Misele ya CCM na kamba fupi ya wapinzani – 1

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,266
33,039
03_10_jaf42y.jpg








HUENDA ikawa ni swali la jumla mno kuelekea uchaguzi na nini wapinzani wafanye. Ukiangalia historia ya uchaguzi, tangu ule wa wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 maswali mengi yanajitokeza.

Baadhi ya maswali hayo ni kama; je, safari hii waungane au kila mtu mtu aende na lwake au wapambane katika ubunge na kuachana na urais au wasaidiane katika kupata mgombea urais? Swali jingine pia ni hili; kipi kiini cha mabadiliko wanayotaka wapinzani hasa?

Wanasiasa wa kambi ya upinzani wamezungumza maneno kadhaa ya wapinzani na pia kuzungumza nao kuelekea uchaguzi.

Baada ya kutiwa saini kwa sheria ya kujikinga na fedha haramu, inayoitwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, kama alivyoahidi Rais Jakaya Kikwete wakati anahutubia Bunge miaka minne hivi iliyopita, kuzuia ununuzi wa kura, mchezo wa siasa na demokrasia huenda ukabadilika sana katika uchaguzi wa mwaka huu.

Kubadilika kwa mchezo huo kunatokana na hofu ya baadhi ya mambo kutafsiriwa kama rushwa na pia kubanwa kwa matajiri kugawa fedha kama njugu katika sherehe za harusi. Lakini shaka ipo na baadhi ya watu wanasema vinginevyo.

"Upinzani haujajua kitu kimoja au kama wanajua hawajakifanyia kazi kwa umakini. CCM (Chama Cha Mapinduzi) ina hela zaidi, matawi zaidi na mtu yoyote mwenye chochote ambaye anataka influence (kukubalika) atajiunga na CCM cause that's where the safe bet is (kwa sababu huko ndiko hasa kwenye usalama wa mambo yake)."

Hilo ni sehemu tu ya majibu ya mmoja wa watu waliofanyiwa mahojiano na mwandishi wa makala hii juu ya nini wapinzani wafanye wakati taifa hili linaelekea katika uchaguzi.

Katika haya, viongozi wa kisiasa wa kambi ya upinzani wamekiri kuwapo kwa msuli mkubwa wa CCM wenye kuwawezesha kuendelea na mambo ya kutawala nchini hapa; huku wakikiri kwamba kwa sasa hawawezi kutanua nchi nzima lakini wanaweza kwa namna fulani, kuhakikisha maeneo ambayo wana nguvu wanayatumia vyema na kuelekeza mashambulio maeneo hayo.

Mashambulio wanayosema wao si ya fitina bali kuwapa wananchi uwezo mpana zaidi wa kutafakari utaifa wao na kuwa na mawazo mbadala yenye uhakika wa nini wanachotakiwa kukifanya kukabiliana na uongozi mbaya unaokwamisha maslahi ya kitaifa.

Mawazo yote hayo yalishabihiana na wanasiasa wa Chadema na CUF na wanazuoni wenye uwezo na maarifa ya kuchambua mwenendo wa kisiasa nchini.

"Njia pekee wapinzani wanaweza kufanya kujizolea ushindi ni kupitia wananchi wenyewe! Wawafanye wananchi waone haja ya wao kuwapo na kuwapigia kura.

Na si tu mwananchi, lakini kufika pale ambapo wapiga kura wengi wapi... vijijini.. na maeneo ambayo bado kuendelezwa," anasema mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa katika Jamii Forum anayeenda kwa jina la ‘Mwanafalsafa 1’.

Anasema ana sababu zake za kufikiria hivyo, nazo amezigawa katika mafungu matatu makubwa: Moja, Watanzania wengi ni masikini na wanaoishi maeneo ya vijijini. Hilo ndilo eneo ambalo wapinzani wanatakiwa kujichimbia.

Hawa wana nafasi kubwa ya kushawishiwa kupiga kura dhidi ya CCM kwa sababu ni rahisi kwao kupiga kura kwa kuwaona CCM kama mabwanyenye na sababu ya wao kuwa maskini. Sababu hii haiangaliwi sana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ambaye anaamini kwamba lugha inayotumiwa na CCM kwa sasa itawafanya wananchi wachelewe kufanya maamuzi ya kubadilika kuingia upinzani kwa kuwa kwa miaka mingi walijengwa na nadharia ya chama kimoja, na wanajazwa hofu ya mabadiliko hali ambayo pia imeelezwa na mwanasiasa mwingine Ismail Jusa Ladhu wa CUF.

Wanasema kwamba hata Tume ya Nyalali ilitaka kuwapo muda wa kutoa elimu ya uraia ili wananchi waondokewe na hofu ya mabadiliko kuwa ni uhaini bali kitu kinachostahili kuendelea kuwapo katika maisha ya kila siku.

Mwanafalsafa1 anaamini kwamba wananchi maskini hukasirishwa na umasikini wao na hasa wanapojua kwamba kuna kundi fulani la chama fulani linafaidika na utajiri wakati wao masikini.

Sababu nyingine ni ule ukweli wa watu wa kati kuwa hawana shida kubwa na nafasi yao ya kipato na maisha yao, lakini anasema hawa ni wachache na mara nyingi hawatajali nani anachukua madaraka katika nchi ili mradi tu maisha yao yanaendelea bila tatizo, na kwa sasa kama watatakiwa kuchagua wataipenda CCM ili kuimarisha nafasi zao.

Sababu ya tatu ni kuwa watu matajiri wanataka mamlaka na nguvu na wanataka kulinda maslahi yao. Swali linakuja ni wangapi watataka kujiondoa CCM au wasiisaidie CCM? Wengi wamejifunza mwaka 1995 na 2000 kwa hiyo wataichagua CCM kwa sababu za maslahi yao.

Shauri la wenye utajiri kuujali CCMm Mnyika pia amelizungumzia katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, akisema kwamba matajiri ndio hasa wanaotoa nafasi kubwa zaidi kwa CCM.

“Katika sherehe za CCM za karibuni sisi tuna uthibitisho kabisa kwamba kampuni tajiri ndizo zimefanikisha sherehe hizo baada ya kuombwa rasmi na CCM," anasema Mnyika.

Kimsingi, chama tawala kina uwezo mkubwa wa kufika maeneo yote ya Tanzania kutokana na mtandao wake na hazina yake kubwa ya fedha na ipo hoja ya kuwataka wapinzani waungane ili kukabiliana na misele ya CCM.

"Hawawezi kukabiliana na misele ya CCM, wana kamba fupi sana ya kuzungushana na CCM, labda waungane," anasema mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino anayesomea shahada ya uzamili katika habari. Ukiangalia kwa makini juhudi za kuungana zilishawahi kufanywa mara kadhaa, lakini tofauti za mitizamo zimewafanya wasione vyema kuwa pamoja huku sheria ya uchaguzi ya mwaka 2008 ikiwakorofisha zaidi kwa kuwa wakiungana ni lazima wakubali matokeo, watalazimika kuachia viti walivyovitwaa na kuanza upya.

Ndio kusema kila mtu lazima awe na lwake. Hili limeonekana katika uchaguzi, Mbeya, Busanda, Kiteto, Biharamulo na Tarime.

"Sisi kama Chadema tumefanya, tumeshawishi muungano, lakini TLP na NCCR walitugeuka na wakafuatiwa na CUF, lakini hata kama tukiungana tutaweza kweli kwa mazingira haya? Nadhani unayajua matokeo ya uchaguzi na hiyo ni ishara," anasema Mnyika.

Anahisi kwamba kuungana ni vyema, japo hawawezi kutengeneza msuli wa hazina kama CCM lakini bado wanaweza kusaidia kufanya mabadiliko ya fikira kwa wananchi katika kampeni ambazo zinatakiwa kuendeshwa kama si kwa nchi nzima eneo ambalo linaonekana linawezekana.

"Hii ndiyo shida kubwa, si kuungana bali namna ya kuwaelimisha wananchi wakatambua, wakaenzi na kufikiria haja ya mabadiliko," anasema Mnyika.

i wazi upinzani walitakiwa kutambua mapema zaidi kwamba pamoja na kuwapo na siasa za vyama vingi si rahisi hata kidogo kuondoa dhana zilizojengwa za dola na chama kimoja ambazo zimetengeneza hofu kwa watanzania wengi.

Kuna tatizo la kuwafikia wananchi lakini ni lazima itafutwe njia ya kuwafikia wananchi na kutumbukiza elimu ya uraia.

CCM ni chama tajiri kupita vyama vingine vyote vckiungana pamoja. Kikiwa kinapata ruzuku ya karibu Sh bilioni mbili kwa mwezi, Chadema na CUF wanapata jumla ya Sh milioni 170, hawawezi kuwa na uwezo na mtaji wa CCM, ukiachia mbali fedha zake nyingine kutoka katika miradi yake ambayo vyama vya upinzani bado wanadai irejeshwe serikalini.

Pamoja na ukweli huo, bado shida ya rasilimali za kuwawezesha kufika vijijini muda mwingi , japo Chadema sasa hivi wanaendesha Operesheni Sangara, bado wachambuzi wa mambo wanaona upinzani unaweza kutumis staili ya CCM kufanikisha masuala ya kuamsha hisia kwa wananchi ambao ni wapiga kura.

Moja ya staili za CCM ni kutopeleka kila mtu wake mkubwa kila mahali nchini. Wanatumia watu wao huko huko kufanya kazi wanayotaka ya kuwaandaa watu.

Hali hii inasaidia kuokoa muda na fedha na jumuiya huwa inajitathmini na kuona kwamba mtu wanayezungumza naye ni mwenzao na anawapatia kile ambacho kinawafanya kufikiri vyema.

Kama muda wote utakuwa unapeleka tu watu wakubwa katika siasa utakuwa unawafanya wafikiri kwamba wewe ni wewe na wao ni wao. Wa kujitolea wapo lakini lazima watambue wazi kwamba wanajitolea kwa nia safi na wanasababu za kujitolea na sasa hili ni suala la namna ya kushawishi wananchi kutambua kwanini washirikiane nawe kuelimisha watu.

Watu hawa ndio wanaweza kuleta changamoto kubwa ya kupunguza idadi ya wabunge wa chama tawala, kwani wakiingia wabunge wengi wa upinzani taratibu nchi hii inaweza kwenda safari inayokusudiwa kama taifa; wapinzani wakiibana serikali kutekeleza wajibu wake au iwapishe.

Ndivyo inavyotokea Israel. Wapinzani wanaamini mabadiliko fulani lazima yawepo bungeni na hili linawezekana kwa kuingiza wabunge wengi wa upinzani ili kuleta presha ya maendeleo.

Kutokata tamaa na kuendelea kwa staili ya aina hii kutasaidia kuwa na mpango mkakati wa kuimarisha demokrasia na kuamsha moyo wa uchungu kwa utaifa Ni ukweli usipingana, anasema Anacletus kutoka Morogoro, kuwa kama upinzani kama unataka kuwa na mafanikio ya kudumu wanabidi waanze kujenga kuanzia chini.

Ingawa inaonekana wazi kuwa kwenye kinyang'anyiro cha urais wapinzani ni wasindikizaji tu, si vyema wakiacha kutumbukiza watu, kwani itasaidia katika kupata ruzuku, lakini ni vyema wakajikita zaidi katika kuhakikisha wanakuwa na madiwani wengi na wabunge wa kutosha kwa kuanzia.

Wapo wanaokiri kwamba mabadiliko ya msingi katika demokrasia ya Tanzania yanategemea zaidi kizazi kipya cha sasa lakini si kizazi kilichochimbuka kutoka kwenye system ya chama kimoja.

"Upinzani kweli ungekuwa na nia, wale viongozi wa mwanzo wangewekeza kwenye kizazi kijacho. It is not too late to do this (hatujachelewa kufanya hili) kwa sababu kijana kwanza ni cost effective (hana gharama.

Hahitaji very big financial incentives (hahitaji fedha nyingi) kujiunga. Pia wana mwamko zaidi na ni risk takers (watu wanaothubutu)…hawa ndiyo waandaliwe kupambana na uongozi ujao wa CCM," anasema mmoja wa wanachama nguli wa Jamii Forum.

Kwa hiyo, nadhani tatizo jingine kubwa la upinzani ni kwamba hawana programu y ya kuanda vijana kukomaa zaidi kisiasa.

Kitaratibu, ili kuwa na uhakika na hali ya baadaye lazima kuwapo urithishiji wa vijiti na katika mazingira ya sasa matawi ya vijana katika upande wa upinzani ni ushahidi zaidi kuliko maandalizi ya uongozi ujao.

Lipo tatizo lililobainishwa na wachangiaji wa masuala ya kisiasa katika Jamii Forum. Tatizo hilo ni kila kiongozi wa upinzani wa sasa kutaka yeye ndiye ajenge historia na kuwa rais wa kwanza kutoka upinzani Tanzania.

"Hii tamaa ndiyo maana inawawia vigumu kuwaweka watu wenye vipaji na hata kupishana. Kuna baadhi ya watu kwenye upinzani wamegombea urais tangu 1995 mpaka uchaguzi uliopita na bado wanabaki viongozi wakuu wa vyama. Nchi nyingine mtu kugombea hata mara mbili inakuwa kazi," anasema mwanachama mchangiaji mwandamizi wa Jamii Forum, Mwanafalsafa 1.

Lakini si hilo tu, ipo haja ya vyama vya upinzani kuangalia miaka 15 wapo katika daraja gani na kuandaa watu kwenda huko si sasa kukabiliana na visivyokubaliana.

Hoja za wachangiaji hao zinaachana na ukweli kuwa mabadiliko lazima yaanze taratibu kwa pamoja na kufikiria miaka 15 ijayo lazima kuangalia njia za mabadiliko. Katika masuala ya elimu ya uraia ambayo ndiyo chachu, Dk. Wilbrod Slaa, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema, katika mahojiano kwa njia ya mtandao anasema kwamba suala la elimu finyu ni tatizo kubwa.

"Lakini siamini kama hili kwa peke yake ni tatizo. Wakati wa kampeni ya Busanda na Biharamulo tumetoa sana elimu ya uraia.

Tumeeleza kwa kina sana uhusiano kati ya kura isiyomakini na ukosefu wa zahanati, elimu bora, barabara, na hata ukosefu wa mlo wa uhakika. Lakini watu waliendelea kupokea rushwa ya kikombe cha chumvi au kipande cha sabuni.

"Nimeshuhudia kwa macho yangu waziri akigawa kipande cha sabuni Biharamulo, na Bussanda nimeshuhudia waziri mwingine na mjumbe wa Halmashauri Kuu (ya Taifa ya CCM) akisimamia kugawa chumvi kwenye kikombe. Hivyo sidhani kama suala ni elimu tu.

Umasikini, haja ya watu wetu kutimiza mahitaji ya sasa ambayo kwao ni priority (muhimu) nadhani ndilo tatizo la msingil" anasema Dk. Slaa. Kwa maoni ya Dk. Slaa, umasikini ni tatizo la muda mrefu.

Namna pekee ya kulidhibiti hili ni kuwa na watu watakaoenda sambamba na wagawaji hao na kuwatimua, ndiyo maana Bussanda na Biharamulo CCM wameshinda kwa asilimia chache tu.

Mabadiliko kwa msingi huo ni kutafuta mbinu za kulinda zaidi wananchi wasifikiwe na hao watoa rushwa, japo ni jambo gumu zaidi pamoja na sheria iliyopo sasa ambayo lengo lake ni kuzuia.

Ni ngumu kwa kuwa kuna hila kubwa ya mficho ambayo kuing'amua ni lazima kuwapo na intelijensia kubwa inayofanyakazi kulinda maslahi ya kitaifa. Dk. Slaa anaamini kwamba wengi wa watu wanafikiria zaidi kinadharia katika kubadili mifumo lakini katika mazingira halisi nadharia hizo haziwezi kufanyakazi, kuna shida kubwa na mbinu lazima zibadilike.

Pamoja na nia ya kupeleka elimu hadi ngazi za chini, Dk. Slaa bado anakiri kwamba rasilimali bado hazitoshi, ukizingatia kuwa vyama vyenyewe havina rasilimali za kutosha kwa kazi hiyo, hata kampeni za Tanzania zikienda kwa kudra za Mungu! Tutaendelea kuwasilisha maoni na kujadili mada hii.
http://www.habarileo.co.tz/makala/?n=6306


Maoni Mimi ninafikiri ni vyema vyama vya upinzani wakakubali kuleta mabadiliko ya dhati kwenye vyama vyao kwanza ndipo wafikirie ya kwenye nchi.Tumejifundisha yaliyotokea nchi jirani ya Kenya kutokuelewana kwa viongozi wa vyama vya upinzani. Hapa kwetu tunaendelea kushuhudia umimi ukichuka nafasi kubwa katika vyama vyao na kupelekea watanzania walio wengi kuendelelea kuamini kuwa CCM ndio chama pekee kinachoweza kuwaletea maendeleo ya kweli.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom