misingi ya utoaji talaka haki ya kuishi na mtoto baada ya ndoa kuvunjika | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

misingi ya utoaji talaka haki ya kuishi na mtoto baada ya ndoa kuvunjika

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by kilimasera, Apr 17, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 17, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  tunaangalia kwa kifupi masuala mbalimbali yahusuyo Sheria ya Ndoa nchini Tanzania ambapo tunajikita zaidi katika misingi ya utoaji talaka na mambo yazingatiwayo katika kugawana mali za familia ambayo ndoa yake imevunjika. Tuliahidi pia kuzungumzia nani anastahili kupatiwa haki ya kuishi na mtoto au watoto baada ya ndoa kuvunjika. Na hiki ndicho tunachokitizama sasa.
  Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 (toleo la 2002) ambayo ndiyo sheria mama inayotawala masuala yote kuhusu migogoro, haki, wajibu na masuala yanayohusu mgawanyo wa mali na watoto imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu misingi na vigezo vinavyotumika katika kufikia uamuzi wa nani apatiwe haki ya kuishi na mtoto pale wanandoa wanapofarakana na kutengana ama kuachana kwa talaka.
  Yote haya yameainishwa katika sehemu ‘h’ ya sheria hii, na hasa kuanzia kifungu cha 125 hadi 137, vinaposomwa kwa kuangalia vifungu vinginevyo vya sheria hii na sheria nyinginezo husika za nchi, ikiwemo Katiba.
  Kifungu cha 125 cha Sheria kinaipa mahakama husika uwezo wa kutoa amri ya kimahakama kwa upande fulani wa ndoa kupewa haki ama fursa ya kuishi na mtoto, maarufu kimombo kama custody.
  Hata hivyo mzazi anayepewa fursa hii hapaswi kubweteka kwa sababu haki hii mara nyingi, kama si zote, hutolewa kwa masharti yaliyo kwa mujibu wa sheria au yale ambayo Hakimu ama Jaji anayesikiliza shauri anaona inafaa kwa maslahi ya mtoto na jamii nzima na pia kwa ajili ya kutendea haki pande zote mbili zinazohusika.
  Ndiyo kusema basi, itokeapo kwamba masharti yaliyotolewa wakati wa kumpa mzazi haki ya kuishi na mtoto yakaacha kuzingatiwa, basi mahakama ina uwezo wa kutoa uamuzi mbadala, ukiwemo wa kumnyang’anya mhusika fursa hiyo kwa kupoteza sifa alizokuwa nazo awali.
  Kifungu vya 127 kinagusia kuhusu uwezo wa mahakama kutamka kukosekana kwa sifa za mzazi au wazazi kuishi na mtoto wakati kifungu kinachofuata kinaeleza kwamba haki ya kuishi na mtoto itachukuliwa kuwa jambo halali kwa vile lilivyo machoni mwa sheria; wakati ambapo kifungu cha 129 kinatoa wajibu wa mzazi au wazazi kuhakikisha mtoto anakuzwa, kulelewa na kuhudumiwa ipasavyo kwa ustawi wake kamili (maintenance).
  Sehemu zinazofuata ndani ya sheria hii zinaelezea kuhusu mamlaka mengienyo iliyonayo mahakama katika masuala kama ni kwa kipindi gani mzazi fulani atapaswa kuishi na mtoto baada ya ndoa kusambaratika na pia utaratibu wa kubadilisha masharti yaliyotolewa kuhusu kuishi na mtoto husika au hata kuingilia na kuelekeza kufanyika kwa mipangilio mbadala kuhusiana na makubaliano ya wazazi walioachana katika kuishi na mtoto.
  Baadhi yetu wanaweza kusema kuwa vipi tena mahakama iingilie uhuru wa wazazi kuhusu mtoto wao wenyewe kama wanakubalina kuhusu makuzi yake hata baada ya ndoa kuvunjika? Jibu la swali hili si gumu.
  Ukweli ni kuwa kihistoria na takribani kote duniani, maslahi ya wazazi hayaangaliwi kama yalivyo maslahi ya mtoto mwenyewe.
  Maana ya hili ni kuwa ,jamii yenyewe imeona ni haki na hekima kuingilia katika kulinda haki na ustawi wa mtoto kwa sababu mtoto anakuwa hajakua au kuwa na uwezo wa kujisemea kikamilifu katika masuala yanayohusu maslahi yake katika familia.
  Na suala jingine la kujiuliza ni hili: Ingekuwaje kama wazazi wangepewa madaraka ya mwisho katika kuamua kuhusiana na masuala ya mtoto wao (hasa unyumba unapokuwa katika mgogoro) na ikatokea kuwa wazazi wote hawafai katika malezi ya mtoto, kama vile hawaachi kutukana matusi makali ya nguoni kila kukicha au wana tabia ya kupeana vichapo au kumpa vipigo mtoto wao au kumfanyanyisha kazi kama punda bila kumpa fursa ya kujisomea au kupumzika?
  Au ikatokea wamemdekeza kupita kiasi kwamba anakuwa mfano mbaya na si taa kwa jamii? Au wao wakawa walevi kupindukia na wakimuacha bila chakula au mazingira mzuri ya kuishi?.
  Ili mradi tu yapo matukio mengi ambayo yamemnyima mzazi au wazazi fulani haki ya kuishi na mtoto wao yakiwemo yale ya kuogofya kama ubakaji ndani ya familia na hata kumtumia mtoto kama kitega-uchumi kimapenzi.
  Yote haya tumeyashuhudia au kuyasikia katika vyombo vya habari na ndiyo yanayoipa jamii mamlaka makubwa zaidi ki-mizania ya kuamua kuhusu maslahi ya ustawi wa mtoto kuhusu wazazi, inagawa ki-ukweli bado wazazi ndio wenye maamuzi muhimu ya kila siku kuhusu uelekeo wa mtoto.
  Nimeyazungumzia haya kwa vile ni baadhi ya mambo yanayozingataiwa katika uamuzi wa nani aishi na mtoto. Basi kama mzazi fulani anaonekana ana dosari kama utumiaji mihadarati au ulevi uliopindukia basi navyo ni vigezo vinavyozingatiwa kumnyima haki ya kuishi na mtoto na kinyume chake mambo kama mzazi anayejali elimu, mwenye uwezo wa kumhudumia mtoto, mwenye kiwango cha ustaarabu kinachokubalika kifamilia, kwa majirani na jamii.
  Vile vile suala kama mwenye kujali ibada kufuata kanuni za usafi, afya na usalama wa familia na mtoto, kumjali mtoto kimavazi na bila kusahau mapenzi na upendo wa dhati, hivi vitaangaliwa kama sifa za mhusika kuelekea kupatiwa mtoto.
  Hata hivyo, ukiacha haya (au pamoja na kuzingatiwa haya), kuna nadharia fulani fulani zitumikazo na mahakama katika kutolea uamuzi nani aishi na mtoto. Moja ya zile zizingatiwazo zaidi kuliko zote ni kujiuliza swali: Maslahi ya mtoto yatalindwa zaidi akiachwa aishi na mzazi yupi?
  Hili ndilo swali la kwanza na la msingi ambao mahakama hujiuliza tangu mwanzo hadi mwisho wa usikilizwaji wa mashauri ya kugombea kuishi na mtoto. Kama tulivyoona hakuna jibu moja katika swali hili, na sababu tulizozitaja hapo juu pamoja na nyinginezo kama vile utashi na mapenzi ya mtoto mwenyewe kupenda aishi na mzazi yupi (japo hili huangaliwa kwa uangalifu na mahakama kwa vile wapo wazazi wasiostahili kuishi na mtoto na wametokea kumrubuni mtoto atoe ushahidi wa kuwanufaisha wao) na ushahidi vitazingatiwa.
  La pili liangaliwalo sana ni nadharia kuwa mtoto anapokuwa mchanga au mdogo zaidi, na hasa chini ya miaka saba, na zaidi chini ya miaka miwili, kushuka chini, basi mara nyingi mama anaonekana kuwa na sifa zaidi ya kupewa haki hii, na hasa ionekanapo mama hana dosari za kumnyima fursa hiyo au pale ambapo inaelekea baba na mama wanaotalikiana wanakuwa na sifa sawa za kustahili kuishi na mtoto.
  Yapo maamuzi mengi tu ya mahakama kuhusiana na mambo hayo na hatutagusia hata mojawapo leo kwa vile yote yamefuata zaidi misingi hii, na mingineyo inayokaribiana nayo.
  N:B Makala haya yanaweza yasijumuishe masuala fulani ambayo huathiri sheria husika kutokana na kanuni zitungwazo na Waziri anayeisimamia Sheria hii au tafsiri zilizotolewazo baadaye katika sheria zetu na Mahakama Kuu au ile ya Rufaa.
  Ki-msingi hata hivyo, hakuna mabadiliko makubwa yaliyotokea kutokana na yale yaliyoandikwa humu lakini mara zote ni muhimu sana kuwasiliana na mtaalam wa sheria ili kupata uhakika wa jambo unalolitafutia ufumbuzi.
   
 2. M

  Mwanaweja JF-Expert Member

  #2
  Aug 22, 2011
  Joined: Feb 8, 2011
  Messages: 3,576
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 135
  mkuu nashukru sana kwa msaada wako maana umenisaidia sna
   
Loading...