa chama kingine cha upinzani na si CCM, maana yake hakubaliki na hiyo ni hatari kwa chama.
"Lakini pia wajumbe mikoani na wajumbe wengi wa kamati kuu wameridhika kuwa uongozi, hasa mwenyekiti, hana mawasiliano mazuri na viongozi wa mikoa. Yapo mengi ambayo hatutaki kuyazungumza hadharani kwa sababu wakati wake haujawadia.
"Kwa hiyo, katika kikao cha kwanza, Mbatia alikwepa shutuma hizo kwa maelezo kuwa huo ni udhaifu wa katibu mkuu na kwa bahati mbaya katibu mkuu hakuwapo na hivyo kikao kiliahirishwa hadi kikao kingine ambako katibu mkuu atakuwapo kujibu shutuma hizo.
"Kikao cha pili kilifanyika Agosti 13 na kwa kweli hakikufika mwisho kutokana na kuibuka vurugu alizoanzisha mwenyekiti baada ya kubanwa na wajumbe ajiuzulu," alisema mmoja wa wajumbe walioshiriki kikao hicho.
Kiongozi mmoja ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya NCCR anaeleza; "Mwenyekiti katika hali ya kawaida ni presidential material (mwenye sifa za kuwa rais) na hivyo kukosa ubunge ni doa kubwa, maana yake wananchi hawakukubali.
"Wenyeviti wengine, Freeman Mbowe, John Cheyo na Augustine Mrema wameshinda ubunge, wa kwetu amefeli tena kwa upinzani na kwa kura nyingi zaidi ya 30,000, mikoani chama kinakosa ushirikiano unaostahili kutoka kwa mwenyekiti hali hii haivumiliki ni lazima tuirekebishe mapema.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa katika kikao hicho Mbatia, akiungwa mkono na Dk. Mvungi anatajwa kujitetea akisema kushindwa ubunge si sababu kwake kujiuzulu uenyekiti akirejea mifano ya viongozi walioshindwa katika chaguzi mbalimbali, akiwamo Dk. Mvungi aliyepata kugombea urais na kushindwa.
Hata hivyo, licha ya utetezi huo wa Mbatia inaelezwa kuwa kuna shinikizo ni kubwa la kumtaka ajiuzulu kutoka ndani ya Halmashauri Kuu ya chama hicho na wajumbe wengine kutoka mikoa kadhaa.
Inadaiwa kuwa shinikizo hilo la Halmashauri Kuu ndiyo chanzo cha uongozi wa chama hicho kuahirisha mara kwa mara kikao cha Halmashauri hiyo Kuu ambacho kinatarajiwa kufanyika kuanzia mwezi ujao.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa uongozi wa chama hicho makao makuu jijini Dar es Salaam umegawanyika na baadhi ya viongozi waandamizi wanaunga mkono uamuzi wa kumtaka Mbatia kujiuzulu.
Hali hiyo inatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ni mwendelezo wa upepo wa kujivua gamba ili kuviongezea mvuto vyama husika vya siasa. CCM kilianza mchakato huo baada ya uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) kuwa viongozi wanaodaiwa wanakipunguzia haiba chama wajiuzulu, na tayari Rostam Aziz amefanya hivyo.
Wengine katika mkumbo huo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Monduli na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, huku viongozi wengine katika chama hicho wakizidi kuchambuana hadharani na safari hii mchuano wa kuumbuana ukiwa ni kati ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi dhidi ya wabunge wa mkoa huo, Iddi Azan wa Kinondoni na Musa Azzan Zungu wa Ilala na Abbas Mtemvu wa Temeke.
Dk. Masaburi amekwishawatuhumu wabunge hao kufumbia macho ufisadi katika baadhi ya miradi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zikiwamo mali za DDC na jengo la Machinga Complex.