Mama huyo, Swabaha Mohamed (Shosi), aliangua kilio mbele ya JPM, kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, Februari 2, akimtuhumu wakili Alfred Akaro wa Tanga kwa kula njama na kughushi wosia wa marehemu Mohamed Yusufu Shosi.
Mbali na wakili huyo pia mama huyo aliwatuhumu watendaji wa vyombo vya utoaji haki kuwa wanamnyima haki. Mama huyo alidai pia kutishiwa maisha.
Kutokana na madai hayo, Rais Magufuli alimwagiza aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kumpa ulinzi mama huyo.
Pia, alimwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kushughulikia matatizo yake na ikiwezekana waihamishe kesi yake ya mirathi kutoka Tanga.
Kutokana na tuhuma hizo dhidi ya Wakili Akaro, wakili huyo na mwenzake Abubakari Shaaban, ambaye ni mfanyakazi wa familia ya marehemu Shosi walifunguliwa kesi ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga.
Katika kesi hiyo walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kughushi wosia wa marehemu Shosi na kuuwasilisha kwa familia ya marehemu Shosi.
Hata hivyo, katika hukumu iliyosomwa jana na hakimu Lutala aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alitupilia mbali tuhuma zilizokuwa zimetolewa na mama huyo dhidi ya wakili huyo na mwenzake.
Chanzo: Mwananchi