Mjadala Kuhusu Nafasi ya Vyama Vya Siasa Baada ya Uchaguzi 2005

Paparazi Muwazi

JF-Expert Member
Dec 23, 2007
310
79
Aprili 17, 2008


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu, Wanahabari,

Asasi ya Maendeleo Tanzania; “Tanzania Development Initiative Programme (TADIP), imeandaa mjadala kujadili “Nafasi ya vyama vya siasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005” utakaofanyika kwenye ukumbi wa Rombo Green View Hotel Jumamosi Aprili 19, 2008 kuanzia saa 04:30 asubuhi hadi saa 10:30 jioni.

Mjadala huu unatarajiwa kushirikisha wawakilishi 120 kutoka kwenye asasi za kiraia, vyama vya siasa, (wakiwemo viongozi wa kitaifa na wanasiasa), taasisi za serikali, taasisi za elimu ya juu, vyombo vya habari, wanahabari, asasi za wanawake, taasisi za kidini, vijana nakadhalika.

Muwasilishaji Mkuu wa mada anatarajiwa kuwa Ndugu Mabere N. Marando – wakili wa kujitegemea atakayewasilisha mada ya “Nafasi ya vyama vya siasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2005”. Mada hii pia itachangiwa na mtoa mada mwingine ndugu Bashiru Ally na mjadala utaongozwa na Dr. Benson Bana, wote kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala – Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Mada hii itafuatiwa na mjadala wa kina kutoka kwa washiriki wote.

Ikumbukwe kuwa mjadala huu ni sehemu ya mfululizo wa Mjadala wa Maendeleo almaarufu “Maendeleo Dialogue” inayoitishwa mara kwa mara na TADIP kwa kushirikiana na shirika la Kijerumani la Konrad Adenauer Stiftung (KAS). Lengo na ajenda ya “Maendeleo Dialogue” ni kuchochea Utawala bora, uhuru, uchumi wa soko la kijamii, usawa wa fursa, ujasiriamali, maendeleo ya taasisi za kidemokrasia, na utawala wa sheria nchini Tanzania kupitia mijadala na utoaji wa elimu ya uraia.

Kimsingi, mjadala wa mwezi huu unalenga kuviamsha vyama vya siasa kutathmini ubora na udhaifu wao baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, na kutathmini nafasi ya mfumo wa sasa wa kisiasa hasa mfumo wa uchaguzi kama unakidhi haja na matakwa ya ukuaji wa demokrasia.

Inatarajiwa kuwa kufikia mwishoni mwa mjadala huu, wadau watakuwa wametoa mapendekezo kadhaa na kuazimia kwa pamoja kuchukua hatua za kuimarisha vyama vya siasa kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kuboresha mfumo wa kisiasa iwapo kutajitokeza haja ya kufanya hivyo.


Zipo haja na hoja kadhaa zilizopelekea TADIP kuitisha mjadala wenye mada hii katika kipindi hiki.

Kwanza, huu ni mwaka wa tatu tangu kuisha kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na ni mwaka wa pili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine wa 2010. Kwa mantiki hiyo, huu ni wakati wa vyama pinzani kuangalia hadi sasa vimefanya nini katika kujiimarisha kisiasa ili visifanye vibaya katika chaguzi zijazo, na wakati huohuo huu ni wakati wa chama kilicho madarakani kujitazama kimetimiza kwa kiasi gani ahadi zake na kina nafasi gani kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Yote hii inalenga kujenga mazingira ya demokrasia yenye ushindani ili kuchochea uhuru, amani, na maendeleo kwa mwananchi wa kawaida.

Pili, ikumbukwe kuwa uchaguzi mkuu wa 2005 uliisha kwa kuacha changamoto mbalimbali ambazo vyama vya siasa na wadau wa demokrasia kwa ujumla, wanapaswa kuzitanzua kwa pamoja. Baadhi ya changamoto hizo ni kama ifuatavyo;


• Vyama vya siasa hasa vile vya upinzani vilipata matokeo mabaya kinyume na matarajio ya wengi jambo lililoamsha hisia kuwa ama vyama hivi vilikuwa ni dhaifu mno au uchaguzi haukuwa huru na haki.
• Malalamiko juu ya mfumo wa uchaguzi unaopendelea chama dola na kutokuwepo kwa tume huru ya uchaguzi yaliendelea kutamalaki.
• Uchaguzi wa 2005 pia uliendelea kuchochea haja ya kuandikwa kwa katiba mpya miongoni mwa wadau.
• Elimu ndogo ya uraia kwa wananchi ilionekana kuwa bado ni tatizo katika ujenzi wa demokrasia nchini.

Kwa ujumla, changamoto hizi na nyingine nyingi zinahitaji kujadiliwa ili kujua vyama vya siasa na wadau wengine wa demokrasia wamefanya nini hadi sasa kutanzua masuala haya, na wanafikiria kufanya nini ikiwa hali bado ni mbaya.

Tatu, izingatiwe kuwa baadhi ya mambo yaliyosababisha matatizo ya kisiasa yaliyotokea katika nchi jirani ya Kenya, kama vile kutokuwa na tume huru ya uchaguzi yanaweza kusababisha hali hiyo hiyo nchini katika siku za usoni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. Ni kwa kulizingatia hilo pia, ndipo TADIP ikishirikiana na KAS inapoitisha mjadala huu ili kutoa fursa ya kubaini matatizo ya kisiasa na kuyapatia ufumbuzi wa haraka.

TADIP inatoa mwito kwa wanahabari kuhudhuria mjadala huo na kuuarifu vyema umma wa Watanzania juu ya yote yatakayojiri katika mjadala huo. Aidha, TADIP inachukua fursa hii kuvishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari kwa kuendelea kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa kwa umma hususani zile za kuchochea maendeleo, demokrasia, na kufichua mafisadi.

Tanzania Development Initiative Programme (TADIP) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na watanzania wenye nia ya dhati ya kuona kunakuwa na maendeleo ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini Tanzania. TADIP ilisajiliwa Septemba 19, 2006 kwa hati ya usajili namba Cap 212, chini ya sheria ya makampuni ya mwaka 2002 ya Tanzania. Hii ni asasi isiyotengeneza faida wala kufangamana na upande wowote ikiwa na dira ya; kuona jamii ilitaarifika, huru, nay a kidemokrasia. Dhima kuu ya TADIP ni kuchochea mijadala kupitia ushawishi, mahusiano ya umma, na shughuli za uwezeshaji.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania


Imetolewa na kusainiwa na:

Steve A. Mmbogo.
Mratibu wa Programu– TADIP
Email; veste2007@yahoo.com
Cell; 0714 77 66 73
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom