Mjue Kanali Seif Bakari, ivumayo haidumu, asubuhi imekaribia

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
74,864
155,822
Unamjua mtu anaitwa Kanali Seif Bakari? Huyu ndie alikuwa kitendea kazi mhimu cha Mzee Karume katika utawala wake. Mathalani, Kiburi cha madaraka kilipokolea, Karume alianza kuwa mwiba kwa Mwl. Nyerere, hasa juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia Mwl. Nyerere kwa lugha ya dharau na bezo juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar. Na kuhusu akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimpa Mwl. Nyerere onyo kali, asithubutu kuitolea macho, akamwambia: “Fedha ya kichwa cha Malkia si yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa chako.” Na kuhusu Muungano, Karume alianza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti tu; likikubana unalivua.”

Ufa huu kati ya viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha Kamati ya Kupendekeza Katiba isiundwe na Bunge la Katiba lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya mwaka 1964. Wadadisi wa mambo ya siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada ya mwaka 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.

Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulikwisha chukua harakati za uasi wa umma, chini kwa chini, kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969. Kwa vigezo vyovyote vile vya utawala na uongozi, Karume alitawala kwa mkono wa chuma cha pua. Alitawala kiimla (utawala mkavu wa unyama) katika nyanja zote za maisha ya Wazanzibari kisiasa, kiuchumi na kijamii!―, pia alikuwa kero kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwl. Nyerere dhidi ya Muungano.

Kwa kusema haya, kitabu hiki hakitafsiri kwamba Karume hakutenda mema kwa Zanzibar na kwa Wazanzibari, bali kinajaribu kutafiti tu kuona ni mazingira na sababu zipi zilizochochea na kuharakisha kuuawa kwake. Ama huenda kati ya sababu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimuungano ndizo zilizoharakisha kifo chake. Tunajua kwa mfano, kwa baadhi ya Wazanzibari, Karume alitawala kikatili, mzandiki asiye na huruma wala hakujua kusamehe. Kwa upande mwingine, alikuwa na sifa za pekee nzuri kama kiongozi na binadamu; alikuwa mhimili na mtetezi wa Waafrika wa Kizanzibari na hakuyumbishwa na siasa za migogoro Visiwani. Alikuwa mwenye fikra zenye kujitegemea, alifanya maamuzi yake bila woga wala kuhofia matokeo; alikuwa kiongozi mwenye kuthubutu na mwenye kujituma.

Licha ya Karume kuitawala Zanzibar kwa mkono wa chuma cha pua, na namna alivyowaengua wote aliodhani hawakuwa upande wake ama kwa kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano, ama kwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, jamii ya Kiarabu wasio Wazanzibari, iliamriwa kuondoka, na wale Waarabu raia waliobaki, waliishi chini ya jicho kali la Serikali; waliweza kukamatwa, kama Wazanzibari wengine na kutiwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka. Walifanyiwa jinsi serikali ilivyofikiri inafaa; mashamba na mali zao zilitaifishwa bila kufidiwa. Wapo waliohukumiwa na Mahakama ya wananchi, kifungo na kuchapwa viboko. Kuonesha kwamba Serikali ya Karume haikuwa ya mchezo mchezo, akaionya jamii ya Ki-Athnasheri wa Kiajemi kwamba kama wangeendelea kuleta mgogoro, wangefukuzwa wote Zanzibar licha ya kuwa raia.

Karume alitangaza utawala wa chama kimoja cha ASP na kuamrisha kila Mzanzibari mtu mzima, kuwa mwanachama. Kila familia ilitakiwa kutundika picha ya Karume nyumbani, na ambaye angekaidi, alikuwa amefanya kosa la jinai lenye kustahili adhabu kali. Kikosi cha Usalama wa Taifa chini ya Kanali Seif Bakari, kilichopewa jina la Viwavi Jeshi, kilichofunzwa Ujerumani Mashariki kikaiva kwa mbinu za utesi na mauaji, kilipewa mamlaka ya kukamata, kutesa, kutia kizuizini na hata kuuwa bila mashitaka (yaani sheria iliwapa haki ya kua kama haki nyingine). Yeyote aliyelalamika, hata juu ya upungufu wa chakula tu, aliitwa adui (au mchochozi kama ilivyo sasa) wa Mapinduzi na hivyo mhaini. Enzi hizo, nduguyo akigongewa mlango usiku na kutakiwa kwa mahojiano na Serikali, usingemwona tena milele na milele.

Wakati wa Karume, wakati wa mkono wa chuma, hapakuwa na utawala wa Sheria wala Katiba. Amri za Rais ndizo zilizotawala nchi. Mapema mwaka 1966, mfumo wa mahakama wa kawaida ulipigwa marufuku; na Oktoba 1966, Rais alijipa madaraka ya kuteua mahakama maalumu za watu wasiozidi kumi na wanne (14), wenye mamlaka ya kusikiliza kesi za makosa ya kisiasa kama vile uhaini, uhujumu uchumi na wizi wa mali ya umma. Mahakama hizi hazikufungwa na kanuni zozote katika kusikiliza kesi; huduma za kisheria kwa watuhumiwa zilifutwa na mawakili kupigwa marufuku Zanzibar. Upande wa mashitaka ndio uliokuwa upande huo huo wa utetezi.

Yaani, mwendesha mashtaka wa serikali alipomaliza kuwasilisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa, aligeuka kuwa mtetezi wa mtuhumiwa huyo huyo. Ilikuwa vichekesho vya kutamausha. Mahakama hizi zilipewa uwezo wa kutoa hukumu ya kifo, iwapo waliona adhabu nyingine ni nyepesi kwa mtuhumiwa. Mwaka huo huo (1966), Baraza la Mapinduzi lilipiga marufuku haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki [EACA] na rufaa zote zikawa kwa Rais Karume pekee. Mwaka 1970, Karume alipitisha amri ya kuanzishwa mahakama (za kienyeji) za watu watatu. Mahakimu wapya wa mahakama hizo waliteuliwa na Karume mwenyewe kutoka miongoni mwa makada wa ASP. Moja ya sifa ya kuteuliwa ni kutokuwa msomi wa sheria, na ikiwezekana uwe hujui kusoma na kuandika....
 
Huu ndio uzuri wa historia naamini bwana huyu akiondoka madarakani tutaambiwa mengi Sana wanaomsifu Leo ndio watakaotuhabarisha mbivu na mbichi alizozitenda wakati wake hapo ndipo tutakapojua Ben alikuwa mifupa siku nyingi au atakuwa mzee mwenye mvi atakaeachiwa huru huko mbeleni. Muda ni mwalimu mzuri.
 
45442015_2555540554457828_2440163657515008000_n.jpg
 
Bujibuji hiki Kitabu gani?

Kanali Seif Bakari alinipigia bonge la pande moja la maisha alivyokuwa Naibu Waziri Wizara ya Ulinzi miaka ya tisini.
 
Hii historia siyo sahihi kabisa. Kuna mkanganyiko mwingi katika timeline yake na facts kuhusu matukio.

Muungano ulikuwa 1964, Azimio lilikuwa 1967, na akiba ya fedha inayoongelewa ni ya mwaka 1972 ambao ndio mwaka Karume aliuwawa.

Halafu kitu watu hawataki kuzungumza ni kuwa Karume alikuwa akitafuta sana ushauri kwa Nyerere katika maamuzi yote aliyokuwa akifanya.

Wakati wa krismas ya mwaka 1971 alikwenda Butiama kumwomba Nyerere ushauri fulani muda mfupi baada ya kifo cha Dr. Kleruu!

Halafu Kanali Seif Bakari pamoja na Kanali Moses Nnauye waliendelea kuwa wahamasiashaji wa jeshi miaka yote ya maisha ya utumishi wao hata wakati wa vita ya Uganda!
 
Hii historia siyo sahihi kabisa. Kuna mkanganyiko mwingi katika timeline yake na facts kuhusu matukio. Muungano ulikuwa 1964, Azimio lilikuwa 1967, na akiba ya fedha inayoongelewa ni ya mwaka 1972 ambao ndio mwaka Karume aliuwawa. Halafu kitu watu hawataki kuzungumza ni kuwa Karume alikuwa akitafuta sana ushauri kwa Nyerere katika maamuzi yote aliyokuwa akifanya. Wakati wa krismas ya mwaka 1971 alikwenda Butiama kumwomba Nyerere ushauri fulani muda mfupi baada ya kifo cha Dr. Kleruu! Halafu Kanali Seif Bakari pamoja na Kanali Moses Nnauye waliendelea kuwa wahamasiashaji wa jeshi miaka yote ya maisha ya utumishi wao hata wakati wa vita ya Uganda!
Mimi nimeshangaa, kwa ukaidi huo uliosemwa, amewezaje ku survive mpaka akawa Naibu Waziri wa Ulinzi mpaka miaka ya tisini?
 
Bujibuji hiki Kitabu gani?

Kanali Seif Bakari alinipigia bonge la pande moja la maisha alivyokuwa Naibu Waziri Wizara ya Ulinzi miaka ya tisini.
Aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Geita, vijana wengi waliosoma Geita Sekondari miaka ya '90 mwanzoni aliwaingiza Jeshini sana alipokuwa naibu waziri!
 
Aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Geita, vijana wengi waliosoma Geita Sekondari miaka ya '90 mwanzoni aliwaingiza Jeshini sana alipokuwa naibu waziri!
Kanali Seif Bakari kwangu alikuwa mtu poa sana, sijui kwa wengine.
 
Huu ndio uzuri wa historia naamini bwana huyu akiondoka madarakani tutaambiwa mengi Sana wanaomsifu Leo ndio watakaotuhabarisha mbivu na mbichi alizozitenda wakati wake hapo ndipo tutakapojua Ben alikuwa mifupa siku nyingi au atakuwa mzee mwenye mvi atakaeachiwa huru huko mbeleni. Muda ni mwalimu mzuri.
Tena huyu ni mbaya kuliko hata Karume na teacher
 
Back
Top Bottom