Mjadala wa Haki ya Ulinzi wa Data binafsi kupitia Clubhouse ya JamiiForums

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
625
938
1637248387196.png

Taarifa binafsi ni taarifa yoyote inayokutambulisha, iwe inahusiana na Maisha yako binafsi, Kitaaluma, au ya umma (Mfano: Majina, Namba za Simu, Anwani n.k)

Ni mara ngapi umeshakutana na taarifa za Watu wengine katika Mazingira ambayo hukupaswa kukutana nazo? Kama ni mara nyingi, basi huenda hata taarifa zako zinazagaa bila wewe kujua

Ungana nasi katika Mjadala wa Haki ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi kupitia Clubhouse ya JamiiForums muda huu Novemba 18, 2021.

Kujiunga gusa link hii hapa chini

UPDATES
Maxence Melo
: Data Binafsi ni Jina, Picha, Namba Binafsi, Kadi ya Utambulisho, Utaifa wako na Fingerprint. Hivi vyote vinakitambulisha wewe. Wakati mwingine Taarifa hukusanywa kwa nia njema. Changamoto ni kwamba wengi hawana namna ya kutunza Data.

Maxence Melo: Mpaka mwishoni mwa 2021, tutakuwa na vifaa vilivyoungana kidigitali takriban Bilioni 46. Kufikia mwaka 2030 tunategemea Vifaa Bilioni 145 vitakuwa vimeungana, taarifa za watu zitakuwa kwenye vifaa hivi.

Maxence Melo: Haki ya Faragha ni Haki ya Msingi ya kila Binadamu kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN). Kama taarifa binafsi zikiishia kwenye mikono isiyo sahihi, utajikuta unatumiwa matangazo ambayo hata hukutarajia.

Maxence Melo: Lazima Sheria au Taratibu inayowekwa na Taasisi au Mamlaka yoyote uweke mipaka ya taarifa zinazochukuliwa. Utaratibu huo lazima uweke mipaka ya taarifa zinazochukuliwa. Pia, taarifa zinazochukuliwa ziwe sahihi kuhusu wewe.

Maxence Melo: Mamlaka inayoweka Utaratibu wa Ulinzi wa Faragha za Watu inatakiwa kuweka kwa Lugha rahisi na inayoeleweka ili mtu anayetaka kuacha taarifa zake aelewe.

Maxence Melo: Faida za kuwa na Sheria hizi, kwanza inahamasisha kampuni ya biashara, iweze kuja iliwa na uhakika wa faragha. Ukiangalia wenzetu Kenya, 2019 walitunga Sheria. Baada tu ya Sheria kutungwa wawekezaji wengi walikimbilia Kenya.

Maxence Melo: Kwa Tanzania, mbali na Katiba hatujawa na Mwongozo unaotuongoza, kwa Bara la Afrika kuna takriban Nchi 42. Naamini Suala la Privacy ni Utu wa mtu unaotakiwa kulindwa kwa utaratibu unaoeleweka.

Maxence Melo: Tuna Sheria nyingi ambazo hazijazingatia Misingi ya Ulinzi wa Taarifa. Hatari ambayo naiona mbele ni utaratibu haupo, na Sheria hazitoi urahisi kwa mtu ambaye Haki yake itakuwa imevunjwa na Wakusanya Taarifa.

Maxence Melo: Kuna Sheria ya Uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA 2015, japo ni TEHAMA haijaweka Misingi ya Taarifa kulindwa. Pia kuna Sheria ya Ndoa, Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sheria ya Mawasiliano, Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sheria ya Serikali Mtandao.

Maxence Melo: Tulifanya utafiti mdogo kuuliza kwanini watu walijisajili NIDA, wengi walisema walisajili kupata Laini za Simu. Tumetafutwa na watu wa mikoani wanaosema wameambiwa laini zao zitafungwa.

Maxence Melo: Service Providers wa Kidigitali wanakusanya vitu vingi sana. Ukijua nini wanajua kuhusu wewe kuna uwezekano ukachukua laini ukatupa. Ukiweza ifuate Kampuni ya Mawasiliano ya Simu kudai Taarifa walizonazo juu yako. Ni Haki yako.

Maxence Melo: Ukishawekwa Utaratibu utasimamia mambo yote. Hatuzuii ukusanyaji wa taarifa lakini kuwe na 'consent'. Data zinazokisanya hasa na Taasisi binafsi zinaenda mbali zaidi ya vile tunavyofikiri. Mfano Data za WhatsApp, Facebook Utaratibu utaweza kuwasimamia.

Mdau 1: Sasa hivi tunaweza kusema Taarifa Binafsi za Mtu hazilindwi. Juzi hapa tumeona Tigo wametoa Faragha za mtu bila ruhusa. Hii ni mbaya.

Kuwe na Mikataba kati ya Mtu na Kampuni za Mawasiliano za Simu, watu wengi siri zao zimetoka lakini hawajui cha kufanya. Elimu itolewe.

Dkt. Ndugulile: Masuala ya Data ni jambo linaloongelewa sana Duniani kwasababu wengi wanajua kwamba 'Data is the New Oil'. Nakiri Data hazisimamiwi vizuri. Sheria zetu nyingi hazina mwamvuli wa kusema zinasimamaia kwa ukamilifu taarifa za Watu.

Dkt. Ndugulile: Nilipokuwa Serikalini tulianza kutengeneza Andiko linalozingatia Matumizi ya taarifa za Watu. Tumejaribu kuangalia ukusanyaji, nani anakusanya, matumizi na zinatunzwa kwa muda gani, zinatumiwa vipi nje ya mipaka ya Nchi na kuangalia namna ya kuweka Utaratibu?

Dkt. Ndugulile: Tuliweka mfumo kwamba kuwe na idhini ya Mteja kwa yule anayekusanya taarifa zake na aridhie namna zinavyokusanywa, zinavyotumika na zitatuzwa kwa muda gani? Niwape Moyo kuwa Andiko ni nzuri na Serikali itakapowashirikisha Wadau naamini tutalinda taarifa binafsi.

Mdau2: Je, tufanyeje ili kuepuka na madhara ya kutoa taarifa zetu. Je, tudanganye?

Dkt. Ndugulile: Mimi sio Mtu sahihi wa kusema Watu wadanganye taarifa zao lakini changamoto ni Wahudumu wanatakiwa na Sheria kukusanya taarifa lakini hakuna Utaratibu zinakwenda wapi, wanazikusanya vipi. Uwekwe Utaratibu wa nani anakusanya na kuwajibika ikitokea uvujaji wa taarifa.

Dkt. Ndugulile: Hata sisi ambao tunatoa taarifa hatujui taarifa zetu zinatumika namna gani ndio maana Mtu anaweza kutoa taarifa zaidi ya zile zinazohitajika. Hatujui taarifa zetu zinatumikaje, hivyo Utaratibu uwepo ili kuzifanya Taasisi zisikusanye taarifa zaidi ya zinazohitajika.

Maxence Melo: Ni jukumu letu sisi kama Wananchi kulinda katiba ya Jamhuri ya Muungano sio ombi, na ibara ya 16 ipo wazi. Lakini pia tuendelee kuhamasisha mamlaka zione umuhimu wa kutungwa sheria hii. lakini pia upande wa uwajibikaji ingate pande zote.

Maxence Melo: JamiiForums kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Twaweza, TLS, Paradigm Initiative, CIPESA, LHRC n.k tunaandaa Muswada mbadala ambao unalenga kuipa Serikali jicho la pili inapoenda kutunga Sheria husika

Aidan Eyakuze: Licha ya Sheria za Ulinzi wa Data Je, sisi kama Taifa tuna Mkakati gani wa Kiuchumi wa Data za Kidigitali? Makampuni yanakusanya taarifa zetu na kuzitumia kujipatia faida, vipi kuhusu sisi ambao ni wazalishaji wa hizo taarifa tunafaidikaje?
 
Hio clubhouse ni nini jamani tutoeni ushamba
Mkuu Rebeca salaam,

Ni App ambayo inatumiwa kuendesha mijadala mbalimbali mtandaoni. Inakupa nafasi ya kushiriki, kutoa mawazo yako na kuuliza jambo lolote kulingana na mjadala uliochagua.

Ipakue kutoka Playstore au App store, iweke kwenye simu kwa kufuata taratibu zote kisha gusa link ili kunufaika na mjadala
 
Mkuu Rebeca salaam,

Ni App ambayo inatumiwa kuendesha mijadala mbalimbali mtandaoni. Inakupa nafasi ya kushiriki, kutoa mawazo yako na kuuliza jambo lolote kulingana na mjadala uliochagua.

Ipakue kutoka Playstore au App store, iweke kwenye simu kwa kufuata taratibu zote kisha gusa link ili kunufaika na mjadala
Asante sana kwa ufafanuzi mkuu
 
Back
Top Bottom