Mizengwe yaanza Wizara ya Nishati - Katibu Mkuu ahujumiwa kwa kudhibiti ulaji | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mizengwe yaanza Wizara ya Nishati - Katibu Mkuu ahujumiwa kwa kudhibiti ulaji

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Jul 16, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jul 16, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Mwandishi Wetu Raia Mwema -

  Toleo la 247
  11 Jul 2012


  • Katibu Mkuu ahujumiwa kwa kudhibiti ulaji
  • Wamkimbilia Waziri Prof. Muhongo, awaruka
  • Mtandao wahusisha bodi, wabunge

  BAADHI ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini wakishirikiana na wenzao ndani ya mashirika na taasisi tanzu za wizara hiyo, wamekuwa wakihujumu jitihada za sasa za kuirejesha wizara katika mstari, Raia Mwema limeambiwa.


  Jitihada hizo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari serikalini, zimekuwa pia zikiwahusisha kwa karibu baadhi ya wenyeviti wa bodi za mashirika na taasisi hizo na watendaji wakuu wake ambao wanahisi ya kuwa, kwa mazingira mapya wizarani, ajira zao zinakaribia ukingoni kutokana na ama utendaji binafsi usiokidhi au kwa kushindwa kudhibiti uozo katika taasisi na mashirika yao.

  Habari zaidi zinasema sasa upo mtandao wa makundi hayo ulioungana kuendesha kampeni ya kuukataa uongozi wa wizara kwa madai kwamba umekuwa ukiendesha mambo kibabe japo wengi nje ya wizara hiyo wanauona uongozi huo kuwa uliodhamiria utendaji kazi kwa viwango vya juu, urejeshaji imani ya umma kwa vyombo vya utoaji huduma na udhibiti mali na mapato ambao ulikwishakukosekana, na ambao ndio uliokuwa ugonjwa mkubwa ndani ya wizara na katika mashirika na taasisi zake.


  Raia Mwema
  limedokezwa pia kwamba nje ya wizara, taasisi na mashirika yake, mtandao huo unaungwa mkono na baadhi ya wabunge, wengine wakiwa katika kamati zinazohusiana na wizara hiyo, na kwamba mipango inayosukwa ili kupeleka ujumbe kwa mamlaka husika kuwa uongozi wa wizara haufai, uondolewe, ni pamoja na kukwamisha bajeti ya wizara itakayowasilishwa bungeni kiasi cha wiki mbili kuanzia sasa.


  Hoja nyingine zanazodaiwa kushadidiwa na mtandao huo kama sababu za ziada kutaka mabadiliko ya uongozi wizarani ni kuwa Waziri mpya, Profesa Sospeter Muhongo, si mwanasiasa, ubunge wake uliompa uwaziri umetokana na yeye kuteuliwa na hilo linawakera baadhi ya wabunge wa majimbo ambao wanaona si vyema wao kuachwa, mtu wa "kuja" akapewa nafasi hiyo kubwa tena katika wizara inayotajwa kuwa tajiri na yenye ulaji kama ya Nishati na Madini.


  Ukiacha hilo, Raia Mwema limeambiwa pia ya kuwa madai mengine ni suala ambalo chimbuko lake ni ukabila. Waziri Profesa Muhongo anatoka Mkoa wa Mara ambako ndiko anakotoka pia Katibu Mkuu, Eliachim Maswi, ingawa inafahamika kwamba wanatoka katika maeneo mawili tofauti ya mkoa huo. Kwa mujibu wa madai ya wana mtandao huo, Profesa Muhongo na Maswi kuwa wanatoka katika Mkoa mmoja na sasa wanafanya kazi ofisi moja ni tatizo.


  Maswi mwenyewe alipoulizwa na Raia Mwema juu ya madai hayo, mwanzoni mwa wiki hii, alisema hana namna ya kuzuia watu wasizungumze wanayoyataka. Alisema yawepo au yasiwepo, yeye na timu wanayoijenga wizarani wameamua kufanya kazi ili kuleta tija katika maeneo waliyokabidhiwa kuyasimamia.


  " Rais Jakaya Kikwete aliyetuteua hakufanya hivyo ili tuje hapa tuchezecheze. Tumepewa majukumu ya kutekeleza. Hebu niambie, nyumbani kwako siku hizi umeme unakatika mara ngapi?


  "Ukiona kuna mawazo kama hayo, ujue tunafanya kazi. Sisi hatutajali yanayosemwa, kipimo chetu ni kama umma unaridhika. Kama unaona baadhi ya kero zilizokuwapo, zilizokuwa ndani ya uwezo wetu, sasa zimepungua kwenye vitu kama umeme, na kama tumeanza kupata stahili yetu kwenye maeneo kama ya migodi ujue wizarani sasa kuna wachapakazi," alisema Maswi.


  Katibu Mkuu Maswi aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Kaimu Katibu Mkuu katikati ya Julai mwaka jana, kiasi cha mwaka mmoja uliopita, akichukua nafasi iliyokuwa imeachwa na David Jairo aliyekuwa ametuhumiwa na Bunge, pamoja na mambo mengine, kwa ubadhirifu.


  Aidha, Profesa Muhongo, mmoja wa Watanzania wachache wataalamu wa jiolojia, amejiunga serikalini mwanzoni mwa Mei, mwaka huu, baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete kwanza kama mbunge kupitia nafasi 10 za Rais kuteua wabunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


  Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ni Shirika la Umeme (TANESCO) ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Jenerali mstaafu na mkuu wa zamani wa Majeshi, Robert Mbona, Mtendaji wake Mkuu ni Mhandisi Godfrey Mhando.


  Mengine ni EWURA ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Simon Sayore; huku Mtendaji Mkuu akiwa Haruna Masebu; Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Balozi Ami Mpungwe na Mtendaji Mkuu ni Dk. Dk Lutengano Mwakahesya; Wakala wa Madini (TMAA) ambalo Mwenyekiti wake wa Bodi ni Dk. Yamungu Kayandabila, Mtendaji Mkuu akiwa Mhandisi Paul Masanja.


  Mengine ni STAMICO ambalo Mwenyekiti wa Bodi ni Ramadhani Omari Hatibu, Mtendaji Mkuu akiwa Grey Mwakalukwa; GST lililo chini ya Uenyekiti wa Bodi wa Profesa Idrissa Kikula na Mendaji Mkuu akiwa Prof Abdul Mruma na TPDC ambalo Mwenyekiti wake ni Michael Mwanda na Mtendaji Mkuu ni Yona Kilagane.


  Kwa karibu mwaka mmoja sasa huduma kama ya umeme imekuwa ikitengemaa baada ya nchi kuwa imeingia katika mgao miaka iliyopita hali iliyoilazimisha Serikali kuanza kutegemea umeme wa kuuziwa na mashirika binafsi ambayo yalichipuka kufuatia mgao huo, mengi yakivuna mapesa mengi katika biashara hiyo na moja kati hayo likizua kashfa ambayo ilimlazimisha aliyekuwa waziri mkuu wa miaka ya mwanzo ya awamu ya Rais Kikwete, Edward Lowassa, kujiuzulu katika kile kilichojulikana kama kashfa ya Richmond.


  Ulaji mwingine ambao Katibu Mkuu kwa kushirikiana na viongozi wenzake wameudhibiti ni ule uliokuwa ukifanyika katika sekta ya madini nchini.


  Ulaji huo ulikuwa ukizihusisha kampuni tatu za uchimbaji madini nchini ambazo sasa zimetakiwa kulipa malimbikizo ya kodi ambazo awali hazikuwa zikilipwa.


  Kampuni hizo ni Tanzanite One inayoendesha uchimbaji wa madini ya vito aina ya tanzanite, Mererani mkoani Arusha, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) na Kampuni ya Resolute (Resolute Mining Tanzania Ltd).


  Kampuni hizo zimetakiwa na uongozi wa sasa wa Wizara ya Nishati na Madini kulipa zaidi ya dola za Marekani milioni 5.2 (zaidi ya Sh bilioni nane). Bado haijulikani "uvumilivu" wa awali miongoni mwa waliokuwa viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini uliofanya kampuni hizo kutolipa kodi hiyo ulikuwa unatokana na nini hasa.


  Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Raia Mwema inazo, kampuni hizo zinakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kulipa kodi hizo, shinikizo linaloambatana na dalili za kuwekewa vikwazo.


  Kati ya vikwazo vinavyoambana na shinikizo la kuzitaka kampuni hizo kulipa fedha hizo ni pamoja na Kampuni ya Tanzanite One kuwa katika hatari ya kupewa leseni baada ya leseni yake ya sasa kwisha muda wake.


  Lakini wakati Tanzanite One wakikabiliwa na shinikizo la namna hiyo, kampuni za uchimbaji dhahabu za GGML na Resolute zinaweza kunyimwa leseni za kusafirisha madini nje ya nchi.   
 2. Kimbunga

  Kimbunga Platinum Member

  #2
  Jul 16, 2012
  Joined: Oct 4, 2007
  Messages: 13,011
  Likes Received: 1,816
  Trophy Points: 280
  Ndugu Maswi hiyo ndiyo mitandao ya ulaji. ukiitikisa inakuwa migumu kweli na ukicheza inakuengua wewe. Pambana tu kwa kuwa yana mwisho haya. Kila mpenda nchi apambane pahala pake wataondoa lakini mwisho wake watashindwa.
   
 3. E

  Erasto..sichila Member

  #3
  Jul 16, 2012
  Joined: Apr 9, 2012
  Messages: 77
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mi namujua katibu mkuu siyo mtu mzuri anaweza kutengeneza fitina kwa mhando wazi wazi huyo anamambo binafsi mfn mkewe wakwanza alimwacha bila huruma hadi sasa ni kichaa wa barabarani pia mke aliyena alipora mchumba wa mtu pale magereza sasa yote pimeni mujifunze juu ya buyo bwana fitina muhando ni kweli anafanyiziwa kama yule wa mhando wa Tbc
   
Loading...