Misa yatangaza tuzo uchunguzi katika rushwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,098
Misa yatangaza tuzo uchunguzi katika rushwa
Mwandishi Wetu
Daily News; Saturday,June 21, 2008 @00:03

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-Tan), imetangaza kutoa tuzo ya uandishi wa habari za uchunguzi katika rushwa na utawala bora.

Tuzo hiyo inatolewa kwa ufadhili wa Millennium Challenge Corporation (MCC) kupitia Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID). Tuzo hiyo inayotolewa kwa ushirikiano na asasi ya PACT Tanzania, itakuwa ya pili kushindaniwa nchini na mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana.

Mwenyekiti wa MISA Tan, Ayoub Ryoba alisema jana kuwa mashindano kwa ajili ya tuzo hiyo yako wazi kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wengine wa vyombo vya habari, magazeti, televisheni na waandishi wa habari wa kujitegemea ili mradi awe raia wa Tanzania.

Alisema wameweka utaratibu na vigezo mbalimbali vya ushindi, maudhui, stadi na uchunguzi, uchambuzi na ubunifu ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo watayatilia mkazo. Sherehe za kutoa tuzo hizo zitafanyika wiki ya mwsiho ya Septemba mwaka huu.

Tuzo hiyo yenye fedha taslimu Sh milioni saba itagawanywa kwa washindi 10. Washindi hao, watano watatoka kwenye magazeti na watano wengine watatoka kwenye vyombo vya utangazaji. Washindi wengine sita wataambulia vyeti na hivyo kufanya idadi ya washindi kufikia 16.

Ryoba alisema pamoja na umuhimu wa kuwa na habari za matukio mbalimbali, lakini utamu, ubora na heshima ya habari vinatokana na uchunguzi. “Ni kuona zaidi ya wengine, kuchimba na kufukua vya kale na vipya na kuviwasilisha kwa kina na kwa njia inayoeleweka ambako kunaupa uandishi heshima yake inayostahili.

“Natarajia waandishi wa habari wengi watasoma maelezo na maelekezo kuhusu tuzo hii; watazingatia umuhimu wa mashindano haya siyo kwa nia ya kupata tuzo bali na hasa kwa kukuza vipaji vyao na heshima ya taaluma yao,” alisema Ryoba.

Alisema mashindano hayo yamelenga kujenga jeshi kubwa la waandishi wa habari wenye uelewa mpana wa jamii; waandishi walio tayari kushiriki katika kufichua rushwa na ufisadi; wenye nia na shauku ya kutoa upande mwingine mzuri wa jamii uliofunikwa na lindi la kiza na husuda.

“Hii ni kazi kubwa, lakini pia ni kazi nzuri,” alisema Ryoba na kuongeza tuzo ni hitimisho la kila mwaka la kutambua kazi bora katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na kujenga jamii isiyo na rushwa au inayopambana na kuondokana na rushwa.

Alisema kushiriki kwa waandishi wa habari katika vita dhidi ya rushwa ni jambo la kujivunia, akisema “Tuandike basi, tuingie kwenye mashindano, tujiunge na jamii pana ya wanaotaka kufanya jamii yetu kuwa mahali pazuri pa kuishi bila uoza na uonevu utokanao na rushwa.”
 
imekaa njema sana hii kama itafanikiwa. Hizo habari sijui watazipata wakati sirikali inazifanya ni siri.
 
Back
Top Bottom