Misamaha ya kodi za posho moto bungeni; Yazua malumbano makali, yapitishwa na bunge | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Misamaha ya kodi za posho moto bungeni; Yazua malumbano makali, yapitishwa na bunge

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by nngu007, Jun 23, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jun 23, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 57
  Trophy Points: 145
  *Yazua malumbano makali, yapitishwa na bunge
  *Wabunge wakerwa kampuni za madini kusamehewa

  Na Grace Michael, Dodoma

  WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana walilumbana vikali bungeni wakati wakipitisha Muswada wa Sheria ya Matumizi, kutokana na hoja ya Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu (CHADEMA) kutaka posho za watumishi wa umma ziondolewe kodi.

  Hoja ya mbunge huyo ilitaka posho hizo zinazozidi sh 100,000 zikatwe kodi kama sheria ya sasa inavyosema hivyo mapendekezo ya serikali ya kutaka zisitozwe kodi ikataliwe, jambo ambalo lilipingwa vikali na wabunge wa CCM na baadhi ya mawaziri.

  Miongoni mwa waliojitokeza kupingana na pendekezo hilo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Bw. William Lukuvu, Waziri wa TAMISEMI, Bw. George Mkuchika, Mbunge wa Musoma Vijijini, Bw. Nimrod Mkono, Mbunge Peramiho, Bi. Jenister Mhagama, Mbunge Kigoma Mjini, Bw. Peter Serukamba, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene na Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamis Kigwangallah wakati Bw. Zitto Kabwe wa Kigoma Kaskazini aliunga mkono hoja ya Bw. Lissu.

  Baadhi ya wabunge hao walisema lengo la mtoa hoja ni kutaka kufuta posho hizo kwa watu muhimu, wakiwamo madiwani, polisi, wanajeshi, na walimu, jambo ambalo lilipingwa na mtoa hoja, akisema lengo lake si kufuta posho hizo, bali kutaka zikatwe kodi, na kwamba kada hizo zilizotajwa hazilipwi posho zaidi ya sh laki moja.

  Katika mjadala huo, Bw. Lissu alitamka kuwa mshahara wa wabunge ni sh. milioni 3.4, kauli iliyoombewa mwongozo wa Spika na Dkt. Kigwangallah na kutolewa ufafanuzi na Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, akisema mshahara huo ni sh. milioni 2.3 kabla ya kodi.

  Kuhusu kodi za madini
  Mapema wabunge hao waliijia juu serikali kuhusu kipengele kinachotoa msamaha wa kodi kwa kampuni za madini ambazo zimekuwa zikipata faida kubwa.Wabunge hao walipingana vikali na kipengele hicho kwa kusema kuwa wema wa nchi hii ndio unaoigharimu kwa sasa kwa kuwa wanaonufaika na rasilimali za madini ni kampuni za nje.

  Kipengele hicho kimo katika maelezo ya Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Pereira Silima wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha ya 2011.

  Wabunge hao waliochangia kipindi cha asubuhi, wengi walionekana kukerwa na kitendo hicho cha serikali kuendelea kuwa na msamaha wa kodi katika kampuni za madini huku ikiacha kodi katika mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo mengi yanatoa huduma za kijamii.Akichangia muswada huo, aliweka wazi kuwa, sababu zinazoigharimu taifa katika sekta ya madini ni misamaha ya kodi inayotolewa katika kampuni hizo, misamaha ambayo ilitungiwa sheria na bunge katika miaka ya 1997 na 1998.

  Alisema kuwa taifa litaendelea kuwa maskini kwa kuwa serikali inapoteza mabilioni ya fedha katika kampuni hizo kutokana na huruma za kutoa misamaha ya kodi.Alisema kuwa kitendo cha kutoa msamaha kinatoa mwanya wa uporaji wa rasilimali hizo za madini hatua inayofanya nchi kuendelea kuwa maskini."Nchi inaangamizwa na misamaha ya kodi, wema mkubwa ambao umetolewa kwa kampuni kubwa ya nchi tajiri ambazo zinajipatia mabilioni ya fedha kutokana na rasilimali zetu ndio unatuponza," alisema Bw. Lissu.

  Alijaribu kurejea mapendekezo mbalimbali ya tume ambazo zilizowahi kuundwa kuchunguza sekta ya madini, alisema kuwa majibu yake yalikuwa ni kuondolewa kwa misamaha inayotolewa kwa kampuni za madini, hivyo akasema bila kuangaliwa kwa umakini suala hilo, nchi hii itaendelea kuwa maskini huku kampuni hizo yakitajirika kupitia rasilimali zetu.Kutokana na hali hiyo, Bw. Lissu alisema ni lazima ifike mahali Watanzania waikatae hali hii kwa kuwa inazidi kuwafanya kuwa maskini.

  "Hili ni Taifa ambalo hatujifunzi kutokana na historia yetu na hii itatufanya tuendelee kutumbukia katika mashimo ambayo tumekuwa tukiingia huko nyuma.Muswada huu unakuja unapendekeza kuongeza misamaha ya kodi katika madini...tunawaongezea badala ya kuwaondolea kama ilivyopendekezwa na tume ya Jaji Bomani ambayo ilisema misamaha ifutwe," alisema Bw. Lissu.

  Alisema kuwa kwa sababu ya kukosa ujasiri, wabunge watapiga makofi kwa kupitisha muswada huo huku kipengele hicho kikiliangamiza taifa kwa kupoteza mapato ambayo ni mabilioni ya fedha.

  "Sheria tulizozitunga ndizo zinatuangamiza na katika mazingira kama haya tutasikia nini na tutaona nini na katika mazingira haya ambayo watu hawakumbuki walikotoka ni vyema tukaliona hili kuwa kipengele hiki kinatuangamiza?" alisema Bw. Lissu.

  Jambo jingine alilopinga Bw. Lissu ni kuhusu kutolewa kwa msamaha wa kodi ya gawio katika kampuni yaliyowekeza katika maeneo huru ya kibiashara.

  Mbunge mwingine aliyepingana na kipengele hicho ni wa Mbozi Mashariki, Bw. Godfrey Zambi ambaye alisema kuwa huruma hii ya kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya madini itaendelea kuiponza nchi.

  Akizungumzia kipindi cha miaka 10 ambacho kinatolewa kwa msamaha wa kodi ya gawio kwa kampuni zilizowekeza katika maeneo huru ya biashara, alisema kuwa muda huo ni mwingi ambao unaigharimu nchi hivyo akapendekeza kupunguzwa kwa muda huo ili iwe miaka mitano.

  Bw. Zambi pia alipingana vikali na upandishwaji wa kodi za mafuta ya taa kwa kigezo cha kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta kwa kusema kuwa kupandisha kodi hiyo ni kulenga kuwaumiza wananchi ambao hawana hatia na akashauri kuwa kama serikali ina nia ya kuondoa tatizo hilo iwabane wafanyabiashara hao wasio waaminifu kwa kuwapa adhabu kali ili waache.

  Naye Mbunge wa Kasulu Mjini, Bw. Moses Machali alihoji sababu za serikali kuendelea kutoa misamaha katika kampuni hizo na akamtaka Waziri wa Fedha kutoa ufafanuzi jambo hilo.

  Suala jingine ambalo lilizua mjadala ni kuhusu gawio la asilimia nne ya tozo ya maendeleo ya ufundi stadi kutunisha mfuko wa bodi ya mkopo ya elimu ya juu ambapo wabunge walipinga na kusema kuwa Bodi ya Mikopo ipate asimilia mbili, VETA ipate asilimia tatu na asilimia moja ipelekwe katika Mfuko wa Vyuo vya NACTE.

  Akichangia suala hilo, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa bila kuangalia kundi ambalo ni kubwa la vijana wanaomaliza darasa la saba na wanaomaliza kidato cha nne ambao wamekosa nafasi za kuendelea na masomo ya juu ni sawa na kukalia bomu ambalo likilipuka litaleta shida katika nchi hii.

  "VETA lazima iwekewe umuhimu wake kwa kuongezwa fedha kwani kuna kundi kubwa la vijana ambao wanaweza wakajiunga na vyuo hivyo na hatimaye wakajipatia ajira na wengine kujiajiri wenyewe lakini kama tutapendelea elimu ya juu tu tutakuwa tunatengeneza bomu la ajabu," alisema Bw. Mahenge.

  Katika maelezo ya Naibu Waziri wa Fedha, katika muswada huo katika kampuni ya madini, alisema kuwa kutakuwa na msamaha maalum wa kodi ya ongezeko la thamani kwa kampuni za madini zenye mikataba na serikali na misamaha hiyo itatolewa kwa mujibu wa masharti yaliyopo ndani ya mkataba.

  Msahama huo pia upo kwenye kampuni za utafiti na uchimbaji wa madini ambapo utahusisha huduma na bidhaa za utafiti na utafutaji pekee ambazo hufanywa na mwekezaji kabla ya kuanza uzalishaji.

  Akizungumzia suala la kodi za mafuta ya taa, alisema kuwa, ushuru wa bidhaa ya mafuta ya taa utatoka sh. 52 hadi kufikia sh. 400.30 ambapo alisema hatua hiyo ina lengo la kuondoa tofauti iliyopo baina ya bei ya dizeli na mafuta ya taa lakini pia kudhibiti uchakachuaji wa mafuta na kuboresha shughuli za kiuchumi hususan usafirishaji wa mafuta kutoka Tanzania kwenda nje.

  Muswada huo unazifanyia marekebisho sheria 12 zinazohusu masuala ya fedha, kodi na ushuru kwa lengo la kuweka, kurekebisha au kufuta viwango vya kodi, ushuru na ada mbalimbali.
   
 2. Kamakabuzi

  Kamakabuzi JF-Expert Member

  #2
  Jun 23, 2011
  Joined: Dec 3, 2007
  Messages: 1,499
  Likes Received: 82
  Trophy Points: 145
  Ndiyooo ndiyoo, ipite - inaliangamiza taifa; halafu tunachekelea (kama baba wa Taifa alivyowaita) kama zuzu
   
 3. s

  smz JF-Expert Member

  #3
  Jun 23, 2011
  Joined: Dec 18, 2010
  Messages: 251
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Unajua sishangai wabunge wa ccm kukubali kodi juu ya mafuta ya taa kwa sababu wao haiwagusi. Niambie ni mbunge gani anatumia mafuta ya taa. Hata yakipanda kufikia 5000 kwa lita hawatapiga kelele kwa vile hawayatumii. Wao matumizi makubwa ni kwenye petroli, Diesel, Gas, umeme nk.

  Lakini hawa watu wananishangaza kidogo; labda wenzetu hata familia zao zilishaondokana na matumizi ya mafuta ya taa huko vijijini walikozaliwa. Kwa sababu inatia aibu kuidhinisha kodi kwenye bidhaa ambayo shangazi yako, mjomba wako, babu yako na wengi wa aina hiyo wanaitegemea sana katika maisha yao ya siku kwa siku. Jamani hivi tumekuwa wepesi wa kusahau kiasi hiki??!!. Mimi sijaipenda hii, mbaya mbaya mbaya sana.
   
 4. B

  Byendangwero JF-Expert Member

  #4
  Jun 23, 2011
  Joined: Oct 24, 2010
  Messages: 872
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Napendekeza hapa jamvini tuanzishe kampeni ya kulitaka bunge kuhairishwa mara moja. Pendekezo langu linatokana na ukweli kwamba baada ya bunge hilo kupitisha bajeti kama ilivyowasilishwa na Mkullo, na halafu likapitisha muswada wa matumizi ambao unatoa kibali cha kuanza kutumika kwa fedha zilizoidhinishwa kwenye bajeti hiyo ifikapo Julai mosi, halina kazi nyingine ya maana kuhusiana na mchakato wa bajeti ya serikali kwa mwaka ujao. Hii mijadala ya kuzungumzia wizara moja moja iliyopangwa kuendelea hadi tarehe 7/Septemba, ni upotezaji tu wa fedha za umma kwasababu haiwezi kubadirisha chochote; maana matumizi ya serikali kwa mwaka ujao katika ujumla wake yaliisha pitishwa, na hivyo katika miezi hii miwili na nusu zitakuwa zinapigwa porojo tu bungeni, ambazo zitakazokuwa zikimgharimu mlipa kodi zaidi ya shs 500 milioni kila siku.
   
 5. B

  Byendangwero JF-Expert Member

  #5
  Jun 23, 2011
  Joined: Oct 24, 2010
  Messages: 872
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Napendekeza hapa jamvini tuanzishe kampeni ya kulitaka bunge kuhairishwa mara moja.Pendekezo langu linatokana na ukweli kwamba  baada ya bunge hilo kupitisha bajeti kama ilivyowasilishwa na Mkullo, na halafu likapitisha muswada wa matumizi ambao unatoa kibali cha kuanza kutumika kwa fedha zilizoidhinishwa kwenye bajeti hiyo ifikapo Julai mosi, halina kazi nyingine ya maana kuhusiana na mchakato wa bajeti ya serikali kwa mwaka ujao. Hii mijadala ya kuzungumzia wizara moja moja iliyopangwa kuendelea hadi tarehe 7/Septemba, ni upotezaji tu wa fedha za umma kwasababu haiwezi kubadirisha chochote; maana matumizi ya serikali kwa mwaka ujao katika ujumla wake yaliisha pitishwa, na hivyo katika miezi hii miwili na nusu zitakuwa zinapigwa porojo tu bungeni, ambazo zitakazokuwa zikimgharimu mlipa kodi zaidi ya shs 500 milioni kila siku.
   
Loading...