Mjadala wa kupanda au kushuka kwa elimu nchini

jyfranca

JF-Expert Member
Oct 3, 2010
297
8
DHANA ya elimu imekuwa ikifafanuliwa na watu kulingana na muktadha tofauti, hasa kutokana na namna ambavyo watu wanavyoona umuhimu wake kwa jamii. Mwono huo umechangia watu kuielezea elimu kama ‘kioo cha jamii’, ‘elimu ni mwanga’, ‘elimu ni maisha’, ‘elimu ni ufunguo wa maisha’, na ‘elimu kwanza’. Lengo la kauli hizo hulenga kueleza kuwa mtu anapopata elimu maana yake anakuwa katika mazingira mazuri ya kujitambua na kujiwezesha kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuwa injini ya maendeleo ya taifa kwa kutumia ujuzi na maarifa yake.

Ndiyo maana elimu ukawa msingi wa maendeleo ya nchi yoyote duniani, kwa kuandaa watalaam na wajuzi wa fani mbalimbali ambao, kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakisaidia kuandaa na kutunga sera. Mfumo wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu umeainishwa katika msingi wa maandalizi ya elimu kwa kujenga na kuandaa watu makini kwa ajili ya maendeleo ya watu na taifa. Pamoja na kuwepo kwa mfumo wa elimu nchini, swali la msingi ambalo limekuwa likiulizwa na wadau wa elimu ni kutaka kujua kama elimu ya Tanzania ni bora au siyo bora.

Ubora wa elimu ya Tanzania unaoulizwa na kujadiliwa katika makala hii ni ile ya chuo kikuu, ili kutaka kufahamu kama elimu inayotolewa nchini inawawezesha wahitimu wa vyuo vikuu kutoa njia muafaka kwa kutumia elimu yao kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake.

Aidha, dhana nyingine ya kutaka kujua ubora wa elimu ni kutaka kujua kama wahitimu wa vyuo vikuu nchini wanaweza kushindana kisoko hasa kama watapambanishwa katika soko la ajira na wahitimu kutoka vyuo vya nje.

Mshauri wa masuala ya elimu nchini Uingereza, Randall anaeleza ubora wa elimu unajengwa katika msingi wa namna gani watu wameweza kuelimika na wanaweza kushindana katika soko la ajira kimataifa.

Randall anaitolea mfano India kama nchi ambayo inaweza kujivunia ubora wa elimu yake, kutokana na kuandaa wataalam wengi wa afya ambao wamekuwa wakionekana bora kimataifa.

Kwa upange wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anayeshughulikia taaluma, Profesa Makenya Maboko akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini hivi karibuni, anasema Tanzania bado inajivunia ubora wa elimu yake kutokana na kuzalisha wataalam wanaoweza kushindana kisoko na wahitimu kutoka vyuo vya nje.

Maboko anasema msingi wa ubora wa elimu unatazamwa kwa kuangalia namna ambavyo wanaohitimu wanaweza kutumia ujuzi wao katika kufanya mambo na pia katika kushindana kisoko kimataifa.

Mathalan, anasema kama wanafunzi wanaomaliza elimu ya sokondari nchini wangekuwa hawana elimu ya kutosha wasingeweza kumudu masomo wanapokwenda kusoma nje ya nchi vyuo vikuu.

“Kuna wanafunzi wetu wanaosoma vyuo vikubwa duniani kama Oxford, Cambrigde, Havard, na North Carolina na wanafanya vizuri kuliko wanavyofanya waliosoma huko, huu ni mfano unaotuonyesha kuwa elimu yetu ni bora,”anasema Profesa Maboko.

Maboko anaeleza pamoja na kwamba kuna baadhi ya watu wanaosema elimu ya Tanzania imeshuka, lakini yeye si mmoja wa watu wanaomini katika hilo, kutokana na ukweli kwamba kuna mifano ya dhahiri inayoonyesha ubora wa elimu nchini.

Anasema kutokana na umuhimu wa elimu nchini wanafunzi kutoka nchini Uganda wamekuwa akijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kila mwaka kwa wingi, badala ya kujiunga na vyuo vikuu vilivyopo nchini mwao.

“Ada inayotozwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa wanafunzi wanaotoka Uganda ni kubwa, lakini hawajali hilo na wanazidi kuja kwa wingi , kitu ambacho siamini kama wanaweza kukimbilia chuo ambacho hakitoi elimu ya uhakika,”anaeleza.

Kimsingi, Profesa Maboko anawataka Watanzania kujiamini na kuthamini elimu inayotolewa nchini, hasa kutokana na ukweli kwamba imeandaliwa katika kuleta ushindani kisoko na ujuzi kimataifa.

Kama alivyoeleza mshauri wa masuala ya elimu nchini Uingereza , Randall, ubora wa elimu upimwe kutokana na ujuzi na maarifa ya wahitimu katika kushindana kisoko kimataifa.

Kwa mfano, Profesa Maboko anasema Tanzania imekuwa ikizalisha Maprofesa wengi na ambao wamekuwa chachu ya elimu nchini tofauti na nchi nyingine Afrika Mashariki.

Anafafanua kuwa karibia kila chuo kikuu nchini, mwanafunzi wake anafundishwa na watu wa kiwango hicho cha elimu, tofauti na ilivyo nchini Uganda na Kenya ambapo vyuo vingi vinafundishwa na walimu wa uzamili na uzamivu pekee.

Anatolea mfano, Chuo Kikuu cha Nairobi ndicho kilicho na Maprofesa huku vyuo vingine vikiwa havina wasomi wa kiwango hicho na wanafunzi wengi wamekuwa wakihitimu bila kupata kufundishwa wataalam hao.

Kwa msingi huo, anaamini kuwa Tanzania inaweza kukabiliwa na changamoto kadhaa katika kutoa elimu ya vyuo vikuu lakini siyo katika kuhitimisha kuidharau elimu hiyo.

Ili kuonyesha kuwa elimu ya Tanzania inakuwa, kinachotakiwa kuangaliwa ni pamoja na ongezeko la wanafunzi vyuo vikuu ambao ndio msingi na injini ya maendeleo ya watu na taifa.

Wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaanzishwa mwaka 1961, kilianza na wanafunzi 11 lakini ikiwa kinakwenda kutimiza miaka 50 mwakani, chuo hicho kimeweza kudahili wanafunzi zaidi ya 20,000.

Takwimu zinaonyesha pia kwamba, hadi kufikia mwaka 1969/1970, Chuo hicho kilikuwa na jumla ya wanafunzi 1,263 tu. Idadi hiyo iliongezeka taratibu mwaka hadi mwaka na ilipofika mwaka 2001/2002, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kilikuwa na jumla ya Wanafunzi 15,939.

Kwa mantiki hiyo, kama idadi hiyo inajumuisha chuo kimoja, vyuo vingine vya umma na binafsi idadi yao inadhihirisha wazi namna ambavyo kiwango cha elimu kinavyopanda.

Pamoja na kwamba kigezo cha ongezeko la wanafunzi kinaweza kisiwe muhimu zaidi kwa watu wengine, lakini msingi wa ongezeko hilo unaendana na ushindani wa kisoko katika soko la ajira kimataifa.

Hakuna shaka kuwa kuna changamoto kadhaa pamoja na kuonekana kwa ubora wa elimu nchini,, kitu ambacho kinatakiwa kushughulikiwa kuendana na matakwa halisia.

Moja ya changamoto ni ile anayoieleza Profesa Maboko kwamba wanafunzi wengi wamekuwa wakijua vitu vingi kutokana na taaluma zao, tatizo ni lugha ya Kiingereza kuvielezea na kuvifafanua vitu hivyo.

Profesa Maboko anaeleza kuwa kinachotakiwa kuondokana na tatizo hilo ni kuandaa mfumo bora zaidi ambao utawawezesha wahitimu wa vyuo vikuu kujiamini na kuifahamu lugha hiyo, ambayo hata hivyo sio kigezo cha ubora wa elimu.

Lugha bado inakuwa siyo kigezo kikubwa cha ubora wa elimu kutokana na nchi nyingi duniani kama China, India, Ureno, Ufaransa, na Uholanzi wanatumia lugha zao kufundishia na kigezo chao ni ujuzi na maarifa kwa wahitimu na siyo Kiingereza.

Lugha inatakiwa kutumika kuimarisha mawasiliano wakati wa kutoa huduma inayotokana na ujuzi alioupata mhitimu, ingawa ujuzi huo unaweza kuelezewa kwa lugha anayoifahamu vyema.

Ndiyo maana Wachina na Wahindi anaonekana wakiongea mchanganyiko wa Kiingereza na lugha zao na hakuna anayeshangaa isipokuwa , Mtanzania akifanya hivyo inaonekana hana kitu kichwani.

Dhana hiyo ya kujidharau na kujishusha imechangia watu wengi kushindwa kuthubutu katika ushindani wa kisoko kiajira na matokeo yake, kuwaacha wageni wanaochanganya lugha kuchukua nafasi hizo.
0000000000
L WAHITIMU wa vyuo vikuu wanatakiwa kuwa injini ya maendeleo ya taifa kutokana na ujuzi na maarifa wanayopata. Mfumo bora wa elimu ndiyo msingi wa ubora wa elimu wanayopata wahitimu hao

L UKUMBI wa Krumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na kutumika kama sehemu ya kufundishiwa wanafunzi pia, umekuwa ukitumika kukutanisha wasomi nchini kujadili masuala mbalimbali yanayoligusa taifa.




 
Yale yale ubora wa elimu ni wingi wa wanafunzi na sio kumpima aliyemaliza chuo
 
Back
Top Bottom