Misingi mitano(5) muhimu ya kufanikiwa kwenye ujasiriamali na biashara

Spirogyra

Senior Member
Mar 6, 2017
160
133
Misingi Mitano(5) Muhimu Ya Kufanikiwa Kwenye Ujasiriamali na Biashara.



Katika ulimwengu wa sasa ambao ajira zimekuwa ngumu na shida kupatikana, ujasiriamali na biashara vimekuwa ndio kimbilio la wengi. Watu wengi wanaingia kwenye biashara kama njia kuu ya kujipatia kipato.

Pamoja na biashara kuonekana kuwa kimbilio la wengi sio wote wanaoingia kwenye biashara wanafanikiwa. Tafiti zinaonesha kwamba asilimia tisini ya biashara zinazoanzishwa zinakufa mwaka mmoja baada ya kuanzishwa.

Na hata hizo zinazovuka mwaka mmoja asilimia tisini hufa baada ya miaka mitano. Hivyo kama mwaka huu zimeazishwa biashara mia moja basi miaka mitano ijayo ni biashara moja tu itakayokuwa bado inadumu.


Kwa ini biashara nyingi zinashindwa kudumu?



Biashara nyingi zinakufa kutokana na ukosefu wa elimu muhimu kuhusiana na biashara na ujasiriamali. Watu wengi wanaoingia kwenye biashara wanaingia kwa kuangalia tu ni kitu gani watu wengine wanafanya na wao kufanya hivyo hivyo.



Biashara ni rahisi sana kufanya ila ni ngumu kuendesha na kuikuza mpaka iweze kukupa faida kubwa sana. Ili uweze kuendesha na kukuza biashara itakayokupa faida kubwa ni muhimu kuchukua muda na kujifunza vitu vya muhimu vinavyohusiana na biashara.


Leo tutajifunza misingi mitano muhimu ya biashara ambayo kila biashara inatakiwa kuizingatia. Wewe kama mjasiriamali una jukumu la kujifunza na kufuata misingi hii ili uweze kufikia malengo yako kwenye ujasiriamali na biashara.


Misingi mitano muhimu ya biashara.

Ili biashara yoyote iweze kudumu na kukua inahitaji kufuata misingi ifuatayo;
  1. Kutengeneza thamani.
Ili biashara iweze kukua na kutengeneza faida ni lazima itengeneze bidhaa au huduma ambayo ni ya thamani kwa wateja. Ni lazima utoe bidhaa au huduma ambayo watu wanaihitaji sana ili kuboresha maisha yao. Kama hujaanza biashara fikiria ni kitu gani cha thamani ambacho watu wanakihitaji ila wanakikosa, kisha anza kuwapatia na utajenga biashara kubwa. Kama tayari unafanya biashara angalia ni kitu gani cha thamani unachotoa kwa watu na angalia jinsi unavyoweza kuboresha ili kupata wateja wengi zaidi.
  1. Soko.
Kuwa na kitu chenye thamani pekee bado haikutoshi kutengeneza biashara kubwa, ni lazima kuwe na soko linalohitaji bidhaa au huduma hiyo. Hata kama soko lipo bado sio rahisi kwa kila mtu kujua kwamba unatoa huduma muhimu. Hivyo ni muhimu kutafuta soko la biashara yako kwa njia mbalimbali zikiwemo matangazo. Inakubidi uhakikishe watu wanajua uwepo wa biashara yako na utengeneze uteja ili watu waje kupata thamani unayotoa. Kukosa soko la uhakika ni chanzo cha kufa kwa biashara nyingi.
  1. Kuuza.
Ili biashara ikue ni lazima uweze kuuza thamani uliyotengeneza. Ni muhimu uweze kuwashawishi watu wanunue bidhaa au huduma unayotoa. Kuuza ndio moyo wa biashara ambapo kama usipokuwa makini ni rahisi kwa biashara kufa.
  1. Kufikisha thamani.
Kama umewaahidi wateja wako kwamba bidhaa ama huduma unayotoa itaboresha maisha yao basi hakikisha hicho ndio kitu kitakachotokea kwa wateja. Ni lazima uweze kufikisha thamani uliyoahidi kwa wateja. Kwa kushindwa kufanya hivi wateja watakuona wewe ni tapeli na hawatanunua tena bidhaa yako. Kama biashara itashindwa kutengeneza wateja wanaojirudia ni lazima itakufa.
  1. Fedha.
Usimamizi wa fedha ni muhimu sana kwenye biashara. Ili biashara iweze kudumu ni lazima iweze kutengeneza mapato makubwa kuliko matumizi na uzalishaji. Ni lazima iweze kuzalisha fedha za kutosha kuiendesha na ibaki faida. Ukosefu wa fedha unaotokana na mauzo kidogo na matumizi makubwa ndio chanzo cha kufa kwa biashara nyingi. Misingi hii mitano ni muhimu sana kwa biashara. Hakuna msingi ambao unaweza kusema ni muhimu zaidi ya mwingine, yote inategemeana.

Ili biashara yoyote iweze kudumu ni muhimu kuzingatia misingi hiyo.
 
Hongera sana Nimependa mno maelezo yako ni mazuri sana,sana binafsi Nitazingatia ili kuipeleka mbele biashara yangu
 
Back
Top Bottom